Kuutazama Ulimwengu
UKIMWI na Maendeleo
Duniani pote, mweneo wa UKIMWI umerudisha nyuma maendeleo ya kibinadamu kwa mwaka 1.3, yasema ripoti moja ya majuzi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo. Nchi fulani za Afrika ndizo zimeathiriwa zaidi—Zambia imepoteza zaidi ya miaka kumi ya maendeleo ya kibinadamu; Tanzania, miaka minane; Rwanda, miaka saba; na Jamhuri ya Afrika ya Kati, zaidi ya miaka sita. UKIMWI pia umerudisha nyuma muda wa tazamio la kuishi. Katika Amerika Kaskazini na Ulaya, UKIMWI umekuwa kisababishi kikuu cha vifo miongoni mwa watu wazima walio chini ya umri wa miaka 45. Ulimwenguni pote, watu 6,000 huambukizwa virusi vya HIV kila siku, mtu 1 kwa kila sekunde 15. Zaidi ya asilimia 85 ya vifo vya UKIMWI hutukia kwa watu walio na umri kati ya miaka 20 na 45.
Stadi za Kusoma na Kazi ya Kuajiriwa
“Kati ya asilimia 56 na 64 ya Wakanada ambao hawana kazi hawajui kusoma na kuandika vizuri,” yasema ripoti moja ya Takwimu za Kanada, kulingana na gazeti la habari The Vancouver Sun. Uchunguzi mmoja uliofanywa 1995 wa kutahini uwezo wa kusoma na kuandika lugha ya kawaida, hati, na hesabu ulifunua kwamba asilimia 36 ya Wakanada walipata ugumu katika hali hizo tatu. Katika “nyanja za ‘zamani’ kama vile kilimo, uchimbaji wa madini, viwanda na ujenzi, . . . uwezo wa kusoma na kuandika huelekea kuwa wa chini zaidi,” lasema gazeti Sun. Kwa kuwa kazi inapungua katika sekta hizo, wafanyakazi wasiojua kusoma na kuandika vizuri hasa ni rahisi zaidi kustaafishwa na kufutwa. John O’Leary, msimamizi wa shirika la kusoma na kuandika, alisema kwamba “kutoweza kusoma na kuandika vizuri katika 1996 ni kukosa fursa nyingi sana za kibinafsi na kitaaluma.”
Mzio wa Mende
Kulingana na University of California at Berkeley Wellness Letter, yasemekana kwamba kati ya watu milioni 10 na milioni 15 Marekani wana mizio ya mende. Anapoguswa na mende, mtu mwenye mzio aweza kupatwa na “mwasho wa ngozi, mafua makali, au dalili za ugonjwa wa pumu.” Karatasi hiyo ya habari ilitaja kwamba “kufikia asilimia 80 ya watoto wote wenye ugonjwa wa pumu huathiriwa kwa urahisi na mende.” Si kwamba mende ni ishara ya jiko chafu. Hata “jiko safi zaidi linaweza kuwa na mende,” yadai Wellness Letter. Imekadiriwa kwamba kwa kila mende aonekanaye, kunaweza kuwa na 1,000 wasioonekana wanaotambaa-tambaa kote nyumbani. Mende wawili wanaweza kupata wazao 100,000 kwa mwaka mmoja tu.
Ongezeko la Umaskini
Idadi ya watu ulimwenguni pote ambao sasa wanaishi katika umaskini hohehahe—yaani wale wanaochuma kiasi kinachopungua dola 370 kwa mwaka—ni bilioni 1.3 hivi, karibu robo ya idadi ya watu wote ulimwenguni. Wengi wanaishi katika nchi zinazoendelea. Kwa kawaida, watu hawa hukosa kupata chakula cha kutosha, maji safi, kutunzwa afya, makao mazuri, elimu, na kazi. Katika visa vingi, wao hudharauliwa katika jamii wanamoishi na hawana uwezo wa kubadili hali zao. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, idadi ya watu ambao ni maskini hohehahe inaongezeka kwa karibu milioni 25 hivi kila mwaka.
