Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 12/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mbao kwa Kulinganishwa na Plastiki
  • Machinjo ya Kila Siku
  • Simama Wima
  • Aksidenti Zinazongojea Kutokea
  • Mbinu za Kukabiliana na Matatizo kwa Watoto
  • Furaha Katika Asia
  • Ukosefu wa Kuwasiliana
  • Kuweka Kazi Mahali Pafaapo
  • Polisi Wajifunza Kuhusu Vidhehebu
  • Biashara Hatari Yarudi
  • Kukumbwa na Mfadhaiko!
    Amkeni!—2005
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1999
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 12/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Mbao kwa Kulinganishwa na Plastiki

Unapokata nyama mbichi na ndege, waweza kudhani kwamba bapa ya plastiki ya kukatia nyama ni safi kuliko ubao. Uchunguzi wa hivi karibuni ulifunua jambo tofauti. Kulingana na Berkeley Wellness Letter, wanabiolojia wawili wa viini katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, U.S.A., walitia kimakusudi kwenye bapa ya plastiki ya kukatia nyama bakteria, kama salmonela, itiayo chakula sumu. Kwa kushangaza, bakteria ziliongezeka sana katika bapa hizo za plastiki huku zile zilizowekwa kwenye ubao zikifa au kupoteza nguvu—nyakati nyingine kwa muda wa dakika tatu tu. Ubao huo mwingine ulipotiwa bakteria na kuachwa ukae usiku kucha, huo haukuwa na bakteria asubuhi iliyofuata, lakini zile za plastiki zikawa na bakteria nyingi sana. Na kuhusu jambo hilo ubao wa zamani ulifanya vizuri zaidi ya ubao mpya. Ilikuwa vigumu pia kuosha plastiki kama ilivyotarajiwa, hasa kama sehemu ya juu ilikuwa imekwaruzwa. Hata ubao uwe wa aina gani, ni muhimu sana kuuosha kwa sabuni na maji moto baada ya kukata nyama mbichi.

Machinjo ya Kila Siku

“Angalau wanawake wanne hufa kila siku katika Brazili kwa sababu ya matatizo yatokanayo na utoaji-mimba—1,460 kila mwaka,” laripoti gazeti la Brazili Folha de S. Paulo. Gazeti hilo lakiri kwamba idadi hiyo ni ya “kukadiria” na kwamba idadi halisi yaweza kuwa mara tatu zaidi ya hiyo. Hilo laongeza kusema hivi: “Wastani katika Amerika ya Latini ni kubwa hata zaidi. Shirika la UM lakadiria kwamba asilimia 50 ya vifo vyote vya akina mama hutokana na utoaji-mimba, jambo limaanishalo vifo vya wanawake elfu 15 kila mwaka—wastani wa wanawake 41 wa Amerika ya Latini wanaouawa kila siku.”

Simama Wima

Simama kizembe, na mgongo wako waumia. Kulingana na ripoti moja katika International Herald Tribune, kusimama vibaya huweka mkazo wa mara 15 kwenye sehemu ya chini ya mgongo kuliko ukiwa umesimama wima. Kusimama kizembe kwaweza kutokeza pia kupumua kijuu-juu na hilo lamaanisha kutumia oksijeni chache zaidi katika kulisha mwili. Kwaweza kukumaliza nguvu na kutokeza maumivu, na hasa kwenye shingo na mgongo. Kwaweza pia kukufanya uonekane mzee-mzee, mnene zaidi, na mtu asiye na hakika kuliko kama umesimama wima. Kusimama vizuri, ripoti hiyo yasema, ni kusimama kama ndewe za masikio yako, mabega, katikati ya nyonga, vilegesambwa, na mifupa ya vifundo vyapasa vilingane kutoka juu. Lakini, hilo halimaanishi tusimame kimdeki kama mwanajeshi huku magoti yakiwa pamoja na mabega na kichwa kikiwa nyuma. Kufanya hivyo huweka mkazo zaidi kwenye uti wa mgongo. Wastadi wasema kwamba kusimama vibaya ni tabia mbaya iwezayo kurekebishwa.

