Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 8/22 kur. 20-22
  • Vijiwe vya Figo—Kutibu Maradhi ya Kale

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Vijiwe vya Figo—Kutibu Maradhi ya Kale
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mweneo na Visababishi
  • Matibabu Mapya
  • Ufundi wa Upasuaji Mdogo
  • Utibabu Bila Upasuaji
  • Uzuiaji
  • Mafigo Yako—Chujio la Kutegemeza Uhai
    Amkeni!—1997
  • ‘Ni ya Muda Tu!’—Maisha Yangu Nikiwa na Maradhi ya Figo
    Amkeni!—1996
  • Nilikubali Maoni ya Mungu Kuhusu Damu
    Amkeni!—2003
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 8/22 kur. 20-22

Vijiwe vya Figo—Kutibu Maradhi ya Kale

INAELEKEA kwamba umepata kusikia juu ya mtu aliyepatwa na ugonjwa wa vijiwe vya figo. Katika United States, watu wapatao 300,000 wanaougua ugonjwa wa vijiwe vya figo hulazwa hospitalini kila mwaka. Uchungu unaweza kuwa mkali sana, kama ule wa kujifungua mtoto.

Watu fulani wanafikiri kwamba vijiwe vya figo ni tatizo la kiafya la karibuni tu, labda likihusika na ulaji au mtindo wa maisha ya kisasa. Hata hivyo, kwa kweli vijiwe katika kijia cha mkojo vimesumbua binadamu kwa karne nyingi. Vimepatikana katika maiti zilizohifadhiwa Misri zenye umri wa maelfu ya miaka.

Vijiwe hivyo hutokea wakati madini katika mkojo yanaposhikamana na kukua, badala ya kuyeyushwa na kuondolewa nje ya mwili. Vijiwe hivyo huchukua umbo tofauti-tofauti na vimefanyizwa na vitu vingi mbalimbali. Clinical Symposia lasema: “Katika United States, karibu asilimia 75 ya vijiwe vyote vya figo hufanyizwa hasa kwa kalsiamu oksalati, na asilimia 5 nyingine zaidi hufanyizwa kwa kalsiamu fosfati isiyo na mchanganyiko wowote.”

Mweneo na Visababishi

Kulingana na ripoti moja, karibu asilimia 10 ya wanaume na asilimia 5 ya wanawake katika Amerika ya Kaskazini watapata ugonjwa wa kijiwe cha figo katika muda wa maisha yao. Na kiwango cha kurudia kwa ugonjwa huo ni cha juu. Mtu mmoja kati ya watu 5 ambao wamepata kijiwe cha figo watapata kijiwe kingine katika muda wa miaka mitano.

Sababu inayofanya watu fulani wapate vijiwe vya figo na wengine wasipate ni jambo ambalo limeshangaza madaktari kwa miaka mingi. Vijiwe vyaweza kufanyizwa kwa sababu nyingi. Hizo zinatia ndani magonjwa ya mfumo wa uyeyushaji wa mwili, maambukizo, magonjwa yaliyorithiwa, ukosefu wa daima wa maji mwilini, na ulaji.

Karibu asilimia 80 ya vijiwe vya figo hujiondoa vyenyewe wakati wa kukojoa. Ili kusaidia kuviondoa, wagonjwa hutiwa moyo wanywe kiasi kingi cha maji. Ingawa vijiwe hivyo huwa vidogo kwa kulinganisha, mara nyingi hata visiweze kuonekana na macho, uchungu unaweza kuwa mkali sana. Kijia cha mkojo kikiwa kimefungwa au kijiwe ni kikubwa mno kisiweze kupita (vinaweza kuwa vikubwa kama mpira wa gofu), basi utibabu utahitajiwa ili kulinda afya ya mgonjwa.

Matibabu Mapya

Kufikia karibu 1980, upasuaji mkubwa ulihitajiwa ili kuondoa vijiwe vya figo ambavyo havingepita vyenyewe. Ili kufikia kijiwe kilichokwama katika figo au katika kijia cha mkojo, mkato wenye uchungu, wenye urefu wa sentimeta 30, ulifanywa kwenye sehemu ya upande. Upasuaji huo kwa kawaida ulifuatwa na majuma mawili ya kupata nafuu katika hospitali na karibu miezi miwili ya mapumziko nyumbani. Lakini “kwa sababu ya maendeleo ya karibuni ya kitekinolojia,” kitabu cha mafundisho cha kitiba Conn’s Current Therapy (1989) chasema hivi, “uhitaji wa upasuaji wa nje ili kuondoa [vijiwe] hutokea mara chache sana.”

Sasa, vijiwe ambavyo ni vigumu kuondolewa vinaweza kuondolewa kwa ufundi unaotumia upasuaji mdogo sana. Ufundi mwingine unaotumiwa zaidi leo, uitwao mshtuko wa juu sana unaofanywa nje ya mwili kuponda vijiwe (ESWL), hauhitaji upasuaji wowote. Kikitaja mambo hayo mapya ya kitiba, Conn’s Current Therapy chasema kwamba upasuaji mkubwa “labda unatumiwa kwa asilimia 1 tu ya [vijiwe vyote vya figo].”

Ufundi wa Upasuaji Mdogo

Ufundi huo, unaohitaji upasuaji mdogo nyakati nyingine huitwa percutaneous ultrasonic lithotripsy. Neno “Percutaneous” lamaanisha “kupitia ngozi,” na “lithotripsy” lamaanisha kihalisi “kuponda.” Upasuaji wa pekee unaohitajika ni mkato wa sentimeta moja katika sehemu ya upande. Kupitia mkato huo, chombo kama kristokopi kinachoitwa nefroskopi kinaingizwa ndani. Sehemu ya ndani ya figo na kijiwe chenye kuleta matatizo vinaweza kuonwa kupitia chombo hicho.

Kijiwe kikiwa kikubwa sana hivi kwamba kisiweze kuondolewa kupitia nefroskopi, basi kitafutaji chenye kutikisika kinapitishwa kwenye kijia kilichopo ndani ya nefroskopi na hivyo kuingia ndani ya figo. Kisha, ili kiponde kijiwe hicho au vijiwe hivyo, kitafutaji hicho chenye tundu kinaunganishwa na jenereta yenye kutikisika sana inayofanya kitafutaji hicho kitikisike mara karibu 23,000 hadi 25,000 kwa sekunde moja. Mitikisiko hiyo ya juu sana inafanya kitafutaji hicho kitende kazi kama chombo cha kekee, kikipasua vijiwe vyote kinavyokuta ila tu vile vigumu zaidi.

Mfyonzo wa kuendelea kupitia kitafutaji hicho huondoa kabisa kitu chochote kilicho ndani ya figo, hivyo kikiiondolea figo vipande vidogo vya vijiwe. Upasuaji na ufyonzaji huo waendelea mpaka ukaguzi wa uangalifu uonyeshe kwamba mabaki yote ya kijiwe yameondolewa kupitia kitafutaji hicho.

Hata hivyo, nyakati nyingine kuna vipande vya kijiwe vinavyokataa kutoka. Katika hali hiyo, daktari anaweza kupitisha kupitia tundu la nefroskopi mrija mwembamba wenye kibano kilichoshikanishwa nacho. Kisha daktari anaweza kufungua vibano hivyo, ashike kijiwe hicho, na kukivuta nje.

Upasuaji wa kupitia ngozi ulipopata maendeleo, njia nyingi zilijaribiwa. Miaka michache iliyopita, jarida Urologic Clinics of North America lilisema hivi: “Njia mpya za kuondoa kijiwe kupitia ngozi huonekana kuwa zatokea kwa kila toleo jipya la mwezi la majarida ya kitiba.” Uwezekano wa kufaulu kwa njia hiyo, jarida hilo lilisema, “wategemea ukubwa na mahali kilipo kijiwe.” Lakini jambo kuu zaidi, jarida hilo likaeleza, ni “ustadi na maarifa ya mpasuaji.”

Ingawa nguvu nyingi zinatolewa za kupasua vijiwe hivyo vipande-vipande, njia hiyo ni salama kwa kulinganisha. “Uvujaji wa damu haujakuwa tatizo kubwa,” lasema jarida Clinical Symposia. Hata hivyo, ripoti moja inasema kwamba kuna uvujaji wa damu kwa karibu asilimia 4 ya wagonjwa.

Mafaa ya njia hiyo yatia ndani maumivu kidogo na muda mfupi wa kupata nafuu. Katika hali nyingi ni siku tano au sita tu zinazotumiwa katika hospitali, wagonjwa wengine hata wakienda nyumbani baada ya siku tatu tu. Mafaa hayo ni ya muhimu hasa kwa wafanyakazi, ambao wanaweza kuwa tayari kurudi kazini haraka iwezekanavyo baada ya kutoka hospitali.

Utibabu Bila Upasuaji

Utibabu mzuri sana ulioanzishwa katika Munich, Ujerumani, katika 1980, unaitwa mshtuko wa juu sana unaofanywa nje ya mwili kuponda vijiwe. Unatumia mshtuko wa juu sana wenye nguvu nyingi kupasua vijiwe vipande-vipande bila mikato yoyote kamwe.

Mgonjwa anaingizwa katika tangi ya chuma isiyopata kutu iliyojazwa kufikia nusu maji moto kidogo. Anawekwa kwa uangalifu hivi kwamba ile figo inayotibiwa inakuwa katikati ya mawimbi ya mshtuko unaotolewa na mfyatuo wa cheche kutoka chini ya maji. Mawimbi hayo yanapenya kwa urahisi mnofu wa binadamu na kufikia kijiwe bila kupoteza nguvu yazo zozote. Mawimbi hayo huendelea kushambulia kijiwe hicho mpaka kivunjike vipande-vipande. Kisha wagonjwa wengi hukojoa masalio ya kijiwe hicho kwa urahisi.

Kufikia 1990, njia ya ESWL ilikuwa ikitumiwa kwa karibu asilimia 80 ya visa vyote vya kuondoa vijiwe. Australian Family Physician liliripoti mwaka uliopita kwamba tangu ufundi huo ulipoanza kutumiwa, “wagonjwa zaidi ya milioni 3 ulimwenguni pote wametibiwa kwa zaidi ya mashine 1100, zenye kutumia jenereta za mawimbi ya mshtuko za aina kadhaa kuvunja vipande-vipande vijiwe vya figo.”

Ingawa njia ya ESWL huleta mshtuko kwa eneo la figo, Australian Family Physician laeleza hivi: “Ni mara chache sana inapoharibu viungo vilivyo karibu kama wengu, ini, kongosho, na tumbo. Mshtuko wa muda mfupi unavumiliwa kwa urahisi bila dhara kubwa kwa wagonjwa na wagonjwa wengi zaidi hulalamikia tu [maumivu kidogo ya misuli na mifupa] katika ukuta wa tumbo na kiasi kidogo cha [damu katika mkojo] kwa muda wa saa 24 hadi 48 baada ya kutibiwa.” Hata watoto wametibiwa kwa mafanikio. Jarida hili la Australia likamalizia hivi: “Baada ya miaka 10 ya uchanganuzi, inaonekana kwamba njia ya ESWL ni utibabu salama kabisa.”

Kwa kweli, utibabu huo una mafanikio sana hivi kwamba Conn’s Current Therapy cha mwaka uliopita kilieleza hivi: “(ESWL) imefanya vijiwe vya ugonjwa kutolewa kwa urahisi sana na kwa maumivu madogo sana hivi kwamba wagonjwa na matabibu wameacha kuzingatia sana utibabu wa ugonjwa wa kijiwe katika kijia cha mkojo.”

Lakini, vijiwe vya figo ni ugonjwa wenye uchungu sana ambao huwezi kutaka upatwe nao. Unaweza kufanya nini kuviepuka?

Uzuiaji

Kwa sababu vijiwe vya figo hurudi mara nyingi, ikiwa umepatwa na kimoja, kwa hekima utatii onyo la upole la kunywa maji mengi. Mkojo wa kiasi kinachozidi lita mbili kila siku hupendekezwa, na hiyo inamaanisha kunywa maji mengi sana!

Kwa kuongezea, ni jambo la hekima kurekebisha ulaji wako. Madaktari wanadokeza upunguze ulaji wako wa nyama nyekundu, chumvi, na vyakula vyenye oksalati (aina ya chumvi) nyingi, ambavyo vinaaminiwa kuwa vinachangia katika kufanyiza vijiwe. Vyakula hivyo vinatia ndani njugu, chokoleti, pilipili nyeusi, na mboga za kijani kibichi za majani-majani, kama spinachi. Madaktari walipendekeza pia kupunguza matumizi ya kalsiamu, lakini badala ya hivyo utafiti wa karibuni unaonyesha kwamba kuongeza matumizi ya kalsiamu katika ulaji kunaelekea kupunguza mfanyizo wa vijiwe.

Lakini, zijapokuwa tahadhari zako zote, ukipatwa na kijiwe kingine cha figo, kwa njia fulani inafariji kujua kwamba kuna njia zenye maendeleo za kuvitibu.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

Leonardo On the Human Body/Dover Publications, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Utibabu wa vijiwe vya figo usio wa upasuaji wenye kutumia mashine inayoitwa “lithotripter”

[Hisani]

S.I.U./Science Source/PR

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki