Euro Fedha Mpya kwa Bara la Zamani
AZIRI wa fedha wa Ufaransa akiwa na shangwe aliuma sarafu mpya na kutangaza hivi: “Hii ni fedha halisi, si ya kuigiza. Ndiyo ya kwanza kutokezwa Ufaransa na vilevile katika Ulaya.” Sarafu hiyo ilikuwa ndiyo euro ya kwanza kutengenezwa kwenye kiwanda rasmi cha kutengenezea sarafu cha Ufaransa. Ilikuwa Jumatatu, Mei 11, 1998.
Euro ni nini? Wake nyumbani, wafanyakazi, watalii na wafanyabiashara Ulaya kote wataathiriwaje nayo? Je, itaathiri kwa vyovyote uchumi wa tufeni pote? Kabla hujatupa deutsche mark, lira, au faranga zako, huenda ukafanya vema kupata majibu ya maswali haya.
Wazo Hilo Lilitokeaje?
Mkataba wa Maastricht ulipogeuza Jumuiya ya Ulaya kuwa Muungano wa Ulaya (EU), mnamo Novemba 1, 1993, mmojawapo wa miradi mikuu ulikuwa kuanzisha aina moja ya fedha itakayotumiwa na mataifa washiriki.a Tangu nyakati za Waroma, Ulaya haijawa na fedha iliyotumika kote kama hiyo. Iliamuliwa kwamba jina la fedha hiyo mpya litakuwa euro. Si nchi zote za EU zinazoshiriki katika muungano huu wa kifedha. Ni nchi 11 tu kati ya 15 za EU ambazo sasa zinaweza kutumia euro. Nchi hizi ni Austria, Finland, Hispania, Ireland, Italia, Luxembourg, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, na Ureno. Ugiriki haikutimiza viwango vya kiuchumi ili kuwa mshiriki. Zile nyingine tatu—Denmark, Sweden, na Uingereza—zimekataa kushiriki kwa wakati huu.
Euro itaanza kutumiwa hatua kwa hatua. Kuanzia Januari 4 mwaka huu, euro ilianza kutumiwa katika masoko ya kimataifa ya kubadilisha fedha katika ubadilishaji usiohusisha fedha halisi. Sarafu na noti za euro zitatolewa katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari 1, 2002—ambapo baada ya hapo sarafu za zamani za nchi washiriki huenda zikaacha kutumiwa kabisa na labda kuwekwa kwenye majumba ya makumbusho na kuwa vitu vya ukumbusho. Imekadiriwa kwamba euro itachukua mahali pa noti bilioni 12 na sarafu bilioni 70, zote zikiwa na uzito wa tani 300,000. Inatumainiwa kwamba baada ya muda, nchi zinazobakia za EU pia zitaweza kujiunga na wanachama wa aina moja ya fedha.
Waziri wa fedha wa Austria alisema hivi juu ya badiliko kuelekea euro: “Tuko mwanzoni mwa enzi mpya ya kuunganisha Ulaya.” Hata hivyo, katika Ulaya maoni ya umma kuhusu euro yanatofautiana kati ya wale asilimia 47 wanaohisi kwamba fedha hiyo moja itafanya Ulaya iwe na nguvu sana kiuchumi na wale asilimia 40 wanaoamini kwamba euro itaharibu uchumi wa Ulaya. Wengine hata wamedokeza kwamba aina moja ya fedha yaweza kuongoza kwenye vita! Pia kuna wale ambao hawajaamua wanaotilia shaka euro, na ambao wanaona faida ya kuwa na aina moja ya fedha katika Ulaya lakini wanatilia shaka mafanikio yake ya baadaye.
Wengine Wanaiona Kuwa Baraka . . .
Baraza kuu zaidi la EU, Tume ya Ulaya, limetangaza hivi: “Kwa kuanzisha aina moja ya fedha, bara la Ulaya litakuwa limewapa raia zake, watoto wake na wenzake . . . ishara halisi ya uchaguzi unaofaa wote ambao umefanywa kwa hiari: ule wa kujenga jumuiya juu ya msingi wa amani na ufanisi.”
Watetezi wa euro wanataja manufaa mengi yanayoweza kupatikana kwa kuwa na aina moja ya fedha. Jambo kuu litakaloathiriwa ni kuondolewa kwa gharama za ubadilishaji wa fedha za kigeni. Nyakati nyingine kielelezo kinachotolewa ni cha msafiri wa Ulaya anayezuru nchi zote 14 za EU mbali na nchi yake. Mathalani, ikiwa anaanza na deutsche mark 1,000 na kubadili pesa zake katika kila nchi, mwishowe atabaki na mark 500 kwa sababu ya gharama ya kubadili fedha peke yake!
Hali kadhalika, vitu vinavyouzwa nje ya nchi na kuingizwa ndani ya nchi havitakuwa na gharama ya ubadilishaji wa fedha za kigeni. Vivyo hivyo, aina moja ya fedha itaondoa gharama isiyokuwa ya moja kwa moja ya kupanda na kushuka kwa thamani ya fedha. Pesa za nchi zinapopoteza thamani, bidhaa zinazotoka nje huwa ghali zaidi katika nchi hiyo. Mara nyingi hali hii huongoza kwenye inflesheni. Hivyo, kwa kutumia aina moja ya fedha, bila kuwepo kwa hatari ya ubadilishaji wa fedha za kigeni, Ulaya itavutia zaidi watega-uchumi wa kigeni.
Pia watetezi wa euro wanaona kwamba bei katika Ulaya zitashuka. Wateja na mashirika ya biashara sasa wanaweza kulinganisha bei kwa urahisi, na wakati sarafu na noti za euro zitakapoanzishwa mwaka wa 2002, itakuwa rahisi hata zaidi. Tofauti ya bei ya bidhaa ileile katika sehemu mbalimbali za Ulaya inatazamiwa kupungua, jambo litakalomnufaisha mteja.
. . . Wengine Wanaiona Kuwa Laana
Wachambuzi wanatoa maoni yao. Wanahisi kwamba euro itabana uchumi wa Ulaya, ikiharibu uwezo wake wa kupanuka na kuzuia ukuzi wake. Wanatabiri kwamba aina moja ya fedha itaongeza ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, itachochea makisio mengi kwenye masoko ya hisa, na kusababisha msukosuko wa kisiasa. Tayari msukosuko huo wa kisiasa umeanza kuonekana. Chukua kwa mfano, bishano kati ya Ujerumani na Ufaransa kuhusu ni nani anayepaswa kuwa kiongozi wa Benki Kuu ya Ulaya, ambayo inasimamia euro. Mabishano zaidi kama hilo yaweza kutazamiwa kila mshiriki wa EU anapofuatia mambo yake mwenyewe.
Katika nchi kadhaa za EU, kwa sasa ukosefu wa kazi ya kuajiriwa umefikia kiwango cha juu zaidi. Wengi wanalaumu wakisema kwamba hali hiyo imesababishwa na kupunguzwa kwa matumizi na kuongezwa kwa kodi kunakohitajiwa ili kujipatanisha na masharti yanayotakikana ili kutumia aina moja ya fedha. Katika Ulaya kote watu wanateta dhidi ya sera kali za kiuchumi zinazotia ndani kupunguza sana mpango wa kutoa huduma za jamii, malipo ya uzeeni, na programu za utunzaji wa afya. Hizo sheria kali za kiuchumi zinaweza kudumu kwa muda mrefu kadiri gani? Je, nchi fulani zitashindwa kushikilia sheria hizi baada ya euro kuanza kutumiwa kihalisi? Je, sera hiyo iliyolegezwa itaharibu mfumo wa aina moja ya fedha wa Ulaya?
Wengine wanataja ufungamano wa kihisia ambao watu huwa nao kuelekea fedha ya nchi yao. Fedha ni yenye maana zaidi kuliko pesa ulizo nazo. Kwa wengi, hiyo pia ni historia ya nchi yao, ishara ya maana kama vile bendera. Fedha ya kitaifa ni njia fulani ya mawasiliano ambayo kupitia hiyo watu huchuma, huhesabu, hukadiria, hujadiliana juu ya bei, na huweka akiba. Kwa kielelezo, huku Wajerumani wakiona takwimu kwenye akaunti zao za benki zikipungua kufikia nusu baada ya kubadilishwa na euro, takwimu za Italia zitapungua sana kwa tarakimu 2,000 euro itakapochukua mahali pa lira. Kulingana na uchunguzi mmoja, badiliko kuelekea euro litakuwa jambo lenye “kufadhaisha” Wanaulaya wengi.
Je, Aina Moja ya Fedha Itawafaa Wote?
Wataalamu fulani wa mambo ya kiuchumi katika EU na Marekani wanakazia kwamba ijapokuwa kuna nia kubwa ya kisiasa ya kuwa na aina moja ya fedha, uchumi wa Ulaya umegawanyika, watu wake wamejiimarisha katika nchi zao, na tamaduni zao zinatofautiana sana. Hivyo, tofauti na wakazi wa Marekani, watu katika Ulaya wanaopoteza kazi zao hawawezi kuondoka tu na kusafiri mbali ili kutafuta kazi. Wataalamu fulani wanaamini kwamba migawanyiko hii hunyima mataifa yanayotumia euro njia zinazohitajiwa kutatua matatizo ya mahali pao ili kushiriki katika mfumo wa kiuchumi na aina moja ya fedha.
Chini ya mfumo wa aina moja ya fedha, wachambuzi wanasema kwamba serikali mojamoja zitapoteza uwezo wao wa kubadilikana katika kushughulikia matatizo ya kiuchumi. Wanasema kwamba euro itaondoa uwezo wa serikali mojamoja na kuipatia uwezo Benki Kuu mpya ya Ulaya, katika Frankfurt, Ujerumani. Hatimaye, jambo hili litaongeza msongo wa kuratibu sheria za kodi na sera nyinginezo za kiuchumi katika bara lote. Wachambuzi wanadai kwamba mabaraza ya kutekeleza na kutunga sheria katika Brussels na Strasbourg yatapata uwezo. Kwa kweli, Mkataba wa Maastricht unataka kuwepo muungano wa kisiasa ambao hatimaye utakuwa na daraka juu ya sera za kigeni na za kujihami na vilevile sera za kiuchumi na kijamii. Je, badiliko hili litakuwa bila magumu na matatizo yoyote? Kupita kwa wakati kutaonyesha.
“Kamari Kubwa Mno”
Wakati huohuo, benki na maduka makubwa tayari yanaanza kufanya mabadiliko kuelekea euro, yakianzisha akaunti za euro na kuweka bei za euro kando ya zile za fedha zao. Lengo ni kufanya badiliko katika mwaka wa 2002 liwe bila matatizo kwa kadiri iwezekanavyo. Gazeti la Kifaransa linalopendwa tayari limegawanya zaidi ya vikokotoo 200,000 vyenye programu ya kubadilisha faranga za Ufaransa kuwa euro.
Je, siku moja euro itakuwa na uwezo sawa na dola ya Marekani? Wengi wanahisi kwamba baada ya euro kukubaliwa, labda Marekani haitatawala kwa urahisi uchumi wa ulimwengu. Wanatabiri kwamba euro itakuwa fedha ya kutumiwa tufeni pote kando ya dola. Jill Considine, wa New York Clearing House Association, asema kwamba: “Kutakuwa na eneo jipya la mashindano.”
Wakati ujao wa euro utakuwaje? Mhariri Mjerumani Josef Joffe aiita euro “kisio kubwa zaidi ya Ulaya” na “kamari kubwa mno.” Aongezea hivi: “Ikikosa kufaulu, huenda ikaharibu mafanikio mengi ambayo Ulaya imepata katika miaka 50 iliyopita.” Waziri wa fedha wa Ufaransa alirudia maoni ya Wanaulaya wengi aliposema: “Kuna matumaini makubwa sana na hofu nyingi sana.”
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi kuhusu Jumuiya ya Ulaya, ona toleo la Amkeni! la Februari 22, 1979, ukurasa wa 4-8, Kiingereza, na la Desemba 22, 1991, ukurasa wa 20-24, Kiingereza.
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
MAMBO YANAYOHUSU EURO
● Euro moja ina thamani inayozidi kidogo dola moja ya Marekani
● Kutakuwa na aina saba za noti za euro: euro 5, 10, 20, 50, 100, 200, na 500
● Upande mmoja wa noti za euro utakuwa na ramani ya Ulaya ikiwa na madaraja kadhaa ya kawaida, na kwenye upande mwingine, mifano ya madirisha au njia
● Maneno “EURO” na “ΕΥΡΩ” yataonekana kwenye noti za benki, kuwakilisha herufi za Kiroma na Kigiriki
● Kutakuwa na aina nane za sarafu za euro: 1, 2, 5, 10, 20, na senti 50 na vilevile euro 1 na 2
● Sarafu zitakuwa na ramani ya Ulaya kwenye upande mmoja na ishara ya kitaifa kwenye upande mwingine
[Ramani katika ukurasa wa 13]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MUUNGANO WA ULAYA
UINGEREZA
DENMARK
SWEDEN
UGIRIKI
Washiriki wa sasa katika muungano wa kifedha
IRELAND
URENO
HISPANIA
UBELGIJI
UFARANSA
UHOLANZI
UJERUMANI
LUXEMBOURG
FINLAND
AUSTRIA
ITALIA
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]
Sarafu zote kwenye ukurasa wa 12 hadi 14: © European Monetary Institute