Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Mapenzi Yaliyovunjika Nina umri wa miaka 17 na nimepata makala “Vijana Huuliza . . . Naweza Kukabilianaje na Mapenzi Yaliyovunjika?” (Mei 8, 1993) kuwa yenye msaada sana. Nyakati zote nilikuwa nikishuka moyo kwa ajili ya kutopendwa na mtu yeyote. Sasa nazingatia mambo mengine na sihangaiki juu ya kuolewa karibuni.
S. M., Australia
Nilijihusisha kimapenzi na mvulana mmoja ambaye hakuwa Mkristo na nikajikuta nikibanwa na mapenzi kumwelekea. Niling’amua yaliyokuwa yakitendeka na kukatiza uhusiano naye, lakini nilikuwa na hisi za kujiua. Nilihisi nisingeweza kuishi bila yeye na nikashuka moyo kwa majuma kadhaa. Makala hiyo ilinisaidia nifikiri kwa njia ifaayo na kujua kwamba kipindi hiki chenye huzuni kitapita.
A. H., United States
Mapishi Makala yenu “Tunda Dogo Lenye Nyuzinyuzi la New Zealand” (Oktoba 22, 1992, Kiingereza) ilionyesha mapishi yatumiayo mvinyo wa chungwa kuwa kiungo chayo cha upishi. Wasomaji wenu wapasa kukumbushwa kwamba hawapaswi kuendesha gari mara tu baada ya kula kitu chochote chenye kileo.
J. S., United States
Kwa kweli ingefaa kujulisha wageni kama chakula kina kileo. Mapishi yanayotajwa yalihitaji matumizi ya kijiko kikubwa kimoja cha mvinyo wa chungwa katika saladi ya matunda yenye kutumiwa na watu sita hivi—ambacho ni kiwango kisichoweza kulevya. Hatari ya kulevya ni hafifu hata zaidi katika mapishi yahitajiyo kupika viungo vya chakula. Na kwa sababu kileo huchemka kwa kiwango kidogo cha moto, kileo kingi kama si chote kitatoweka.—Mhariri.
Tamaa ya Joshua Asanteni sana kwa kuchapisha makala ya “Tamaa ya Joshua.” (Juni 22, 1993) Ilinitia moyo sana. Kama aliweza kuwa mwaminifu jinsi hiyo akiwa na maradhi hatari [leukemia], ni rahisi zaidi kwangu kama nini kuwa mwaminifu pia! Nina umri wa miaka tisa.
M. M., United States
Niliguswa moyo sana na “Tamaa ya Joshua.” Ushujaa wake, imani yake, na upendo wake kwa Yehova ilinigusa moyo sana.
K. M., United States
Wafia-Imani wa Kisasa Nimetoka tu kumaliza kusoma mfululizo wa makala zenye kichwa “Washindi Wajapokabiliwa na Kifo.” (Mei 8, 1993) Nimehuzunishwa sana na mambo mabaya yasiyo ya haki ambayo ndugu zetu wa Kikristo walitendwa. Ninapofikiria uvumilivu wao, machozi hunitoka. Jambo linivutialo ni imani yao na uaminifu wao hata wakabilipo kifo. Yehova na atupe nguvu na uvumilivu tuendelee kuwa waaminifu, kama walivyokuwa.
B. D., Italia
Nilipokutana mara ya kwanza na suala la kubaki mwaminifu wakati wa majaribu katika funzo langu la Biblia, sikuona kwamba kuna pindi ambazo twakabiliana na majaribio makali ya imani. Lakini baada ya kusoma maono yenye kugusa moyo ya Wakristo waliobaki waaminifu wajapokabiliwa na kifo, siwezi kuzuia machozi yasinitoke. Nimethamini sana mfululizo huo wa makala.
J. P., Ufilipino
Kupanga Uzazi Mfululizo wa makala zenu “Kupanga Uzazi—Suala la Duniani Pote” (Februari 22, 1993) ulisema kwamba wakati mipachiko ya projestini-tu itumiwapo [ikiwa njia ya kudhibiti uzazi], kuna uwezekano wayo kuharibu mimba. Daktari wangu asema hiyo si kweli.
M. D., United States
Watafiti hawajui kabisa jinsi mipachiko ya Projestini-tu huzuia mimba. Baadhi yao huamini kwamba hizo huzuia mimba kwa kuzuia kutoka kwa yai. Wengine hudai kwamba kuna ushuhuda wa kwamba nyakati nyingine hizo huzuia mimba kwa kuzuia yai lililotungwa lisijishikanishe kwenye tumbo la uzazi—na hivyo, ikiharibu mimba. Kwa sababu njia hii ya kudhibiti uzazi si kuharibu mimba kihalisi sana, ni lazima mume na mke Wakristo waamue wenyewe kama waweza kuitumia kwa dhamiri safi au la. (Wagalatia 6:5)—Mhariri.