“Hakika Anga Liko Wazi”!
“TAMAA ya kusafiri angani ni ya kale kama mwanadamu,” akasema mwanahistoria Berthold Laufer katika The Prehistory of Aviation. Kumbukumbu za Wagiriki, Wamisri, na Waashuri wa kale pamoja na hekaya za Mashariki zina hadithi nyingi sana za wafalme, miungu, na mashujaa waliojaribu kupata nguvu za kuruka angani. Katika karibu visa vyote, hadithi hizo zinahusisha watu wakiiga ndege wanaopaa.
Kwa kielelezo, Wachina husimulia hadithi juu ya Maliki Shun mwenye hekima na mjasiri, anayedhaniwa kuwa aliishi miaka zaidi ya 2,000 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kulingana na hekaya, Shun, alijikuta amenaswa juu ya ghala iliyokuwa ikiwaka moto, akajivika manyoya, na kutoroka kwa kupuruka. Simulizi lingine lasema kwamba aliruka kutoka kwenye mnara na kutumia vyepeo viwili vikubwa vya mafunjo kama miavuli naye akatua ardhini salama.
Miongoni mwa Wagiriki, kuna hadithi ya miaka 3,000 ya Daedalus, msanii mkuu na mvumbuzi, aliyejenga mabawa yaliyotengenezwa kwa manyoya, kitani, na nta ambayo yangemwezesha yeye na mwana wake Icarus kutoroka Krete, mahali ambapo walizuiwa wakiwa uhamishoni. “Hakika anga liko wazi, na ndiyo njia tutakayofuata,” akatangaza Daedalus. Mara ya kwanza, mabawa yalifanya kazi kikamilifu. Lakini Icarus, akiwa amevutiwa na uwezo wake wa kupaa juu, alizidi kupuruka juu zaidi mpaka nta iliyounganisha mabawa yake ilipoyeyushwa na jua. Mvulana huyo alitumbukia kwenye bahari iliyokuwa chini akafa.
Hadithi za namna hiyo zilichochea fikira za wavumbuzi na wanafalsafa waliotamani sana kupaa angani. Mapema kufikia karne ya tatu W.K., Wachina walikuwa wakijenga tiara na kuzijaribu, wakidhihirisha kwamba walielewa kanuni fulani za elimu ya anga muda mrefu kabla majaribio ya aina hii hayajaanza katika Ulaya. Katika karne ya 15, Giovanni da Fontana, tabibu wa Venice, alifanyia majaribio roketi sahili zilizotengenezwa kwa mbao na karatasi zilizorushwa kwa mlipuko wa baruti. Yapata mwaka wa 1420, da Fontana aliandika hivi: “Mimi, kwa kweli, sina shaka lolote kwamba inawezekana kumfungia mwanadamu mabawa yanayoweza kusogezwa, ambayo yatamwezesha kupaa hewani na kusafiri kutoka mahali pamoja hadi pengine na kupanda minara na kuvuka bahari.”
Mapema katika karne ya 16, Leonardo da Vinci, aliyekuwa mchoraji, mchongaji, na mhandisi aliye stadi, alichora ramani zisizo stadi za helikopta na miavuli na vilevile za nyiririko zenye ncha za mabawa yanayopigapiga. Uthibitisho unadokeza kwamba angalau alijenga miundo ya mashine kadhaa za angani ambazo alikuwa amedokeza. Hata hivyo, hakuna muundo hata mmoja wa Vinci ulioweza kutumika.
Katika karne mbili zilizofuata kuna masimulizi kadhaa ya jitihada za wanaume hodari waliojifunga mabawa waliyojitengenezea na kujaribu kuyapigapiga walipokuwa wakiruka kutoka kando za vilima na kwenye minara. Hawa ‘marubani wa majaribio’ walikuwa hodari na wajasiri—lakini jitihada zao hazikufua dafu.
Puto za Moto na “Hewa Yenye Kuwaka Moto”
Katika mwaka wa 1783 habari kuhusu mafanikio yenye kutazamisha ya usafiri wa angani zilienea Paris kote na katika mikoa ya Ufaransa. Ndugu wawili, Joseph-Michel na Jacques-Étienne Montgolfier, waligundua kwamba wangeweza kufanya puto ndogo za karatasi ziinuke haraka na kwa wepesi angani kwa kuzijaza hewa yenye moto. Puto yao ya kwanza kubwa ya moto, kama ilivyoitwa, ilitengenezwa kwa karatasi na kitani na ilijazwa moshi wenye harufu mbaya uliotoka kwenye moto mkubwa. Puto hiyo ambayo haikuwa na mtu iliruka na kufikia mwinuko wa zaidi ya meta 1,800 wakati wa safari yake ya kwanza ya angani. Mnamo Novemba 21, 1783, puto hiyo ilibeba abiria wawili—walioitwa na umma wanaanga—kwa safari ya dakika 25 juu ya Paris. Katika mwaka huohuo, mvumbuzi mwingine, Jacques Charles, alifunua puto ya kwanza iliyokuwa imejazwa gesi, iliyojazwa hidrojeni, au “hewa inayoshika moto,” kama ilivyojulikana wakati huo.
Tekinolojia ya puto ilipozidi kuboreka, anga lilianza kufikiwa na wanaanga wajasiri. Kufikia mwaka wa 1784, puto zilikuwa zikipaa na kufikia mwinuko unaozidi meta 3,400. Mwaka mmoja tu baadaye, Jean-Pierre-François Blanchard alifanikiwa kuvuka Mlango-Bahari wa Uingereza akiwa ndani ya puto ya hidrojeni akibeba barua za kwanza ulimwenguni zilizosafirishwa angani. Kufikia mwaka wa 1862, wanaanga walikuwa wamefunga safari Ulaya na Marekani kote na walikuwa wamefaulu kufikia miinuko inayozidi kilometa nane!
Lakini wanaanga wa mapema bado walikuwa wakipelekwa popote pale na pepo; hakukuwa na njia ya kudhibiti upande au mwendo wa safari za anga za puto. Kutokezwa kwa vyombo vya anga vinavyoendeshwa na petroli na umeme mwishoni mwa karne ya 19 kulifanya usafiri wa angani uwezekane kwa kiwango kikubwa, lakini vyombo hivyo vya anga vyenye umbo la soseji na vyepesi kuliko hewa vilisafiri polepole—kwa kawaida vikisafiri kati ya kilometa 10 hadi 30 kwa saa. Jambo jipya lilihitajiwa ikiwa mwanadamu ‘angepaa hewani na kusafiri kutoka mahali pamoja hadi pengine,’ kama alivyotabiri da Fontana.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Daedalus na Icarus wanaosimuliwa katika hekaya
[Picha katika ukurasa wa 4]
Leonardo da Vinci
[Hisani]
From the book Leonardo da Vinci, 1898
[Picha katika ukurasa wa 4]
Akina Montgolfier walibuni puto ya kwanza ya gesi moto ya kubeba abiria