Uigizaji-Vitu—Tatizo la Ulimwenguni Pote
Hadi mwishoni mwa karne ya 18, katika Ufaransa watu walikuwa wakichemshwa wangali hai kwa sababu ya kosa hilo. Kuanzia 1697 hadi 1832, katika Uingereza, kosa hilo lilikuwa uhalifu ambao adhabu ilikuwa kifo, na tendo hilo lilionwa kuwa uhalifu dhidi ya serikali. Zaidi ya Waingereza 300 walinyongwa kwa sababu yalo, huku idadi zisizohesabika zikihamishwa hadi kwenye koloni ya adhabu katika Australia ili kufanya kazi ngumu ikiwa adhabu.
KWA zaidi ya miaka 130, serikali ya Marekani imekuwa ikifunga wale wenye hatia ya kosa hilo hadi miaka 15 katika magereza ya serikali. Na zaidi, maelfu ya dola yakiwa faini yamekuwa yakitozwa ili kuongezea hiyo adhabu. Hata leo hii, bado adhabu ya kifo inatolewa katika Urusi na China.
Licha ya hizo adhabu kali zinazoamriwa na mataifa mengi, uhalifu huo bado waendelea. Hata hofu ya kifo haijatosha kuzuia mipango ya kuwa-tajiri-haraka ya wale walio na stadi za kiufundi zinazohitajiwa. Wakuu wa serikali wamefadhaika. “Itakuwa vigumu kupata kizuizi kifaacho,” wao husema, “kama ambavyo imekuwa kwa karne nyingi.”
Uigizaji-vitu! Mmojawapo uhalifu wa kale zaidi katika historia. Mwishoni mwa karne hii ya 20, umekuwa tatizo la ulimwenguni pote na waendelea kuongezeka. Robert H. Jackson, hakimu mshirika wa Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani, alisema hivi kuuhusu: “Uigizaji-vitu ni kosa ambalo halifanywi kiaksidenti kamwe, wala kwa kutojua, wala kwa msukumo wa tamaa, wala kwa sababu ya umaskini wa kupindukia. Ni uhalifu uliobuniwa kwa ustadi na mtu ambaye ana ustadi wa kiufundi na anayetumia fedha nyingi sana kwa vifaa.”
Kwa kielelezo, fedha za Kimarekani zinatokezwa kinyume cha sheria ulimwenguni pote na kwa kiwango kikubwa zaidi ya wakati mwingineo wote. “Fedha za Kimarekani,” akasema msemaji mmoja wa Idara ya Hazina, “sizo fedha zenye kutamanika tu kuliko zote ulimwenguni. Pia hizo ndizo zilizo rahisi zaidi kuigizwa.” Kile ambacho kimefadhaisha serikali ya Marekani ni kwamba nyingi za noti hizo bandia zinatengenezwa nje ya Marekani.
Fikiria hili: Katika 1992, noti bandia zenye thamani ya dola milioni 30 zilikamatwa ng’ambo, likaripoti gazeti Time. “Mwaka uliopita jumla ilifikia dola 120 milioni, na inatarajiwa kuvunja rekodi hiyo katika mwaka wa 1994. Kiwango kikubwa zaidi ya hicho huenezwa bila kugunduliwa,” likaripoti hilo gazeti. Tarakimu hizi hazielezi habari kamili. Inaaminiwa na wataalamu wa tatizo la uigizaji-vitu kwamba jumla ya noti bandia zinazoenezwa nje ya Marekani yaweza kuwa juu sana kufikia dola bilioni kumi.
Kwa kuwa fedha za Kimarekani zinatamaniwa sana na nchi nyingi—hata kuliko fedha zazo zenyewe—na kwa kuwa ni rahisi sana kuzinakili, mataifa mengi na watu wafanyao mambo kichinichini wanazitengeneza. Katika Amerika Kusini, walanguzi wa dawa za kulevya wa Kolombia wamekuwa wakiigiza fedha za Kimarekani kwa miaka mingi ili kuongeza mapato yao yasiyo halali. Sasa nchi fulani za Mashariki ya Kati zinakuwa washirika wakubwa katika biashara ya duniani kote ya kuigiza vitu, likaripoti U.S.News & World Report. Hilo gazeti liliongeza kwamba moja ya nchi hizo “inatumia njia tata za uchapaji zinazoiga zile zinazotumiwa na Idara ya Hazina ya Marekani. Likiwa tokeo, [inaweza] kutengeneza noti bandia za dola 100 zinazoitwa ‘noti bora zaidi,’ ambazo zaelekea kutoweza kugunduliwa kabisa.”
Watu katika Urusi, China, na nchi nyinginezo za Asia pia wanajiunga na utengenezaji wa fedha bandia—hasa fedha za Kimarekani. Inashukiwa kwamba asilimia 50 ya fedha za Kimarekani zinazoenezwa katika Moscow leo ni bandia.
Baada ya Vita ya Ghuba, katika 1991, kulipokuwa na uenezaji wa mamilioni ya dola za Kimarekani, “wanabanki wa kimataifa walishtuka kupata kwamba asilimia 40 ya noti za dola 100 zilikuwa bandia,” likasema Reader’s Digest.
Ufaransa ina matatizo yayo yenyewe yanayohusu fedha bandia, sawa na nchi nyinginezo nyingi za Ulaya. Kuigiza fedha si tatizo la Marekani pekee, kama mataifa mengine duniani pote yawezavyo kutoa ushahidi.
Kuigiza Vitu Kwarahisishwa
Hadi kufikia miaka kadhaa iliyopita, ilichukua mafundi wa kisiri—wasanii, wachoraji stadi, wakata nakshi, na wachapishaji—saa nyingi za kazi yenye kuchosha kunakili fedha za taifa lolote, ikitokeza, nakala hafifu za fedha halisi. Hata hivyo, leo, kukiwa na mashine za kufanya nakala za tekinolojia ya hali ya juu zenye rangi nyingi, mashine za kuchapa pande zote mbili za karatasi, na vifaa vinavyorekodi picha kwenye karatasi kwa kutumia miale vinavyopatikana katika maofisi na nyumbani, inawezekana kiufundi kwa yeyote kufanya nakala za fedha anazotaka.
Enzi ya kuigiza vitu kwa kutumia kompyuta imefika! Kile ambacho wakati mmoja kilihitaji stadi za wachoraji na wachapishaji wataalamu sasa kinaweza kufanywa na wafanyikazi wa ofisini na watu walio na kompyuta nyumbani. Mifumo ya uchapishaji ya kompyuta ndogo sana za kibinafsi ambayo haigharimu zaidi ya dola 5,000 yaweza kutengeneza fedha bandia ambazo zaweza kuwa vigumu sana kugunduliwa hata na wataalamu waliozoezwa. Hii ingeweza kumaanisha kwamba mtu ambaye anahitaji fedha anaweza kuepuka kisafari cha kwenda banki kwa kuchapisha fedha zake mwenyewe—na kwa thamani itakayotosheleza mahitaji yake! Tayari mifumo hii ni vifaa vyenye nguvu mikononi mwa watengenezaji wa leo wa vitu vya kuigiza. “Wanapofanya hivyo, wahalifu hawa wenye akili wanashinda mamlaka za kutekeleza sheria na siku moja wangeweza kutokeza hatari kwa fedha zenye thamani kubwa sana ulimwenguni,” likaandika U.S.News & World Report.
Kwa kielelezo, katika Ufaransa, asilimia 18 ya Franka milioni 30 (dola milioni 5, za Kimarekani) za fedha bandia zilizokamatwa katika 1992 zilitengenezwa kwenye mashine za ofisini. Ofisa mmoja wa Banque de France aona hili kuwa tisho si kwa mfumo wa kiuchumi tu bali pia kwa itibari ya umma katika serikali. “Watu wajuapo kwamba unaweza kuigiza noti iliyo halali kwa tekinolojia inayopatikana kwa watu wengi, itibari yaweza kutoweka,” akaomboleza.
Ikiwa sehemu ya jitihada ya kupambana na wingi wa fedha bandia katika Marekani na nchi nyinginezo, namna mpya za noti za banki ziko katika hatua ya kutengenezwa, na katika nchi fulani noti mpya tayari zinaenezwa. Kwa kielelezo, kwenye fedha za Kimarekani, ile picha ya Benjamin Franklin kwenye noti ya dola 100 itaongezwa ukubwa kwa nusu na itasogezwa robo tatu za inchi kwenda upande wa kushoto. “Mabadiliko mengine 14 katika michoro na maumbo mengineyo ya kisiri ya kusaidia usalama yatawekwa pia,” likaripoti Reader’s Digest. Mabadiliko mengine mengi, kama vile alama na wino ambazo hubadilika rangi zinapoangaliwa kutoka pembe tofauti, yanafikiriwa.
Kwa muda fulani Ufaransa imekuwa ikiingiza vizuizi vipya katika namna zayo za noti za banki ambavyo, yatumainiwa, vitakinza kwa kiwango fulani watengenezaji wa fedha bandia. Hata hivyo, msemaji wa Banque de France akiri kwamba “bado hakuna njia madhubuti kabisa ya kiufundi ya kushinda wawezao kuwa watengenezaji wa noti bandia, lakini,” akaongeza, “sasa twaweza kuunganisha vizuizi vingi sana katika noti ya banki yenyewe hivi kwamba ni kazi [ngumu], na yenye gharama sana kuigiza.” Yeye afafanua vizuizi hivi kuwa “hatua ya kwanza ya kulinda dhidi ya uigizaji.”
Ujerumani na Uingereza zimekuwa zikifanya mabadiliko ya usalama katika fedha zazo kwa muda fulani sasa kwa kuongeza nyuzi za usalama ambazo hufanya iwe vigumu zaidi kufanya nakala ya fedha zao. Noti ya Kanada ya dola 20 ina mraba mdogo wenye kung’aa unaoitwa kifaa cha usalama cha kinuru, ambacho hakiwezi kuigizwa kwenye mashine za kufanyia nakala. Australia ilianza kuchapisha noti za banki za plastiki katika 1988 ili kutia maumbo ya kusaidia usalama ambayo haingewezekana kutiwa katika karatasi. Finland na Austria hutumia jaribosi za msambazo kwa noti. Hizi humetameta na kubadilika rangi kama ifanyavyo hologramu. Hata hivyo, watu wenye mamlaka serikalini wanahofu, kwamba haitawachukua watengenezaji wa fedha bandia muda mrefu kufanya marekebisho yanayohitajiwa ili kuendeleza utendaji wao wa kihalifu—kwamba haidhuru ni hatua zipi za kurekebisha zichukuliwazo, jitihada zao za uvumbuzi huenda zikakosa kuwa na matokeo kama ambavyo zimekuwa wakati uliopita. “Ni kama usemavyo ule msemo wa kale,” akasema ofisa mmoja wa Idara ya Hazina, “unajenga ukuta wa futi nane, na jamaa wabaya wanajenga ngazi ya futi kumi.”
Kuchapisha fedha bandia ni upande mmoja tu wa ubingwa wa mtengenezaji wa vitu vya kuigiza, kama makala zifuatazo zitakavyoonyesha.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
Mifumo ya uchapishaji ya kompyuta ndogo sana za kibinafsi ambayo haigharimu zaidi ya dola 5,000 yaweza kutengeneza fedha bandia ambazo zaweza kuwa vigumu sana kugunduliwa hata na wataalamu waliozoezwa