Kuutazama Ulimwengu
Matatizo ya Afya ya Ulimwengu
“Tuingiapo karne ya 21, bado twaona maradhi ya kuambukiza yakichangia asilimia 33 ya vifo ulimwenguni pote,” asema Dakt. David Heymann wa Shirika la Afya Ulimwenguni. Tatizo hili limechangiwa na mambo mengi. Jarida The Journal of the American Medical Association lasema kwamba mambo yanayochangia tatizo hili ni ongezeko la idadi ya watu, kutofaulu kwa mipango ya kuchanja watu, msongamano wa watu, mabadiliko ya kimazingira, na kuzorota kwa mfumo wa afya ya umma ulimwenguni pote. Mambo mengine yanatia ndani kulazimika kuhama, wakimbizi, na ongezeko la safari za ulimwenguni pote—mambo haya yote huchangia kueneza maradhi ya kuambukiza. “Kwa kweli hakuna sababu kwa mambo haya kutokea,” asema Dakt. Heymann. “Zana za kupigana na au za kuondoa maradhi haya zapatikana.”
Wamormon na Siasa
Kanisa la Church of Jesus Christ of Latter-day Saints (LDS) limewatia moyo washirika wake Marekani washiriki zaidi katika siasa, laripoti gazeti Christian Century. Baraza kuu zaidi la LDS, Ofisi ya Usimamizi, hivi majuzi ilitoa barua ikiwahimiza washiriki wawe “tayari kutumikia kwenye kamati za shule, mabaraza na tume za jiji au za wilaya, bunge, na nyadhifa nyingine za kuchaguliwa au kuteuliwa, kutia ndani kujihusisha na chama cha kisiasa wakipendacho.” Barua hiyo ilitaarifu kwamba kanisa halikubali wagombeaji au chama chochote hasa cha kisiasa. Gazeti hilo lilisema kwamba katika miaka ya mapema ya dhehebu hilo, “Wamormon waliepuka kujihusisha na siasa kubwa-kubwa na wakajaribu kuanzisha theokrasi yao wenyewe katika eneo ambalo kwa sasa linaitwa Utah.”
Mkazo Huongeza Aksidenti za Magari
Mtazamo wa mtu kuelekea kazi yake unaathiri sana tabia yake anapoendesha gari, wataarifu uchunguzi wa shirika la Professional Association for Health Service and Social Welfare, katika Ujerumani. Watu wenye mkazo kutokana na kazi yao wanakabili hatari kubwa isivyo kawaida ya kusababisha aksidenti ya barabarani, ndivyo lilivyoripoti Süddeutsche Zeitung. “Mfadhaiko uliofungiwa moyoni kuhusu mkubwa au wafanyakazi wenzi waweza kusababisha ukosefu wa kumakinika wakati wa kuendesha gari,” yasema ripoti hiyo. Katika uchunguzi huo, asilimia 75 ya watu waliosababisha aksidenti ya barabarani walipokuwa wakienda au kutoka kazini mwao, walilaumu “ukosefu wa kumakinika, mbio nyingi mno, kujaribu kuwahi sikuzote, au mkazo.” Ingawa ilisemekana kuwa wanaume walielekea kusababisha aksidenti zaidi walipopatwa na mkazo usiofaa, uchunguzi huo pia ulipata kwamba mama wenye watoto wadogo walikabili hatari ya kipekee. Gazeti hilo la habari lasema hivi: “Mara nyingi mama walipatwa na mkazo, kwa kuwa walihitaji kuwachukua watoto wao kutoka nasari au kupika wakati wa pumziko la mchana.”
Ndoto za Kutisha Ni Kawaida kwa Watoto
Karibu watoto wote hupatwa na ndoto zenye kutisha. Kulingana na uchunguzi wa Taasisi Kuu ya Matatizo ya Kiakili katika Manheim, Ujerumani, watoto 9 kati ya 10 wanakumbuka wakiamshwa na ndoto. Ndoto za kawaida zinatia ndani watoto kukimbizwa, kuanguka kutoka sehemu zilizo juu, au kusumbuliwa na vita au msiba wa asili. Katika visa vingi ndoto hizo huwa mchanganyiko wa mambo ya kuwazia na mambo halisi. Kwa kawaida wavulana husahau ndoto zao. Kwa upande mwingine, mara nyingi wasichana huzungumza juu ya ndoto zao au hata kuziandika. Watafiti wanapendekeza kwamba ili kuondoa wasiwasi unaoletwa na ndoto hizo zenye kutisha, watoto wanapaswa kuzungumza juu ya walichoona katika ndoto, wachore picha, au waigize ndoto hizo, laripoti Berliner Zeitung. Kwa kawaida ndoto hizo zitapungua kwa majuma machache na baadaye hazitaogopesha iwapo mapendekezo haya yatafuatwa.
Madaktari Wenye Uraibu wa Dawa za Kulevya
Kulingana na wenye mamlaka ya kitiba katika Uingereza, “daktari mmoja kati ya 15 anasumbuliwa na uraibu wa vileo au dawa za kulevya,” laripoti The Medical Post la Kanada. Katika jitihada za kukabili tatizo hilo, mashirika ya kitiba yaliyo mashuhuri katika Uingereza yangependa kuanzisha majaribio ya ghafula-ghafula ili kutambulisha madaktari wanaotumia dawa za kulevya au vileo. Inakadiriwa kwamba madaktari wanaume na wanawake 9,000 katika Uingereza, huenda wakawa wanatumia isivyofaa vileo au dawa za kulevya. Kwa kushangaza, madaktari fulani “hawatafuti msaada kwa sababu hawajui ni huduma zipi zinazoweza kupatikana,” lasema gazeti hilo.
Kupasha Chakula Moto Hakuui Sumu
Nyama iliyopikwa na kuachwa nje kwa muda wa saa mbili bila kuwekwa ndani ya friji haipaswi kuliwa, lataarifu jarida Tufts University Health & Nutrition Letter. Lakini je, kuipika tena hakuwezi kuua bakteria zenye kudhuru? “Kupasha moto tena nyama ambayo imeachwa nje kwaweza kuua bakteria zilizo juu yake, lakini hakutamaliza sumu inayosababisha ugonjwa ambao hutokezwa na aina fulani za bakteria,” lasema Nutrition Letter. Sumu itokezwayo na bakteria ya kawaida inayoitwa staphylococcus yaweza kusababisha kuumwa na tumbo, kuharisha, kichefuchefu, kuhisi baridi, homa na kuumwa kichwa. “Na hata kupasha chakula moto sana hakuwezi kuua sumu hiyo.”
Sherehe za Carnival Katika Brazili
“Yawezekana carnival imefanya jiji la Rio de Janeiro liwe mashuhuri, lakini Wabrazili wengi hawapendezwi tu,” laripoti Nando.net. Watu wengi ulimwenguni pote huamini kwamba Wabrazili hupenda sana msherehekeo huu wa kila mwaka. Hata hivyo, uchunguzi wa Taasisi ya Brazili ya Utafiti wa Jamii watoa maoni tofauti kabisa. Ulipata kwamba asilimia 63 ya Wabrazili hawashiriki katika misherehekeo hii, asilimia 44 walisema kwamba “hawakupendezwa hata kidogo,” na asilimia 19 walisema kwamba “walichukia carnival.” Gazeti la habari Jornal do Brasil liliripoti kwamba idhaa kubwa ya kitaifa ya televisheni hata haikutangaza mashindano ya mwaka huu ya dansi za samba. Hata hivyo, maelfu ya watalii humiminika Brazili ili kujionea msherehekeo huo. Na kwa kuwa Brazili ni mojawapo ya nchi zilizo na mweneo mkubwa zaidi wa UKIMWI ulimwenguni, wizara ya afya iliwapa mamilioni ya watu kondomu wakati wa hiyo carnival.
“Mti wa Bahati Nasibu”
Wanakijiji wenye hasira karibu na Bangkok, Thailand, wametisha kuwadhuru wataalamu wa bahati nasibu wanaowashuku kuwa wanajaribu kuchoma “mti [wao] wa bahati nasibu,” laripoti South China Morning Post. Huu “mti wa bahati njema” ulitambuliwa katika taifa nzima kwa kutoa mashauri juu ya tiketi zitakazoshinda bahati nasibu, hivyo wanakijiji walikasirika kwelikweli walipopata habari kwamba mti huo ulikuwa umechomwa moto kimakusudi. “Kwa kweli nimekasirika,” akasema Dongmalee. “Mimi binafsi nilishinda pesa kwa kutumia mti huo na nilipata faida kwa kuwashauri wengine namna ya kuutumia mti huo.” Hata hivyo, inasemekana kwamba tangu shambulizi hilo, mzimu wa mti huo ulikasirika, na wanakijiji wanadai kwamba mzimu huo hautoi shauri la bahati nasibu. Ripoti hiyo ilisema kwamba wanakijiji wanapanga kuwaleta watawa wa kiume wa dini ya Buddha ili kushawishi mzimu wa mti huo uanze kutoa tena shauri la bahati nasibu.
Kutazama Sana Televisheni, Kusoma Kidogo
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Audiovisual Media Institute ya Ugiriki, kuna televisheni milioni 3.8 katika nyumba milioni 3.5 katika nchi hiyo; nyumba 1 kati ya 3 pia zina mashine ya kurekodia kaseti za vidio. Gazeti la habari la Athens To Vima liliripoti kwamba wastani wa muda unaotumiwa kila siku na Wagiriki kutazama televisheni ulikaribia saa nne katika 1996, ukilinganishwa na muda unaopungua saa mbili na nusu katika 1990. Haishangazi kwamba muda uliotumiwa kusoma ulipungua sana. Uchunguzi ulifunua kwamba Mgiriki wa kawaida alisoma magazeti ya habari 42.2 katika 1989, lakini katika 1995 tarakimu hiyo ilipungua na kufikia 28.3. Vivyo hivyo, usomaji wa magazeti ulipungua kwa asilimia 10 katika kipindi hichohicho.
Wazee-Wazee Wasiolishwa Chakula cha Kutosha
“Mara nyingi wazee-wazee hawali chakula cha kutosha na ndiyo sababu wanapatwa na magonjwa kwa urahisi,” laripoti gazeti Nassauische Neue Presse, la Frankfurt Ujerumani. Mkataa huu ulifikiwa baada ya wanaume na wanawake zaidi ya 2,500 wenye umri uzidio miaka 70 kufanyiwa uchunguzi katika nchi kumi za Ulaya. Watu wengi hufikiri kuwa wazee-wazee wanahitaji chakula kidogo, lakini kalori chache hudhoofisha uwezo wa mwili wa kupigana na magonjwa. Isitoshe, kwa kuwa watu hupika chakula kingi na kukiweka kwa muda mrefu, mara nyingi chakula cha wazee-wazee hakiwi chenye lishe sana. Kwa kuongezea, wengi hula matunda na mboga chache sana zilizotoka tu shambani, hasa wakati hazipo kwenye msimu. Uchunguzi huo ulimalizia kwa kusema kwamba matabibu wapaswa kuwakumbusha wagonjwa wazee-wazee “wale vizuri na kwa ukawaida.” Pia ulipendekeza kwamba wazee-wazee wapewe mazoezi zaidi, kwa kuwa kutumia nguvu za kimwili huongeza hamu ya kula chakula.
Biblia Yapatikana Katika Lugha 2,197
“Visehemu vya Biblia vilitafsiriwa katika lugha nyinginezo 30 mwaka jana, zikifanya jumla ya idadi ya lugha ambazo Maandiko yaweza kupatikana kuwa 2197,” laripoti ENI Bulletin, la Geneva, Uswisi. Sasa Biblia nzima inapatikana katika lugha 363, kutia ndani lugha zilizobuniwa kama vile lugha ya Esperanto. Chama cha Sosaiti za Biblia (UBS) huweka idadi ya lugha ambazo angalau ina kitabu kimoja cha Biblia. Katibu mkuu wa UBS, Fergus Macdonald, alisema kwamba mradi wao ni kufanya “Neno la Mungu lipatikane katika lugha za kwanza za watu.”