Aksidenti Zinazongojea Kutokea

“Misiba mingi yenye kuelea inangojea kutokea”—kulingana na International Environmental Update, hivyo ndivyo wachambuzi fulani wameziita meli kubwa za mafuta za ulimwengu. Jarida hilo ladai kwamba “ulimwengu bado wategemea mamia ya meli kubwa zenye kutu, zinazozeeka, zisizodumishwa na zenye wafanyakazi wasiozoezwa vizuri ili kusafirisha mafuta yao yahitajiwayo sana.” Meli kubwa hutazamiwa idumu kwa miaka 15 hivi. Lakini asilimia 65 hivi za meli hizo ulimwenguni ni nzee kadiri hiyo. Hata baadhi ya maofisa wa biashara ya mafuta wakiri kwamba meli nyingi ambazo zimechakaa zapasa kuondolewa. Inaonekana kwamba hakuna hata shirika moja ambalo lina mamlaka ya kuamuru meli hizo zisisafiri. Hata hivyo, tatizo laweza kutokana na jinsi meli hizo hushughulikiwa kuliko kutokana na meli hizo zenyewe. Jarida hilo lanukuu mmoja wa wataalamu wa uchafuzi wa mafuta kuwa akisema hivi: “Hesabu kubwa zaidi ya aksidenti za meli husababishwa na makosa ya kibinadamu.”

Mbinu za Kukabiliana na Matatizo kwa Watoto

Ni nini huwezesha watoto fulani wakabiliane na misongo mizito ya maisha ya kisasa? Ili kujua hilo watafiti katika Chuo Kikuu cha Loyola cha Chicago, U.S.A., kilifanya uchunguzi wa watoto 400, wenye umri wa miaka 9 hadi 13, wanaotoka malezi mbalimbali. Miongoni mwa karibu nusu ya wale waliokabiliana na magumu kwa njia nzuri, watafiti hao walipata mambo matatu yafananayo katika tabia yao, laripoti gazeti American Health. Kwanza, wao walikuwa wakiomba msaada, wakieleza wengine mahangaiko yao, na kutafuta utegemezo wa kimwili kutoka kwa mtu mzima—mara nyingi kutoka kwa mzazi ingawa si kila wakati. Pili, walikuwa na mwelekeo wa kuchukua madaraka kwa ajili ya mwenendo wao wenyewe na kutafuta kushawishi marika yao waepuke mabaya. La tatu, wao walitafuta wakati wa utulivu na tafrija ili kuondoa mkazo wa akili. Kwa upande mwingine, watafiti walipata mielekeo mitatu iliyopunguza uvumilivu wa watoto: kutoa ukali; mwenendo wa kujiharibu mwenyewe kama vile kutumia dawa za kulevya; na kuepuka matatizo badala ya kuyashughulikia.

Furaha Katika Asia

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Utafiti wa Uchunguzi wa Hong Kong ulipata kwamba watu wenye furaha zaidi ya wote katika Taiwan na vilevile Jamhuri ya Korea ni watu maskini walio katika umri wa miaka ya 30. Katika Ufilipino, ambamo jumla ya thamani ya mazao ya kila mtu ni dola 500 na ambako asilimia 41 ya watu huishi kwa umaskini, asilimia 94 ya watu wadai kuwa wenye furaha. Mtazamo uo huo kuelekea maisha waonyeshwa na karibu majirani wao wote katika Asia, ila nchi moja. “Katika eneo ambalo kwa ujumla watu huwa wenye furaha,” likasema Mainichi Daily News, nchi tajiri zaidi ya Asia “ilikuja kuwa isiyo yenye furaha kuliko zote.” Hata wakiwa na jumla ya thamani ya mazao ya kila mtu ipitayo dola 27,000, asilimia 40 ya wajapani wakiri kwamba wao hawana furaha.

Ukosefu wa Kuwasiliana

“Waume na wake wa kawaida katika Ujerumani hutumia muda ukaribiao dakika 10 tu kila siku katika kuzungumziana,” laripoti gazeti la Kijerumani Nassauische Neue Presse. Kwa hiyo waume na wake wengi hutumia muda wa saa chache sana kujaribu kusuluhisha matatizo yao. Kwa kuongezea, washauri wa familia katika Ujerumani waona kwamba waume na wake wachanga hasa hawajui namna ya kushughulikia tofauti zao za maoni. Hilo ni kisabibishi kikuu cha utengano wa mapema katika ndoa; ndoa mbili kati ya tano huvunjika katika muda wa miaka minne ya kwanza. Gazeti hilo lamnukuu mshauri Rosemarie Breindl kuwa akisema: “Ni kama hakuna kabisa watu walio violezo wanaoonyesha kwa kielelezo chao namna ya kusuluhisha mahitilafiano.” Ripoti hiyo yaongezea hivi: “Kwa hiyo kuna mwelekeo unaoendelea kukua wa kutatua matatizo ya ndoa kwa utengano tu.”

Kuweka Kazi Mahali Pafaapo

Vidonda vya tumbo, maradhi ya moyo, uchovu wa neva, kukosa kwenda kazini, na aksidenti—hizo ndizo gharama za mkazo mwingi wa akili, jambo linalogharimu mwajiriwa na vilevile mwajiri. Kulingana na ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Kimataifa ya Wafanyakazi ya Ufaransa, matatizo yahusikayo na mkazo yamekuwa “moja ya matatizo makubwa zaidi ya wakati wetu.”[1] Katika Ulaya, kupunguzwa kwa wafanyakazi na madaraka ya wafanyakazi yanayoendelea kukua, pamoja na tamaa ya kupata mazao na faida zaidi, yameongeza sana mkazo katika mahali pa kazi, lataja jarida la kitiba Le Concours Médical, likiongezea kwamba watu fulani katika Ufaransa hata wanakufa kutokana na kufanya kazi kupita kiasi.[2] Kwa kupendeza, uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba mtu hukinza mkazo wa akili kwa njia bora zaidi anapositawisha urafiki wenye uchangamfu na wenye upendo pamoja na watu walio karibu naye. Madaktari hupendekeza pia kustarehe, mazoezi ya viungo vya mwili, lishe ifaayo, na kuweka kazi mahali pafaapo—kutenga wakati kwa ajili ya familia na tafrija.[3]

Polisi Wajifunza Kuhusu Vidhehebu

Polisi kutoka nchini kote walikusanyika katika Rhode Island, U.S.A., mapema mwaka huu kwa ajili ya mkutano wa siku tatu kuhusu suala lisilo la kawaida: ibada ya kishetani, vidhehebu, na uchawi. Gazeti Daily News la New York liliripoti kwamba kusudi la mkutano huo lilikuwa ni kuwazoeza polisi wenye maarifa ya muda mrefu ya kazi waweze kugundua ujeuri uenezwao na vidhehebu kama hivyo. Sajini Edmund Pierce wa Idara ya Polisi ya Warwick alinukuliwa kuwa akisema: “Jambo tunalofanya ni kutilia maanani uhalifu mbalimbali kutoka ukatili kwa wanyama, ukufuru wa makaburi na unyang’anyi wa kimabavu, hadi mashambulizi, desturi za kutenda watoto vibaya na uuaji wa kimakusudi.” Gazeti Daily News lamnukuu Dr. Carl Raschke, profesa katika Chuo Kikuu cha Denver, akisema hivi: “Naona vidhehebu vingi vinavyofanyizwa, na matendo mabaya ya kijeuri yakitukia kwa kisetiri cha itikadi za kidhehebu.” Wataalamu katika mkutano huo walionya vilevile juu ya vikundi vyenye chuki kama neo-Nazis (vikundi vya kupendelea Wanazi) na Ku Klux Klan (Kikundi kinachotetea ukuu wa weupe) vinatumia uchawi katika kuvutia washiriki na kuwadhibiti.

Biashara Hatari Yarudi

Yajapokuwa maendeleo fulani katika miaka ya karibuni, jitihada za hifadhi katika India zimerudishwa nyuma na wawindaji-haramu, laripoti India Today. Katika 1988 kulikuwa na simba-milia wapatao 4,500 waliobaki porini katika India. Kufikia 1992, idadi hiyo ilikuwa imepungua ikawa 1,500. Simba-milia huuzwa kwa ajili ya ngozi yake, damu yake, na mifupa yake (ambayo hutumiwa katika dawa za kienyeji), makucha yake, na sehemu zake za uzazi. Lakini si simba-milia pekee wawindwao na vikundi vya wawindaji-haramu. Vifaru 48 wa India walichinjwa kwa ajili ya pembe zao katika 1992, idadi kubwa zaidi katika miongo ya miaka ya karibuni. Ndovu wa India wamepungua idadi kutoka 5,000 miaka kumi iliyopita hadi karibu 1,500 leo. Inaripotiwa kwamba walinzi wa misitu wanawaogopa sana wawindaji-haramu wa kisasa wenye silaha zilizo hatari hivi kwamba siku hizi baadhi yao hawavai mavazi yao rasmi ya kazi; wengine hukataa katakata kufanya kazi yao mpaka wapewe vifaa vya kutosha vya kujikinga.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki