Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 12/22 kur. 16-19
  • Majeraha ya Mkazo wa Kurudia-rudia—Unayopaswa Kujua

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Majeraha ya Mkazo wa Kurudia-rudia—Unayopaswa Kujua
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Ni Ugonjwa Mpya?
  • Kupungua na Kuongezeka kwa RSI
  • Visababishi, na Taaluma Zinazohusika
  • Hausababishwi na Miendo Pekee
  • Kuutambua Ugonjwa Huo
  • Kupambana na RSI
  • Kujikinga Nyumbani na Kazini
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2004
  • Misuli—Kazi Bora za Ubuni
    Amkeni!—1999
  • Mambo Yanayowahatarisha Wafanyakazi
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 12/22 kur. 16-19

Majeraha ya Mkazo wa Kurudia-rudia—Unayopaswa Kujua

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI

MARCELO, mpaka-rangi wa nyumba mwenye umri wa miaka 24 anayeishi Brazili, alizoea kufanya yafuatayo karibu kila asubuhi bila kufikiria. Alikuwa akivaa saa yake kwenye kiwiko cha mkono na kuufunga ukanda wa ngozi wa saa hiyo. Lakini wakati huu alisumbuka kuufunga ukanda huo. Ndipo akakiangalia kiwiko chake akaona kuna tatizo. Kilikuwa kimevimba na ukanda wa saa haungeweza kutoshea.

Baada ya muda, hata kushika kitana au mswaki kulisababisha maumivu mkononi mwake. Basi Marcelo akaenda kumwona daktari. Baada ya kumpima Marcelo na kutambua kwamba kwa miaka miwili alikuwa akikwangua, akipiga plasta, na kupaka kuta rangi, daktari akamwambia: “Maumivu unayoyahisi yanahusiana na kazi. Una jeraha la mkazo wa kurudia-rudia [RSI].”

Je, Ni Ugonjwa Mpya?

Wafanyakazi wengi wa viwandani na ofisini wanapatikana kuwa na tatizo kama la Marcelo. RSI unaenea kwa haraka sana hivi kwamba gazeti Folha de S. Paulo liliuita “ugonjwa mkuu unaohusiana na kazi wa mwisho wa karne hii.” Si ajabu watu wengi wamekata kauli kwamba RSI lazima uwe mmoja wa magonjwa ya kisasa! Je, ni hivyo?

Kwa kweli, kama Marcelo angaliishi Ulaya mapema katika karne ya 18, huenda daktari angalitambua dalili hizo. Bila shaka, tatizo hili halikuitwa jina hili wakati huo. Daktari Mwitalia Bernardino Ramazzini alilifafanua tatizo hili kuwa uvimbe wa kiwiko wenye uchungu unaoathiri kano na sehemu zinazozizunguka, akaliita ugonjwa “wa waandishi na makarani.” Miendo ya kurudia-rudia iliyohitajika katika kazi hizo iliwapa makarani aina ya RSI ya karne ya 18. Lakini mwishoni mwa karne hiyo, idadi ya wafanyakazi waliougua RSI ilikuwa imepungua. Kwa nini?

Kupungua na Kuongezeka kwa RSI

Makarani wa ofisi wa siku za Ramazzini waliishi wakati unaoitwa enzi ya kabla ya usitawi wa viwanda. Siku hizo, watu walifanya kazi kwa muda wa saa nyingi bila kutumia mashine. Iliwalazimu kufanya kazi kwa miendo ya kurudia-rudia na daima wakiikaza akili. Hili lilitokeza magonjwa aina ya RSI.

Hata hivyo, kufikia mwisho wa karne ya 18, Ulaya ilikuwa imeingia katika enzi ya usitawi wa viwanda na mashine zikaanza kuchukua kazi zilizofanywa na mwanadamu. Mwanadamu sasa akawa bwana-mkubwa na kuziachia mashine kazi za kurudia-rudia. Badiliko hilo, asema daktari aliyechunguza historia ya RSI, huenda lilipunguza RSI miongoni mwa wafanyakazi.

Ni kweli kwamba wakati wa enzi ya usitawi wa viwanda, aksidenti za kazini ziliongezeka na magonjwa ya kazini miongoni mwa wafanyakazi viwandani yaliongezeka pia. Hata hivyo, vitabu vya kitiba vinavyoshughulikia kipindi hicho hutaja visa vya RSI miongoni mwa vikundi fulani tu. Kwa mfano, wapiga-piano na wapiga-fidla wa karne ya 19 waliugua ugonjwa wa kano katika sehemu za juu za mikono, na wacheza-tenisi walipata uvimbe wa kano za kisugudi.

Hata hivyo, katika karne yetu RSI unaohusiana na kazi umerejea. Kwa nini? Sababu moja ni kwamba mashine zinazoendelea kuwa bora mara nyingi hueleza binadamu la kufanya na jinsi awezavyo kulifanya kwa haraka zaidi. Badiliko hili limewafanya wafanyakazi wasiridhike na kupatwa na matatizo ya kiafya. Wafanyakazi hutumia muda wa saa nyingi katika kazi zinazowalazimisha kufanya miendo ya kurudia-rudia na kuwalazimisha kukaza akili zao daima. Tokeo? RSI umekuwa ugonjwa unaochangia zaidi ya asilimia 50 ya magonjwa yote yanayohusiana na kazi miongoni mwa wafanyakazi katika Marekani na Brazili—tukitaja nchi mbili tu.

Visababishi, na Taaluma Zinazohusika

Kisababishi kikubwa cha RSI ni ile miendo ya kurudia-rudia haraka inayohitajiwa katika kazi nyingi. Kwa kuhuzunisha, wafanyakazi hawana namna ila kuendelea na kazi ambazo huenda zikadhuru afya yao. Wafanyakazi wengi wanaweza kumhurumia mwanamke mmoja Mbrazili aliyefanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza magari na kulazimika kuunganisha vipande vya redio kwa muda unaopungua dakika moja kwa kila redio. Mfanyakazi mwingine, laripoti gazeti Folha de S. Paulo, alilazimika kufanya majaribio yaliyomlazimu kugonga vyombo 63 kwa kila saa akitumia nyundo ya mpira. Hao wanawake wawili wakaanza kupata maumivu katika sehemu za juu za mikono yao na baadaye wakafutwa kazi kwa sababu ya ulemavu uliosababishwa na RSI.

Juhudi zinazochosha sana misuli na viungo (kama kubeba magunia mazito) na juhudi za kutosonga (yaani, juhudi za misuli za kuziweka sehemu za mwili pamoja) ni baadhi ya visababishi vya RSI. Vitendo kama hivi huenda hasa vikasababisha majeraha wakati mtu afanyapo kazi katika hali isiyostarehesha.

Baadhi ya watu ambao watafiti husema waelekea sana kupata RSI ni wahunzi, makarani wa benki, opereta wa kibodi, opereta wa simu, makeshia wa duka, wahudumu hotelini, wapaka-rangi wa nyumba, waunganishaji wa vichezeo, washonaji, watengeneza nywele, wafumaji, wakata-miwa, na wengine wanaofanya kazi za mikono.

Hausababishwi na Miendo Pekee

Ijapokuwa watu wengi hufikiri kwamba RSI husababishwa tu na kazi inayohitaji miendo ya kurudia-rudia, wataalamu waliohudhuria Semina ya Kwanza ya Kitaifa juu ya RSI, iliyofanywa Brasília, jiji kuu la Brazili, walisisitiza kwamba kuna mengi yanayohusika kuliko miendo ya kurudia-rudia.

Dakt. Wanderley Codo, mshauri wa mambo ya utimamu wa akili na kazi katika Chuo Kikuu cha Brasília, alieleza: “Namna ambavyo kazi hupangwa—kazi, mahusiano kati ya wasimamizi na wafanyakazi, mazingira ya kazi, kiwango cha kushiriki kwa wafanyakazi, na utaratibu wa kazi ambao hujirudia—ni mojawapo ya mambo yanayohusianishwa sana na ugonjwa huu.”

Wataalamu wa kitiba wengine waliohudhuria semina hiyo ya RSI walikazia uhusiano uliopo baina ya ugonjwa huu na utaratibu wa mahali pa kazi. Wao walisema ubaya mmoja wa tekinolojia mpya ni kwamba hizo hutokeza taratibu mpya za kazi ambapo mfanyakazi hupoteza udhibiti wote wa kazi yake—jambo ambalo huchangia kupatwa na RSI.

