Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 9/8 kur. 6-8
  • Tumaini na Upendo Zitowekapo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tumaini na Upendo Zitowekapo
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Ni Sifa Yenye Kuokoa Uhai?
  • Kukata Tumaini Kwaweza Kutokea
  • Kujiua—Pigo la Vijana
    Amkeni!—1998
  • Tatizo la Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—2001
  • Kwa Nini Watu Hukata Tamaa ya Kuishi?
    Amkeni!—2001
  • Kujiua Tatizo Lililojificha Linaloenea Kasi
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 9/8 kur. 6-8

Tumaini na Upendo Zitowekapo

MSICHANA mmoja wa Kanada mwenye umri wa miaka 17 aliandika sababu zake za kutaka kufa. Miongoni mwa sababu hizo, yeye aliorodhesha mambo yafuatayo: ‘Nahisi upweke na naogopa wakati ujao; nahisi nikiwa wa hali ya chini mbele ya wafanyakazi wenzangu; vita ya nyuklia; kuharibiwa kwa tabaka ya ozoni; nina sura ya kutisha, kwa hiyo sitapata mume kamwe na nitaishia kuwa peke yangu; sidhani kama kuna mambo mengi ya kufanya nistahili kuishi, basi kwa nini ningoje ili niyagundue; kifo changu kitaondolea kila mtu mzigo; sitaumizwa tena na mtu yeyote kamwe.’

Je, hizo zaweza kuwa baadhi ya sababu zinazofanya vijana wajiue? Nchini Kanada, “bila kuhesabu aksidenti za magari, kujiua ndicho kisababishi kikuu cha vifo miongoni mwao.”—The Globe and Mail.

Profesa Riaz Hassan, wa Chuo Kikuu cha Flinders cha South Australia, asema katika insha yake inayoitwa “Maisha Zilizokatizwa: Mielekeo Katika Kujiua kwa Vijana”: “Kuna sababu kadhaa za kijamii zinazohusu swali hilo na kuonekana kuwa zimechangia sana kujiua kwa vijana. Sababu hizo ni kiwango cha juu cha vijana kukosa kazi; mabadiliko katika familia za Australia; ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya; ongezeko la ujeuri wa vijana; matatizo ya akili; na ongezeko la pengo kati ya ‘uhuru wa kusema tu’ na uhuru wa kujipatia.” Insha hiyo yaendelea kutaja kwamba matokeo ya uchunguzi kadhaa yameonyesha kwamba kuna hali ya kutotumaini wakati ujao na kudokeza kwamba “idadi kubwa ya vijana wana hofu na wasiwasi kuhusu wakati wao ujao na wa ulimwengu. Wao waona ulimwengu ulioharibiwa na vita ya nyuklia na kuharibiwa na uchafuzi na uharibifu wa mazingira, jamii iliyoharibiwa ambamo tekinolojia haiwezi kudhibitiwa na kujaa kwa ukosefu wa kazi.”

Kulingana na uchunguzi wa Gallup uliofanyiwa watu wenye umri wa kati ya miaka 16 na 24, visababishi vingine zaidi vya kujiua ni pengo linalozidi kuongezeka kati ya matajiri na maskini, ongezeko la familia zenye mzazi mmoja, ongezeko la matumizi ya bunduki, kutendwa vibaya kwa watoto, na “kukosa imani [kwa ujumla] juu ya wakati ujao.”

Gazeti Newsweek laripoti kwamba nchini Marekani, “kuwapo kwa bunduki huenda kukawa ndicho kisababishi kikuu cha [kujiua kwa vijana]. Uchunguzi mmoja uliolinganisha kujiua kwa vijana ambao hawakuonekana kuwa na matatizo ya akili na watoto ambao hawakujiua ulipata tofauti moja tu: bunduki yenye risasi nyumbani. Yapinga kabisa wazo la kwamba bunduki haziuwi watu.” Na mamilioni ya familia zina bunduki zenye risasi!

Hofu na jamii isiyojali zaweza kuwasukuma vijana haraka wafikie hatua ya kujiua. Ebu fikiria: Kiwango cha uhalifu wenye ujeuri uliofanyiwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 12-19 kinashinda kwa mara mbili uhalifu uliofanyiwa watu kwa ujumla. Uchunguzi uligundua kwamba “wasichana wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24 huelekea zaidi kushambuliwa,” laripoti gazeti Maclean’s. “Wanawake hushambuliwa mara nyingi zaidi na kuuawa na watu wanaodai kuwa wanawapenda.” Matokeo ni nini? Hofu hizi na nyinginezo “hutowesha uhakika na usalama wa wasichana hao.” Katika uchunguzi mmoja, karibu thuluthi moja ya wale waliobakwa ambao walihojiwa walikuwa wamefikiria kujiua.

Ripoti moja ya New Zealand yataja jambo jingine kuhusu kujiua kwa vijana, ikisema: “Maadili ya kilimwengu yaliyoenea ya kufuatia vitu vya kimwili ambayo huona mafanikio ya mtu kuwa mali, sura nzuri, na uwezo huwafanya vijana wengi wahisi kuwa bure kabisa na kupuuzwa na jamii.” Kwa kuongezea, gazeti The Futurist lasema: “[Vijana] wana mwelekeo wenye nguvu wa kutaka kuridhika mara moja, wakitaka vyote na kuvitaka haraka iwezekanavyo. Programu za televisheni ambazo wanapenda zaidi ni vipindi vya mfululizo vyenye kuendelezwa. Wangependa ulimwengu wao ujae watu walewale wenye sura nzuri, wenye kuvalia mavazi ya kisasa zaidi, wenye pesa nyingi na umashuhuri, na wasiohitaji kufanya kazi kwa bidii.” Mambo hayo yote yasiyo halisi na matazamio ambayo hayafanikiwi huonekana kama huwafanya vijana wakate tumaini na kwaweza kufanya wajiue.

Je, Ni Sifa Yenye Kuokoa Uhai?

Shakespeare aliandika: “Upendo hufariji kama jua la baada ya mvua.” Biblia yasema: “Upendo haushindwi kamwe.” (1 Wakorintho 13:8) Katika sifa hiyo kuna suluhisho kwa tatizo la vijana wenye mwelekeo wa kujiua—kutamani kwao upendo na mawasiliano. Kitabu The American Medical Association Encyclopedia of Medicine chasema: “Watu wenye mwelekeo ya kujiua mara nyingi hujihisi wakiwa wapweke sana, na fursa ya kuzungumza na mtu mwenye kusikiliza na mwenye hisia-mwenzi nyakati nyingine hutosha kuzuia tendo hilo la kukata tumaini.”

Mara nyingi vijana huhitaji sana upendo na kujiona kuwa hawako peke yao. Kutimiza uhitaji huo huendelea kuwa kugumu kadiri siku zipitavyo katika ulimwengu huu usio na upendo na wenye uharibifu—ulimwengu ambamo hawana uwezo. Kukataliwa na wazazi kwa sababu ya kuvunjika kwa familia na talaka zaweza kuchangia vijana kujiua. Na kukataliwa huko kwaweza kudhihirika kwa njia nyingi.

Ebu fikiria kisa cha wazazi ambao ni nadra sana wawe pamoja na watoto wao nyumbani. Huenda Mama na Baba wakawa wanajishughulisha mno na kazi zao au wanafuatia sana vitumbuizo fulani ambavyo havihusishi watoto. Ujumbe usio wa moja kwa moja kwa watoto wao ni kukataliwa waziwazi. Mwandishi mashuhuri wa habari aliye pia mtafiti Hugh Mackay asema kwamba “wazazi wanazidi kujipenda. Wanajitanguliza ili waendeleze mitindo yao ya maisha. . . . Tukisema wazi, watoto hawapendwi tena. . . . Maisha ni magumu nayo huwafanya watu waelekee kufuata mambo yao wenyewe.”

Kisha, katika tamaduni fulani watu wenye kutaka waonekane kuwa wanaume hawataki kuonwa kuwa walezi. Mwandishi wa habari Kate Legge asema hivi: “Wanaume wenye mwelekeo wa kupenda kufanya utumishi wa umma kwa kawaida hupendelea kazi zenye kuokoa uhai au ya kuzima moto kuliko kazi za malezi . . . Wao hupendelea ile hali ya kishujaa ya kupambana na mambo ya nje kuliko kazi za malezi.” Na, bila shaka, mojawapo ya kazi za malezi zaidi leo ni kuwa mzazi. Kuwa mzazi mbaya ni kama kumkataa mtoto. Tokeo ni kwamba mwana wako au binti yako aweza kujiona vibaya na asiweze kukuza stadi za kuchangamana na jamii. Gazeti The Education Digest lasema: “Bila kujiona vizuri, watoto hawana msingi wa kufanya maamuzi ya mambo yawafaayo zaidi.”

Kukata Tumaini Kwaweza Kutokea

Watafiti wanaamini kwamba kukata tumaini ni sababu kubwa ya kujiua. Gail Mason, mwandishi juu ya kujiua kwa vijana katika Australia, alisema: “Kukata tumaini huonwa kuwa kunahusiana sana na mawazo ya kujiua kuliko mshuko wa moyo. Nyakati nyingine kukata tumaini husemwa kuwa dalili moja ya mshuko wa moyo. . . . Mara nyingi hiyo huwa kukata tumaini na kukosa tumaini juu ya wakati ujao wa vijana, na hasa kuhusu wakati wao ujao wa kiuchumi: na kwa kiwango kidogo kukata tumaini kuhusu hali ya duniani pote.”

Mifano mibaya inayowekwa na viongozi wa umma wasiofuatia haki haichochei vijana kuinua maadili yao wenyewe. Basi wanakuwa na mtazamo, “Kwa nini nisumbuke kuwa mwenye kufuatia haki?” Gazeti Harper’s Magazine lasema juu ya uwezo wa vijana wa kuona unafiki, likisema: “Vijana, wakijua sana kutambua unafiki, wanajua kusoma sana—lakini si kusoma vitabu. Lakini kile wanachosoma sana ni ishara za kijamii zinazotoka katika ulimwengu ambao wanalazimika kuishi.” Na ishara hizo zasemaje? Mwandishi wa vitabu Stephanie Dowrick asema: “Hatujapata kuwa na habari nyingi hivi juu ya jinsi tunavyopaswa kuishi. Hatujapata kuwa matajiri kiasi hiki na kuwa na elimu hivi, lakini watu wamekata tumaini kotekote.” Na kuna watu wachache sana wenye mifano ya kuigwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa na wa kidini. Dowrick auliza maswali machache yenye kutuhusu: “Tutapataje hekima, kujirekebisha na hata kupata umaana kutokana na kuteseka kusiko na maana? Tutasitawishaje upendo katika hali ya ubinafsi, chuki na pupa?”

Utapata majibu ya maswali haya katika makala yetu ifuatayo, na majibu hayo yaweza kukushangaza.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Idadi kubwa ya vijana wana hofu na wasiwasi kuhusu wakati wao ujao na wa ulimwengu”

[Blabu katika ukurasa wa 7]

“Fursa ya kuzungumza na mtu mwenye kusikiliza na mwenye hisia-mwenzi nyakati nyingine hutosha kuzuia tendo hilo la kukata tumaini”

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Dalili Fulani za Kujiua

• Matatizo ya usingizi, kukosa hamu ya kula

• Kujitenga na kutochangamana na watu, kuwa na mwelekeo wa kufanya aksidenti

• Kutoroka nyumbani

• Kufanya mabadiliko makubwa sana kwa njia ya kuvalia na kujipamba

• Kutumia vileo vibaya na/au dawa za kulevya

• Kukasirika na uchokozi

• Kuzungumza kuhusu kifo; kuandika mambo yahusuyo kujiharibu; kuchora picha za jeuri, hasa kufanyiwa ujeuri huo

• Kuhisi kuwa na hatia

• Kukata tumaini, wasiwasi, kushuka moyo, na kulialia

• Kupeana vitu vya kibinafsi

• Kutoweza kukaza fikira kwa muda mrefu

• Kutopendezwa tena na utendaji wenye kufurahisha

• Kujichambua

• Kufanya ngono kiholela

• Kushuka kwa ghafula kwa maksi za shule, na matatizo ya kuhudhuria shule

• Kushiriki na madhehebu au genge

• Kufurahi sana baada ya kushuka moyo

Zinategemea Teens in Crisis (Shirika la Marekani la Wasimamizi wa Shule) na Depression and Suicide in Children and Adolescents, cha Philip G. Patros na Tonia K. Shamoo

[Picha katika ukurasa wa 7]

Upendo mchangamfu na huruma unaweza kusaidia kijana athamini uhai

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki