Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 8/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uhuru wa Kidini Wachunguzwa Upya Ugiriki
  • Lugha ya Kilatini Bado Yatumika
  • “Nakala” za Sanamu
  • Utapiamlo Wawaua Watoto
  • Je, Kuna Maji Kwenye Mwezi?
  • Tahadhari kwa Dawa ya Kutuliza Maumivu
  • Masomo Kuhusu Utekwaji-Nyara
  • Arudi Baada ya “Kutoweka”
  • Je, Ni “Dawa Bora ya Kulevya Isiyo na Madhara”?
  • Jinsi Chokoleti Inavyotengenezwa
    Amkeni!—2005
  • Visababishi Vilivyotia Mizizi, Athari Mbaya za Utapiamlo
    Amkeni!—2003
  • Msiba Mkubwa Sana
    Amkeni!—2003
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 8/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Uhuru wa Kidini Wachunguzwa Upya Ugiriki

“Yaonekana kwamba hivi karibuni serikali ya [Ugiriki] imekuwa ikihangaishwa na masuala yanayohusu haki ya uhuru wa kidini, pia ikifikiria uamuzi unaongojewa wa kusahihishwa kwa katiba,” laripoti gazeti la habari la Athens To Vima. “Kamati isiyo rasmi katika Idara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni imeundwa ili kuchunguza upya mfumo wa kisheria unaohusika na masuala ya uhuru wa kidini, zile sheria za dikteta Metaxa ambazo hufanya kugeuza watu kidini kuwa kinyume cha sheria, na hali ambazo katika hizo dini ndogondogo zisizo za Othodoksi huruhusiwa kujenga makanisa na mahali pa kukutania.” Ripoti hiyo yaendelea kusema kwamba hatua hii imechukuliwa hasa kwa sababu ya kesi nyingi ambazo Mashahidi wa Yehova nchini Ugiriki wamewasilisha katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

Lugha ya Kilatini Bado Yatumika

Bado Kilatini ndiyo lugha rasmi ya Vatican City, hata ingawa lugha hiyo iliacha kutumiwa katika ibada za Katoliki ya Kiroma katika miaka ya 1960. Wataalamu hutafsiri hati za papa katika lugha ya Kilatini, lakini sasa haitumiki sana huko Vatican kwenyewe. Hata hivyo, katika Novemba 1997, papa aliombolezea kuacha kutumiwa kwa lugha ya Kilatini na kuhimiza ianze kutumiwa tena. Wakati huohuo, kikundi cha wasomi wa Vatican kimekamilisha mradi wa miaka minane wa kuandika kamusi ya Kilatini iliyo ya kisasa. Maneno ya kisasa kama vile “kipulizaji,” “uwanja wa ndege,” “duka kubwa,” “teksi,” na “msongamano wa magari” sasa yanapatikana katika lugha ya Kilatini. Hata simu ya kushika kwa mkono iliyoenea sana sasa inaitwa kwa Kilatini telephonium cellulare. Kwa mashabiki wa Kilatini kuna habari njema hata zaidi. Kasisi mmoja katika Roma sasa ameweka mahali pa Kilatini katika mfumo wa Internet, laripoti The Times la London.

“Nakala” za Sanamu

Kufikia mwaka wa 2000, sanamu zote katika bustani za umma za Roma zaweza kuwa miigizo. Kwa nini? “Ikiwa twataka kuhifadhi vitu vya ukumbusho hatuna namna ila kutengeneza nakala,” aeleza Carla Benocci mshiriki wa mojawapo ya sosaiti za kihistoria za Roma. Aliongezea kwamba baadhi ya sanamu hizo ziko katika “hali mbaya na ya kusikitisha sana, zikiwa zimeharibiwa na muda ambao umepita, zikaharibiwa na magari, watu, na wanunuzi wa vitu vilivyoibwa.” Majaribio yanafanywa ili kuhakikisha ni vifaa gani vitakavyotumiwa ili kutokeza uvutio wa kisanaa kama ule wa awali na wakati huohuo kukinza zisiharibiwe na ukungu na watu. “Nakala” nyingine zimetengenezwa kwa utomvu; nyingine zimetengenezwa kwa simiti na kufunikwa kwa vumbi ya marumaru. Nakala hizi “zafanana sana na zile za awali,” asema Benocci, “hivi kwamba pindi moja wezi walivunja nakala moja ili kuiba kichwa chake na kujaribu kuiba nyingine ikiwa nzima.” Na namna gani zile za awali? Zitawekwa katika majumba ya ukumbusho, ambapo zitatazamwa bila kuhatarishwa.

Utapiamlo Wawaua Watoto

“Utapiamlo huua watoto wengi zaidi kuliko ugonjwa wowote wa mlipuko, msiba wa asili, au vita,” laripoti gazeti la kila siku la Ufaransa Le Monde. Inakadiriwa kuwa karibu watoto milioni saba hufa kila mwaka kutokana na utapiamlo. Ripoti ya Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) ya mwaka wa 1997 yaonyesha kwamba utapiamlo ndicho kisababishi cha vifo kwa asilimia 55 ya watoto milioni 12 walio na umri wa chini ya miaka mitano ambao hufa kila mwaka. Mbali na kuwaua watoto, utapiamlo ndicho kisababishi cha maradhi mengi sana ya kimwili na kiakili na vilevile kudhoofika kwa mifumo ya kinga. Katika Asia Kusini, mtoto 1 kati ya 2 huwa na utapiamlo, na katika Afrika, 1 kati ya 3. Hata hivyo, tatizo hili huathiri pia nchi zilizositawi. Kwa kielelezo, shirika la UNICEF laripoti kwamba katika Marekani, mtoto 1 kati ya 4 chini ya umri wa miaka 12 hapati lishe anayohitaji.

Je, Kuna Maji Kwenye Mwezi?

Chombo cha angani Lunar Prospector kimegundua kitu kama barafu katika ncha za mwezi, laripoti gazeti The New York Times. Vifaa katika chombo hicho vyaonyesha kuwapo kwa hidrojeni, na inafikiriwa kwamba njia pekee ambayo hidrojeni ingeweza kuwa katika mwezi ni ikiwa katika namna ya maji. Inafikiriwa kwamba maji hayo yako katika namna ya vipande vidogo vya barafu vilivyochanganyika na mchanga. Yaonekana yanawakilisha asilimia moja au chini ya hiyo ya udongo wenye mawemawe. Tayari wanasayansi fulani wanabashiri kwamba maji hayo yangeweza kutegemeza jamii ya binadamu na kutokeza hidrojeni na oksijeni zikiwa fueli kwa vyombo vya angani vinavyosafiri kutoka kwenye mwezi. Wengine wana wasiwasi kwamba hata ingawa maji hayo yako, ungekuwa mradi ghali sana. Dakt. Bruce Murray, wa Taasisi ya Tekinolojia ya California, alisema kwamba ingegharimu kiasi kidogo cha fedha kupeleka maji kutoka duniani kuliko kuyachimba katika mwezi.

Tahadhari kwa Dawa ya Kutuliza Maumivu

“Kupitisha kidogo-kidogo vipimo vya acetaminophen—ambayo ni sehemu kuu ya dawa ziitwazo Tylenol, Excedrin, dawa nyinginezo nyingi za kutuliza maumivu ambazo hazihitaji agizo la daktari—kwaweza kusababisha madhara makubwa ya ini hasa zinapochanganywa na alkoholi,” laonya gazeti Health, na kwaweza kusababisha kifo. “Watu wengi hufikiri kwamba wanaweza kuzidisha vipimo vya dawa mara mbili au tatu na wasipatwe na madhara,” asema William Lee, mtaalamu wa tiba ya maradhi yasiyohitaji upasuaji katika Chuo Kikuu cha Texas Southwestern Medical Center. “Sivyo ilivyo na acetaminophen.” Mwili uvunjapo acetaminophen, hutokeza sumu kwa ini. Ini hujikinga kwa kutokeza kiuasumu kiitwacho glutathione. Hata hivyo, kutumia kupita kiasi acetaminophen kwaweza kushinda nguvu uwezo wa ini wa kujikinga. Alkoholi humaliza kiuasumu glutathione, kwa hiyo kutumia dawa hii ni hatari hasa baada ya kunywa chupa chache za alkoholi. Na kwa kuwa acetaminophen hupatikana katika aina mbalimbali 300 za dawa, ni rahisi kuitumia kupita kiasi bila kutambua.

Masomo Kuhusu Utekwaji-Nyara

Sasa watoto katika shule za Taiwan wana mtaala mpya—masomo kuhusu utekwaji nyara. “Katika Taiwan watoto wanaelekea sana kutekwa nyara kuliko mahali popote ila Filipino, kukiwa na wastani wa kisa kimoja cha kutekwa nyara kwa kila siku mbili na nusu,” lasema Asiaweek. Wazazi, wakihofu kwamba watoto wao watatekwa nyara kadiri uhalifu uendeleapo kuongezeka, waliomba programu hiyo. Mtaala huo huwazoeza watoto kuwa wenye tahadhari wanapotembea peke yao, wanapokaribia kuingia lifti, na wanapotumia usafiri wa umma. Wanajifunza kuwa macho waonapo watu wenye kushukiwa na namna ya kufanya watekwapo nyara. Ijapokuwa kuna mambo yasiyofaa katika mtaala huu, jitihada zinafanywa kuwasaidia watoto kuwa na mtazamo unaofaa kuelekea maisha.

Arudi Baada ya “Kutoweka”

Aina fulani ya bundi wa msitu, aliyefikiriwa kuwa ametoweka kwa sababu hakuonekana kwa miaka 113, ameonekana na kupigwa picha katika msitu ulio karibu na Shahada, India, kusini-mashariki ya Mumbai. Ndege huyu mwenye urefu wa inchi nane ana macho makubwa na madoadoa, mdomo mkubwa, miguu mikubwa, na kucha ndefu kupita kiasi. “Anafikiriwa kuwa mmojawapo wa ndege wa ajabu wa India,” akasema Pamela Rasmussen, wa Jumba la Ukumbusho la Kitaifa la Historia ya Asili katika Washington, ambaye pamoja na wafanyakazi wenzake wawili walimpiga picha ndege huyu. “Hili ni jambo lililo nadra sana maishani.” Aina mbili za ndege wenye kustaajabisha wa India, ambao hakuna ushuhuda uliorekodiwa wa kwamba waliokoka, ni aina ya bata wenye vichwa vyenye rangi ya waridi, ambao walionekana mara ya mwisho katika miaka ya 1930, na wengine aina ya kipululu walioishi katika milima ya Himalaya, ambao hawajaonekana kwa karibu miaka 100.

Je, Ni “Dawa Bora ya Kulevya Isiyo na Madhara”?

Ubora wa chokoleti wa kuchangamsha, wa kuondoa mfadhaiko na wa kuchochea hamu ya ngono umesifiwa kwa mamia ya miaka. Hata hivyo, utafiti wa karibuni waonyesha kwamba kwa kweli chokoleti huathiri “viwango vya wasiwasi, amani ya akili, na mwenendo wa kingono,” laripoti gazeti la habari la Kifaransa Le Monde. Wanasayansi wamegundua kitu fulani kilichoko katika chokoleti ambacho hufanana na amfetamini na kingine “kinachofanana kabisa na dawa ya kuondoa mfadhaiko.” Pia utafiti mpya umefunua kuwapo kwa anandamide, kifereji cha neva cha kupitisha habari “kinachozidisha uchangamfu na furaha” sawa na ifanyavyo bangi. Jambo hili pamoja na kiwango cha chini cha sumu cha chokoleti lilifanya gazeti moja la habari kufikia mkataa huu: “Kwa kuchochea utendaji wa kimwili na wa kiakili, kwa kutokeza nguvu na hisi ya furaha na kujisikia bila athari zozote na kiwango cha chini cha uraibu, chokoleti yakaribia kuwa dawa bora ya kulevya isiyokuwa na madhara.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki