Kadi za Mkopo na Hundi za Malipo—Halisi au Bandia?
ZINAFAA kama nini! Ndogo mno, rahisi mno kubeba. Zatoshea vizuri sana katika pochi ya mwanamume au katika kibeti cha mwanamke. Bila hata ndururu mfukoni mwako, unaweza kununua vitu vingi mno. Utumizi wa kadi za mkopo unatiwa moyo na makampuni ya ndege, meli, mahoteli, na makao ya starehe ya waenda likizo ulimwenguni pote. Watu wanashauriwa hivi: “Usiondoke nyumbani bila hiyo.” Biashara fulani huona ni afadhali kukubali kadi za mkopo kuliko fedha taslimu. Tofauti na fedha taslimu, hizo zikiibwa au kupotea, nyingine zaweza kutolewa badala yazo. Ni fedha zako mwenyewe zilizofanywa kuwa za kibinafsi, zikiwa na jina lako na nambari ya akaunti ikiwa imetiwa nakshi upande wa mbele wa kadi.
Nyingi mwazijua kuwa fedha za plastiki—kadi za mkopo na za kutozwa. Katika 1985 banki fulani zilianzisha hologramu zazo zenyewe zilizobuniwa kwa leza, ambazo zaonekana kana kwamba zina pande tatu, na zenye maumbo mengine ya kusaidia usalama, kuanzia mfumo wa kipekee wa viishara katika ukanda wa kismaku unaopita nyuma hadi alama isiyoweza kuonekana isipokuwa chini ya nuru ya kiukaurujuani. Yote hayo ni kwa ajili ya kuzuia uigizaji! Inakadiriwa kwamba zaidi ya kadi za mkopo milioni 600 zinatumiwa duniani pote.
Inafikiriwa kwamba hasara ya ulimwenguni pote kutokana na aina tofauti za kadi za mkopo za ulaghai katika miaka ya mapema ya 1990 ilikuwa angalau dola bilioni moja. Kati ya namna hizo tofauti, uigizaji unaripotiwa kuwa wenye kuongezeka kwa haraka zaidi—angalau kwa asilimia 10 ya hasara zote.
Kwa kielelezo, katika 1993, uigizaji uligharimu banki zinazoshirikiana na moja ya kampuni kubwa zaidi zenye kutoa kadi za mkopo dola 133.8 milioni, ongezeko la asilimia 75 kuliko mwaka uliotangulia. Kampuni nyingine kuu ya kadi za mkopo, yenye ukubwa wa kimataifa, pia iliripoti hasara zenye kushangaza kwa sababu ya uigizaji. “Hilo lafanya uigizaji wa kadi kuwa tatizo kubwa si kwa banki, kampuni za kadi na wanabiashara wanaozikubali kwa malipo tu bali pia kwa wateja ulimwenguni pote,” likaandika gazeti moja la habari la New Zealand. Ingawa wenye kadi halali si wenye kusababisha hasara hizo, kwa wazi gharama hupitishwa kwa wateja.
Namna gani maumbo ya kusaidia usalama yaliyofanyizwa ndani ya kadi ambayo yalikuwa kama kizuizi kwa waigizaji—kama vile hologramu zilizobuniwa kwa leza na kanda za kipekee zenye mfumo wa kismaku? Kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya maumbo hayo kuanzishwa, kadi za kwanza zilizoigizwa za hali ya chini zilianza kutokea. Muda mfupi baada ya hapo, maumbo yote ya kusaidia usalama yaliigwa au kufichuliwa kwa wahalifu. “Ni lazima sikuzote mboreshe,” akasema ofisa mmoja wa banki wa Hong Kong. “Wahalifu sikuzote hujaribu kuwashinda kiakili.”
Kwa kupendeza, nusu ya hasara zote zilizotokana na uigizaji wa kadi katika miaka ya mapema ya 1990 zilitokea katika Asia, kulingana na wataalamu, na karibu nusu yazo zilifuatiwa hadi Hong Kong. “Kama tu vile Paris lajulikana sana kwa kutengeneza mavazi ya fashoni ya juu ndivyo Hong Kong ilivyo na sifa mbaya ya kutengeneza kadi bandia za mkopo,” akatangaza mtaalamu mmoja. Wengine wameshutumu Hong Kong kwa kuwa jiji lenye kutokeza ulimwenguni la kitovu cha duniani pote cha utendaji wa kihila katika uigizaji wa kadi za mkopo hilo latia ndani Thailand, Malasia na sasa kusini mwa China. “Polisi wa Hong Kong wanasema kwamba vikundi vya huko vinavyohusiana na vikundi vilivyopangwa vya Wachina vya uhalifu wa kisiri huchora, kukata nakshi na kubadili kadi bandia vikitumia nambari zilizotolewa na wachuuzi wafisadi. Kisha wanapeleka tu kadi bandia ng’ambo,” likaripoti hilo gazeti la habari la New Zealand.
“Mashine ya kukata nakshi kwenye kadi ya mkopo, iliyonunuliwa [katika Kanada] na washiriki wa genge la Asia, sasa inatumika kutengeneza kadi bandia za mkopo. Mashine hiyo huchapisha kadi za mkopo 250 kwa saa moja, na polisi wanaamini kwamba imetumiwa kwa ulaghai wa mamilioni ya dola,” likaripoti gazeti la habari la Kanada Globe & Mail. Kwa miaka michache iliyopita, Wachina wa kutoka Hong Kong wameshikwa wakitumia kadi bandia za mkopo katika angalau nchi 22 kutoka Austria hadi Australia, kutia ndani Guam, Malasia, na Uswisi. Kadi za mkopo za Japani ndizo hasa zinatafutwa, kwa kuwa hizo hutoa kiwango cha juu sana cha mkopo kwa watumizi wazo.
Ongezeko hili katika visa vya udanganyifu wa uigizaji wa kadi za mkopo humaanisha kwamba “wenye kuzitoa wanalazimika kusambaza miongoni mwa watumizi wazo gharama ya kiwango kinachoongezeka cha ulaghai,” akasema ofisa mmoja wa banki wa Kanada. Kwa kuhuzunisha, ndilo jambo linalotukia. Kwa kweli huenda kadi ya mkopo ikafaa na kusaidia sana wakati mtumizi wayo hana fedha taslimu za kutosha. Hata hivyo, kumbuka kwamba kitu tu wanachohitaji waigizaji ni nambari yako ya akaunti na tarehe ya kumalizika kwa kadi nao wanaingia kazini. “Ni fedha za plastiki,” akaonya mkuu mmoja wa usalama wa mkoa wa American Express International, “lakini watu hawajaanza kuzitumia kwa busara kama wanavyozitumia fedha taslimu.”
“Udhaifu mwingi umejaa katika mfumo wa kadi za mkopo,” akasema msimamizi mmoja wa polisi. “Na walaghai wamepata udhaifu wa huo mfumo. Na lo, wametumia udhaifu huo kwa ukatili,” akasema kuhusu waigizaji-vitu.
Uigizaji wa Hundi
Kukiwa na enzi mpya ya uchapishaji wa kikompyuta ambao waweza kufanya nakala ya karibu kila noti bila kasoro, kile kilichofuata kilikuwa kisichoepukika. Waigizaji-vitu wangeweza sasa kufanya nakala za hati aina nyingi mno: pasipoti, vyeti vya kuzaliwa, kadi za uhamiaji, vyeti vya umiliki wa hisa, vyeti vya ruhusa ya kufanya biashara, agizo la daktari la kupokea dawa, na hati nyinginezo nyingi. Lakini faida kubwa kuliko zote ingechumwa kutokana na kufanya nakala ya hundi za malipo.
Ufundi huo ni rahisi ajabu. Mara hundi ya malipo kutoka kampuni kubwa yenye mamilioni ya dola akibani katika banki za mahali fulani au zilizoenea taifani ipatikanapo na mtengenezaji wa vitu vya kuigiza, yuko tayari kuiigiza. Kwa mashine yake ya kuchapisha ya juu ya dawati, mashine iwezayo kusoma mwandiko wa mkono na kufanya nakala, na vifaa vingine vya kielektroni vipatikanavyo kwa utayari, yeye anaweza kubadili hundi hiyo ifae kusudi lake mwenyewe—akibadili tarehe, kufuta jina la mwenye kulipwa na kuweka lake, na kuongeza sufuri kadhaa kwenye kiasi cha dola. Kisha anachapa hundi hiyo iliyobadilishwa kwenye mashine yake mwenyewe ya kuchapia ya leza, akitumia karatasi aliyonunua kwenye duka la vifaa vya ofisini lililo karibu yenye rangi sawa na hiyo hundi. Akichapa hundi bandia nyingi, au zaidi kwa wakati mmoja, yeye aweza kwenda kutoa fedha kwenye tawi lolote la banki hiyo katika jiji lolote.
Ongezeko la uigizaji wa hundi kwa njia hii rahisi na isiyo ghali ni kubwa sana, wanasema maofisa wa banki na wa kutekeleza sheria, hivi kwamba gharama ya uchumi ingefika dola bilioni moja. Katika kisa kimoja chenye ujasiri mno, likaripoti The New York Times, genge lenye makao katika Los Angeles lilisafiri kote nchini likitoa fedha kwa hundi bandia za malipo kwenye banki mbalimbali, fedha hizo zikifikia zaidi ya dola milioni mbili. Wachanganuzi wa viwanda wanakadiria kwamba gharama ya jumla ya kila mwaka ya ulaghai wa hundi sasa ni dola bilioni kumi katika Marekani pekee. “Tatizo la uhalifu Na. 1 kwa mashirika ya kifedha,” akasema ofisa mmoja wa FBI, “ni vifaa viwezavyo kubadilishwa, kama vile ulaghai wa hundi na wa hawala za fedha.”
Akisema juu ya uigizaji-vitu wa kikompyuta, mpelelezi wa Idara ya Polisi ya Los Angeles alisema: “Kila kitu tunachoona kinatokezwa na kompyuta, kwa hiyo vitu vilivyoigizwa vinafanana sana na vile vya asili—kwa kweli kuliko vilivyokuwa zamani. Mambo yalianza kukosa udhibiti karibu miaka mitatu hivi iliyopita na sasa yameenda zaidi ya hapo—kwa wazi yamekosa udhibiti kabisa.”
Kuigiza fedha, hundi, na hati kwaweza kupimwa kwa hasara ya fedha iletwayo kwa biashara, viwanda, na watu mmoja-mmoja. Lakini kuna visa vya uigizaji-vitu ambao waweza kupimwa kwa hasara ya uhai, kama makala ifuatayo itakavyoonyesha.
[Blabu katika ukurasa wa 7]
Faida kubwa zaidi hutokana na kunakili hundi za malipo