Kwa kuwa jinsi ambayo kazi huratibiwa na kufanywa imehusianishwa kwa ukaribu na RSI, wafanyakazi fulani katika miongo iliyopita waliweza kutekeleza miendo ya kurudia-rudia bila kupata RSI. Huo ndio mkataa wa wataalamu fulani.

Kuutambua Ugonjwa Huo

Ukumbuke kwamba RSI haurejezei ugonjwa mmoja bali kikundi cha magonjwa kadhaa. Magonjwa yote katika kikundi hiki huathiri misuli, kano, viungo, na mishipa, hasa zile za sehemu za juu za mikono na miguu. Kwa kuwa RSI hutambulisha kikundi cha magonjwa, basi ishara na dalili tofauti-tofauti hutokezwa. Dalili huenda zisiwe dhahiri, na uhusiano kati ya visababishi na dalili huenda visitambuliwe mara moja. Zifikirie ishara muhimu hizi zifuatazo.

Ishara moja ni kuhisi uzito na usumbufu katika sehemu ya mwili iliyoathiriwa (kwa mfano, bega na/au mkono) ambayo hupatwa na maumivu yasiyokoma na kuwasha. Pia, vinundu, au vivimbe vidogo, huenda vikajitokeza ngozini. Katika hali ambapo RSI umeendelea sana, kuvimba na maumivu huenda yakawa makali sana hivi kwamba mtu hawezi kufanya kazi ndogondogo kama vile kuchana nywele na kusugua meno. Usipotibiwa, RSI huenda ukasababisha ulemavu na kutojiweza.

Kupambana na RSI

Ikiwa kazi yako ya wakati huu huhitaji miendo ya kurudia-rudia na tayari unatambua dalili za RSI, huenda ukataka kutafuta msaada kutoka kwa huduma ya matibabu ya kampuni yenu. Kama haiwezekani, unaweza kwenda kwenye kituo cha afya ambapo daktari wa mifupa anaweza kuchunguza tatizo lako na kuchukua hatua zinazohitajika ili kukusaidia. Uwezekano wa kupata nafuu utakuwa mkubwa zaidi ikiwa utashughulikia ugonjwa wa RSI mapema.

Njia nyingine muhimu ya kupambana na RSI ni kuzingatia taaluma ya mazingira. Taaluma ya mazingira ni nini? Hiyo ni “sayansi inayohusika na kuunda na kupanga vifaa ambavyo watu wanatumia ili kwamba watu na vifaa waingiliane kwa ufanisi na kwa usalama zaidi.”

Hivyo, taaluma ya mazingira inahusiana na kupafanya mahali pa kazi pafae kwa mwanadamu vivyo hivyo mwanadamu apafae mahali pa kazi. Hata hivyo, hiyo ni zaidi ya kuboresha umbo la kibodi au nyundo. Hiyo inahusisha kujali mahitaji ya kiakili na kihisia-moyo ya mfanyakazi. Ili kutimiza hilo, asema mtaalamu wa mazingira Dakt. Ingeborg Sell, taaluma ya mazingira “hutumia data, habari, na ujuzi za taaluma zinazoshirikishwa [na] hujitahidi kufikia ujuzi kamili kuhusu mwanadamu na kazi yake.”

Ni kweli kwamba huenda wafanyakazi wengi wasiweze kubadilisha mazingira ya mahali pa kazi. Lakini wataalamu wa kitiba kwenye semina ya RSI katika Brasília walieleza kuwa “taaluma ya mazingira yenye kushirikisha wafanyakazi” haiko hivyo. Ni nini kinachomaanishwa na taaluma ya mazingira yenye kushirikisha wafanyakazi?

Mwajiri anayetia moyo taaluma ya mazingira yenye kushirikisha wafanyakazi mahali pa kazi huyafikiria maoni ya wafanyakazi. Huomba mfanyakazi ashiriki katika kuamua jinsi ambavyo aweza kuboresha sehemu yake ya kazi. Mwajiri kama huyu atapendelea pia kuwepo kwa kamati ya RSI inayohusisha wafanyakazi na wasimamizi. Kikundi hiki kitakuwa chonjo kudumisha mazingira salama na yenye starehe mahali pa kazi. Hushughulikia visababishi vya RSI, huchangia kinga, na hufafanua majukumu ya mwajiri na waajiriwa katika kudhibiti au hata kuondolea mbali visa vya RSI katika kampuni.

Kujikinga Nyumbani na Kazini

Kuzuia RSI huanzia nyumbani. Unaweza kufanya nini? Uamkapo, iga mbwa wako au paka wako. Chunguza jinsi ambavyo mnyama wako anyoshavyo misuli yake kabla ya kuanza siku mpya. Fanya vivyo hivyo. Na, unapoendelea kufanya hivyo, rudia kujinyosha mara kadhaa wakati wa mchana. Hili ni muhimu ili kuitunza mifupa na misuli ikiwa yenye afya. Fanya mazoezi fulani ili kusisimua misuli yako. Hili litazidisha kuzunguka kwa damu mwilini na kuongeza kiwango cha oksijeni inayohitajika ili misuli yako ifanye kazi yake. Bila shaka, wakati wa baridi na pia kabla ya kushiriki michezo, kuchukua hatua hii ni muhimu hata zaidi. Fanya mazoezi fulani ambayo yataimarisha misuli hususa unayotumia zaidi. Misuli yenye nguvu itakusaidia kufanya kazi za lazima.

Mbali na hatua hizi nyumbani, kuna uhitaji pia wa programu ya kujikinga mahali pa kazi. Huenda mwajiri akazuia matatizo ya RSI miongoni mwa wafanyakazi kwa kupanga ratiba inayotia ndani vipindi vya mapumziko au mabadiliko na ambayo hubadilisha aina mbalimbali za kazi miongoni mwa wafanyakazi.

Jambo jingine kuhusu kuzuia RSI ni kumwandalia mfanyakazi vifaa vinavyostahili. Hili laweza kutia ndani, miongoni mwa mambo mengine, meza na viti vya urefu unaofaa, mito midogo ya kuwekea visugudi, kekee na koleo ambazo hazihitaji nguvu nyingi za mikono, kibodi za kompyuta zenye kufaa mtumiaji, au vyombo vizito vilivyo na vifaa vya kuzuia mtikisiko wa kupita kiasi.

Marcelo, aliyetajwa mwanzoni, alifuata mengi ya madokezo haya. Haya pamoja na matibabu aliyopata yameondolea mbali zile dalili za RSI alizokuwa nazo. Inawezekana apone kabisa. Bila shaka, juhudi za kibinafsi na mabadiliko ya mipango zahitajika ili kupambana na RSI, lakini kwa kuwa idadi ya wanaougua RSI mahali pa kazi inaongezeka, faida za kufanya mabadiliko haya huenda zikawa zenye manufaa zaidi zikilinganishwa na gharama.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

RSI Miongoni mwa Wanamuziki

Jeraha la mkazo wa kurudia-rudia (RSI) ni la kawaida miongoni mwa wanamuziki wataalamu. Kulingana na uchunguzi mmoja uliochapishwa mwaka wa 1986, nusu ya wanamuziki wote katika makundi manane ya okestra za simfoni katika Ulaya waliugua RSI. Katika karne ya 19, ugonjwa huu uliitwa mkakamao wa mwanamuziki. Kimoja cha visa vilivyoripotiwa kwanza kilikuwa cha Robert Schumann. RSI ulimfanya aache kucheza piano akajishughulisha tu na utungaji.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Mambo Yanayosababisha RSI

1. Kukaa vibaya

2. Kufanya kazi kwa muda wa saa nyingi

3. Mkazo kazini

4. Majeraha ya zamani katika misuli na kano

5. Kutoridhika na kazi

6. Kuathiriwa na baridi

[Sanduku katika ukurasa wa 18]

Kuzuia RSI

MAMBO YA KUEPUKA

1. Kubeba vitu vizito kwa vipindi virefu

2. Kuweka mkazo mwingi sana kwenye viungo

3. Kutumia mikono ikiwa juu ya usawa wa moyo kwa muda mrefu

4. Kufanya kazi katika hali zisizostarehesha

MAMBO YA KUFANYA

1. Badilisha mikono unapofanya kazi—hata zikiwa kazi nyepesi

2. Gawanya kazi mbalimbali ili uzifanye wakati tofauti-tofauti katika siku

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Ukurasa 16 na 17: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki