Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Msiba wa Anga? Nina umri wa miaka kumi, nami nilifurahia makala “Maoni ya Biblia: Je, Msiba wa Anga Utaangamiza Ulimwengu Wetu?” (Desemba 8, 1998) Ilinisaidia kuona kwamba hakuna msiba wa anga utakaoharibu sayari yetu kwa sababu Yehova anataka tuishi katika paradiso duniani.
J. P., Marekani
Upasuaji Bila Damu Nataka kuwashukuru kwa makala “Madaktari Wafikiria Upya Upasuaji Bila Damu.” (Desemba 8, 1998) Nilisisimuka sana nilipoisoma, kwa kuwa nilikuwa na mafanikio makubwa kutokana na tiba hiyo nilipowekwa nyonga. Nilikuwa katika chumba kimoja na mtu aliyefanyiwa upasuaji huohuo lakini kwa kutiwa damu. Niliweza kuondoka hospitalini kwa muda usiozidi juma moja. Lakini ilimbidi mtu huyo abaki, kwa kuwa alipatwa na magumu ya virusi.
N. H., Marekani
Acha Kuvuta Sigareti! Ile makala “Waweza Kuacha—Sisi Tuliacha!” ilikuwa ya pekee kwangu. (Desemba 8, 1998) Nimemaliza tu kujifunza Biblia na mvutaji wa sigareti. Yeye huja kwenye mikutano yetu yote, lakini anakabili kizuizi cha kiroho kwa sababu ya uraibu wake. Nimempa makala nyingine zinazohusu kuacha kuvuta sigareti, lakini nasali kwamba makala hii imsaidie kushinda kizuizi chake hatimaye.
E. C., Marekani
Kemikali na Afya Hivi majuzi nilianza mtaala wa kemia, na nilipoona toleo la Desemba 22, 1998, lilinivutia mara moja. Kama ilivyo sikuzote, mwajua jinsi ya kuandika habari iliyo ngumu kwa njia ambayo kila mtu aweza kuielewa. Kwa kuwa vichafuzi na kemikali huathiri watu wote, ingehitaji makubaliano ya kimataifa ili kutatua tatizo la uchafuzi daima. Lakini ubinafsi na pupa ya mwanadamu huzuia jambo hilo lisiwezekane. Kwa uzuri, Yehova anajua jinsi ya kutatua tatizo hilo daima.
C. V., Kanada
Kupoteza Wazazi Asanteni kwa kuandika makala nzuri jinsi hiyo, yaani, “Vijana Huuliza . . . Naweza Kuishije Bila Wazazi?” (Desemba 22, 1998) Ilisaidia kunihakikishia uwezo wa Yehova wa kutulinda sisi vijana tukipoteza wazazi wetu. Sijapoteza wazazi wangu katika kifo, lakini mara nyingi hujiuliza ningepatwa na nini kama wangekufa. Kielelezo kizuri cha Horacio kilinitia moyo sana.
M. J., Trinidad
Mkazo wa Kurudia-Rudia Ni vigumu kueleza unavyohisi unapopata makala inayoshughulika na tatizo ulilo nalo. Ndivyo ilivyokuwa na ile makala “Majeraha ya Mkazo wa Kurudia-Rudia—Unayopaswa Kujua.” (Desemba 22, 1998) Nilikuwa na jeraha la aina hiyo kwenye kiwiko changu, na sasa tu ndipo ninapotambua kilichosababisha jeraha hilo. Shauri la jinsi ya kushughulikia tatizo hilo lilinisaidia sana.
S. T., Yugoslavia
Nafanya kazi katika kampuni inayotengeneza vifaa vya kulinda wafanyakazi dhidi ya majeraha ya mkazo wa kurudia-rudia (RSI). Ugonjwa wa RSI umetokeza udadisi na ubishi, lakini makala yenu iliandikwa vizuri sana. Ilishughulika na somo hilo kwa njia ya haki na bila kutegemea maoni ya mtu yeyote. Baraza letu la wakurugenzi lilivutiwa sana hivi kwamba liliagiza nakala kadhaa zipelekewe wawakilishi wetu kotekote Brazili.
J. P. M., Brazili
Mimi ni mke nyumbani ninayefanya kazi nje ya nyumba inayohusisha kupakia masanduku mazito ya mbao. Tokea mwanzoni, niliumiza mgongo wangu, mikono, na viwiko vyangu. Miaka miwili hivi iliyopita, nilianza kunyoosha misuli yangu kwa dakika kumi kabla ya kuamka. Nilifikiri kwamba mazoezi hayo yangenisaidia, lakini makala hii ilinipa njia nyingine zinazosaidia zaidi za kukabiliana na jambo hilo. Wakati ujao, nitawapa wafanyakazi wenzangu nakala ya gazeti hili.
K. Y., Japani