Sarafu ya Pekee ya Afrika Magharibi
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Sierra Leone
JE, UMEPATA kuona fedha inayofanana na hii? Ni sarafu ya Wakissi. Baadhi ya sarafu hizi zimewekwa kwenye Jumba la Makumbusho ya Taifa la Sierra Leone, huko Freetown. Kadi ya habari yasema hivi: “Aina hii ya fedha ya ajabu ni ya kawaida katika Sierra Leone na Liberia. Ilikuwa ikitumiwa katika mikoa hiyo hadi kufikia 1945. Kwa kuwa ilikuwa ishara ya kichwa (mwisho wa mviringo) na wayo (ncha zilizochongoka) ilitajwa kuwa fedha iliyo na roho. Chifu alipokufa, sarafu nyingi za Wakissi zilivunjwa-vunjwa na kubandikwa kwenye kaburi lake. Thamani ya kubadilishana ya mwisho ilikuwa ni sarafu 50 za Wakissi kwa Shilingi moja ya Afrika Magharibi.”
Kulingana na kitabu The African Slave Trade, kilichoandikwa na Basil Davidson, zamani za kale watumwa walinunuliwa kwa kubadilishana na “vipande vya chuma.” Je, hizo zilikuwa sarafu za Wakissi? Wataalamu fulani wanaamini hivyo. Wengine wanakataa. Hata hivyo, ingawa huenda sarafu hizo hazikutumiwa kununua watumwa, kwa hakika zilitumiwa kununua wake.
Kama inavyoonyeshwa juu, nyakati nyingine sarafu hizi zilitumiwa katika shughuli za kidini, hasa kuhusiana na itikadi isiyo ya Kimaandiko ya kutokufa kwa nafsi. Mtu alipokufa, ilionwa inafaa kumzika katika kijiji cha kwao. Bila shaka, ikiwa kifo kilitukia mbali sana, haikuwezekana sikuzote kuileta maiti nyumbani. Suluhisho lilikuwa kuhamisha nafsi yake kupitia sarafu ya Wakissi.
Mtu wa jamaa wa yule aliyekufa angesafiri kijijini ambako kifo kilitukia na kujipatia sarafu kutoka kwa mganga, ambaye kupitia mizungu, eti angeambatisha nafsi ya mtu huyo aliyekufa kwenye sarafu hiyo. Kisha ilikuwa kazi ya mtu huyo wa jamaa kubeba nafsi hiyo (hiyo sarafu) nyumbani na kuizika katika kaburi la mababa wa kale.
Mtu wa jamaa angeifunga sarafu hiyo katika kitambaa safi na kuanza safari yake, ambayo ilipaswa kukamilishwa akiwa kimya. Iliaminiwa kwamba kama angeliongea na mtu fulani njiani, nafsi ingeiacha sarafu hiyo na kurudi kijijini ambako mtu yule alifia. Kisha mtu wa jamaa angelazimika kurudi na kuichukua tena—bila shaka baada ya kumlipa mganga tena!
Ikiwa ingekuwa lazima azungumze akiwa safarini, mtu wa jamaa angefanya hivyo kama angaliiweka ile sarafu chini kwa uangalifu, kabla ya kuzungumza, ingawa hangeiweka kwenye ardhi. Mara sarafu ilipookotwa tena, ilimbidi awe kimya tena.
Sarafu za Wakissi zilizokuwa na urefu wa inchi 13 hadi 14, hazikufaa kuwekwa mfukoni wala kwenye kibeti. Hata hivyo, muundo wake ulifaa siku zao, kwa kuwa zingeweza kufungwa kwa urahisi katika matita na kubebwa kichwani. Matajiri walihifadhi sarafu hizo katika dari zao. Hali za hewa zilipokuwa nzuri, mtonesho ungefanyizwa kwenye fedha hizo na kutona-tona kwenye chumba kilicho chini. Kiasi cha “mvua” hiyo kilikuwa ishara nzuri ya utajiri wa mtu ambaye ulikuwa umeketi nyumbani kwake.