Kuutazama Ulimwengu
Vitabu Vilivyookolewa
Mamilioni ya vitabu huharibika kwa sababu ya kuchakaa, madhara, au uchafuzi. Nchini Ujerumani pekee, imebidi mabuku yapatayo milioni 60 yaliyoharibika yaondolewe yasitumiwe, lasema gazeti Leipziger Volkszeitung. Kuvirekebisha vitabu kwa kutumia mikono ni utaratibu mrefu sana unaohitaji juhudi nyingi. “Katika muda unaotumiwa kurekebisha kitabu kimoja kwa kutumia mkono, vitabu vinne au vitano vingine huharibika,” asema Dakt. W. Wächter, mkurugenzi wa masuala ya kiufundi katika Kituo cha Kuhifadhi Vitabu, kilichoko Leipzig. Kituo hicho kimeshughulikia kutengeneza mashine zinazoweza kuhifadhi vitabu kwa wingi. Moja ya hizo mashine inaondoa asidi, nayo inaweza kushughulikia vitabu 100,000 kwa mwaka ikifuata zamu moja ya kazi. Pia, kuna mashine ya kutenganisha karatasi ambayo huimarisha ukurasa mmoja-mmoja kwa kutenganisha sehemu ya mbele na ya nyuma ya kila ukurasa na kuweka kikaratasi chembamba sana na chenye nguvu nyingi katikati ya ukurasa huo. Mashine hiyo yaweza kushughulikia karatasi 2,000 kwa siku, ikilinganishwa na karatasi 100 hadi 200 kwa siku ikiwa mikono yatumiwa—na pia mashine hiyo hupunguza gharama kwa asilimia 94 kwa kila ukurasa. Zaidi ya wenye maktaba na hifadhi za nyaraka, watu mmoja-mmoja pia huleta vitabu vyao kwenye kituo hicho ili virekebishwe.
Kanzu Fupi kwa Pilgrimu
Watalii wanaozuru sehemu takatifu za Katoliki nchini Italia mara nyingi huzuiwa kwa sababu wanakuja, hasa wakati wa miezi yenye joto la kiangazi, wakiwa wamevalia T-shati na suruali fupi. Sasa katika sehemu fulani wanaweza kuingia ikiwa wanavaa “Kanzu Fupi ya Pilgrimu,” kanzu yenye rangi ya mchanga inayofikia magotini. Hiyo kanzu fupi yenye saizi moja, inayovaliwa na watu wa jinsia zote, tayari inauzwa katika miji ya Venice na Roma. Mjini Roma imeongezewa vitu vilivyo katika kanzu ya papa na maneno “Yubile 2000.” Lakini je, hizi kanzu fupi zaweza kuvaliwa katika makanisa yote ya Kikatoliki? Ingawa Venetian Curia inazikubali, watalii fulani wa kiume wanaozuru St. Peter’s Basilica wamezuiwa kuingia hata ingawa waliinunua na kuivaa hiyo kanzu fupi. “Watumishi wa Makao ya Papa waliliona vazi hilo kuwa lawafaa wanawake pekee,” laeleza gazeti la Italia Corriere della Sera. “Wanaume walizuiwa—miguu mitupu ilionwa kuwa yenye ‘kuaibisha.’”
Uhusiano na Watoto Walioasilishwa
Nyakati nyingine wazazi wanaopanga kuasilisha mtoto huuona uhusiano huo kuwa ni mkamilifu—wakifikiri kwamba mtoto huyo atakuwa mzuri sana sikuzote na kwamba magumu yataeleweka na kushindwa kwa urahisi. Lakini kwa kawaida haiwi hivyo, gazeti la Brazili O Estado de S. Paulo laripoti. Mwanasaikolojia Heloísa Marton asema: “Kwa ujumla, wazazi hawajui kutatua hali za kutoelewana.” Wengine watakaoshtushwa ni “wenzi wanaotarajia kwamba mtoto huyo atakuwa mwenye shukrani sikuzote,” asema Profesa Miriam Debieux Rosa, wa Chuo Kikuu cha São Paulo. Hakuna mtu anayefurahi sikuzote, asema, akiongezea: “Mara nyingi wazazi husema kwamba magumu husababishwa na ukosefu wa uhusiano wa damu, na hilo si kweli.” Kuhusu uhitaji wa kuonyesha mtoto aliyeasilishwa shauku na upendo, huyo Profesa asema: “Haitoshi tu kuwa na uhusiano rasmi na wenye ubaridi.” Uhusiano wa kihisia pamoja na mtoto huyo wahitajika pia.
Kunyoa kwa Urahisi
Manyoya yaweza kupatikanaje bila mkazo wa mwili na majeraha ya kukatwa ambayo hutokea kwa ukawaida kondoo wanapokatwa manyoya? Katika Australia hilo hufanywa kwa kumdunga kondoo sindano ya protini inayopatikana kiasili katika mfumo wao wa damu. Kiwango kilichoongezeka cha protini hudumu kwa saa 24, nacho hulegeza unyoya kutokana na ngozi. Halafu manyoya hunyolewa kwa lundo moja, nayo huanza kumea tena. Kila kondoo huvalishwa wavu ambao hushikilia manyoya yake, ambayo hufunguliwa katika kipindi cha juma moja. Utaratibu huo huendeleza ubora wa manyoya na hufanya isiwe lazima kukata mara ya pili. Huo pia hupunguza chawa na ugonjwa wa ngozi, bila kutumia madawa, na haufanyi kondoo apatwe na mkazo. Utaratibu huo mpya unaendelea kuhitajiwa sana katika Australia, laripoti The Sunday Times la London, lakini huenda usifae sana katika nchi kama Uingereza, ambako halihewa lazima ifikiriwe wakati wa kunyoa. Kushuka kwa ghafula kwa joto baada ya sindano ya protini kutaliacha kundi la kondoo katika hali ya baridi sana baada ya manyoya kukatwa, akasema msemaji mmoja anayeshughulikia kazi hiyo.
Barafuto Zinazoyeyuka Zafichua Maajabu Zaidi
Barafuto za Alpine zaendelea kufichua maajabu ziyeyukapo kwa sababu ya kuongezeka kwa joto. Mnamo mwaka 1991, katika mpaka wa Austria na Italia, kuyeyuka kwa barafuto za zamani kulifichua maiti ya mwindaji wa zamani sana iliyohifadhiwa. Mnamo mwezi wa Agosti 1998, ili kuondoa mavumbuzi mengine—maiti za wanajeshi na gruneti za mkono na makombora ambazo bado hazikuwa zimelipuka—wenye mamlaka katika Italia kaskazini walilazimika kupiga marufuku kutembea katika sehemu kadhaa za milima. Vitu hivyo vyote ni vya kipindi cha vita ya ulimwengu ya kwanza, eneo hilo lilipokuwa uwanja wa mapigano kati ya majeshi ya Italia na Austria. Wakati wa kuondoa maiti hizo na silaha hizo, “wakazi wote, na hasa watalii na watembeaji, walionywa wajihadhari sana” na kutafuta mwelekezo kuhusu njia za kupitia kutoka kwa wenye mamlaka, likasema gazeti Corriere della Sera la Italia, kwa sababu “kuna hatari ya kutokea kwa milipuko wakati wowote.” Nyingi kati ya silaha hizo ni hatari sana na zaendelea kujeruhi vibaya watu wanaozipata.
Udongo Ulioganda
Ekari milioni 70 za udongo katika Ulaya “zimeharibiwa kabisa kwa kuganda kwa udongo,” laripoti gazeti New Scientist. Uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Kiel cha Ujerumani waonyesha kwamba matingatinga mazito, yenye uzito wa tani tano kwenye kila gurudumu, yapitiapo shamba mara sita, wingi wa wadudu kama vile araknida na minyoo ulipungua kwa asilimia 80 kufikia kina cha meta moja. Wadudu hao wadogo husaidia kudumisha rutuba kwenye udongo, kwa hivyo wanapoangamizwa, mazao ya mimea hupungua kwa kadiri hiyo. Mizizi ya mimea haiwezi kupenya udongo wa juu ulioganda, hivyo basi mimea huathiriwa wakati wa kiangazi. Maji ya mvua hayawezi kupenya chini; badala yake, hupitia juu, yakimomonyoa udongo wa juu. Kwa kweli, kulima kwa plau kikawaida huzidisha tatizo hilo, ukifanya mgando huo kwenda chini zaidi. Wanasayansi hao Wajerumani hudai kwamba kulima kina kifupi, kwa kuvunja udongo wa juu kufikia kina cha sentimeta nane tu, uharibifu unaokumba udongo waweza kupunguzwa kwa theluthi moja.
Ujumbe Unaozidi Kiasi
“Vyombo vya mawasiliano vya siku hizi vinavyotegemea tekinolojia vinasababisha hatari mpya ya kiafya mahali pa kazi: mkazo unaosababishwa na ujumbe,” lasema gazeti Computing Canada, linaloshughulikia usimamizi wa tekinolojia ya kompyuta. Uchunguzi wa hivi karibuni kuhusu mawasiliano mahali pa kazi, uliofanywa na Stamford, ambalo ni shirika la Pitney Bowes Inc., lenye makao makuu huko Connecticut, uligundua kwamba mfanyakazi wa ofisi wa kawaida hupeleka au hupokea “jumbe zinazokadiriwa kuwa 190 kwa siku kupitia njia mbalimbali,” kama vile mashine za simu zinazojibu ujumbe, simu, faksi, pager, beeper, na E-mail. “Hilo lamaanisha,” lasema gazeti hilo “kwamba sasa kazi, kwa kiwango fulani, huathiriwa na uhitaji wa kupokea ujumbe, na hilo huzidisha mkazo na hali ya kulemewa na mambo.” Uchunguzi huo uligundua kwamba wafanyakazi wengi wanapendelea zaidi mawasiliano ya uso kwa uso au ya simu. Watafiti hupendekeza kwamba “wafanyakazi wote wapewe mwongozo kuhusu utumizi unaokubalika wa vyombo vyao vya mawasiliano—na jinsi ya kuvitumia ifaavyo” kwa njia hiyo wakipunguza ujumbe unaozidi kiasi.
Mengi Zaidi Juu ya Upumbavu wa Kuvuta Sigareti
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni nchini Uholanzi wasema kwamba “uvutaji wa sigareti huongeza mara mbili hatari ya kupata kasoro za akili au ugonjwa wa Alzheimer,” laripoti jarida International Herald Tribune. Uchunguzi huo uliofanyiwa watu 6,870 wenye umri wa miaka zaidi ya 55 ulionyesha kwamba wavutaji wa sigareti wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa Alzheimer mara 2.3 zaidi kuliko wale wanaoepuka uvutaji wa sigareti maisha yao yote. Hatari iliyowakabili wale ambao wameacha kuvuta sigareti ilikuwa juu kidogo tu kuliko wale ambao hawajavuta kamwe sigareti. Ugonjwa wa Alzheimer, unaohusu kuharibiwa polepole kwa chembe za ubongo, ndiyo “aina ya kawaida zaidi ya kasoro za akili.”
Hayasomeki
“Huenda tuzo la Nobeli lamngojea mtu ambaye atatambua maana ya maandishi waliyoandika watu wa Indus,” lasema jarida India Today. “Maandishi hayo, pamoja na maandishi ya Waetruska wa Italia, ndiyo maandishi pekee ya Enzi ya Shaba ambayo maana yake bado hayajatambuliwa.” Sababu moja ni kwamba hakuna hati yoyote yenye lugha mbili imepatikana ambayo ingesaidia kutambua maana ya maandishi hayo. Maana ya michoro ya Misri ilitambuliwa baada ya watu wa Napoleon kulipata Jiwe la Rosetta, likiwa na michoro, Kimisri cha kawaida, na Kigiriki. Maana ya maandishi ya kikabari ya Sumer ilijulikana Henry Rawlinson alipogundua Maandishi ya Behistun, yaliyokuwa na kidokezi alichohitaji ili kutambua maana yake. Hadi leo, hakuna kinachojulikana kuhusu maandishi ya watu wa Indus isipokuwa tu kwamba waliandika kutoka kulia kuelekea kushoto—hilo laonyeshwa na alama za mistari—na kwamba huenda maandishi hayo yalitegemea silabi. Hati hiyo, ambayo kwa sehemu kubwa imefanyizwa kwa herufi zilizochongwa, ina ishara zipatazo 419.