Kuutazama Ulimwengu
Kuwatenda Vibaya Watoto Ni Kawaida
“Uchunguzi mpya wa afya ya vijana wabalehe [Marekani], umepata kwamba zaidi ya mvulana 1 kati ya 8 wenye umri wa kwenda shule ya sekondari walisema walikuwa wametendwa vibaya kimwili au kingono,” laripoti gazeti The New York Times. Uchunguzi huo ulipata kwamba “kutendwa vibaya kimwili kwa wavulana ni kwa kawaida zaidi kuliko kutendwa vibaya kingono, na kwamba thuluthi mbili ya kutendwa vibaya kimwili kulifanywa na mshiriki wa familia na kulifanyiwa nyumbani.” Vijana Wamarekani wenye asili ya Asia ndio waliodai kutendwa vibaya zaidi kingono, asilimia 9 yao wakisema kwamba walikuwa wametendwa vibaya. Miongoni mwa wavulana wa Kihispania, asilimia 7 walisema walikuwa wametendwa vibaya kingono, ilhali asilimia 3 ya weusi na weupe waliripoti kutendwa vibaya kingono. Orodha hiyo ya maswali haikufafanua maana ya kutendwa vibaya. Iliuliza tu iwapo mvulana huyo aliwahi kutendwa vibaya kimwili au kingono.
Je, “Ni Babu wa Jadi Mkuu?”
Maaskofu kutoka Asia yote hivi karibuni walikusanyika katika Vatican City ili kuzungumzia njia za kueneza Ukatoliki katika nchi za Asia. “Katika nchi nyingi za Asia, Ukristo huonwa kuwa dini ya Magharibi iliyoletwa na wakoloni,” asema Askofu Oswald Gomis wa Sri Lanka. Hivyo, mwito wa ushindani ni “kumwasilisha Yesu katika maana watakayoelewa Waasia,” laripoti shirika la habari la Associated Press. “Maaskofu hao walizungumza juu ya kufanya kanisa la Roma lifaane na desturi na lugha za Kiasia, na kinyume cha hilo.” Kielelezo kimoja kinachotolewa ni zoea la kuabudu wazazi wa kale waliokufa. Ili kuwapendeza wazoeao desturi hii ya kale, Askofu John Tong Hon wa Hong Kong alipendekeza kwamba Wakatoliki waiwasilishe polepole dhana ya mungu wa “Kikristo” kuwa “babu wa jadi aliye wa mwisho.”
Upasuaji kwa Kutumia Roboti
Madaktari-wapasuaji wawili katika hospitali moja ya Paris wamefaulu kufanya upasuaji wa kwanza wa moyo wakitumia roboti inayoongozwa na kompyuta, laripoti gazeti la habari la Kifaransa Le Figaro. Watu sita walifanyiwa upasuaji, kutia ndani mgeuzo wa damu kutoka sehemu moja hadi nyingine kupitia kwa ateri za damu. Njia hii inahusisha kupasua moja kwa moja mkato wa sentimeta nne. Wakiwa wameketi kando ya mashine iratibuyo shughuli hiyo iliyo meta kadhaa kutoka mahali alipo mgonjwa, madaktari-wapasuaji hutazama ndani ya mwili wa mgonjwa kwa kutumia kamera na kutumia seti mbili za usukani kuelekeza mkono wa roboti hiyo. Kwa kuwa kompyuta hupunguza mwendo wa mkono wa daktari-mpasuaji kadiri ya mara tatu kufikia tano, upasuaji huwa sahihi zaidi na bila kuingilia sana sehemu nyingine za mwili. Manufaa nyingine ni kwamba mgonjwa hahisi maumivu mengi anapoendelea kupata nafuu.
Misiba ya Barabarani Yaongezeka
Kila mwaka, zaidi ya watu 500,000 hufa kwenye barabara kuu, na ulimwenguni pote, misiba ya barabarani inaongezeka, charipoti kichapo Fleet Maintenance & Safety Report. Kuna uwezekano gani wa wewe kupatwa na aksidenti mbaya ya barabarani? Kulingana na ripoti hiyo, “katika nchi zenye ‘magari mengi,’ angalau mtu 1 kwa kila watu 20 hufa au hujeruhiwa kwa kugongwa kwenye barabara kuu kila mwaka, na 1 kwa kila watu 2 hulazwa hospitalini angalau mara moja maishani mwao kwa kujeruhiwa barabarani.”
Sehemu Zisizokuwa Safi
Kama isivyoweza kutarajiwa, kikalio cha choo nyumbani mwako chaweza kuwa safi kuliko ubao wa kukatia vyakula jikoni mwako. Huo ndio mkataa uliofikiwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Arizona baada ya kutumia majuma 30 wakichunguza bakteria zilizopatikana katika nyumba 15. Kundi hilo lilichukua sampuli kutoka maeneo 14 katika kila nyumba, kutia ndani vishikio vya mfereji, sehemu za juu za sinki, mbao za kukatia vyakula, vitambaa vya kupangusia sahani, na vikalio vya choo. Walipata nini? “Watafiti walipata bakteria mara milioni moja zaidi kwenye vitambaa vya kupangusia sahani vilivyokamuliwa maji, kuliko zile walizopata kwenye vikalio vya choo,” lasema gazeti New Scientist. “Hata mbao za kukatia vyakula zilikuwa na zaidi ya mara tatu ya bakteria hizo.” Msemaji mmoja wa uchunguzi huo, Pat Rusin, alikisia kwamba “vikalio vya choo huwa vikavu sana visiweze kutegemeza bakteria nyingi zinazopendelea mazingira yenye unyevu,” laripoti gazeti hilo. Ili kuboresha usafi wa kiafya, Rusin apendekeza vitambaa vya kupangusia sahani vifuliwe kila juma. “Mwaga tu kikombe kimoja cha dawa ya klorini ndani ya maji yaliyojaa kwenye sinki, tia ndani kitambaa cha kupangusia sahani na ukiache kilowe maji kwa dakika 10 kabla ya kuyamwaga maji hayo,” yeye asema.
Kupunguza Hatari ya Vijiwe vya Figo
Watafiti wakichunguza milo ya wauguzi zaidi ya 80,000 katika Marekani kati ya 1986 na 1994 walipata kuwa vinywaji fulani vyaweza kumsaidia mtu aepuke kuwa na vijiwe vya figo zaidi ya vingine, charipoti kichapo Science News. Miongoni mwa vinywaji 17 vilivyochunguzwa, chai ilipunguza hatari ya kuwa na vijiwe vya figo kwa asilimia 8, ilhali kahawa ya kawaida au kahawa iliyoondolewa kafeini ilipunguza hatari hiyo kwa asilimia 9 hivi. Unywaji wa kiasi wa divai ulisaidia kupunguza hatari ya mtu kuwa na vijiwe vya figo kwa asilimia 20 au zaidi. “Kwa kushangaza, kunywa kiasi cha gramu 240 hivi za maji ya matunda ya zabibu kila siku kuliongeza hatari ya kuwa na vijiwe hivyo kwa asilimia 44,” uchunguzi huo ulionyesha. “Hakuna kinywaji kingine kilichokuwa na matokeo mabaya jinsi hiyo.” Dakt. Gary Curhan, mtaalamu wa magonjwa ya figo, aliye pia mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko katika Boston alinukuliwa akisema hivi: “Kubadili kidogo kutumia vinywaji hivi kwaweza kufanyiza tofauti,” lakini ikiwa tu sehemu moja ya mbinu ya tiba ihusishayo mambo mengi.
Maana ya Sikukuu ya Ista Katika Australia
Gazeti la habari la Sun-Herald la Australia lilifanya uchunguzi ambapo watu mbalimbali waliulizwa sikukuu ya Ista ilichomaanisha kwao. Matokeo yaliyochapishwa yalikuwa katika mpangilio huu: mayai ya chokoleti ya Ista (asilimia 54), likizo ndefu ya mwisho-juma (asilimia 39), Royal Easter Show (asilimia 21), sherehe ya kidini (asilimia 20). David Milikan, mhudumu wa Kanisa la Muungano, alisema hakushangaa kwamba ni watu wachache katika Sydney waliohusianisha sikukuu ya Ista na dini. Aliongeza kusema hivi: “Makanisa yanadidimia . . . Madhehebu makubwa yote yanapoteza washiriki kwa wingi.” Askofu mkuu wa Katoliki ya Roma ya Sydney aliomboleza hivi: “Kwa watu wengi, sikukuu ya Ista haina umaana wa kidini wowote; hiyo ni sherehe nyingine tu ya kilimwengu.”
Ponografia kwa Wanawake
“Pole kwa pole wanawake wanakaribia wanaume katika kupendezwa na habari za ngono za waziwazi zinazowasilishwa na vyombo vya mawasiliano,” laripoti gazeti The New York Times. Idadi ya sehemu kama hizo zinazokusudiwa wanawake huambatanisha “picha za ngono zisizo wazi . . . na ununuzi-vitu dukani.” Baada ya sehemu moja kutokea ambayo imekusudiwa hasa wanawake wanaofanya ngono na wanaume, gazeti la Times lilisema kwamba “hiyo ni sehemu nyingine tu inayoonyesha mambo ya kingono waziwazi, na mambo hayo ya kingono yameenea sana katika mifumo ya ulimwengu wa mawasiliano.”
Waraibu wa Ununuzi-Vitu Dukani
“Idadi yenye kuongezeka ya watu katika Ujerumani ni wanunuzi wa vitu wasiojidhibiti,” laripoti gazeti la habari Grafschafter Nachrichten. Kulingana na mwanasaikolojia wa shughuli za biashara Alfred Gebert, wanunuzi wa vitu wasiojidhibiti huhisi msisimuko unaotoweka upesi baada ya kulipia bidhaa zao. Wao hata hujitenga na wengine, asema Gebert. “Wao hutetemeka, hutokwa jasho, na kupatwa na matatizo ya tumbo.” Kutokana na hili, matajiri ndio waelekeao kupatwa na hatari kubwa ya kuwa wanunuzi wa vitu wasiojidhibiti kuliko maskini. Visababishi vya uraibu huu vyaweza kutia ndani ‘upweke, kutojistahi, mkazo, na matatizo kazini.’ Ili kusaidia kukabiliana na tabia hii ya kukosa kujidhibiti, Gebert apendekeza kuwa na shughuli ya kujifurahisha. Jambo muhimu hasa, Gebert asema, ni mahusiano ya kijamii. “Bila msaada wa wengine, uraibu hujidhihirisha tu madeni yaingiapo na baki la malipo ya benki liishapo,” yeye asema.
Kuwapeleleza Watoto
Wazazi fulani katika Japani wameanza kuwaajiri wapelelezi wa kibinafsi wawapeleleze watoto wao ili kuwalinda kutokana na watoto wanaodhulumu wengine shuleni. Kulingana na gazeti la habari la The Daily Yomiuri, profesa mmoja katika Chuo Kikuu cha Osaka aliyewafanyia uchunguzi zaidi ya wanafunzi 6,000 alisema hivi: “Kwa kawaida watoto wanaodhulumiwa ni wepesi kuficha familia zao jambo hilo, wakiogopa watafikiriwa kuwa wadhaifu.” Wazazi fulani wanaoshuku kwamba watoto wao wanasumbuliwa wanaficha kinasa-sauti ndani yao ili wasikilize mazungumzo yao. Wengine wamewaajiri wapelelezi wa kibinafsi wamfuate “mtoto kwa umbali ufaao, wakirekodi ithibati dhidi ya watesaji, na kutoa msaada mara moja kama malaika mlinzi, ili kuokoa maisha ya mtoto yanayohatarishwa.” Lakini watetezi wa watoto, lasema gazeti la habari hilo, “wanashutumu kupelelezwa kwa watoto na wazazi, kuwa hatua yenye kuogofya ielekeayo kuwatenga watoto hao walio wachanga wanaohitaji sana kutumaini mtu mzima, na kumweleza matatizo yake.” Hata hivyo, wazazi hudai kwamba ni njia moja ya kuwasaidia watoto wao wanaotaabika, mawasiliano yakosekanapo.