Ukimwi—Kuna Tumaini Gani kwa Wakati Ujao?
MBALI na ukosefu wa dawa za kuponya au kuzuia ambukizo la HIV, kuna mambo mengine yanayofanya isiwezekane kukomesha maradhi haya. Mojawapo ni kwamba watu wengi, wasiokuwa tayari kubadili mtindo-maisha wao, wako tayari kujasiria ambukizo. Kwa kielelezo, katika Marekani, kiwango cha ambukizo kimebaki kwa kiwango kilekile, licha ya kupungua kwa idadi ya watu ambao wamepatwa na UKIMWI. Sababu iliyopendekezwa na Shirika la Habari la Associated Press ni kwamba “watu wengi hawatii maonyo kuhusu kujikinga.”
Katika mataifa yanayositawi ya ulimwengu, ambayo yanaripotiwa kuwa na asilimia 93 ya watu walioambukizwa HIV, kuna matatizo ya ziada ya kukabiliana na maradhi hayo. Nyingi za nchi hizi ni maskini sana zisiweze kuandaa hata huduma za msingi za kiafya. Hata ikiwa dawa mpya zingepatikana katika nchi hizi—na kwa kiwango kikubwa hazipatikani—bei ya matibabu ya mwaka mmoja ingegharimu zaidi ya kiasi ambacho watu wengi huchuma katika muda wote wa maisha yao!
Lakini, acheni tudhanie kwamba dawa mpya, isiyokuwa ghali inatokezwa ambayo kwa kweli ingeponya maradhi haya. Je, watu wote wanaohitaji dawa hiyo wangeipata? Labda sivyo. Kulingana na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, watoto wapatao milioni nne hufa kila mwaka kutokana na maradhi aina tano yawezayo kuzuiwa kwa dawa za chanjo zilizopo za gharama ya chini.
Vipi juu ya watu walioambukizwa katika nchi ambazo hawawezi kupata dawa ili kutibiwa? Ruth Mota, wa Shirika la Kimataifa la Afya katika Santa Cruz, California, amesaidia kupanga programu za kuzuia na kushughulikia HIV katika makumi ya nchi zinazositawi. Asema hivi: “Kutokana na niliyojionea, mtazamo unaofaa ni muhimu kama vile kupata matibabu. Najua watu ambao wameishi na HIV kwa miaka 10 hadi 15 na ambao hawajapata matibabu kamwe. Matibabu hunufaisha, lakini kuponya huhusisha mengi zaidi ya kujaza dawa mwilini mwako. Kunatia ndani mtazamo, kuungwa mkono na jamii, hali ya kiroho, na lishe.”
Kutakuwako Suluhisho
Je, kuna sababu yoyote ya kuamini kwamba siku moja UKIMWI utashindwa? Ndiyo, kunayo. Tumaini bora lapatikana katika maneno ya ile ambayo watu wengi huiita Sala ya Bwana au Baba Yetu. Katika sala hiyo, iliyorekodiwa katika kitabu cha Biblia cha Mathayo, tunasihi kwamba mapenzi ya Mungu yafanywe duniani kama ilivyo mbinguni. (Mathayo 6:9, 10) Si mapenzi ya Mungu wanadamu watatizwe na magonjwa milele. Mungu atajibu sala hiyo. Kwa kufanya hivyo, atakomesha si UKIMWI tu bali maradhi yote mengine yanayowatatiza wanadamu. Kisha, “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.
Kwa wakati uliopo, mbinu bora ni kuzuia. Kwa maradhi mengi, kuna mambo mawili: Ama waweza kuyazuia ama labda kuyaponya. Kuhusu HIV, hakuna namna. Inaweza kuzuiwa, lakini kwa wakati uliopo haiwezi kuponywa. Kwa nini uhatarishe uhai wako? Bila shaka kuzuia ni bora kuliko kukosa tiba.
[Blabu katika ukurasa wa 9]
“Kuponya huhusisha mengi zaidi ya kujaza dawa mwilini mwako. Kunatia ndani mtazamo, kuungwa mkono na jamii, hali ya kiroho, na lishe.”—Ruth Mota
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
“Kutaniko Lilikuwa la Ajabu”
Mtume Paulo aliwahimiza Wakristo wenzake hivi: “Acheni sisi tufanye lililo jema kuelekea wote, lakini hasa kuelekea wale ambao katika imani ni jamaa zetu.” (Wagalatia 6:10) Mama ya Karen, aliyetajwa katika makala ya kwanza, asimulia jinsi kutaniko la Mashahidi wa Yehova lilivyoitikia lilipofahamu kwamba Karen na Bill walikuwa na ugonjwa wa HIV. Asema: “Kutaniko lilikuwa la ajabu. Bill aliposhikwa na nimonia, Karen mwenyewe alikuwa mgonjwa na alikuwa aking’ang’ana kumtunza pamoja na watoto. Ndugu walisafisha nyumba yao, wakatengeneza gari lao, na kuwafulia nguo. Waliwasaidia kushughulikia mambo yao ya kisheria na kuhamia makao mengine. Walinunua chakula na kuwapikia. Kulikuwa na mmiminiko wa kweli wa utegemezo wa kihisia-moyo, kiroho, na wa kimwili.”
[Picha katika ukurasa wa 8]
Uaminifu wa ndoa waweza kuzuia ambukizo la HIV