Miwani Yenye Lenzi Mbili—Ni Nani Aliyekuwa wa Kwanza Kuwa Nayo?
Karne mbili zilizopita, Benjamin Franklin alichukua jozi mbili za vioo, moja ikiwa ni kwa ajili ya kuona mbali na nyingine ya kuona karibu, kisha akakata kila kioo katika sehemu mbili kimlalo. Kisha, akaweka katika fremu moja ile lenzi nusu ya kuona mbali juu ya lenzi nusu iliyo chini ya kuona karibu, na tazama, ikawa jozi ya kwanza ya miwani yenye lenzi mbili!
Leo, maendeleo ya tekinolojia yamefanya iwezekane kutengeneza miwani yenye lenzi mbili kutoka kwa kipande kimoja tu cha kioo, chenye mapindo yenye urefu mbalimbali kwenye sehemu ya juu na ya chini. Na hata kuna miwani zenye lenzi mbili zinazoambatanishwa na mboni. Lakini je, ulijua kwamba mapema kabla sayansi inayoshughulika na miwani haijatokeza miwani yenye lenzi mbili, samaki mmoja asiyejulikana wa maji baridi alikuwa na miwani ‘ya kisasa’ yenye lenzi mbili?
Utampata samaki huyu mwenye urefu wa futi moja, anayefanana na mino na ambaye wanasayansi wanamwita Anableps, katika bahari inayoanzia kusini mwa Mexico hadi kaskazini mwa Amerika Kusini. Umbo lake, kuanzia mkia hadi kwenye shavu halivutii, lakini umbo lake hustaajabisha sana utazamapo mbele ya shavu lake.
Unapowatazama samaki hawa kwa mara ya kwanza huonekana wakiwa na macho manne—mawili yakiwa yanaangalia juu na mawili yakiwa yanaangalia chini—yakiwafanya watu wawaite samaki wenye macho manne. Lakini huo ni udanganyo wa macho. Wana macho mawili makubwa ya duara, lakini kila jicho limegawanywa na ukanda wa ngozi kimlalo katika sehemu mbili. Kwa kuwa samaki hawa huogelea sambamba na uso wa maji, nusu ya sehemu za juu za macho yao hufanana na darubini ambazo hujitokeza juu ya maji kuchunguza anga kikamili, huku sehemu za chini zikibaki majini kuchunguza chini ya maji. Samaki mwenye macho manne hutafuta chakula majini katika njia hii na wakati uleule akiwa macho—au kwa njia bora zaidi, akitumia macho mawili—kutazama ndege wala-samaki wenye njaa walio juu.
Hata hivyo, ili kuangalia chini ya maji, samaki huyu anahitaji lenzi iliyo nene zaidi kuliko anapoangalia hewani. Tatizo hilo hutatuliwaje? Kwa miwani yenye lenzi mbili! Kila jicho huwa na lenzi, yenye umbo la yai na iliyo nene upande wa chini kuliko wa juu. Hivyo kila kitu kilicho chini ya maji huangaliwa kupitia upande ule mnene wa lenzi, huku upande ulio mwembamba ukichunguza anga.
Lakini uwezo wa kuona wenye sehemu mbili wa samaki hawa utakuwa tu mwangavu maadamu wanasafisha lenzi zao. Wao husafishaje lenzi zao? Wakati wowote ule lenzi zikaukapo, samaki hawa hutumbukiza tu vichwa vyao majini na kisha huibuka tena wakiwa na miwani zenye lenzi mbili zinazong’aa. Kwa hakika lenzi hizo zenye kung’aa hudhihirisha hekima ya Muumba wao!
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Painting by Charles Willson Peale/ Dictionary of American Portraits/ Dover
©Dr. Paul A. Zahl, The National Audubon Society Collection/PR
©William E. Townsend, Jr., The National Audubon Society Collection/PR