Kadi za Mkopo—Je, Zitakutumikia au Zitakutumikisha?
“KILA mwezi wakati nifunguapo taarifa zangu za kila mwezi za kadi ya mkopo ni kama msiba wa kuchekwa,” aonelea mwalimu wa Kiingereza katika Marekani. “Natazama kiasi ninachodaiwa kwa mshangao, kana kwamba utu wangu mwingine, ule mbaya, ulikuwa umekwenda katika ununuzi usiodhibitiwa katika maduka ya vichezeo, maduka ya vifaa vya nyumba, maduka makubwa ya bidhaa tofauti-tofauti na vituo vya petroli.”
Dolores pia aona ikiwa rahisi kulimbikiza deni kwa kulipa kwa kadi ya mkopo. Yeye asema: “Kutumia kadi za mkopo hakutii mtu wasiwasi. Singeweza kutumia fedha halisi jinsi hiyo. Lakini kufanya ununuzi kwa kadi za mkopo ni tofauti. Huoni kamwe fedha ulizotumia hasa. Unachofanya tu ni kutoa kadi yako, nayo yarudishwa kwako.”
Si ajabu kwamba deni la kadi za mkopo Marekani katika Juni 1995 lilifikia jumla ya dola bilioni 195.2—wastani wa zaidi ya dola 1,000 kwa kila mmiliki kadi! Hata hivyo, kampuni za kadi za mkopo huendelea kubembeleza wateja wapya kwa vichocheo kama vile viwango vya chini vya riba ya mwanzoni na kutokuwapo kwa malipo ya kila mwaka. Ni sihi ngapi za kadi za mkopo ambazo umepokea katika miezi ya majuzi? Nyumba ya wastani ya Marekani hupokea 24 hivi kila mwaka! Mmiliki kadi wa kawaida katika Marekani alitumia kadi kumi za mkopo katika 1994 ili kununua kwa mkopo asilimia 25 zaidi kuliko alivyofanya mwaka uliotangulia.
Katika Japani, kadi za mkopo ni nyingi zaidi kuliko simu; kuna wastani wa kadi mbili kwa kila Mjapani mwenye umri wa zaidi ya miaka 20. Katika sehemu iliyobaki ya Asia, zaidi ya kadi za mkopo milioni 120 hutolewa, 1 hivi kwa kila wakazi 12. James Cassin, wa MasterCard International, asema: “Asia ndiyo kwa mbali eneo lenye kukua haraka zaidi kwa shughuli za kadi za mkopo.” Msimamizi wa Visa International, Edmund P. Jensen, atabiri: “Tutakuwa jamii yenye kutegemea kadi kwa muda mrefu.”
Kadi za mkopo kwa wazi zitaendelea kuathiri maisha za watu kwa kiwango kikubwa. Zinapotumiwa vizuri, zaweza kufaidi. Hata hivyo, kuzitumia vibaya kwaweza kusababisha maumivu makali. Kuwa na ujuzi wa msingi kuhusu kadi za mkopo kwaweza kukusaidia kutumia kifaa hiki cha kifedha kwa manufaa yako.
Aina za Kadi
Kadi zilizo na sifa nzuri sana ni kadi za benki kama vile Visa na MasterCard. Kadi hizi hutolewa na mashirika ya kifedha na huwa na ada ya kila mwaka, kwa kawaida dola 15 hadi 25 kwa mwaka. Nyakati fulani, ada hii haitozwi, kutegemea rekodi nzuri ya kulipa ya mteja na utumizi wake wa kadi hiyo. Yawezekana kulipa malipo kamili kila mwezi, kwa kawaida bila kutozwa riba yoyote, au yawezekana kulipa kwa sehemu kila mwezi jambo ambalo huhusisha kutozwa riba ya juu. Kikomo cha utumizi huwekwa kutegemea rekodi nzuri ya kulipa ya mteja. Kikomo hicho mara nyingi hupandishwa kadiri uwezo wa kulipa unavyodhihirishwa.
Kadi za benki pia zina maandalizi ya kupata fedha za kabla ya chumo kwa kutumia mashine za kuweka na kutoa fedha akibani au hundi zilizotolewa na benki. Hata hivyo, kupata fedha kwa njia hii hugharimu sana. Kwa kawaida mtu hutozwa kati ya dola 2 na 5 kwa kila dola 100 zilizokopwa. Na riba kwa fedha hizo za kabla ya chumo hujikusanya kuanzia siku ile fedha zatolewa.
Mbali na benki, maduka mengi na mfumo wa maduka ya kitaifa yanayohusiana hutoa kadi za mkopo ambazo hukubaliwa kwenye maduka yao. Kwa kawaida hakuna ada ya kila mwaka kwa kadi hizo. Hata hivyo, ikiwa kiasi kinachodaiwa hakilipwi chote, riba yaweza kuwa juu zaidi kuliko kadi za benki.
Makampuni ya mafuta pia hutoa kadi za mkopo ambazo hazina ada za kila mwaka. Kadi hizi kwa kawaida hukubaliwa kwenye vituo vya petroli vya makampuni hayo tu na nyakati fulani katika mahoteli fulani. Sawa na kadi zinazotolewa na maduka, hizo hurusu malipo kikamili bila riba au malipo baada ya muda fulani kukiwa na riba.
Pia kuna kadi za kusafiri na za vitumbuizo, kama vile Diners Club na American Express. Aina hii ya kadi ina ada ya kila mwaka lakini haitozi riba, kwa kuwa malipo kamili yapaswa kufanywa mara tu bili ya kila mwezi ipokewapo. Hata hivyo, hakuna tofauti zilizo wazi kati ya kadi hizi na kadi za benki. Kwa kielelezo, American Express hutoa pia kadi ya Optima, ambayo inatoza riba na ni sawa na kadi ya benki.
Aina tofauti ya kadi inayoingia katika soko la Marekani ni smart card, ikiitwa hivyo kwa sababu ya chipu ya kumbukumbu ya kompyuta iliyotiwa ndani yayo. Yaweza kutumiwa kama kadi ya kupata fedha za kabla ya chumo, kwa kuwa mtumizi aweza kuruhusu chipu hiyo iratibiwe kwa ajili ya kiasi cha fedha kilichowekwa. Gharama ya ununuzi yaweza kutolewa kutoka kwayo na mchuuzi anayehusika. Kufikia mwaka jana Wafaransa tayari walikuwa wakitumia smart cards milioni 23 na Wajapani milioni 11. Imetabiriwa kwamba idadi ya kadi hizo ulimwenguni pote itapanda kufikia zaidi ya bilioni moja kufikia mwaka 2000.
Kabla ya kupata kadi ya mkopo, mtu angetenda kwa hekima kutoa uangalifu kwa masharti ya mkopo. “Masharti ya muhimu ya mkopo ya kufikiria,” kulingana na broshua iliyochapishwa na Federal Reserve System ya Serikali ya Marekani ni “kiwango cha asilimia cha kila mwaka (APR), ada ya kila mwaka, na kipindi cha kuhurumiwa.” Miongoni mwa mambo mengine ya kufikiria ni fedha za kabla ya chumo na ada zinazotozwa mtu akipita kikomo na vilevile malipo yanayotozwa kwa kuchelewa kulipa mkopo.
Utozwaji wa Fedha—Ni wa Juu Kiasi Gani?
Utozwaji wa fedha ambao watu hupaswa kulipa wanaposhindwa kulipa fedha zao za kila mwezi kikamili waweza kuwa wa juu sana kuliko wanavyofikiri watu wengi. Kwa kielelezo, fikiria ile APR, ambayo ni kiwango cha gharama halisi ya mkopo. Uhusiano wa kiwango cha riba ya kila mwaka na APR waweza kutolewa kielezi hivi. Tuseme unamkopesha rafiki dola 100 naye akulipa dola 108 mwishoni mwa mwaka. Katika kisa hicho, rafiki yako akulipa riba ya kila mwaka ya asilimia 8. Hata hivyo, tuseme yeye akulipa mkopo huo wa dola 100 nusu-nusu kwa miezi 12 kila mwezi akilipa dola 9. Jumla mwishoni mwa mwaka bado itakuwa dola 108, lakini wewe, mkopeshaji, umeweza kutumia fedha hizo kadiri malipo yalivyofanywa kila mwezi. Hiyo APR kwenye mkopo huo hupigwa hesabu kuwa asilimia 14.5!
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Federal Reserve System ya Marekani mwaka jana, APR ya kadi za mkopo za benki huanzia na asilimia 9.94 na kuendelea hadi asilimia 19.80, kawaida ikiwa kati ya asilimia 17 na 19. Ingawa mashirika fulani hutoa viwango vya chini vya kuanzia, kwa kawaida asilimia 5.9, hayo yaweza kuongeza mara tu kipindi cha kuanza kinapokwisha. Viwango pia hupandishwa ikiwa shirika la kutoa kadi lagundua kuongezeka kwa hatari. Watoaji fulani huadhibu wenye kuchelewa kulipa kwa kuongeza kiwango chao cha riba. Adhabu pia hutolewa kwa kupita kikomo cha utumizi.
Katika nchi za Asia, viwango vya asilimia vya kila mwaka kwenye kadi vyaweza kuwa juu sana. Kwa kielelezo, kadi fulani za benki hutoza asilimia 24 katika Hong Kong, asilimia 30 katika India, asilimia 36 katika Indonesia, asilimia 45 katika Filipino, asilimia 24 katika Singapore, na asilimia 20 katika Taiwan.
Kwa wazi, kadi za mkopo huandaa mkopo kwa urahisi lakini mkopo ulio ghali sana. Kuingia ndani ya duka na kupata madeni utakayolipa kwa kadi ya mkopo ni kama kuingia ndani ya benki na kukopa fedha kwa kiwango cha juu mno cha riba. Hata hivyo, karibu wamiliki kadi 3 kati ya 4 katika Marekani hufanya hivyo hasa! Hao huwa na deni kubwa sana ambalo hulipa kwa riba ya juu mno. Katika Marekani, deni la wastani la kila mwezi kwa Visa na MasterCard mwaka uliopita lilikuwa dola 1,825, na watu wengi huwa na madeni ya kiasi hicho katika kadi kadhaa za mkopo.
Mtego Uwezao Kukutumikisha
Ruth Susswein, mkurugenzi mkuu wa Bank Cardholders of America, asema kwamba watumizi wa kadi hawatambui matatizo ya kifedha yawezayo kuwapata. Yeye ataja kwamba kwa mtumizi wa kadi anayelipa malipo ya chini zaidi—dola 36 kwa mwezi—kwa deni la kadi ya mkopo la dola 1,825 ingemchukua miaka zaidi ya 22 kulipa deni hilo.a Kwa sababu ya malipo ya riba yaliyoongezeka, kwa wakati huo mteja huyo angelipa dola 10,000 hivi kwa deni la dola 1,825! Na itakuwa hivyo ikiwa hakutoza chochote kingine kwenye kadi yake! Kwa hiyo, ikiwa una mwelekeo wa kufanya ununuzi kupita kiasi, kadi za mkopo pochini mwako zaweza kuwa mtego.
Watu huingiaje mtegoni? Robert, aliyetajwa katika makala ya kwanza, asema: “Tulinunua vitu ambavyo hatukuvihitaji. Tukajiunga na klabu cha mazoezi ya mwili ambacho hatukuenda. Tulinunua nyumba iwezayo kuhamishwa, na kutumia maelfu ya dola kuitengeneza bila kufikiri kama ilistahili hayo yote. Hatukufikiria kamwe matokeo ya madeni yetu.”
Reena, aliyetajwa pia katika makala iliyotangulia, aeleza kilichompata yeye na mume wake, Michael: “Tulitumbukia katika deni tu. Baada ya ndoa tulinunua kila kitu tulichohitaji, tukitumia kadi za mkopo. Kwa ada za bima na ununuzi ambao hatukuweza kutumia kadi, tulitumia chaguo la fedha za kabla ya chumo kwenye kadi zetu za mkopo. Mnamo mwaka mmoja deni letu lilifikia dola 14,000. Kutambua kwamba mengi ya malipo yetu ya kadi za mkopo yalikuwa yakilipa riba kulitufungua macho.”
Je, Umiliki Kadi?
Baada ya kufikiria matatizo ya kifedha ambayo kadi za mkopo zimetumbukiza mamilioni ya watu, wengine huenda wakajibu la. Daphne, mwenye umri wa miaka 32, asema: “Wazazi wangu hawakuwa kamwe na kadi ya mkopo, na hawakuitaka.” Kwa wazi, mmiliki kadi 1 kati ya 4 wa Marekani hutumia kadi yake kwa hekima. Yeye hupata manufaa bila kupatwa na maumivu ya kulipa utozwaji wa riba ulio juu mno. Maria ni mtu wa aina hiyo. “Mimi hupenda urahisi wayo,” yeye asema. “Sihitaji kubeba fedha nyingi. Nikiona kitu ninachohitaji mahali ambapo vitu vimepunguzwa bei, naweza kukipata.”
Maria aendelea: “Sikuzote mimi huhakikisha nina fedha za kutosha kulipia ununuzi huo. Sijapata kutumia chaguo la fedha za kabla ya chumo. Na sijapata kamwe kulipa utozwaji wowote wa kifedha.” Ni rahisi kutumia kadi ya mkopo wakati wa kuagiza chumba mapema katika hoteli, na ni ya lazima katika Marekani wakati wa kukodi gari.
Hata hivyo, watu fulani huongozwa na msukumo kwa habari ya ununuzi. Huenda wakaweza kufanya ununuzi kuwa jambo la uangalifu mwingi zaidi kwa kutumia fedha taslimu. Michael na Reena hawakutaka kuwa katika deni kuwe njia ya maisha. Kwa hiyo waliamua kutotumia kadi zozote za mkopo kwa miaka mitano—isipokuwa wakati wa dharura.
Iwe utaamua kutumia kadi za mkopo au la ni uamuzi wa kibinafsi. Lakini ukiamua, zitumie kwa uangalifu. Zitumie zikiwa kifaa cha kufanya mambo kuwa rahisi. Na uepuke kabisa kulimbikiza madeni. Kudhibiti utumizi wa kadi ya mkopo ni hatua muhimu ya kushughulikia fedha zako kwa mafanikio. Fikiria mengine zaidi uwezayo kufanya.
[Maelezo ya Chini]
a Malipo ya chini kabisa yaweza kuwa dola kumi au kiasi kilicho sawa na asilimia ndogo ya deni jipya, ikitegemea ni lipi lililo kubwa.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kutumia kadi za mkopo hakutii mtu wasiwasi—hadi bili zinapokuja