Kuutazama Ulimwengu
Ukimwi Katika Paris
“Katika Paris, kifo 1 kati ya kila vifo 3 miongoni mwa wanaume wa miaka kati ya 25 na 44 husababishwa na vairasi ya UKIMWI,” lasema gazeti la Kifaransa Le Monde. Takwimu hizo za karibuni zilitolewa kwa umma hivi karibuni na INSERM (Taasisi ya Kitaifa ya Ufaransa ya Utafiti wa Afya na Tiba). Ripoti hiyo yafunua pia kwamba kati ya 1983 na 1990, uambukizo wa vairasi ya UKIMWI uliongeza idadi ya vifo miongoni mwa kikundi icho hicho kwa asilimia 50. Dkt. Jonathan Mann, mkurugenzi wa WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni), alitabiri hivi: “Mabaya zaidi bado yako mbele; ugonjwa huo unaendelea kila mahali.” Kulingana na WHO, watu elfu tano huambukizwa kila siku ulimwenguni pote.
Watoto na Kunyonyeshwa Chupa
Karibu asilimia 25 ya watoto wa Japan hupatwa na magumu ya ulaji. Tatizo laweza kuwa kunyonyeshwa chupa. Kwa muda wa miaka zaidi ya 20, laripoti gazeti Asahi Evening News, walimu wa shule za nasari wameona kwamba watoto wengine wanapata matatizo ya kutafuna chakula kigumu. Watoto wengine wanapata tatizo la kukimeza, wengine hukitema, na wengine bado huwa nacho kinywani baada ya usingizi wao wa alasiri. Madaktari wameona kwamba taya za watoto hao hazina nguvu na videvu vyao ni kidogo. Daktari wa meno Naohiko Inoue na mtaalamu wa afya ya umma Reiko Sakashika wanadai kuwa wamegundua sababu ya matatizo hayo kuwa huanza wakati wa utoto kwa sababu ya kunyonyeshwa chupa. Inaonekana kwamba watoto wanaponyonya chupa, wanahitaji kunyonya tu bila kusogeza taya zao. Lakini, watoto wanaponyonya matiti, wanatumia taya zao sana na kuimarisha misuli ambayo watahitaji kutumia baadaye kutafuna chakula.
Tatizo la Kasa wa Bahari
Ingawa maji ni makao ya kasa wa bahari, wanataga mayai yao katika nchi kavu. Baada ya kuzunguka-zunguka katika bahari za ulimwengu, kasa wa bahari hurudia fuo fulani hususa ili watage. Baada ya kujamiiana baharini, kasa jike hujikokota ufuoni—yawezekana kuwa ule ufuo alipozaliwa—na kutaga mayai yake kwa utulivu katika mahali palipoteuliwa kwa uangalifu. Jambo hilo lafanywa kwa kurudia-rudia kwa siku chache, mpaka mayai yote—karibu elfu moja—yawe yametagwa na kufunikwa kwa uangalifu. Lakini ndipo tatizo hutokea. Jarida la Afrika Kusini Prisma laliita “kule kuchukuliwa kwa mayai yote kwa ukawaida” na mwanadamu katika “tamaa [yake] kubwa na uovu mkubwa sana wa kutojali mazingira,” ambako “kumeathiri sana tabia ya uzazi ya kasa.” Aina fulani za kasa hao zinakabili hali ya kutoweka.
Watangazaji wa Tumbako Watumia Vibaya Wanawake
“Umefanya maendeleo sana, kisura.” Kwa miaka mingi katika United States, wanawake wanaovuta sigareti wametiwa moyo kwa shime za matangazo zenye kushawishi kama hizo. Wanawake hao wametumiwa vibaya, alalamika Kathy Harty, mkuu wa programu ya kupinga uvutaji wa sigareti katika mojapo majimbo ya kaskazini [ya U.S.A.]. Harty ameshiriki kutayarisha matangazo ya TV na redio yanayokazia ujumbe huo. Tangazo moja la kupinga uvutaji wa sigareti laonyesha mwanamke mrembo akizima sigareti kwenye kichwa chenye upara cha ofisa mmoja wa matangazo ya biashara. Tangazo la redio laonyesha mwanamke akiwaambia watengenezaji wa sigareti hivi: “Asanteni sana kwa kufanya nywele zetu zinuke kama kisahani cha majivu ya sigareti. Asanteni kwa kutia meno yetu rangi na kuongeza gharama zetu za kufua nguo kwa sababu ya harufu. Asanteni kwa visa 52,000 vya kansa ya mapafu mnayosababisha katika wanawake kila mwaka. Tunatumaini tu kwamba siku moja tutawafanyia vivyo hivyo.” Harty aeleza: “Tunataka [wanawake] wafikirie jambo hili kwa uzito: ‘Je! kweli ninataka sigareti hii? Je! kweli ninataka kumfanya mtu fulani kuwa tajiri na mimi niwe mgonjwa?’”