Uraibu wa Dawa za Kulevya Katika Ulaya
Shirika moja jipya la Ulaya ambalo limejitoa kuchunguza matumizi na matumizi mabaya ya dawa za kulevya hivi majuzi lilichapisha ripoti yalo ya kwanza ya kila mwaka. Uchunguzi wao, kulingana na gazeti la kila siku la Ufaransa Le Monde, ulifunua kwamba kuna waraibu “kati ya 500,000 na milioni moja” wa heroini katika Muungano wa Ulaya. Ingawa yaonekana waraibu wa heroini hawaongezeki au hata kupungua katika majiji makubwa ya Ulaya, uraibu huo wa heroini unaongezeka katika miji midogo. Vitu vinavyotokana na mbangi kama vile hashishi na bangi bado ndivyo vinavyotumiwa zaidi katika Ulaya. Wastadi wanahangaikia ufanisi unaonawiri wa zile ziitwazo kwa ukawaida cocktails, ambamo dawa za kulevya huchanganywa na dawa za kawaida na alkoholi. Katika Ulaya ya Kaskazini, amphetamines, Ecstasy (ambayo hutokana na methamphetamine), na LSD zinazidi kupendwa miongoni mwa vijana.
“Msongo wa Wembamba”
Chini ya kichwa “Kupambana na Msongo wa Wembamba,” laripoti The Irish Times: “Idadi kubwa sana za wasichana wabalehe wanaugua ugonjwa wa ukosefu wa damu kwa sababu ya kufuata mitindo ipendwayo ya ulaji.” Madaktari wameonyesha hangaiko kubwa kuhusu mtindo huo. Katika visa fulani biashara ya mavazi ya mtindo hulaumika “kwa athari zazo zenye kuharibu sana vijana ambao hushawishika kwa urahisi.” Ripoti hiyo yasema kwamba katika kizazi kilichopita kiolezo wa kawaida wa mitindo ya mavazi alikuwa na uzito uliopungua ule wa mwanamke wa kawaida kwa asilimia 8. Siku hizi kiolezo ana uzani mdogo kwa asilimia 23 kuliko mwanamke wa kawaida. “Mikono na miguu myembamba sana,” lasema The Irish Times, “ni mtindo upendwao sana, na hali ya kukonda kupita kiasi—yenye rangi ya kijivu, iliyo changa, na yenye tatizo la ulaji . . .—sasa hupendekezwa kuwa mtindo wa kawaida.” Chini ya msongo wa kuwa kawaida, wasichana wengi wachanga katika kutafuta wembamba hutumia vyakula ambavyo haviwapi chuma, protini, na vitamini ambazo ni muhimu sana.
Upendezi Usiotazamiwa wa Biblia
“Nusu milioni za nakala za Agano Jipya katika lugha ya Denmark [tafsiri ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo] zimepeanwa—nakala moja kwa asilimia 98 hivi za nyumba zilizo Copenhagen,” laripoti ENI Bulletin. Hiyo ilifanywa kuwa sehemu ya kusherehekea fungu la Copenhagen kuwa Jiji Kuu la Kitamaduni la Ulaya la 1996. Ilikuwa imetabiriwa kwamba kati ya asilimia 10 na 20 ya nyumba za Copenhagen zingekataa zawadi hiyo. Lakini kulingana na Morten Aagaard, katibu mkuu wa Shirika la Biblia la Denmark, “ni asilimia moja au mbili tu za nyumba” zilizokataa toleo hilo. Ugawanyaji wa aina hiyo umepangiwa Stockholm, Sweden, katika 1998.
Rafiki wa Maisha
Katika Ujerumani, watu 9 kati ya 10 wasema kwamba wana rafiki wa maisha, laripoti Nassauische Neue Presse. Jambo hilo lilifunuliwa na uchunguzi uliofanywa na Shirika la Takwimu za Utafiti wa Sayansi ya Kijamii, ambalo lilihoji zaidi ya watu 1,000 wenye umri wa kati ya miaka 16 na 60. Uwasiliano na ufuatiaji wa haki ulionwa kuwa muhimu sana miongoni mwa mambo yaliyo katika urafiki wa kudumu. Karibu wote waliohojiwa walikubali kwamba ukosefu wa uaminifu-mshikamanifu na usaliti bila shaka ungekomesha urafiki kama huo. “Ni asilimia 16 pekee wanaotazamia rafiki mzuri kuwakopesha pesa wakati wa dharura,” kulingana na gazeti hilo. Kwa upande mwingine, idadi kubwa waliona kutegemezwa na rafiki katika nyakati za ugonjwa kuwa muhimu kabisa.
Kula Matunda Kila Siku
Kula matunda ya karibuni kila siku kunahusianishwa na upungufu wa hatari za maradhi ya moyo, kulingana na uchunguzi wa miaka 17 uliofanyiwa watu 11,000, na ambao ulichapishwa katika British Medical Journal. Miongoni mwa wale waliochunguzwa ambao walikuwa wakila matunda ya karibuni kila siku, mlikuwa na vifo vichache kwa asilimia 24 vya maradhi ya moyo na vifo vichache kwa asilimia 32 vya mishtuko ya akili. Kati ya wale waliokula matunda kila siku, kulikuwa na vifo vichache kwa asilimia 21 kwa kulinganisha na wale ambao hawakuwa wakila matunda kwa ukawaida. Mlo unaokosa matunda ya karibuni waweza kuchangia ongezeko la magonjwa ya mishipa kama vile maradhi ya ghafula na maradhi ya moyo miongoni mwa watu fulani, chasema kikundi fulani cha wanasayansi wa Uingereza na Hispania. Kwa manufaa makubwa zaidi kiafya, watafiti sasa wanapendekeza kula angalau mboga na matunda mara tano kwa siku. Iwapo hakuna matunda na mboga za karibuni, basi matunda na mboga zilizowekwa kwenye friji zaweza kuandaa manufaa hizohizo, kulingana na British Medical Journal.
Kuwatunza Wenye Akili Punguani
“Uji wa moto, muziki wa kichinichini na mazingira yaliyoundwa kwa uangalifu si uvumbuzi mpya wa kitiba, lakini zinabadili utunzaji wa wazee-wazee,” lasema The Globe and Mail la Kanada. Kutumia mabadiliko yaliyo sahili na yasiyogharimu katika njia ambazo mgonjwa anaogeshwa na kulishwa husaidia kupunguza kuvurugika kwao na hangaiko lao. Kwa mfano, ripoti hiyo ilisema kwamba kuleta kila chakula kwa wakati tofauti huondolea mgonjwa uhitaji wa kuamua ni chakula kipi atakula kwanza, jambo ambalo mara nyingi humvuruga akili mtu aliye punguani. Utayari wa kujaribu njia mpya umetokeza upungufu mkubwa katika matumizi ya dawa za kubadili hisia za mgonjwa.
Ni Hatari Zaidi ya Kuvuta Sigareti?
Kulingana na Takwimu za Kanada, “maisha ya kukaakaa ni hatari kwa afya zaidi ya mara mbili kuliko kuvuta sigareti,” laripoti The Medical Post. Ingawa inaelekea Wakanada wapatao milioni saba watapatwa na matatizo mazito ya kiafya na vifo vya mapema kwa sababu ya kuvuta tumbaku, watu kati ya milioni 14 na milioni 17 wanakabili hatari kama hizo kwa sababu hawafanyi mazoezi. Kukosa wakati, nishati, na kichocheo kunatajwa kuwa mambo makuu yanayohitilafiana na mazoezi ya kawaida. Watu wa kukaakaa pia wanaelekea kula mafuta mengi na kutokula matunda na mboga sana. “Lengo la sasa la kupata manufaa bora zaidi ya moyo ni kuwafanya watu wafanye mazoezi . . . angalau dakika 30 kwa kiasi au kwa kasi,” lasema gazeti Post.