Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 12/8 kur. 24-27
  • Hekima na Manufaa za Kupanga Urithi wa Mali

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Hekima na Manufaa za Kupanga Urithi wa Mali
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupanga Urithi wa Mali Ni Nini?
  • Hatua za Kuchukua
  • Ni Nani Awezaye Kusaidia?
  • Sanduku la Swali
    Huduma Yetu ya Ufalme—2012
  • Wao Hufanya Lile Wawezalo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Kumtumikia Mungu kwa “Moyo na Nafsi Moja”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Jinsi Ambavyo Wengine Hutoa Upaji kwa Ajili ya Kazi ya Kuhubiri Ufalme
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 12/8 kur. 24-27

Hekima na Manufaa za Kupanga Urithi wa Mali

AKINA Peterson walivunjika moyo.a Wao walikuwa wametegemea fedha ambazo wangepokea kwa kuuza mali zao ili kuwasaidia kujiruzuku baada ya kustaafu na hatimaye hata zitoshe kuwapa watoto wao zawadi nono. Matazamio yao yakatoweshwa na kodi kubwa walizotozwa wakati mali zao zilipokuwa zikiuzwa.

Akina Smith pia walikuwa na mali zilizoongezeka thamani sana kadiri miaka ilivyopita. Kupitia mpango wa kipekee wa kuuza mali hizo, wao waliweza kufanya mipango ya kupata mapato wakati wamestaafu, kuwatunukia watoto wao zawadi nzuri, na kutoa upaji kwa shirika walipendalo la kutoa msaada.

Rose Jones alifadhaika na kuvurugika. Punde tu baada ya mume wake kufa kwa ghafula, alianza kupokea hati ambazo yeye hakuelewa kutoka kwa mamlaka ya jimbo na ya serikali kuu. Mumewe, John, alikuwa akiyatunza daima mambo yao ya kifedha, kutia ndani kulipa kodi, kupata bima ya maisha, na kadhalika. Alimwambia daima asiwe na wasiwasi—“kila kitu ni shwari.” Lakini kwa sababu alikufa bila kuandika wasia, baadhi ya mali alizotegemea kwa ajili ya mapato zikadhibitiwa. Alishauriwa kwamba sasa alihitaji kumwajiri wakili ambaye angemsaidia kujua mali ambazo mume wake aliacha na njia za kuziandikisha kwa jina lake. Pia akaambiwa kwamba, kulingana na sheria, baadhi ya mali hizo zingepewa watoto ambao mume wake alikuwa amepata katika ndoa yake ya awali, japo Rose alijua kwamba mume wake hakutaka kuwapa hao watoto mali hizo. Akikabili mzigo wa kuwa mjane, hali ikawa mbaya zaidi kwa sababu hakujua jambo la kufanya na vilevile wasiwasi juu ya gharama ambayo ingetumika ili kutatua matatizo hayo.

Mary Brown pia alipatwa na msiba mume wake alipokufa kwa ghafula. Yeye alipata faraja kwa sababu alijua kwamba mume wake alikuwa amefanya mipango ya kutosha ya bima ya maisha ili yeye na watoto wao wawili wapate riziki. Pia alijua mali ambazo angerithi mara tu mume wake akifa na mali ambazo angepata kupitia wasia wa mume wake. Japo alikuwa akikabiliana na magumu ya ujane, yeye alishukuru sana mume wake kwa kuonyesha kujali sana na kupanga mambo yake, hivi kwamba kifo chake hakikumwathiri kifedha wala watoto.

Kuna tofauti gani kati ya akina Smith na Mary Brown? Ni kupanga urithi wa mali.

Kupanga Urithi wa Mali Ni Nini?

Kupanga urithi wa mali ni utaratibu tu wa kuamua jinsi mali yako itakavyogawanywa ukifa kisha kuchukua hatua ya kuhakikisha kwamba maamuzi yako yatatekelezwa ifaavyo na kifedha. Hatua kama hizo zaweza kuhusisha kuandikisha mali, kutaja wenye kuzirithi, na kuandika hati za wasia na amana. Katika hali ngumu, jambo hilo laweza kuhusisha mambo mengi zaidi.

Ingawa labda watu wengi hukubaliana na hekima ya kufanya mipango kama hiyo, ni wachache wameifanya mipango hiyo. Kwa kushangaza, asilimia 70 ya watu wazima nchini Marekani hawana wasia! Udhuru wa kawaida ni: “Nina shughuli nyingi sana; nitaifanya baadaye.” “Sina pesa nyingi wala mali nyingi za kurithisha wengine.” “Sina wakili.” “Sitaki kufikiri kwamba nitakufa.” “Hata sijui nianzie wapi.”

Ni kweli kwamba wazo la kupanga urithi wa mali huenda likawa lenye kuogofya. Lakini usiogope. Hatua ya kwanza ni kuratibu tu mambo yako na kujua maamuzi unayotakikana kufanya. Kama ilivyo na mambo mengi, si vigumu kupanga urithi wa mali ikiwa inafanywa hatua kwa hatua.

Hatua za Kuchukua

Hatua ya kwanza ni kufanya orodha ya mali zako. Unapaswa kuorodhesha vitu unavyomiliki na vilevile gharama ya kila kitu kimoja na jinsi unavyokimiliki au jinsi kimeorodheshwa kisheria. (Ona sanduku “Daftari ya Jumla ya Mali.”) Mali nyingi zaweza kuorodheshwa chini ya hati za kifedha (hisa katika kampuni, dhamana, fedha zinazomilikiwa pamoja na wengine), mali zisizohamishika (nyumba yako, ya kukodi au ya biashara), akaunti za benki (akaunti ya akiba, akaunti ya hundi, na fedha za mikopo), mali za kibinafsi (vitu, sanaa, vito, magari, fanicha), bima ya maisha, marupurupu ya kustaafu, na biashara. Baada ya kuorodhesha mali zako, orodhesha madeni yako, kama vile rehani, mikopo, na madeni ya kadi za mkopo. Kuondoa madeni hayo kwenye jumla ya mali zako kutaonyesha jumla ya thamani ya mali zako. Katika nchi nyingi kodi hutozwa kwenye kila mali ambayo inaandikishwa kwa jina la mtu mwingine ikiwa mwenye mali afa. Kiasi cha kodi chategemea jumla ya thamani ya mali zilizoandikishwa kwa jina la mtu mwingine, basi ni muhimu kujua jumla ya thamani ya mali zako.

Hatua ya pili ni kufikiria malengo yako—si kwa habari ya kiasi cha fedha, bali kwa habari ya mambo unayotaka kutimiza kwa manufaa yako na kwa manufaa ya warithi wako. Kwa kawaida, mtu ambaye amefunga ndoa hutaka mwenzi wake awe na usalama. Mzazi anaweza kuandalia watoto wake ulinzi fulani wa kifedha. Mtu anaweza kupanga utunzaji wa mzazi wake ambaye amezeeka. Kwa kuongezea, huenda ukakumbuka marafiki fulani au upaji fulani kwa mashirika ya kutoa msaada katika mipango yako ya urithi wa mali. Ni muhimu kuandika ni nani anayepaswa kutiwa ndani ya mipango yako ya urithi wa mali na lengo lako kuelekea kila mmoja wao.

Usisahau kufikiria mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuathiri kupanga urithi wa mali. Kwa mfano, namna gani ikiwa mtu anayepaswa kurithi mali yako afa mbele yako? Je, ungependa mali ambayo angerithi ichukuliwe na mwenzi wake wa ndoa, watoto wake, au labda mtu mwingine?

Hatua ya tatu ni kuchagua wale ambao watatekeleza mapenzi yako. Kwa kawaida utahitaji mrithishi na labda mtunzi au msimamizi wa mirathi. Hata uwe umechagua nani, angalau uwe na mtu wa pili, na uhakikishe kwamba kila mtu unayemteua yuko tayari kufanya kazi yake. Mrithishi ni mtu ambaye atachukua mali zako baada ya kifo chako, ashughulikie mambo yoyote ya kisheria na, hatimaye, azigawe mali zako kupatana na mapenzi yako. Kwa kawaida inafaa kumpa mshiriki wa familia daraka hilo, ingawa shirika kama idara ya benki ya dhamana ya fedha inaweza kufanya vizuri ikiwa hali yako ni ngumu. Mtunzi apaswa kutajwa katika wasia wako ili alee watoto wako iwapo wewe au mwenzi wako afa ikiwa watoto wako hawajakuwa watu wazima. Ikiwa mpango wako wahusisha kuwaachia watoto wako amana, huyo mtunzi aweza pia kutajwa kuwa msimamizi wa mirathi, maadamu yeye ana ujuzi wa kushughulikia fedha. Ikiwa mtunzi hana ujuzi wa kusimamia fedha, idara ya benki ya dhamana ya fedha inaweza kupewa daraka la kuwa msimamizi wa pekee au msimamizi wa kushirikiana na mtunzi.

Hatua ya nne ni kujua vifaa vinavyopatikana vinavyoweza kukusaidia utimize malengo yako. Je, wataka kumpa mrithi wako zawadi ya moja kwa moja, au ungependelea tu mali iwekwe amana kwa manufaa ya mtu huyo? Kuna tofauti kubwa kati ya mambo hayo mawili. Ukitoa mali yako moja kwa moja, mali hiyo inakoma kuwa yako ukifa. Hata hivyo, hata baada ya kifo chako, unaendelea kumiliki kwa kiasi fulani mali iliyoachwa chini ya amana. Mtu utakayemteua atasimamia mali hiyo na kutumia mali zako kwa manufaa ya warithi wako kulingana na maagizo ya amana. Kwa mfano, kwa watoto wachanga, mipango inaweza kufanywa watunzwe kulingana na mahitaji yao mmoja-mmoja kisha utoe maagizo umri ambao watoto hao watamiliki mali zilizotajwa katika amana.

Ni Nani Awezaye Kusaidia?

Katika karibu hali zote, unaweza kumwomba mashauri mtu ambaye amefahamu mambo ya kupanga urithi wa mali ili akusaidie kuelewa vifaa vinavyoweza kukusaidia kutimiza malengo yako. Unapaswa kupanga kurithisha mali kwa njia inayotimiza malengo yako ya kipekee na hali zako. Kupanga urithi wa mali huenda kukahitaji msaada wa washauri mbalimbali, kama vile mhasibu, mtaalamu wa kifedha, na mwakilishi wa bima. Ikiwa mipango yako yahusisha upaji kwa shirika la kutoa msaada, unaweza kupokea msaada bila malipo wa idara ya upaji uliopangwa ya shirika unalotaka kulipa upaji. Kwa mfano, Dawati la Upaji Uliopangwa la Watch Tower Bible and Tract Society huwasaidia wale ambao wanataka kutia ndani Sosaiti katika mipango yao ya urithi wa mali. Wengi wamenufaishwa na utumishi huu wenye madokezo ya wazi ya jinsi ya kupanga mambo kwa njia bora ili kupunguza kodi na kunufaisha zaidi wapendwa wao na Sosaiti.b

Ingawa wengi wanaweza kuhusika katika hatua za kupanga urithi, mpango wa mwisho wa urithi wa mali na hati za lazima zapasa zitayarishwe na wakili aliye mtaalamu wa kupanga urithi wa mali. Uwe huru kuomba mshauri yeyote historia yake na ujuzi wake wa kupanga urithi wa mali. Ikiwa una hangaiko fulani hususa, kama vile kuipa familia yako biashara fulani au kutunza mtu wa ukoo ambaye hajiwezi, uliza huyo mshauri ikiwa ana ujuzi wowote wa mambo hayo. Katika hali hizo zote, uliza juu ya ada atakayokutoza kwa ajili ya utumishi wake, na mapatano hayo yaandikwe.

Kukosa ujuzi wa mambo ya kupanga urithi wa mali kwaweza kutokeza msiba. Chukua mfano wa wenzi tutakaowaita Paul na Mary. Walitaka binti zao watatu wagawane mali katikati. Kwa kuwa binti yao Sarah alikuwa jirani yao, waliamua kuongeza jina lake kwa mali walizomiliki, wote wakionyeshwa kuwa wanamiliki mali hizo. ‘Kwa njia hii,’ wao walifikiri, ‘Sarah ataweza kusimamia mali zetu tukifikia hali ya kutojiweza. Na zaidi, kuorodhesha Sarah kuwa mmoja wa wamiliki kwamaanisha kwamba Sarah atamiliki mali zote peke yake sisi tufapo, na tutaepuka uhitaji wa kuandika wasia na mambo ya kisheria. Yeye aweza tu kugawa mali hizo kati yake na dada zake baada ya sisi kufa.’