Tumaini la Waastronomia
Katika programu ya miaka kumi iliyosimamiwa na U.S. National Aeronautics and Space Administration (Usimamizi wa Kitaifa wa Ufundi wa Angani wa U.S.), waastronomia wanapanga kutumia dola milioni 100 za U.S. katika jitihada ya kuvumbua matangazo ya redio kutoka kwa viumbe vyenye akili katika sayari nyinginezo. Kulingana na International Herald Tribune, mpango wao ni kufuata kwa pamoja njia za mamilioni ya mawimbi madogo sana katika darubini za redio zilizomo katika Argentina, Australia, India, Puerto Rico, United States na Urusi. Ingawa baadhi ya wanasayansi wanatazamia mafanikio ya mapema, wengine wasema kwamba utafutaji 50 uliofanywa tangu 1960 haukuwa na matokeo.
Kupanga Mapema Televisheni?
“Kutotazama TV sana ni jambo zuri zaidi kwa watoto, hasa TV yenye jeuri,” chasema American Academy of Pediatrics (Chuo cha Tiba ya Watoto cha Amerika) katika uchunguzi uliochapishwa katika The Journal of the American Medical Association. Makala hiyo ilisema kwa-mba “watoto wachanga wenye umri kama miezi 14 hutazama na kuiga tabia wanazoona katika televisheni.” Mambo mengi wanayoona ni yenye asili ya ukali au ujeuri. Katika jitihada ya kurudisha mamlaka ya wazazi, ripoti hiyo yadokeza utumizi wa tekinolojia ya kisasa ya kufuli ya kielektroni ya kutegemea saa na wakati na kituo cha TV ili kwamba programu, na vituo vya TV, na wakati zipangwe mapema. Katika njia hiyo, hata wakati wazazi hawako nyumbani, wanaweza kudhibiti mambo yale ambayo watoto wao wanatazama katika televisheni na wakati wa kuyatazama.
Asali—Kiponyi
Tangu nyakati za kale, asali ya nyuki imetumiwa kwa ajili ya uwezo wayo wa kuponya. La Presse Médicale, gazeti la Kifaransa, laripoti kwamba sayansi ya tiba ya kisasa inaanza sasa kugundua tena uwezo wa asali wa kuponya. Katika uchunguzi wa karibuni, madaktari walifanya majaribu ya kutumia asali ya asili isiyochanganywa na chochote kwa majeraha ya mwili ya kuchomeka na ya aina nyinginezo. Asali ilipakwa moja kwa moja kwenye majeraha na kisha kufungwa kwa bendeji kavu safi. Bendeji hiyo ilibadilishwa baada ya kila muda wa saa 24. Matokeo yanaonyesha asali kuwa yenye matokeo sana ikiwa kisafishi na kiponyi. Inaua vijidudu vingi mara moja na kuchochea ukuzi mpya wa mnofu. La Presse Médicale lamalizia hivi: “Kwa sababu ni rahisi na si ghali, asali yapasa ijulikane zaidi na kuongezwa kwenye orodha ya dawa zinazotumiwa kwa kawaida kuzuia ukuzi wa vijidudu kwenye jeraha.”
Wanariadha Hodari Wasiokuwa na Afya Nzuri
“Mazoezi ya kupita kiasi na mkazo wa kihisia-moyo yanayotangulia mashindano makubwa huwa na tokeo lisilo la kawaida juu ya mifumo ya kinga ya mwili wa wanariadha,” laripoti O Estado de S. Paulo. “Tokeo laweza kuwa upungufu katika kinga dhidi ya maambukizo yanayofanana sana na ishara za UKIMWI.” Utafiti uliofanywa na Dkt. Gerd Uhlenbruck na Dkt. Heinz Liesen unafunua kwamba wanariadha hodari au wanaofanya mazoezi sana wana uwezekano wa juu zaidi wa kupata mavimbe hatari na maambukizo. Wanadokeza kwamba huenda ikawa hali hiyo inasababishwa na mkazo unaoletwa na “mazoezi makali na ugumu wa mashindano.” Ripoti hiyo yaongezea: “Kwa upande mwingine, mazoezi ya kiasi ya michezo huimarisha mwili na kusaidia si kuzuia tu kansa bali pia kuongeza urefu wa maisha ya mtu.”
Upasuaji wa Kufanyiwa Kutoka Mbali kwa Wakati Ujao?
“Mgonjwa yuko Roma, daktari-mpasuaji ampasua akiwa Milan,” laeleza gazeti la kila siku la Italia linaloitwa Il Messagero linapoelezea juu ya “majaribio ya kwanza kabisa ya upasuaji wa kufanyiwa kutoka mbali kwa kutumia roboti [mashine zenye umbo la kibinadamu].” Akiwa umbali wa mamia ya kilometa, na akitumia simu na vidio, huyo daktari-mpasuaji atambua “mahali hususa pa kupasuliwa, atoa kibali chake, na roboti inaanza kazi. Mkono wa roboti hiyo ukiwa na kisu cha upasuaji unateremshwa kwa mwili wa mgonjwa na kupasua.” Katika onyesho hilo, upasuaji ulioigizwa katika mkutano wa Upasuaji wa ‘92 huko Roma, mgonjwa alikuwa tu mfano wa mtu, kwa sababu sheria ya Italia hairuhusu mashine zifanyie watu upasuaji, lakini kwa miaka sita au saba ijayo, upasuaji wa kufanyiwa kutoka mbali, yaani “upasuaji unaodhibitiwa kwa mashine,” huenda ukatumika kihalisi. Kulingana na Licinio Angelini, profesa wa upasuaji wa kawaida katika Chuo Kikuu cha La Sapienza, Roma, wakati ujao “kazi hizo zote zinazofanywa na daktari-mpasuaji kwa shida ya kadiri fulani zitaachiwa mashine.”
Ukosefu wa Kazi na Afya
Ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana ni mojapo matatizo makubwa zaidi ya ulimwengu wa Magharibi, adai Dkt. Anne Hammarström wa Taasisi ya Karolinska katika Stockholm, Sweden. Ugunduzi wake, kama ilivyoripotiwa katika British Medical Journal, waonyesha kwamba wanaume vijana wasio na kazi huelekea kuwa na tabia mbaya, kama kuongeza kunywa vileo na kuhusika katika uhalifu. Hata hivyo, wasichana wasio na kazi huathiriwa kwa njia tofauti, wakipatwa zaidi na magonjwa ya kimwili, pamoja na hisi za hatia, wakihangaika kwamba wanatwika familia zao mzigo. Wanaume hupata uangalifu mwingi zaidi wa umma, kwa sababu itikio lao kwa ukosefu wa kazi waonekana wazi zaidi, aonelea Hammarström. Yeye apendekeza kwamba mashirika ya afya yapaswa yawe macho zaidi kwa athari za ukosefu wa kazi juu ya wanawake.” Journal lamalizia kwamba “suluhisho la pekee linalofaa kabisa ni kupata kazi nzuri.”
‘Ujerumani ni Nchi ya Kipagani’
“Muungano wa Jamhuri [ya Ujerumani] umekuwa nchi ya kipagani yenye mabaki machache ya Wakristo. Watu milioni sita wameacha kuamini katika Mungu. Idadi ya watu ambao hawana dini ni kubwa zaidi kuliko idadi ya wale wanaoenda kanisani. Ni asilimia 10 tu ndio huenda kanisani kila Jumapili.” Hayo yalikuwa ndiyo magunduzi ya uchunguzi uliosimamiwa na gazeti la Ujerumani Der Spiegel. Majibu yalilinganishwa na matokeo ya uchunguzi kama huo katika 1967. “Wapagani hao wapya,” kama vile gazeti hilo lilivyowaita wale walioacha kanisa, “wameacha kanisa bila kuwa na uchungu wowote wala hasira. Haikuwa kwa sababu ya hamaki bali ni kutokujali kulikonyang’anya makanisa wafuasi wayo.”