Ubongo Wako Unaweza Kuutumiaje kwa Njia Bora?
Usomapo maneno haya, ubongo wako wachochea kumbukumbu ambazo zilihifadhiwa miaka mingi ulipojifunza jinsi ya kusoma kwa mara ya kwanza. Lakini ili ufikirie kwa hekima yale ambayo umejifunza, unahitaji kusitawisha uwezo wa ubongo wa kufikiri.
WANASAYANSI wamegundua kwamba miunganisho iliyo kati ya chembe za neva katika ubongo hubadilika-badilika daima. Chembe za neva na miunganisho yake hufa zisipotumiwa au kuchochewa. “Ubongo huboreka kwa matumizi,” yasema ripoti moja ya hivi majuzi. “Kwa watu wanaohangaikia hali ya ubongo wao—au wanaotaka ubongo wao uwe bora—inaonekana shauri zuri ni kutumia ubongo kwa mambo mengi na kufanya mazoezi mengi ya akili.”
Ni Muhimu Kufanya Mazoezi ya Akili
Ili ufahamu vizuri ubora wa “mazoezi mengi ya akili,” ebu ona jambo ambalo wanasayansi wamegundua juu ya watoto wachanga. Watoto wanapozaliwa, huwa si vipofu. Wao huhitaji tu kusitawisha uwezo wa kuona. Mwanzoni, wao wanaweza kuona vizuri vitu vilivyo karibu pekee. Baadaye, wao husitawisha uwezo wa kuona vizuri vitu vyote wanapoanza kutambua tofauti za vitu ambavyo wanaona kwa macho. Lakini jicho moja likifunikwa kwa bendeji wakati wa ukuzi huu, mtoto huyo aweza kukua bila kuona vizuri akitumia jicho hilo. Kwa nini? Kwa sababu vitu vinavyoonwa na jicho lile jingine hujaa kwenye ile visual cortex ya ubongo.
Vitu vya kuchezea ambavyo huchochea upendezi wa mtoto husaidia kutayarisha ubongo ili ufahamu mazingira ya mtoto huyo.
Utafiti wa karibuni pia wadokeza kwamba muziki waweza kusaidia kukuza lugha na stadi za kuchangamana kijamii. Watoto ambao walipata masomo ya ziada ya muziki walikuwa bora katika lugha na walijifunza kusoma kwa urahisi zaidi kuliko wale ambao hawakupata masomo ya ziada ya muziki. Watoto waliopiga muziki pamoja pia walidhihirisha ushirikiano zaidi kati yao.
Ingawa ubongo umegawanyika katika sehemu mbili, kushoto na kulia, kila sehemu inatimiza fungu muhimu. Kwa mfano, upande wa kulia hutusaidia kutambua hisia na kuelewa sauti. Hata hivyo, pande hizo mbili zinashirikiana. Ripoti moja yasema kwamba wanafunzi wa muziki walipoanza masomo, kusikiliza muziki kulichochea hasa upande wa kulia wa ubongo. Miaka mitatu baadaye, baada ya kufundishwa muziki kindani na jinsi unavyotungwa, upande wa kushoto wa ubongo ulikuwa ukichanganua yale waliyoyasikia. Basi, mazoezi ya akili yanahitajiwa ili kuchochea ubongo wote ili sehemu za uchanganuzi na za kihisia-moyo zihusike pia.
“Kutumia Ubongo kwa Mambo Mengi”
Watu wengi wamejifunza kanuni za dini ya familia yao. Lakini walipoanza kusababu juu ya mafundisho ya makanisa hayo, wao waliona kwamba mambo hayapatani wakaona kwamba hakuna kusudi halisi. Jambo hilo limewafanya wengine watafute kanuni za itikadi ambazo zinawapa majibu ya maswali yao na vilevile kuwapa tumaini thabiti kwa wakati ujao.
“Maisha yangu yalikuwa yamejaa maumivu mengi na matatizo mengi, tangu ujana na kuendelea,” aeleza Jean. “Ijapokuwa nilikuwa mfuasi wa dini ya Kanisa la Uingereza, sikupata mwongozo wala amani ya akili. Mafundisho mengi ya kanisa yalinisumbua—kwa mfano, moto wa helo na hali ya wafu. Makasisi waliniambia kwamba ni lazima Mungu awe ananiadhibu.
“Basi nikaamua kuacha Kanisa la Uingereza, na baadaye nikaolewa na mtu ambaye hakuwa mfuasi wa dini yoyote. Ujeuri wake nyumbani ulinisononesha sana.” Jean akaamua kujiua. Lakini kabla ya kujiua, alitoa sala moja ya mwisho kwa Mungu. Pindi iyo hiyo, mlango ulibishwa. Alipofungua mlango, alipata wanawake wawili ambao walikuwa Mashahidi wa Yehova. Walizungumza kuhusu uhai kuwa una kusudi wakampa Jean kichapo cha Biblia ili kimsaidie ajifunze zaidi.
“Baada ya hao kuondoka,” Jean akaendelea kusema, “niliingia ndani nikaanza kusoma kitabu hicho mara moja. Nikahisi kana kwamba nimefumbuliwa macho na sasa ningeweza kuona kwa mara ya kwanza. Kadiri nilivyosoma, ndivyo nilivyoendelea kuona kwamba hii ni kweli.” Jean alikuwa amepata chakula chenye kuridhisha akili yake.
Kitabu cha Biblia cha Mithali chakazia ubora wa ufahamu na hekima ya kimungu. Lakini, ili mtu azipate ni lazima atie bidii na awe na tamaa ya kujifunza kuhusu Mungu. Mithali sura ya 2 yatoa mwito huu: “Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, na kuyaweka akiba maagizo yangu; hata ukatega sikio lako kusikia hekima, ukauelekeza moyo wako upate kufahamu; naam ukiita busara, na kupaza sauti yako upate ufahamu; ukiutafuta kama fedha, na kuutafutia kama hazina iliyositirika; ndipo utakapofahamu kumcha BWANA, na kupata kumjua Mungu. Kwa kuwa BWANA huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.”—Mithali 2:1-6.
Mwalimu William Lyon Phelps aliandika hivi kuhusu Biblia: “Kila mtu ambaye anajua Biblia kabisa aweza kwa kweli kuitwa mtu aliyeelimika.” Wasiliana na Mashahidi wa Yehova wa kwenu au uandike barua ukitumia anwani iliyo karibu zaidi na wewe kwenye ukurasa wa 5. Wao watafurahi kukusaidia ujue jinsi Biblia iwezavyo kuyajibu maswali yako na kukuandalia mambo mengi ya kufikiria akilini. Tumia uwezo wa ubongo wako wa kufikiri ili uelewe kiolezo cha kweli ambacho Biblia inataja. Kutumia ubongo wako kwa njia bora kwaweza kufanya upate furaha ya milele.