Lakini mambo hayakwenda kama walivyopanga Paul na Mary. Baada ya wazazi wake kufa, Sarah aligawana mali hizo na dada zake, lakini kuandikisha mali hizo kwa majina ya dada zake kulitokeza kodi ambayo ilipunguza sana mali ya Sarah. Isitoshe, jambo la kwamba alikuwa mmiliki-mshiriki halikumpa Sarah uwezo wote wa usimamizi ambao wazazi wake walitaka. Paul na Mary walikuwa na malengo mazuri. Walitaka kuhakikisha kwamba wangetunzwa iwapo wangekuwa wasiojiweza. Pia walitaka njia rahisi ya kuandikisha majina ya watoto wao kwenye urithi wa mali. Lakini walitumia njia isiyofaa ya kutekeleza malengo yao.

Kupanga urithi wa mali si jambo la kufanya mara moja tu maishani. Ni lazima upitie mipango yako pindi kwa pindi kwa sababu sheria za kodi, sheria za urithi, na hali za maisha hubadilika. Kifo cha mtu wa ukoo, kuzaliwa kwa mjukuu, kupokea urithi, na ukuzi wa mali, yote ni mambo yanayoweza kutokeza uhitaji wa kupitia tena mpango wako wa urithi wa mali.

Ndiyo, ni vigumu kupanga urithi wa mali. Kunahitaji wakati, nishati, na kujitoa. Na mara nyingi kunahusisha kufanya maamuzi magumu. Kupanga urithi wa mali ni jambo linalohusu hisia-moyo sana. Kunahusisha watu na makusudi ambayo unayajali na matakwa yako ya wakati ujao. Huhitaji kufikiria sana ili ujue mambo unayotaka kufanya na mali zako na kuamua njia bora zaidi ya kutimiza malengo hayo. Lakini, mtu asipofikiria vizuri kupanga urithi wa mali, matatizo mazito yanaweza kutokea, kama ilivyoonyeshwa mwanzoni mwa makala hii. Ndiyo, thawabu utakazopata zashinda kwa mbali gharama utakazotumia. Thawabu kubwa zaidi ni amani ya akili kwa sababu unajua kwamba una mpango mzuri wa kuwalinda wapendwa wako.

[Maelezo ya Chini]

a Mifano inayotumiwa katika makala hii, japo ni ya kuwaziwa, inategemea mchanganyiko wa mambo halisi yaliyotokea maishani. Kwa kuongezea, habari inayotolewa katika makala hii inategemea hasa sheria ya Marekani, lakini kanuni zilizopo zinatumika katika nchi nyingi pia.

b Kwa habari zaidi, tafadhali soma broshua Planned Giving to Benefit Kingdom Service Worldwide, iliyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

Hatua za Kuchukua

• Tayarisha orodha ya mali zako, ukiorodhesha mali zako na madeni yako

• Tambua miradi, malengo, na mahitaji yako na ya familia yako

• Teua watu ambao watatekeleza mapenzi yako kama mrithishi, msimamizi wa mirathi, na mtunzi wa watoto wako, na uhakikishe kwamba wako tayari kukubali daraka hilo

• Tafuta njia zinazopatikana za kupanga urithi wa mali kwa kuomba mashauri mtu ambaye ana ujuzi wa kupanga urithi wa mali

[Chati katika ukurasa wa 25]

Daftari ya Jumla ya Mali

Mali Katika Katika Jina la Katika Jina Lako

Jina Lako Mwenzi Wako na Wengine

Nyumba (bei ya sasa) Sh. Sh. Sh.

Mali nyinginezo zisizohamishika Sh. Sh. Sh.

Akaunti za Benki (za hundi na akiba)Sh. Sh. Sh.

Akaunti nyinginezo za pesa Sh. Sh. Sh.

Hisa, fedha za dhamana, na fedha

zinazomilikiwa pamoja na wengine Sh. Sh. Sh.

Bima ya maisha (malipo) Sh. Sh. Sh.

Biashara zinazomilikiwa pamoja na wengine Sh. Sh. Sh.

Akaunti za kustaafu Sh. Sh. Sh.

Mali ya kibinafsi Sh. Sh. Sh.

Mali nyinginezo (taja hususa) Sh. Sh. Sh.

Jumla ya mali Sh. Sh. Sh.

Madeni

Rehani Sh. Sh. Sh.

Mikopo mingine au madeni

(madeni ya kibinafsi, kadi za mkopo,

na kadhalika) Sh. Sh. Sh.

Jumla ya madeni Sh. Sh. Sh.

Jumla ya mali yote (ukiondoa madeni) Sh. Sh. Sh.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kupanga urithi wa mali kwahusisha kupangia wakati ujao wa wapendwa wako

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki