Ladha—Zawadi ya Muumba Mwenye Upendo
“KATIKA hisi [tano],” akasema Linda Bartoshuk, mtafiti mashuhuri wa hisi ya kuonja, “hisi ya kuonja ni ya hali ya juu zaidi.” Kuonja ni jambo lenye kupendeza ambalo hutulinda kwa kutusaidia kupambanua kitu kinachokubalika na kinachodhuru.
Maajabu ya ladha hutuwezesha kufurahia utamu wa chungwa lililotoka tu kuchumwa, ladha yenye kuburudisha ya aiskrimu, ladha chungu ya kikombe cha kahawa asubuhi na ladha yenye kupendeza ya mchuzi wa mpishi. Ladha ni yenye nguvu sana hivi kwamba tabia za utu zimeshirikishwa nayo.
Labda umewatambulisha watu fulani kuwa wazuri. Kwa upande mwingine, huenda ulisema mtu mwingine alikuwa mkali. Mtu anayefungia wengine kinyongo aweza kusemwa kuwa mchungu. Kwa kielelezo, Biblia husema juu ya “watu wenye uchungu wa nafsi,” na hurejezea pia kwenye “maneno ya uchungu.”—Waamuzi 18:25; Zaburi 64:3; 2 Samweli 17:8.
Ladha na Historia ya Ulimwengu
Jambo kuu katika safari za baharini za uvumbuzi katika karne za 15 na 16 lilikuwa ladha. Karibu miaka 500 iliyopita, Vasco da Gama aliabiri kuzunguka ncha ya Afrika kufikia India na kurudi Ureno, akiwa na shehena ya viungo. Karne tatu zilizofuata, mataifa ya Ulaya yaliingia katika mapambano, huku Hispania, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Ureno, zikishindania kudhibiti maeneo yaliyotokeza viungo.
Huenda ukajiuliza ni ‘kwa nini mataifa yangepigana na kufa kwa ajili ya viungo?’ Ili kutosheleza ladha! Ndiyo, hali ya Wazungu ya kuonja viungo ilikuwa yenye nguvu sana. Kufikia leo hii viwanda vya kisasa, biashara, na sayansi vyote huandaa ladha zinazopendwa.
Lakini ladha ni nini? Na hushirikianaje na hisi zetu nyinginezo?
Fungu la Ulimi
Kiungo kikuu katika hisi yetu ya kuonja ni ulimi. Nyingi za seli onji zetu ziko katika ulimi, ijapokuwa nyingine ziko katika sehemu nyingine za kinywa na umio. Chunguza kwa umakini ulimi wako kwenye kioo. Ona michomozo mingi sana midogo ambayo hufanya ulimi wako uwe kama mahameli. Michomozo hii huitwa papillae. Seli onji ndogo-ndogo hujikusanya ndani ya papillae kwenye uso wa ulimi. “Kila seli onji ina chembe 100 au zaidi za kuonja,” lasema gazeti Science, “ambazo zinapochochewa, huamsha chembe ya neva ambayo hupeleka ujumbe kwenye ubongo.”
Idadi ya seli onji yaweza kutofautiana sana katika watu mbalimbali na hivyo kuathiri ladha. Ulimi wa mwanadamu waweza kuwa na seli onji 10,000 au chache kama 500. Inglis Miller, aliyechunguza muundo wa seli onji alisema hivi: “Watu walio na seli onji nyingi huonja ladha nyingi; watu walio na seli onji chache huonja ladha chache.”
Jinsi Ambavyo Kuonja Hufanya Kazi
Hisi ya kuonja ni yenye utata sana. Kwa kweli, ni jambo la kikemia. Vipande vilivyoyeyuka vya kemikali kutoka kwenye chakula mdomoni mwetu huchochea vipokea ladha ambavyo hujitokeza kwenye vitundu vidogo katika ulimi wetu. Chembe za vipokea ladha hufanya kazi na kuchochea chembe za neva (nyuroni) kupeleka ishara kutoka kwa seli onji mpaka kwenye ubongo.
Kwa kushangaza, seli onji moja yaweza kuchochea nyuroni nyingi tofauti-tofauti, na nyuroni moja yaweza kupokea ujumbe kutoka kwa seli onji kadhaa. Hakuna mtu ajuaye kabisa jinsi vipokezi vya ladha na mfumo wake ulio tata hufanya kazi. Kitabu The Encyclopedia Americana chasema: “Hisi zinazohisiwa katika ubongo kwa wazi hutokana na mfumo tata wa mipwito ya elektroni inayopitishwa na chembe za kupokea ladha.”
Pia hisi nyingine huhusika na ladha. Kitabu The New Book of Popular Science kilisema hivi: “Nyakati nyingine mtu hata hatambui kama anaonja au ananusa kitu fulani.” Mathalani, twaweza kupita karibu na mahali pa kuoka mikate na kunukia mikate iliyotoka tu kuokwa. Kinywa chetu chaanza kudondosha mate. Kisha tuingiapo ndani ya duka hilo na kuona hiyo mikate na labda kugusa gamba lake, hisi zetu huchochewa hata zaidi. Twawa na hamu ya kuumega!
Kwa hiyo basi, hisi hii ya kuonja ni nini? Gazeti Omni laeleza hivi: “Kile ambacho mtu wa kawaida hufafanua kuwa kuonja, kwa kweli ni mchanganyiko wa hisi kadhaa: harufu, ladha, mguso, umbile, mwono, kusumbuliwa kwa kemikali (kuwasha kwa pilipili, utulivu wa mnanaa), na halijoto.”
Kwa upande mwingine, kama makala hiyo iendeleavyo kusema, “hisi ya kuonja . . . ni sahili sana. Sisi hutofautisha asili nne (na ni asili nne pekee) za kuonja: utamu, -enye chumvi, chachu, na chungu.” Ijapokuwa watu wamependa kugawanya ulimi katika sehemu za kuhisi ladha, sasa inaaminiwa kwamba seli onji moja iliyo mahali popote katika ulimi yaweza kugundua asili kadhaa au zote nne za ladha.
Lakini, bado kuna mambo mengi sana yasiyojulikana kuhusu kemia ya kuonja. Kwa kielelezo, haijulikani ni kwa nini kuongeza matone machache ya maji ya limau yaliyo chachu kwenye chakula chako itaboresha ladha yake ya chumvi. Na inapendeza kwamba asili za kuonja utamu, chachu na kitu chenye chumvi hupeleka ishara kwenye chembe za ladha, lakini kitu kichungu huelekea kufanya chembe hizo zitokeze ujumbe wa kemikali.
Kukuza Ladha
Yaelekea umeanza kupendezwa na vitu kadhaa ambavyo hukuvipenda hapo awali. Hii yaweza kuwa kweli kuhusu vitu kama vile zeituni, jibini ya samawati, tanipu, viungo vikali, na vyakula vichungu. Kutoka nyakati za mapema “mboga zenye uchungu,” kama vile endive na chicory, zimeongezea ladha ya kipekee kwenye milo na saladi. Lakini ladha yako yapasa kuzoezwa ili kufurahia ukali huo.—Kutoka 12:8.
Uchunguzi unaonyesha kwamba kupendezwa na ladha ya chakula kwategemea mazingira ambayo unapata chakula hicho. Kwa kielelezo, mwanamke mmoja hakuwa amewahi kuonja soseji. Hata kuiona na harufu yake yenyewe ilimchukiza kwa sababu mama yake alizichukia sana soseji hizo. Lakini siku moja alipokuwa katika umri wa miaka ya 20, mwanamke huyu alikuwa na njaa kali sana na hakupata chochote cha kula ila soseji. Kwa hiyo alikula chache na alishangaa kuona kwamba alipenda sana ladha yake!
Kwa hiyo, ikiwa wataka kupendezwa na chakula fulani kipya, kijaribu unapokuwa na njaa kwelikweli. Na ikiwa wewe ni mzazi, kumbuka kwamba namna unavyotenda kuelekea vyakula fulani, vilevile hali ambazo unavitokeza, kwaweza kuwaathiri watoto wako. Fanya hali ipendeze unapojaribu vyakula vipya. Husisha mtoto wako. Mwandishi mmoja alipendekeza hivi:
“Wakati wa kutayarisha chakula weka mtoto wako jikoni katika kiti kilichofungwa cha kuchezea au juu ya kiti. Atakuwa akiona na kufurahia harufu nzuri ya vyakula vya familia katika hali yenye kustarehesha—na kuvijua hata kabla hajawa mkubwa vya kutosha kuvila. Miezi michache baadaye unaweza kumpa vipande vya vyakula unavyotayarisha, vikiwa vibichi au vikiwa havijaiva kabisa.”
Aliongezea hivi: “Huenda ikataka ufanye mipango ya mapema na muda wa ziada, lakini kwa mlo wa pindi moja moja tafuta njia sahili ambazo mtoto wako aweza kukusaidia kutayarisha mlo mpya au usiopendwa. Watie moyo wakionje wanapokitayarisha. Msaidizi wako atakuwa mwenye furaha na mwenye njaa atakapoonja—hali bora kabisa kwa kukianza chakula.”
Wakati Hisi ya Kuonja Ipunguapo
Kwa kusikitisha, hisi ya kuonja yaweza kupungua wakati uzeekapo, kama vile rafiki mzee wa Mfalme Daudi Barzilai alivyoonyesha aliposema: “Nimepata leo miaka themanini. . . . Mimi mtumwa wako, je! naweza kuonja nilacho au ninywacho?” (2 Samweli 19:35) Mambo mengine pia yaweza kuhusika katika kupungua kwa hisi ya kuonja au hata kuipoteza.
Tatizo laweza kuwa tokeo la kujeruhiwa kichwa, mzio, ambukizo, dawa, kuwa karibu na kemikali, au hata homa tu. Kutamauka sana kwa wale wasioweza kunusa na kuonja kulionyeshwa kwa njia yenye kugusa moyo na mtu mmoja aliyepata madhara hayo. Aliandika hivi: “Tunachukua kivivi hivi tu harufu kali ya kahawa na ladha tamu ya machungwa hivi kwamba tunapopoteza hisi hizi, inakuwa kana kwamba tumesahau namna ya kupumua.”
Ile inayosemekana kuwa ladha bandia ni kasoro yenye kusumbua ambayo mtu huhisi ladha ya kitu kisichokuwako. Wagonjwa wa kansa wanaopewa tibakemikali nyakati nyingine huchanganyikiwa na hisi za kuonja na kunusa.
Baraka Kutoka kwa Mungu
Inapendeza kama nini wakati hisi yetu ya kuonja inapofanya kazi sana! Watu wengi wenye umri mkubwa zaidi hukumbuka kwa furaha ladha walizofurahia walipokuwa vijana—za matunda yaliyoiva yaliyochunwa kutoka kwenye mti au ladha ya vyakula vilivyotayarishwa kwa njia ya pekee. Jambo la kwamba Muumba wetu hutamani tufurahie ladha za kuonja linaonyeshwa na maneno yanayopatikana katika ahadi yake ya karamu “ya vinono vilivyojaa mafuta” katika ulimwengu wake mpya wenye uadilifu, wakati ambapo kuteseka, kuzeeka, na kifo havitakuwapo tena.—Isaya 25:6-9; Ayubu 33:25; Ufunuo 21:3, 4.
Kwa kweli ladha huboresha maisha zetu. Bila hisi hiyo, kula kungechosha kama vile kujaza gari mafuta. Kwa kweli, ladha ni baraka kutoka kwa Muumba mwenye hekima na mwenye upendo!
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mfunze mtoto wako kufurahia vyakula vyenye lishe