Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 11/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UKIMWI na Asia
  • Mizio Katika Ujerumani
  • Nawa Mikono!
  • Kutenda Vibaya Watoto na Mfumo wa Kinga
  • Uhusiano wa China na Mesopotamia
  • Vifo Kutokana na Mchochota wa Ini Aina ya B
  • Uchafuzi wa Hewa Ndani ya Nyumba
  • Vita vya Maji
  • Uhalifu Wenye Jeuri Katika Venezuela
  • Kuendeleza Mtindo-Maisha Wenye Afya
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Je! Wanadamu Wanaweza Kuleta Amani na Usalama Wenye Kudumu?
    Amani na Usalama wa Kweli—Wewe Unaweza Kuupataje?
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1992
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 11/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

UKIMWI na Asia

Ijapokuwa mataifa fulani ya Magharibi yamepata upungufu kidogo katika idadi ya visa vilivyothibitishwa vya UKIMWI, ugonjwa huu umeenea sana katika sehemu nyingi za Asia. Visa vya ugonjwa huu katika India “viliongezeka mara 71 katika nusu ya kwanza ya miaka ya 1990,” kulingana na ripoti moja ya Asiaweek. Thailand, ambayo ilikuwa namba 57 ulimwenguni katika visa vya ugonjwa huo katika 1990, ilikuwa namba 5 kufikia katikati mwa miaka ya 1990. Kambodia ilisonga juu kutoka namba 173 hadi namba 59. Na Filipino ilipata ongezeko la asilimia 131 katika kipindi hichohicho. Wengi wanajua ya kwamba biashara ya ngono ya watoto inayositawi katika baadhi ya nchi hizi imechangia kwa kiasi fulani, lakini Asiaweek lataarifu kuwa wanasiasa fulani ambao nchi zao “hutegemea sana dola za watalii . . . hawataki kuchukua hatua zifaazo” dhidi ya biashara hiyo.

Mizio Katika Ujerumani

Uchunguzi mmoja uliochapishwa na Shirika la Serikali la Ujerumani la Mipango ya Bima ya Afya ya Makampuni umefunua kwamba Mjerumani 1 kati ya 4 walio na umri wa zaidi ya miaka 14 huugua kutokana na mzio. Mzio ulioenea sana ni wa homa ya nyasi kavu, ambayo huathiri karibu watu milioni sita huko. Karibu watu milioni 2.3 husumbuliwa na jua, na zaidi ya milioni 2 wana mizio ya manyoya ya wanyama, laripoti gazeti Süddeutsche Zeitung. Zaidi ya asilimia 40 ya wale wanaougua kutokana na mizio hutumia dawa kwa ajili ya tatizo lao, na asilimia 10 hutaarifu kwamba dalili za ugonjwa huzuia sana kawaida zao za kila siku za maisha. Uchunguzi huo pia ulifunua kwamba watu katika “kazi na taalamu fulani, kama vile waokaji, maseremala, wauguzi, na madaktari, wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupatwa na mizio.”

Nawa Mikono!

“Kunawa mikono ndiyo njia bora zaidi, rahisi zaidi, na isiyo na gharama zaidi ya kuzuia kuenea kwa maambukizo mengi,” lataarifu gazeti la habari la Italia Corriere della Sera. Na bado, “zaidi ya Waitalia 3 kati ya kila 10 hawanawi mikono wanapotoka msalani, hata ikiwa wanaenda kula punde tu baada ya hapo.” Matokeo ya uchunguzi huu karibu yafanane na uchunguzi mwingine kama huo uliofanywa katika nchi nyinginezo. “Mikono yaweza kupitisha vijidudu kwenye chakula na kuanzisha mweneo wa uchafuzi,” aeleza mtaalamu wa mikrobiolojia Enrico Magliano. Mweneo huu waweza kukomeshwaje? Nawa mikono—chini ya kucha pia—kwa sabuni na maji moto au yaliyo vuguvugu kwa angalau sekunde 30 (muda wa chini zaidi uhitajiwao kuondosha bakteria). Hii yatia ndani kuisugua pamoja kwa sekunde 10 hadi 15. Isuuze na uikaushe vizuri, ukianzia kwenye kigasha kuelekea kwenye vidole, makala hiyo yasema.

Kutenda Vibaya Watoto na Mfumo wa Kinga

Kulingana na watafiti katika Chuo Kikuu cha Mie huko Japani, mtoto anapotendwa vibaya kwa muda mrefu, mfumo wake wa kinga hudhoofika, ukimwacha mtoto akiwa katika hali rahisi kushambuliwa na magonjwa. Chuo Kikuu hicho kilichunguza miili ya watoto 50 kati ya umri wa mwezi mmoja na miaka tisa ambao walikuwa wamekufa kutokana na mvujo wa damu katika ubongo au hali nyingine zilizosababishwa na kutendwa vibaya kimwili. Matezi ya thymus ya watoto hao, “ambayo hudhibiti utendaji mbalimbali wa mfumo wa kinga, yalikuwa yamekuwa madogo kufikia nusu ya uzito wa kawaida,” laripoti Mainichi Daily News. Kadiri kutendwa vibaya kuendeleavyo ndivyo matezi hayo huzidi kupunguka. Kwa kweli, “tezi la mtoto ambaye alikuwa ametendwa vibaya kwa zaidi ya miezi sita lilikuwa dogo mara 16 kuliko la mtoto asiyetendwa vibaya,” likasema gazeti hilo la habari. Watafiti wameona upungukaji wa tezi kama huo katika watoto ambao wametendwa vibaya kiakili au wamepatwa na utapiamlo kutokana na ukosefu wa wazazi wao kuandaa chakula.

Uhusiano wa China na Mesopotamia

Kwa muda mrefu imedhaniwa kuwa ustaarabu wa kale wa Kichina ulitokana na Bonde la China la Hwang He, lililokuwa huru kutokana na uvutano wa nje. Baada ya uvumbuzi wa juzijuzi wa kiakiolojia, nadharia hiyo sasa yatiliwa mashaka. Gazeti la Ufaransa Courrier International laripoti kuwa katika eneo moja karibu na Ch’eng-tu, katika Mkoa wa China wa Szechwan, kikundi cha waakiolojia kimefukua mabaki ya lionekanalo kuwa hekalu la kale lililojengwa ndani ya sehemu iliyozungushiwa ukuta. Waakiolojia hao waripoti kuwa muundo na umbo la hekalu zafanana sana na minara ya piramidi ya hekalu ya Mesopotamia ya kale. Profesa Ichiro Kominami, wa Chuo Kikuu cha Kyoto alitaarifu kuwa “yawezekana kuwa [Szechwan] ilikuwa chanzo cha ustaarabu wa kale wa kipekee wa China ambao ulihusika kwa karibu na ule wa Indus na wa Mesopotamia.”

Vifo Kutokana na Mchochota wa Ini Aina ya B

Shirika la Afya Ulimwenguni lakadiria kwamba zaidi ya watu milioni moja hufa kila mwaka kutokana na mchochota wa ini aina ya B. Daktari wa watoto Jagdish Chinnappa asema kuwa karibu visa 150,000 vya vifo hivi hutokea katika India. Katika mkutano mmoja uliopangwa na kampuni moja ya madawa iliyo katika mataifa mengi, alieleza kwamba India ina “wabebaji wa HBV [virusi ya mchochota wa ini aina ya B] milioni 35 hadi 40 ambao hujumuika kuwa asilimia 10 ya jumla ya ulimwenguni pote,” laripoti The Times of India. Gazeti hilo laongezea kuwa “kimoja kati ya visa viwili vya ugonjwa wa ini wenye kudumu na vinane kati ya visa kumi vya kansa ya ini ya msingi husababishwa na maambukizo ya Mchochota wa Ini Aina ya B.”

Uchafuzi wa Hewa Ndani ya Nyumba

Uchunguzi wa karibuni uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Nishati ya Tata (TERI) katika New Delhi, India, waonyesha kwamba Wahindi milioni 2.2 hufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusiana na uchafuzi wa hewa. Gazeti The Indian Express laripoti kuwa kulingana na uchunguzi huo, uchafuzi wa ndani ya nyumba ni kisababishi kikuu. Wanawake wanaoishi katika mitaa ya mabanda ambao hutumia makaa ya mawe, kuni, na samadi kupikia huelekea kuhatarishwa zaidi. Huku hatua zikichukuliwa ili kudhibiti uchafuzi wa hewa wa nje, wataalamu walihisi kuwa ni machache sana yanayofanywa ili kupunguza hatari kwa mamilioni ndani ya nyumba zao wenyewe. “Tatizo lililofichika laendelea ambalo haielekei kuna suluhisho la mara moja liwezekanalo,” akataarifu mkurugenzi wa TERI, R. K. Pachauri.

Vita vya Maji

Utabiri wenye kuogofya kuhusu wakati ujao wa ugavi wa maji ulimwenguni ulitolewa katika Mkutano wa Ulimwengu Kuhusu Maji wa kwanza, ambao ulifanyika huko Marrakech, Moroko, katika Machi 1997. Uchafuzi, ukame, na ongezeko la idadi ya watu huzidi kuweka misongo mikubwa kwa vyanzo vya maji. Kama vile gazeti la habari la Ufaransa Le Monde liripotivyo, “uhitaji wa maji unaongezeka mara mbili zaidi ya idadi ya watu ulimwenguni.” Kulingana na Shirika la Ulimwenguni la Metorolojia, kufikia mwaka wa 2025, thuluthi mbili za idadi ya watu ulimwenguni wataishi katika sehemu ambazo hazitakuwa na maji ya kutosha. Isipokuwa suluhisho lifaalo lipatikane, wenye mamlaka fulani wahofia kwamba maji yatakuwa sababu ya vita katika karne ya 21. Tayari, “UM limeonyesha karibu sehemu 300 zilizo na uwezekano wa kutokeza pambano,” lasema gazeti Le Monde.

Uhalifu Wenye Jeuri Katika Venezuela

Ikiwa na idadi ya watu 20,000,000, Venezuela huwa na wastani wa mauaji ya kimakusudi 400 kila mwezi, lasema gazeti la habari El Universal. Uchunguzi uliofanywa na shirika moja wataarifu kuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa jeuri si ya kiuchumi, bali ni ya kijamii na kitamaduni. Chini ya kichwa “Umaskini Si Kisababishi Kikubwa cha Mwenendo Mbaya,” hilo gazeti la habari lilisema kuwa kulingana na ripoti hiyo, jeuri ya Venezuela yatokana na ukosefu wa viwango vya kibinadamu na mazoezi ya wazazi nyumbani. Ili kuboresha hali hiyo, wataalamu wanapendekeza kufunza uzazi wenye madaraka na kutia moyo watu wahangaikie zaidi familia zao.

Kuendeleza Mtindo-Maisha Wenye Afya

Katika ripoti yake ya World Health Report 1997, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) laonya kwamba binadamu akabili “tatizo la kuteseka” linaloongezeka. Kila mwaka, kansa na maradhi ya moyo, pamoja na matatizo mengine ya afya yenye kudumu, husababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 24 na yatisha kuongeza mzigo wenye kulemea kwa mamia ya mamilioni wengine. Idadi ya visa vya kansa katika nchi nyingi yatarajiwa kuongezeka kufikia mara mbili, katika miaka 25 ijayo. Maradhi ya moyo na mshtuko wa akili, yale magonjwa yenye kuua zaidi katika mataifa tajiri, yatakuwa ya kawaida zaidi katika nchi maskini. Kwa sababu ya uwezekano huu, WHO latoa mwito wa kampeni ya ulimwenguni pote “yenye juhudi nyingi na yenye kudumu” ili kuendeleza mitindo-maisha yenye afya na kupunguza mambo yenye kuhatarisha—milo isiyo ya afya, kuvuta sigareti, uzito kupita kiasi, na kukosa mazoezi—ambayo mara nyingi hutokeza maradhi yenye kufisha.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki