Lugha Ambayo Waiona!
ULIJIFUNZAJE lugha yako? Yawezekana ulipokuwa mchanga uliwasikiliza washiriki wa familia na marafiki walipokuwa wakiongea. Watu wengi hujifunza lugha kwa kuisikia na kujieleza kwa kusema. Wanapofanyiza mawazo, watu wanaoweza kusikia hukariri maneno na vifungu vya maneno katika akili zao kabla ya kuyasema. Lakini, mtoto anapozaliwa akiwa kiziwi, je, aweza kufanyiza mawazo katika akili yake katika njia nyingine? Je, kuna lugha iwezayo kubadili fikira, za mambo ya kuwazika na za mambo halisi, kutoka kwa akili moja hadi nyingine bila sauti kutokezwa kamwe?
Yaonekana Lakini Haisikiki
Mojawapo ya maajabu ya akili ya kibinadamu ni uwezo wetu wa kujifunza lugha na kuweza kuirekebisha. Hata hivyo, bila uwezo wa kusikia, kwa kawaida mtu hujifunza lugha kupitia macho, wala si masikio. Kwa kufurahisha, tamaa ya kuwasiliana huwa yenye nguvu sana ndani ya binadamu, ikituwezesha kushinda kipingamizi chochote kinachoonekana. Uhitaji huu umewachochea Viziwi wengi kusitawisha lugha nyingi za ishara ulimwenguni pote. Kwa kuwa wamekutana na wengine waliozaliwa katika familia za Viziwi au kulelewa pamoja katika shule za kipekee na katika jumuiya, matokeo yamekuwa kusitawishwa kwa lugha ya hali ya juu inayohusu macho hasa—lugha ya ishara.a
Kwa Carl, anayetoka Marekani, lugha hii ilikuwa zawadi kutoka kwa wazazi wake Viziwi.b Ingawa alizaliwa akiwa kiziwi, aliweza kubandika vibandiko kwenye vitu, kuunganisha ishara, na kufafanua mambo katika Lugha ya Ishara ya Marekani (ASL) akiwa na umri mchanga sana. Watoto wengi wachanga walio Viziwi ambao wazazi wao Viziwi huwasiliana kwa ishara, huanza kutokeza ishara yao ya kwanza wanapofikia umri wa miezi 10 hadi 12. Katika kitabu A Journey Into the Deaf-World, inasemekana kwamba “wajuzi wa lugha sasa wanatambua kwamba uwezo wa kujifunza lugha kiasili na kuipitisha kwa watoto uko ndani kabisa ya akili. Kama uwezo huo utajitokeza ukiwa lugha ya ishara au inayozungumzwa si muhimu.”
Sveta alizaliwa Urusi katika familia ya Viziwi ya baba, wanawe, na mjukuu. Pamoja na ndugu yake Kiziwi, alijifunza Lugha ya Ishara ya Urusi. Wakati alipoandikishwa kwenye shule ya matayarisho ya watoto Viziwi akiwa na umri wa miaka mitatu, alikuwa amesitawisha ustadi wa kiasili katika lugha ya ishara kwa kiwango cha hali ya juu. Sveta akiri hivi: “Watoto wengine Viziwi hawakujua lugha ya ishara na wangejifunza kutoka kwangu.” Watoto wengi Viziwi walikuwa na wazazi wawezao Kusikia ambao hawakutumia lugha ya ishara. Mara nyingi watoto wachanga zaidi walifundishwa lugha ya ishara shuleni na watoto Viziwi wenye umri mkubwa zaidi, wakiwawezesha kuwasiliana kwa urahisi.
Leo wazazi wengi zaidi wawezao Kusikia wanajifunza ishara pamoja na watoto wao. Tokeo ni kwamba, Viziwi hawa wachanga wanaweza kuwasiliana kwa matokeo kabla ya kuhudhuria shule. Katika nchi ya Kanada, ndivyo ilivyokuwa kwa Andrew, ambaye wazazi wake wanaweza kusikia. Walijifunza lugha ya ishara na kuitumia pamoja naye alipokuwa na umri mchanga, wakimwandalia msingi wa lugha ambao angeweza kutegemea kwa miaka ambayo ingefuata. Sasa familia nzima yaweza kuwasiliana katika jambo lolote katika lugha ya ishara.
Viziwi wanaweza kufanyiza mawazo, ya mambo ya kuwaziwa na ya mambo halisi, bila uhitaji wa kufikiri katika lugha inayozungumzwa. Kama vile tu kila mmoja wetu hufanyiza mawazo katika lugha yake mwenyewe, Viziwi wengi hufikiri katika lugha yao ya ishara.
Lugha za Namna Nyingi
Ulimwenguni pote, jumuiya za Viziwi ama zimetokeza lugha zao wenyewe za ishara au zimeshirikisha mambo fulani ya lugha nyinginezo za ishara. Baadhi ya msamiati wa leo wa ASL ulitokana na Lugha ya Ishara ya Kifaransa miaka 180 iliyopita. Msamiati huu uliunganishwa na ule ambao tayari ulikuwa ukitumiwa awali Marekani, na sasa umekuwa ASL. Lugha za ishara husitawi kwa miaka mingi nazo hurekebishwa-rekebishwa na kila kizazi kinachofuata.
Kwa kawaida, lugha za ishara hazifanani na lugha za nchi. Kwa kielelezo, katika Puerto Riko, ASL hutumiwa ingawa lugha ya Kihispania ndiyo husemwa huko. Ingawa Kiingereza husemwa katika nchi ya Uingereza na Marekani, Uingereza hutumia Lugha ya Ishara ya Uingereza, ambayo hutofautiana sana na ASL. Pia, Lugha ya Ishara ya Mexico hutofautiana na lugha nyingi za ishara za Amerika ya Latini.
Unapojifunza lugha ya ishara, utavutiwa na ufasaha wenye kutatanisha na namna nyingi za kujieleza. Mada nyingi, au mawazo yaweza kuelezwa kwa lugha ya ishara. Kwa kufurahisha, kuna mwelekeo unaoongezeka wa kutokeza fasihi kwa ajili ya Viziwi kwenye kaseti za vidio, kutumia lugha ya asili ya ishara kusimulia hadithi, kuimba mashairi, kutoa habari za kihistoria, na kufunza kweli za Biblia. Kujifunza lugha ya ishara kunaongezeka katika nchi nyingi.
Kusoma Mambo Ambayo Hayajapata Kusikiwa
Wanaposoma, kwa kawaida watu wawezao Kusikia hurejezea kumbukumbu la kusikia wanapokumbuka sauti ya maneno. Kwa hiyo, mambo mengi wanayosoma hueleweka kwa sababu wameyasikia hapo awali. Katika lugha nyingi maneno yaliyoandikwa hayafafanui au kufanana na mawazo yanayowakilisha. Watu wengi wawezao Kusikia hujifunza mfumo huu usio na msingi maalumu au mfumo wa sheria iliyoandikwa kwa kuuhusisha na sauti za maneno ya lugha inayosemwa ili kuweza kuisoma kwa uelewevu. Ingawa hivyo, jaribu kufikiria kwamba hujasikia sauti, neno, au lugha ikisemwa katika maisha yako yote! Laweza kuwa jambo gumu na lenye kuvunja moyo kujifunza mfumo wa sheria iliyoandikwa usio na msingi maalumu kwa lugha ambayo haiwezi kusikika. Yaeleweka basi kwa nini ni vigumu sana kwa Viziwi kusoma lugha kama hiyo, hasa kwa wale waliopoteza uwezo wao wa kusikia tangu walipokuwa wachanga au wale ambao hawajapata kusikia!
Vituo vingi vya elimu kwa watoto Viziwi ulimwenguni pote vimegundua manufaa ya kutumia lugha ya ishara wakati mtoto anapokuwa na umri mchanga aanzapo kujifunza lugha. (Ona masanduku katika ukurasa wa 20 na wa 22.) Vituo hivyo vimepata kwamba Kiziwi mchanga aanzapo kufunzwa lugha ya ishara ya asili na kusitawisha msingi wa lugha, atafanikiwa kielimu na kijamii na vilevile wakati wa baadaye ajifunzapo lugha iliyoandikwa.
Tume ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni kwa Viziwi lilitaarifu hivi: “Sasa haikubaliki tena kupuuza lugha ya ishara, au kuepuka kuchukua daraka kubwa katika kuikuza katika miradi ya kielimu kwa viziwi.” Ingawa hivyo, lazima isemwe kwamba, hata wazazi wafanye uamuzi upi wa kielimu kwa ajili ya watoto wao Viziwi, daraka la wazazi katika kusaidia mtoto aisitawishe ni la maana sana.—Ona makala “Nilijifunza Lugha Nyingine Ili Kuwasiliana na Mtoto Wangu,” katika Amkeni! la Novemba 8, 1996.
Kuyaelewa Maisha ya Viziwi
Watoto Viziwi wanapokuwa watu wazima, mara nyingi wanakiri kwamba walichotaka zaidi kutoka kwa wazazi wao kilikuwa mawasiliano. Wakati mamake mzee alipokuwa akifa, Jack ambaye ni Kiziwi, alijaribu kuwasiliana naye. Mamake aling’ang’ana sana kumwambia jambo fulani lakini hakuweza kuliandika na hakujua lugha ya ishara. Kisha akazimia kwa muda mrefu na baadaye akafa. Jack alisumbuliwa sana na pindi hizo za mwisho zenye kuvunja moyo. Jambo hili lilimchochea kutoa shauri hili kwa wazazi wenye watoto Viziwi: “Ikiwa mwataka kuwasiliana kwa ufasaha na kuwa na mazungumzo yenye maana, hisia-moyo na upendo pamoja na mtoto wenu kiziwi, tumieni lugha ya ishara. . . . Nimechelewa mno. Je, umechelewa mno?”
Kwa miaka mingi watu wengi wameelewa vibaya maisha ya Viziwi. Wengine wamekuwa na maoni kwamba viziwi hawajui karibu jambo lolote kwa sababu hawasikii lolote. Wazazi fulani wamewazuia kupita kiasi watoto wao Viziwi au wakawa na hofu ya kuwaruhusu kuchangamana na watoto wawezao Kusikia. Katika tamaduni fulani Viziwi wamechukuliwa kimakosa kuwa “bubu,” ingawa kwa kawaida Viziwi hawana kasoro ya sauti. Hawawezi tu kusikia. Wengine wameiona lugha ya ishara kuwa isiyostaarabika au ya hali ya chini inapolinganishwa na lugha isemwayo. Haishangazi basi kwamba kwa sababu ya hali hiyo ya kutojua, Viziwi fulani wamehisi kuwa wameonewa na kueleweka vibaya.
Akiwa mtoto mchanga huko Marekani katika miaka ya 1930, Joseph aliandikishwa katika shule ya pekee kwa watoto Viziwi ambayo ilikataza kutumiwa kwa lugha ya ishara. Mara nyingi, yeye pamoja na wanadarasa wenzake walitiwa nidhamu kwa sababu ya kutumia ishara hata wakati walipokosa kufahamu usemi wa walimu wao. Jinsi walivyotamani kuelewa na watu kuwaelewa! Wengine hukua wakiwa na elimu kidogo sana ya msingi katika nchi ambazo elimu kwa watoto Viziwi ni chache. Kwa kielelezo, mleta-habari wa Amkeni! katika Afrika Magharibi alisema hivi: “Kwa Waafrika wengi walio Viziwi maisha ni magumu na yenye taabu. Kati ya watu wote wasiojiweza, labda Viziwi ndio wamepuuzwa zaidi na ndio hawaeleweki vizuri.”
Sote tuna uhitaji wa kutaka kueleweka. Kwa kusikitisha, wengine wamwonapo Kiziwi, hufikiri tu juu ya kasoro za mtu huyo. Kutambua kasoro kwaweza kuzuia kuonekana kwa uwezo wa Kiziwi. Tofauti na hilo, Viziwi wengi hujiona kuwa watu wenye uwezo. Wanaweza kuwasiliana kwa ufasaha mtu na mwenzake, kusitawisha staha ya kibinafsi, na kupata mafanikio ya kimasomo, kijamii, na kiroho. Kwa kuhuzunisha, Viziwi wengi wametendwa vibaya hivi kwamba wengine wao hawaamini watu wawezao Kusikia. Hata hivyo, watu wawezao Kusikia wanapoonyesha upendezi wa moyo mweupe katika kuelewa utamaduni wa Viziwi na lugha ya ishara ya asili na kuwaona Viziwi kuwa watu wenye uwezo, wote hunufaika.
Ikiwa ungependa kujifunza lugha ya ishara, kumbuka kwamba lugha huwakilisha jinsi tufikirivyo na kufanyiza mawazo. Ili kujifunza lugha ya ishara vizuri, mtu ahitaji kufikiri katika lugha hiyo. Ndiyo sababu kujifunza ishara katika kamusi ya lugha ya ishara hakungesaidia kusema vizuri lugha hiyo. Kwa nini usijifunze kutoka kwa watu watumiao lugha hiyo katika maisha zao za kila siku—Viziwi? Kujifunza lugha kutoka kwa watu waliokua wakiitumia lugha ya ishara hukusaidia ufikiri na ufanyize mawazo katika njia iliyo tofauti, lakini ya asili.
Ulimwenguni pote, Viziwi wanapanua uwezo na mataraja yao kwa kutumia lugha ya ishara yenye kupendeza. Njoo ujionee mwenyewe lugha yao ya ishara.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa makala hizi, tutatumia herufi kubwa “K” kwa neno “Kiziwi” tunaporejezea utamaduni au simulizi la mtu la maisha na kutumia herufi ndogo “k” kwa neno “kiziwi” tunapoelezea kutoweza kusikia. Kwa sababu iyo hiyo tutatumia herufi kubwa “K” tunaporejezea utamaduni wa watu wawezao kusikia.
b Katika Marekani pekee, inakadiriwa kwamba kuna viziwi milioni moja walio na “lugha na utamaduni wa kipekee.” Kwa kawaida wao wamezaliwa wakiwa viziwi. Kwa kuongezea, kuna watu wapatao milioni 20 ambao hawana uwezo wa kusikia lakini ambao wanaweza kuwasiliana hasa katika lugha zao.—A Journey Into the Deaf-World, cha Harlan Lane, Robert Hoffmeister, na Ben Bahan.
[Sanduku katika ukurasa wa 20]
“New York Kuwafunza Viziwi Lugha ya Ishara, Kisha Kiingereza”
Kichwa hicho cha habari kilitokea katika The New York Times la Machi 5, 1998. Felicia R. Lee aliandika hivi: “Katika hatua inayosifiwa kuwa badiliko lenye umaana mkubwa katika elimu ya wanafunzi viziwi, shule moja tu ya umma ya jiji hilo ambayo hufundisha viziwi itafanyiwa marekebisho ili walimu wote wafundishe hasa lugha ya ishara inayotegemea ishara za mikono.” Aeleza kwamba walimu wengi “wanasema kwamba utafiti waonyesha kuwa lugha ya msingi ya viziwi ni kuona, si kuzungumza, na kwamba shule zinazopendelea njia yao, iitwayo Lugha ya Ishara ya Marekani, huwafundisha wanafunzi vizuri zaidi ya shule nyinginezo.
“Wanasema kwamba wanafunzi viziwi wapaswa kutendewa kama wanafunzi wanaojua lugha mbili, si kama wasiojiweza.”
Profesa Harlan Lane, wa Chuo Kikuu cha Northeastern, Boston, alisema: “Nafikiri [shule ya New York] ndiyo mtangulizi wa harakati hii.” Aliliambia Amkeni! kwamba mradi wa mwisho ni kufundisha Kiingereza kikiwa lugha ya pili, ya kusomwa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]
Ni Lugha!
Watu fulani wawezao Kusikia wamefikia mkataa wenye makosa kwamba lugha ya ishara ni aina tata ya mchezo wa kuigiza. Hata imefafanuliwa kuwa lugha ya picha. Ingawa lugha ya ishara huhusisha uso, mwili, mikono, na sehemu za mwili zilizo karibu kwa matokeo, ishara nyingi hufanana kidogo sana au hukosa kufanana kabisa na mawazo zinayowakilisha. Kwa kielelezo, katika Lugha ya Ishara ya Marekani (ASL), ishara inayotoa wazo la “kufanya” hufanywa kwa kutumia mikono yote miwili ikiwa imekunjwa kuwa ngumi, ngumi moja ikiwa juu ya nyingine pamoja na mwendo wa kupindwa. Ingawa ishara hii ni ya kawaida, haionyeshi waziwazi maana yake kwa mtu asiyetumia lugha ya ishara. Katika Lugha ya Ishara ya Urusi (RLS), ishara inayofananisha wazo la “kuhitaji” huonyeshwa kwa kutumia mikono miwili, kila kidole gumba kikigusa kidole cha tatu na kwenda sambamba katika mwendo wa mzunguko. (Ona picha katika ukurasa huu.) Hivyo, kukiwa na mawazo mengi ya kuwazika, haiwezekani kuyaonyesha katika lugha ya picha. Visa vya kipekee kwa jambo hili vingekuwa ishara kwa vitu ambavyo vyaweza kushikika viwezavyo kufafanuliwa, kama vile ishara iwakilishayo “nyumba” au “mtoto.”—Ona picha katika ukurasa huu.
Kanuni nyingine ya lugha ingekuwa matumizi ya muundo wa msamiati unaokubalika na jumuiya. Lugha za ishara zina muundo wa kisarufi kama huo. Mathalani, kwa kawaida mada ya sentensi hutajwa kwanza katika ASL, ikifuatiwa na maelezo kuihusu. Pia, jambo la msingi katika lugha nyingi za ishara ni kupanga mambo kwa kufuatana na wakati yalipotokea.
Pia ishara nyingi za uso hutumika kuwa mambo ya kisarufi kama vile kusaidia kupambanua kati ya swali na amri, maneno yenye uwezekano, au taarifa sahili. Asili ya kuona ya lugha ya ishara imeiruhusu kusitawisha ishara za uso na nyingine nyingi za kipekee.
[Picha]
“Kufanya” katika ASL
“Kuhitaji” katika RLS
“Nyumba” katika ASL
“Mtoto” katika ASL
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Ni Lugha Halisi
“Kinyume na kueleweka vibaya kulikoenea, lugha za ishara si miigizo na ishara za mwili, ubuni wa walimu, au ishara za lugha inayosemwa ya jumuiya ya mahali hapo. Hupatikana mahali popote palipo na jumuiya ya viziwi, na kila moja ni lugha kamili, itumiayo mambo yaleyale ya kisarufi yapatikanayo katika lugha zinazosemwa ulimwenguni pote.”
Katika Nikaragua “shule zilikazia mafunzo kamili yenye kurudiwa-rudiwa kwa watoto [viziwi] katika kusoma mdomo na usemi, na kama ilivyokuwa katika kila kisa ambacho jambo hili lilijaribiwa, matokeo yalikuwa mabaya. Hata hivyo, walijifunza kuwasiliana. Kwenye viwanja vya michezo na katika basi za shule watoto walibuni ishara zao wenyewe . . . Upesi mfumo huo ulibadilika ukawa lugha ambayo sasa inaitwa Lenguaje de Signos Nicaragüense.” Sasa kizazi kichanga cha watoto viziwi kimesitawisha lugha yenye ufasaha zaidi ambayo iliitwa Idioma de Signos Nicaragüense.—The Language Instinct, cha Steven Pinker
[Picha katika ukurasa wa 23]
Hii ni njia moja ya ishara ya kusema “Baada ya kwenda dukani, ataenda kazini” katika ASL
1 Duka
2 yeye
3 –enda kwa
4 maliza
5 –enda kwa
6 kazi