Kadi za Mkopo—Je! Uzitumie?
MTU mmoja kutoka Kalifornia, aitwaye na watu fulani “Bw. Kadi Maarufu,” alikusanya kadi za mkopo 1,265 zilizo halali. [1] Ni kweli kwamba mtu huyo hawakilishi mtu wa kawaida mwenye kadi za mkopo. Hata hivyo inakubaliwa kotekote kwamba matumizi ya kadi za mkopo yamekuwa sehemu iliyositawi ya jumuiya ya kisasa ya nchi za Magharibi.
Jarida American Demographics lasema kwamba katika 1986 karibu robo-tatu za nyumba za U.S. zilikuwa na kadi moja au zaidi za mkopo.[2] Kuna kadi za mkopo zaidi ya 25,000 za aina mbalimbali zipatikanazo katika United States pekee.[3] Makampuni ya mafuta, maduka ya rejareja, na makampuni ya ndege hutoa kadi zayo yenyewe. Katika 1991, Waamerika walikuwa na kadi halali za mkopo milioni 232 za makampuni ya MasterCards na Visas, ambazo ni kadi zipendwazo zaidi ya zote.[4]
Shughuli hiyo iitwayo biashara ya kadi za mkopo inakua pia katika Ulaya, ikisababisha mashindano makali kati ya mabenki na makampuni yashindanayo kwa ajili ya wateja wenye hamu ya kuzitumia kadi hizo. Jumla ya kadi zote za mkopo zilizo halali ulimwenguni pote ni zaidi ya bilioni moja![5] Kwa nini kuna kadi nyingi za mkopo kadiri hiyo? Ni nani hunufaika zaidi ya wote kwa matumizi yazo? Ni zipi baadhi ya hatari na matatizo yakabiliwayo na wenye kadi za mkopo?
Ni Nani Hufaidika?
Mabenki na makampuni ya kadi za mkopo hupata faida kubwa sana, si kutokana na ada pekee—kutia ndani ada za kila mwaka za uanachama, ada za kukawisha malipo, ada za kutumia kadi za mkopo kupita kiasi kilichoidhinishwa—bali vilevile kutokana na riba za juu yanayotoza kwa fedha yanayowiwa. Na bila shaka wao hawawezi kupata faida kutokana na ada za malipo ila tu kama wenye kadi za mkopo wapata madeni makubwa. Katika United States pekee, mamilioni ya watu wametumia kadi za mkopo mpaka wakaingia ndani ya madeni ya daima. Karibu asilimia 75 ya Waamerika wenye kadi za mkopo wana madeni makubwa katika akiba ya akaunti zao, ambazo zawafanya walipe riba za juu sana kila mwezi. Mwamerika wa kawaida mwenye kadi ya mkopo huwa na deni la zaidi ya dola 2,000 kwa akaunti yake ya kila mwezi.[6]
Katika kitabu chake The Credit Jungle, Al Griffin aonelea kwamba “asilimia 15 hadi 20 ya wenye kadi ambao hulipa kikamili madeni yao mara tu wapatapo taarifa hawachangii hata hela ule utendaji wa benki.” Yeye aongezea kwamba “ile asilimia nyingine 80 hadi 85 ya wenye kadi hufanya shughuli ya kadi za mkopo iwe utendaji wenye faida zaidi ya wote ambao benki inao. Utendaji wa kiasi wa kadi ya benki wenye dola milioni 10 waweza kuleta faida ya dola milioni 1.8 kila mwaka.”[7] Katika 1990 benki ya U.S. ambayo ina ushiriki mkubwa zaidi katika biashara ya kadi za mkopo ilipata faida inayokaribia dola bilioni 1 kutokana na utendaji wayo na wateja, hasa kutokana na idara yayo ya kadi za mkopo.[8]
Jihadhari
Kuna upande usiofaa wa kadi hizo ndogo za plastiki. Kwa kielelezo, je, umepata kupokea simu kutoka kwa kampuni isiyojulikana ikikueleza juu ya zawadi uliyotoka tu kushinda? Wengi wamepokea. Unahitaji tu kujibu maswali fulani ya msingi ili upate zawadi yako. Lakini mwenye kupiga simu akuuliza juu ya nambari ya kadi yako ya mkopo. Kwa nini? Kwa sababu kwa kweli hujashinda zawadi yoyote. Mpiga simu kama huyo ataka tu nambari ya kadi yako ya mkopo ili aweze kuagiza bidhaa au anunue vitu kupitia simu akitumia akaunti yako.
Kuna aina kadhaa za ulaghai wa kadi za mkopo, zikigharimu mamilioni ya dola kila mwaka. Na hata wakati tatizo hilo halikuathiri moja kwa moja, kama una kadi ya mkopo, labda unalipia ulaghai huo kwa kutozwa ada na riba za juu zaidi.a
Hatari kubwa zaidi za kadi za mkopo ni magumu na mateseko ambayo hutokea unapotumbukia katika deni kubwa. Kitabu The Credit Jungle chaonelea kwamba “watu wengi wanaoweza kukinza kishawishi cha kununua vitu vya anasa ambavyo hawangeweza kulipia kwa fedha taslimu, hushindwa kabisa kukinza kishawishi hicho wanapokuwa na kadi za mkopo mkononi. Familia nyingi hula maharagwe kwa majuma kadhaa baada ya kulipia chakula [cha hali ya juu] kilichotozwa kwa kadi ya mkopo mwezi uliopita.”[9]
Lakini mambo mengi zaidi ya ulaji wako yaweza kuzorota kama sehemu kubwa ya mapato yako yatumiwa kulipia madeni yako. Kitabu Credit—The Cutting Edge charipoti kwamba “kwa wastani, Waamerika hutumia asilimia zipatazo 75 za mapato yao ya kila mwezi kulipia mikopo, madeni, na kadi za mkopo.”[10]
Inasikitisha kwamba kwa wanunuzi wengi, kadi ya mkopo si mlango wa kupata mafanikio ya kiuchumi, bali ni anguko la kuingia ndani ya deni na hangaiko lenye kudumu. Kwa kielelezo, katika miaka ya karibuni wanunuzi Waamerika wamekuwa wakirundika madeni ya kadi za mkopo, jambo ambalo limetokeza matatizo mengi ya kadi za mkopo, ukosefu wa kulipa madeni na ufilisi. Katika 1990, wanunuzi wa U.S. walikuwa na madeni yapatayo dola trilioni 3.2 ya kadi za mkopo, mikopo ya ununuzi wa magari, na rahani! Nyumba ya kawaida ilikuwa na deni inayokaribia dola 35,000 na ililipa riba ipatayo dola 3,500 kwa mwaka.[11]
Basi haishangazi kwamba ufilisi wa watu binafsi umeongezeka sana. Katika 1990 idadi kubwa sana ya Waamerika 720,000 walitoa maombi ya ufilisi, ongezeko la karibu asilimia 17 zaidi ya 1989. Katika 1991 idadi hiyo iliongezeka kufikia 800,000, na katika 1992 rekodi mpya iliwekwa ya ufilisi 971,517 mbalimbali wa watu binafsi.[12]
Watu fulani wanaopata ugumu wa kudhibiti matumizi yao ya kadi za mkopo wameamua kuacha kuzitumia. Kwa upande mwingine, wengi wameweza kutumia kadi za mkopo kwa hekima bila kutatanisha maisha yao.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi juu ya njia za kuepuka ulaghai wa kadi za mkopo, tafadhali ona makala “Kadi za Mkopo—Je! Ni ‘Mtego wa Plastiki’?” katika Amkeni! la Desemba 8, 1986, Kiingereza.