Kuutazama Ulimwengu
Watoto Waliozaliwa Karibuni Huhisi Maumivu
Watafiti katika London’s University College wamethibitisha kwamba watoto waliozaliwa karibuni huhisi maumivu zaidi na kwa muda mrefu kuliko watu wazima. “Ni miaka 10 tu iliyopita watafiti walipokiri kwamba watoto wachanga na wale waliozaliwa karibuni huhisi maumivu,” lataarifu The Sunday Telegraph la London. Kabla ya utafiti huo, watoto waliozaliwa kabla ya wakati wao walitibiwa kwa njia zenye maumivu mengi na walifanyiwa upasuaji bila kupewa dawa za kutuliza maumivu. Madaktari sasa wanaamini kwamba tiba ya aina hiyo inaweza kuathiri kwa muda mrefu jinsi watoto wanavyotenda wanapohisi maumivu, hata wapitapo umri wa utoto. Hii ni kwa sababu njia ya asili ya kupunguza uchungu katika watoto wakubwa na katika watu wazima haitendi vyema katika watoto waliozaliwa kabla ya wakati wao. Vilevile maumivu ya watoto wachanga huenea sehemu kubwa zaidi mwilini, na jeraha dogo ngozini laweza kufanya sehemu yote iliyoathiriwa iwe na maumivu makali inapoguswa muda mrefu baada ya jeraha kupona, laripoti gazeti hilo.
Dokezo la Mwanafunzi Latokeza Uvumbuzi
Wakifuata dokezo la mwanafunzi wa chuo kikuu anayesomea fizikia ya angani, waastronomia wameongeza sayari nyingine kwenye orodha ya sayari zinazozunguka nyota nyinginezo tofauti na jua. Kevin Apps, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza, aliwadokezea waastronomia Dakt. Geoffrey W. Marcy na Dakt. R. Paul Butler, ambao wamegundua kwa pamoja sayari nyingine tisa kama hizo, kwamba wachunguze nyota 30 zinazofanana na jua ambazo zilikuwa zimepuuzwa. Walipochunguza walipata sayari inayotoshana na Sumbula ikizunguka mojawapo ya nyota hizo. Ili kuzichagua nyota alizopendekeza zichunguzwe, Dakt. Marcy alisema kwamba Apps “alitumia habari za karibuni zaidi juu ya anga kisha akatenga nyota zilizoelekea kuwa na sayari.” Sayari hiyo iliyogunduliwa—pamoja na nyingine iliyogunduliwa na waastronomia hao wawili—zimeongeza idadi ya sayari zilizo nje ya mfumo wa jua ambazo zinajulikana kufikia 12, zote zikiwa zimegunduliwa katika kipindi cha miaka mitatu, laripoti The New York Times.
Kifaa Kinachoigiza Uzee
Watu wengi wanapojaribu kudumisha ujana na nguvu, kuna vazi ambalo limetengenezwa ili kumfanya mtu ajihisi akiwa mzee na dhaifu, laripoti gazeti Die Zeit la Ujerumani. Kampuni moja inayotengeneza nguo na kutoa mashauri, pamoja na madaktari wa kitiba, walitengeneza vazi hilo la kuiga uzee ili kuwasaidia wauguzi na watengeneza bidhaa kuelewa “jinsi wazee wanavyouona ulimwengu.” Kifaa hicho chatia ndani bendeji na mikunjo ya kupunguza mwendo, kilogramu 14 za madini ya risasi ili kutoa hisi ya misuli iliyo dhaifu, vifundo vigumu vilivyo ndani ya jozi ya glavu ili kukaza vidole, vipokea sauti vinavyobanwa kichwani ili kufyonza sauti za juu, na kiwambo kinachopunguza uwezo wa kuona kwa nusu na kutia ukungu machoni. Hilo gazeti Die Zeit lapendekeza hivi: “Kila mtu ambaye hajafikia umri wa miaka 60 anapaswa atembee kwa muda wa saa chache akiwa amevaa vazi hili, hii ikiwa njia ya kufahamu tofauti iliyoko kati ya vizazi.”
Historia Yapatikana
“Karne mbili baada ya pigano la kihistoria lililovunja matumaini ya Napoleon ya kuangamiza milki ya Uingereza, meli za huyo maliki Mfaransa zimepatikana kwenye maji yasiyo na kina katika ghuba ya Mediterania,” laripoti The Toronto Star. Wakati wa Pigano la Nile mwaka wa 1798, meli kuu iliyoitwa L’Orient na pia meli ya La Seriuse na La Artemise zilizamishwa na Jeshi la Wanamaji la Uingereza, likiongozwa na Admeri Horatio Nelson. Mwakiolojia wa mambo ya baharini aliye Mfaransa Franck Goddio aligundua meli hizo katika maji yenye kina cha meta 11 na umbali wa kilometa mbili kutoka pwani ya Alexandria, Misri. “Hapa ndipo wakati ujao wa Ulaya ulipoamuliwa,” akaeleza Goddio.
Ndege Wanaosafiri Hupunguza Uzito wa Ziada
Mafigo, ini, na viungo vingine vya mwili vya baadhi ya ndege hupunguka kabla ya safari ndefu ya kuhama, laripoti New Scientist. Ndege wa majini waitwao bar-tailed godwits wanaotoshana na shakwe na ambao husafiri kati ya Alaska na New Zealand, hula kupindukia kabla ya kufunga safari ya umbali wa kilometa 11,000 bila kutua. Watafiti Theunis Piersma, wa Chuo Kikuu cha Groningen nchini Uholanzi, na Robert Gill, wa Uchunguzi wa Jiolojia wa Marekani, waligundua kwamba ndege hao husawazisha uzito wanaoupata kwa kupunguza ukubwa wa viungo vya mwili vinavyosaga chakula kwa kiwango cha asilimia 25. Gill ataarifu: “Ndege hawa huhifadhi uwezo ufaao wa viungo vya mwili ili, wanapotua tena, waweze kusaga chakula na kujenga tena viungo vyao vya ndani.”
Onyo Kuhusu Asali kwa Watoto Wachanga
Asali ina vitamini, madini, na vitu vinavyozuia ongezeko la oksijeni, laripoti Science News. Kwa kawaida, kwa kadiri asali iwapo nyeusi zaidi, ndivyo inavyokuwa na vitu vinavyozuia ongezeko la oksijeni. Hata hivyo, UC Berkeley Wellness Letter yatoa onyo hili: “Usiwape kamwe asali watoto ambao hawajafikia umri wa mwaka mmoja.” Viiniyoga visivyotenda vinavyoitwa clostridium botulinum vimo katika wastani wa asilimia 10 ya asali na vinaweza kusababisha kusumishwa kwa watoto wachanga. “Kadiri ya kusumishwa yaweza kuwa ugonjwa kidogo hadi kupooza kubaya sana na hata kifo cha ghafula, kusipotibiwa,” yataarifu Wellness Letter. Hata hivyo, kwa watoto wakubwa asali inaonwa kuwa salama.
Kuvuta Sigareti ili Kuwa Mwembamba
“Tamaa ya kuwa mwembamba” inawafanya wasichana matineja wavute sigareti, laripoti gazeti The Globe and Mail la Kanada. Katika mahoji waliyofanyiwa wasichana Wakanada 832 na 1,936 wa Uingereza wenye umri wa miaka 10 hadi 17, wengi wao “walisema kwamba uvutaji wa sigareti ni kibadala cha kula” na waliuona kuwa hupunguza hamu ya kula. Wasichana wengi matineja walisema kuwa waliamini kwamba “ikiwa wangeacha kuvuta sigareti wangekula chakula zaidi na hivyo kunenepa zaidi.” Gazeti Globe lilisema “ripoti zaonyesha kwamba huenda wasichana matineja ndio wanaosababisha ongezeko kubwa la uvutaji wa sigareti wa matineja kwa ujumla na hilo linafunua sababu inayofanya kuwe na ongezeko la kansa ya mapafu miongoni mwa wanawake.”
Hofu ya Kufutwa Kazi Yaweza Kudhuru Afya
Hofu ya kupoteza kazi yaweza kudhuru afya yako, laripoti Science News. Kati ya watumishi wa serikali 10,000 waliohojiwa kwenye uchunguzi mmoja wa afya wa muda mrefu huko Uingereza, kikundi cha wanaume na wanawake zaidi ya 600 walisikia uvumi kwa miaka minne kuwa idara yao ingeuziwa shirika la mtu binafsi. Wakati huohuo, afya ya wale waliokuwa katika kikundi hicho ilidhoofika kwa wastani ilipolinganishwa na ya wale wengine waliofanyiwa uchunguzi na ambao kazi zao zilikuwa salama. Kiwango cha kolesteroli katika damu ya waliohofu kufutwa kazi kiliongezeka na kulikuwa pia na ongezeko la asilimia 40 hadi 60 katika visa vya ugonjwa wa kuziba kwa mishipa ya moyo. Gazeti Science News laripoti: “Wafanyakazi hawa walikuwa pia na mwelekeo wa kuacha kufanya mazoezi, kunenepa, kupoteza usingizi kwa zaidi ya muda wa saa 9, na kutaliki au kutengana na mwenzi wa ndoa.”
Umakini wa Mbwa
Ni nini kinachomfanya mbwa awe mzuri kunusa dawa za kulevya? Takwa moja ni hisi bora ya kunusa na “umakini bora,” laeleza gazeti New Scientist. “Mbwa mzuri wa kunusa lazima awe na uwezo wa kukazia fikira kazi ya kutafuta dawa za kulevya, japo hekaheka na vikengeusha fikira katika uwanja wa ndege au bandari yoyote,” yaeleza ripoti hiyo. Japo kuchunguza barua kwaweza kuchukua muda wa saa nyingi, “mbwa aweza kuwa makini sana hivi kwamba . . . hata gramu 0.5 za heroini . . . iliyofichwa katika mfuko uliojaa barua haitakosa kugunduliwa.” Programu ya kuwazoeza mbwa iliyoanzishwa mwaka wa 1993 imefanikiwa sana; zaidi ya asilimia 50 ya hao mbwa wamefaulu kutumiwa wakiwa wanusaji wa dawa za kulevya katika Idara ya Forodha ya Australia. Wakufunzi walipokuwa wakiwazoeza mbwa, walitafuta sifa nyingine kama vile kupenda kusifiwa, silika yenye nguvu ya kuwinda, nguvu, na ujasiri.
Ramani ya Zamani Zaidi Inayoonyesha Umbali
Waakiolojia Wachina wamepata bamba la shaba nyekundu la miaka 2,300 iliyopita likiwa na maandishi yaliyochongwa ambalo kwa kweli ni ramani yenye kuonyesha umbali kwa tarakimu, laripoti shirika la habari la Agence France-Presse. Ramani hiyo, ambayo huonyesha sehemu ndogo ambayo sasa ni Mkoa wa Hopeh, kaskazini mwa China, inatumia kipimo cha wastani cha 1:500. Inatia ndani mchoro wa makaburi ya kifalme ya Mfalme Wang Cuo, aliyeishi katika karne ya nne K.W.K. Du Naisong, mtafiti wa shirika la China’s Forbidden City, alitaarifu hivi: “Hiyo si ramani tu ya zamani zaidi iliyowahi kupatikana nchini China bali ramani ya zamani zaidi ulimwenguni yenye tarakimu.”
Watu Bilioni Sita Mwaka wa 1999
Wakati fulani mwaka huu idadi ya watu ulimwenguni itapita bilioni sita, laripoti gazeti la Kifaransa Le Monde. Hata hivyo, ukuzi wa idadi ya watu ulimwenguni unapungua. Ukuzi wa kila mwaka umepungua kwa asilimia 30 kuliko ulivyokuwa katika miaka ya 1960. Upungufu huu wa ukuzi unasababishwa kwa kiasi fulani na ongezeko la matumizi ya vizuia-uzazi na pia kuelimishwa zaidi kwa wasichana. Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 sasa ni zaidi ya bilioni moja, huku wakiwapo watu zaidi ya milioni 578 wenye umri unaozidi miaka 60.