Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 11/22 kur. 11-14
  • ‘Ni ya Muda Tu!’—Maisha Yangu Nikiwa na Maradhi ya Figo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • ‘Ni ya Muda Tu!’—Maisha Yangu Nikiwa na Maradhi ya Figo
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Mbona Mimi?”
  • Maisha ya Tiba ya Kuondolewa Uchafu Katika Damu
  • Kutafuta Figo Mpya
  • Siogopi Kufa
  • ‘Ni ya Muda tu, Lee!’
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Mafigo Yako—Chujio la Kutegemeza Uhai
    Amkeni!—1997
  • Nilikubali Maoni ya Mungu Kuhusu Damu
    Amkeni!—2003
  • Vijiwe vya Figo—Kutibu Maradhi ya Kale
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 11/22 kur. 11-14

‘Ni ya Muda Tu!’—Maisha Yangu Nikiwa na Maradhi ya Figo

Ningali nakumbuka siku hiyo mapema Januari 1980 kana kwamba ni jana. Mama yangu alikuwa amenituma dukani kununua mkate, lakini nilipokuwa nikiondoka tu nyumbani, simu ililia. Ni daktari wangu aliyekuwa akipiga simu kutupatia matokeo ya upimwaji wangu katika maabara. Kwa ghafula, mama akabubujika machozi. Katikati ya kwikwi zake, akaniambia hizo habari mbaya. Figo zangu zilikuwa zikidhoofika. Zingetumika kwa mwaka mmoja au miaka miwili tu. Huyo daktari alikuwa amesema kweli—mwaka mmoja baadaye nilianza “dialysis,” ambayo ni tiba ya kuondoa uchafu katika damu.

NILIZALIWA Mei 20, 1961, nikiwa kifungua mimba cha watoto sita. Nilipofikia karibu umri wa miezi sita, mama yangu aliona damu katika mkojo katika nepi zangu. Baada ya kupimwa sana, hali yangu iligunduliwa kuwa ugonjwa wa Alport, kasoro ya kurithiwa iliyo nadra sana. Kwa sababu ambazo hazieleweki, mara nyingi figo za wanaume wenye maradhi hayo hushindwa kufanya kazi baada ya muda fulani. Wazazi wangu nami hatukuambiwa jambo hilo, kwa hiyo sikuwa na wasiwasi kuhusu maradhi ya figo.

Kisha, katika kiangazi cha 1979, nilihisi harufu kama ya amonia katika pumzi yangu wakati wa asubuhi. Sikufikiria sana jambo hilo, lakini nikaanza kuhisi uchovu. Nikadhani nilikuwa tu nimekosa kufanya mazoezi, hivyo nikalipuuza tatizo hilo. Katika Desemba nilienda kwa upimwaji wangu wa kila mwaka, na Januari nilipata hiyo simu ambayo imetajwa hapo juu.

Nilipokuwa nikienda dukani—kwani mama bado alitaka mkate—nilikuwa nimeshtuka sana. Sikuamini kwamba jambo hilo lilikuwa likinipata. “Nina umri wa miaka 18 pekee!” Nikalia. Nikapeleka gari kando ya barabara na kusimama. Uzito wa kilichokuwa kikinipata ukaanza kuniingia.

“Mbona Mimi?”

Nikiwa nimeketi hapo kando ya barabara, nilianza kulia machozi. Huku machozi yakinitiririka, nikasema kwa sauti: “Kwa nini iwe ni mimi, Mungu? Kwa nini iwe ni mimi? Tafadhali usiruhusu figo zangu zidhoofike!”

Kadiri miezi ya 1980 ilivyozidi kupita, ndivyo nilivyozidi kuhisi vibaya; na ndivyo sala zangu zilivyozidi kuwa zenye kukata tamaa na zenye machozi. Kufikia mwisho wa mwaka, nilikuwa nikizimia na kutapika mara kwa mara kwa sababu ya kuongezeka kwa uchafu wa sumu katika damu yangu, sumu ambazo hazikuwa zikichujwa na figo zangu ambazo zilikuwa zikidhoofika. Novemba nilienda safari ya mwisho ya kupiga kambi na marafiki fulani. Lakini nikawa mgonjwa sana hivi kwamba niliketi tu katika gari mwisho-juma wote, nikitetemeka—nilishindwa kupata joto, japo jitihada zangu zote. Hatimaye, katika Januari 1981, jambo ambalo halikuweza kuepukika likatendeka—figo zangu zilishindwa kabisa kufanya kazi. Ilikuwa ni lazima nianze tiba ya kuondolewa uchafu katika damu au nife.

Maisha ya Tiba ya Kuondolewa Uchafu Katika Damu

Miezi michache mapema, daktari wa familia yetu alikuwa ameniambia juu ya aina mpya ya tiba ya kuondoa uchafu katika damu ambayo haihusishi sindano na ambayo inasafisha damu ndani ya mwili. Tiba hiyo inaitwa peritoneal dialysis (PD). Hiyo ikanivutia mara moja, kwa kuwa nimechukia sana sindano. Hiyo ilikuwa imekuwa tiba inayofanya kazi ya badala kwa wagonjwa wengine wa kuondolewa uchafu katika damu.

Kwa kushangaza, miili yetu ina utando ambao unaweza kufanya kazi kama figo bandia. Kile kitambi cha tumbo—utando laini wenye kupenyezwa na nuru ambao hufanyiza kifuko kuzingira viungo vya kumeng’enya chakula—chaweza kutumiwa kama kichujio cha kusafisha damu. Sehemu ya ndani ya utando huo ina nafasi inayoitwa uvungu wa kitambi cha tumbo. Hicho kitambi cha tumbo ni kama mfuko mtupu, kikiwa kimebanwa katikati ya viungo vya fumbatio.

Hivi ndivyo PD inavyofanya kazi: umajimaji wa kipekee wa kuondoa uchafu katika damu huwekwa katika uvungu wa kitambi cha tumbo kupitia katheta (mrija) ambayo imepachikwa kupitia upasuaji katika sehemu ya chini ya fumbatio. Umajimaji huo una deksitrosi, na kwa njia ya osmosi, uchafu wa mwili na umajimaji wa ziada kutoka kwa damu huvutwa kupitia kitambi cha tumbo na kuingizwa katika umajimaji wa kuondoa uchafu ambao upo katika uvungu wa kitambi cha tumbo. Uchafu ambao kwa kawaida ungeondoshwa ukiwa mkojo sasa umo katika umajimaji wa kuondoa uchafu. Mara nne kwa siku, ni lazima uondoe umajimaji uliotumiwa na kisha uujaze uvungu kwa umajimaji safi. Kufanya hivyo huchukua karibu dakika 45. Ni kama tu kubadili oili katika gari—ondoa chafu na kuweka mpya ili kuongeza mwendo na kusaidia mwili utende kwa uanana!

Mwanzo wa Januari 1981, niliwekewa katheta iliyohitajika katika sehemu ya chini ya upande wa kulia wa fumbatio langu. Kisha, nikazoezwa kwa majuma mawili kutumia njia hiyo. Njia hiyo isipofanywa vizuri, kwa kutumia hali ya juu ya usafi, mtu aweza kupatwa na mchochota wa kitambi cha tumbo—ambukizo hatari liwezalo kuua.

Katika kiangazi cha 1981, karibu miezi sita baada ya kuanza tiba ya PD, wazazi wangu walipata simu nyingine ambayo ilikuja kuathiri sana maisha yangu.

Kutafuta Figo Mpya

Tangu Januari 1981, nilikuwa nimekuwa katika orodha ya kitaifa ya kupachikwa figo.a Nilitumaini kwamba kwa mpachiko maisha yangu yangerudia kawaida. Kumbe sikujua yaliyokuwa yakija!

Simu iliyopigwa katikati ya Agosti ilituarifu kwamba mpaji mmoja alikuwa amepatikana. Nilipoenda hospitalini, karibu saa 4 za usiku, walipima damu ili kuhakikisha kwamba nilifaana na mpachiko. Figo hiyo ilitolewa na familia ya kijana mmoja aliyekuwa amekufa katika aksidenti mapema siku hiyo.

Upasuaji ukapangiwa asubuhi iliyofuata. Kabla ya upasuaji huo kufanywa, ilikuwa ni lazima suala kubwa lijadiliwe, kwa kuwa mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova na dhamiri yangu iliyozoezwa na Biblia hainiruhusu kutiwa damu mishipani. (Matendo 15:28, 29) Usiku huo wa kwanza daktari nusukaputi akaja kuniona. Akanihimiza nikubali damu iwekwe katika chumba cha upasuaji, hali ya dharura ikitokea. Nikakataa.

“Nifanye nini shida ikitokea? Nikuache ufe?” yeye akauliza.

“Fanya jambo jingine lolote unalopaswa kufanya, lakini nisiwekwe damu, hata hali iweje.”

Baada ya yeye kuondoka, madaktari wapasuaji wakaja. Nikajadili suala lilo hilo pamoja nao, na jambo lililonituliza sana ni kwamba walikubali kunifanyia upasuaji bila kutumia damu.

Upasuaji huo wa muda wa saa tatu na nusu ulifanywa bila tatizo lolote. Daktari mpasuaji alisema kwamba nilipoteza damu kidogo sana. Nilipoamka katika chumba cha kupata nafuu, mambo matatu yakaja akilini mara hiyo—kwanza njaa ikifuatwa na kiu kisha maumivu! Lakini yote hayo yakatoweka nilipoona mfuko sakafuni, ukijaa kwa umajimaji wenye rangi ya kimanjano na nyekundu-nyeupe. Ulikuwa ni mkojo kutoka kwa figo langu jipya. Hatimaye nilikuwa nakojoa! Ile katheta ilipoondolewa kutoka kwenye kibofu changu na nilipoweza kukojoa kama kila mtu, nilifurahi sana.

Hata hivyo, shangwe yangu ikawa ya muda tu. Siku mbili baadaye nilipata habari za kunishusha moyo kabisa—figo langu jipya halikuwa likifanya kazi. Ilikuwa ni lazima nianze tiba ya kuondoa uchafu katika damu nikitumaini kwamba hilo litalipa figo jipya wakati wa kuanza kufanya kazi. Niliendelea na tiba ya kuondoa uchafu mwilini kwa majuma kadhaa.

Sasa ilikuwa ni katikati ya Septemba, na nilikuwa nimekuwa hospitalini kwa karibu mwezi mmoja. Hiyo hospitali ilikuwa karibu kilometa 80 kutoka nyumbani, hivyo ilikuwa vigumu kwa ndugu na dada zangu Wakristo kunizuru. Nilihisi nimekosa kutaniko sana. Nilipokea mirekodio ya kaseti ya mikutano ya kutaniko, lakini nilipozisikiliza, nilishindwa na hisia. Nilitumia muda wa saa nyingi za upweke nikizungumza na Yehova Mungu katika sala, nikimwomba anipe nguvu ya kuendelea kuvumilia. Sikujua wakati huo kwamba majaribio magumu hata zaidi yalikuwa mbele.

Siogopi Kufa

Majuma sita marefu yalikuwa yamepita tangu ule mpachiko, na kwa sasa ilikuwa wazi kwa njia yenye kutia uchungu kwamba mwili wangu ulikuwa umekataa figo hilo. Fumbatio langu lilikuwa limefura vibaya; madaktari wakaniambia kwamba ni lazima figo hilo lililokataliwa litolewe. Tena suala la damu likazuka. Madaktari wakaeleza kwamba wakati huu upasuaji ulikuwa hatari zaidi, kwa sababu nilikuwa na damu kidogo sana. Kwa subira na kwa uthabiti nilieleza msimamo wangu unaotegemea Biblia, na hatimaye wakakubali kunifanyia upasuaji bila damu.b

Baada ya upasuaji, mambo yaliharibika haraka sana. Nilipokuwa katika chumba cha kupata nafuu, mapafu yangu yalianza kujaa umajimaji. Baada ya usiku kucha wa kuondolewa uchafu mwingi katika damu, nilihisi afadhali kidogo. Lakini siku mbili baadaye mapafu yangu yakajaa tena. Usiku mwingine tena wa kuondolewa uchafu katika damu ukafuata. Sikumbuki mambo mengi yaliyotendeka usiku huo, lakini nakumbuka baba yangu akiwa kando yangu, akisema: “Pumua mara moja tu tena, Lee! Jaribu. Unaweza kufaulu! Pumua mara moja tu. Ndiyo, unafanya vizuri, endelea kupumua!” Nilikuwa nimechoka sana, kuliko wakati mwingine wowote. Nilitaka tu mambo yaishe na niamke katika ulimwengu mpya wa Mungu. Sikuogopa kufa.—Ufunuo 21:3, 4.

Asubuhi iliyofuata hali yangu ikawa mbaya sana. Kiwango cha chembe zangu nyekundu katika damu yenye kuzunguka kilikuwa chini sana, chini kufikia hematokriti 7.3—kawaida zinakuwa zaidi ya 40! Madaktari hawakutazamia nipone. Walijaribu kwa kurudia-rudia kunifanya nikubali kutiwa damu mishipani, wakisema ni muhimu ili nipate nafuu.

Nilipelekwa katika chumba cha utibabu wa dharura, kisha kiwango cha chembe zangu nyekundu za damu zikapungua hadi hematokriti 6.9. Lakini kwa msaada wa mama yangu, chembe nyekundu zangu za damu zikaanza kuongezeka polepole. Katika kikorogeo nyumbani, yeye alikuwa akitengeneza vinywaji kutoka kwa vyakula vyenye chuma kingi na kuniletea. Hata alivinywa pamoja nami ili kunitia moyo. Upendo wa mama kwa watoto wake ni kitu cha ajabu sana.

Niliporuhusiwa kutoka hospitalini katikati ya Novemba, kiwango cha chembe zangu nyekundu kilikuwa hematokriti 11. Mapema katika 1987, nilianza kutumia EPO (erithropoietini), homoni ya kisanisia ambayo huchochea uboho wa mifupa kupeleka chembe nyekundu za damu katika mkondo wa damu, na sasa kiwango cha chembe zangu nyekundu ni karibu hematokriti 33.c

‘Ni ya Muda tu, Lee!’

Nilifanyiwa upasuaji mwingine katika 1984, 1988, 1990, 1993, 1995, na 1996—huo wote kwa sababu ya mafigo yangu kushindwa kufanya kazi. Katika miaka hii mingi ya kuishi na maradhi ya figo, wazo moja ambalo limeniendeleza ni, ‘Ni ya muda tu.’ Hata matatizo yetu yawe gani, ya kimwili au yoyote ile, yatasahihishwa chini ya Ufalme wa Mungu katika ulimwengu mpya unaokuja. (Mathayo 6:9, 10) Wakati wowote nikabilipo ugumu mpya na kuanza kuhisi nimeshuka moyo, mimi hujiambia tu, ‘Ni ya muda tu, Lee!’ na hiyo hunisaidia kuona mambo kwa njia ifaayo.—Linganisha 2 Wakorintho 4:17, 18.

Mwaka wa 1986 ulikuwa na mshangao mkubwa zaidi kwangu—nilifunga ndoa. Nilikuwa nimefikiri sitafunga ndoa. ‘Ni nani angependa kufunga ndoa nami?’ Nilijiuliza. Lakini Kimberly akatokea. Akaniona jinsi nilivyo kwa ndani, si jinsi nilivyogonjeka kwa nje. Yeye aliona pia kwamba hali yangu ni ya muda tu.

Mnamo Juni 21, 1986, Kimberly nami tukafunga ndoa katika Jumba la Ufalme la kwetu katika Pleasanton, California. Tumeamua tusizae watoto wowote, kwa kuwa maradhi yangu ni ya kurithiwa. Labda hii pia ni ya muda tu. Katika ulimwengu mpya wa Mungu, tungependa kuzaa watoto ikiwa ni mapenzi ya Yehova.

Leo nina pendeleo la kutumikia nikiwa mzee katika Kutaniko la Highland Oaks katika California, na Kimberly anatumikia akiwa mweneza-evanjeli wa wakati wote. Siku hizi afya yangu ni afadhali; hilo pigo la 1981 lilimaliza mwili wangu na kufanya nikose nguvu. Tangu wakati huo, dada yangu amesitawisha aina hafifu ya ugonjwa wa Alport, na figo za ndugu zangu wawili zimeshindwa kufanya kazi na sasa wanatibiwa kwa njia ya kuondoa uchafu katika damu. Ndugu zangu wengine wawili wana afya nzuri.

Ninaendelea kutibiwa kwa njia ya peritoneal dialysis, na nina shukrani kwa uwezo inayonipa wa kufanya mambo. Natazamia wakati ujao kwa tumaini na uhakika kwa sababu matatizo ya leo—kutia ndani maradhi ya figo—ni ya muda tu.—Kama ilivyosimuliwa na Lee Cordaway, aliyekufa kabla ya makala hii kupigwa chapa.

Amkeni! halipendekezi njia yoyote hususa ya tiba. Makala hii haikusudii kuvunja moyo njia nyinginezo za tiba, kama vile hemodialysis. Kuna mabaya na mazuri ya kila aina ya tiba, na ni lazima kila mtu binafsi afanye uamuzi wake wenye kutegemea dhamiri kuhusu ni tiba gani ambayo atatumia.

[Maelezo ya Chini]

a Kama Mkristo atakubali mpachiko au hapana ni uamuzi wa kibinafsi.—Ona Mnara wa Mlinzi la Septemba 1, 1980, ukurasa 24.

b Kwa habari zaidi kuhusu upasuaji bila damu, ona Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., kurasa 16-17.

c Ikiwa Mkristo atakubali EPO au hapana ni uamuzi wa kibinafsi.—Ona Mnara wa Mlinzi la Oktoba 1, 1994, ukurasa 31.

[Mchoro katika ukurasa wa 13]

Jinsi “peritoneal dialysis” inavyofanya kazi

Ini

Vitanzi vya utumbo mwembamba

Katheta (hupokea myeyusho safi; huondoa myeyusho mchafu)

Kitambi cha tumbo

Uvungu wa kitambi cha tumbo

Kibofu

[Picha katika ukurasa wa 12]

Nikiwa na mke wangu, Kimberly

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki