Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 11/22 kur. 15-18
  • Simbamarara! Simbamarara!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Simbamarara! Simbamarara!
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maisha ya Familia ya Simbamarara
  • Kukua Wakiwa Simbamarara
  • Fungu la Baba
  • Wala-Watu?
  • Wakati Ujao wa Paka Huyo Mkuu
  • Simbamarara wa Siberia—Je, Ataokoka?
    Amkeni!—2008
  • Usalama wa Kweli—Mradi Ulio Mgumu Kufikia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 11/22 kur. 15-18

Simbamarara! Simbamarara!

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA

‘WAKATI fulani nilikuwa nikitembea kandokando ya kilima fulani chembamba,’ akumbuka Dakt. Charles McDougal, ambaye ametumia miaka mingi akijifunza kuhusu simbamarara katika Hifadhi ya Kitaifa ya Royal Chitwan katika Nepal. ‘Nilipokuwa nikitembea, simbamarara alikuwa akija kutoka upande ule mwingine. Ni kama tulikutana kileleni, na kulikuwa na hatua chache kati yetu—hatua 15 hivi.’ Dakt. McDougal alisimama tuli. Badala ya kumtazama simbamarara machoni, jambo ambalo simbamarara huona kuwa mwito wa ushindani, yeye alitazama bega la simbamarara. Simbamarara huyo alibaki akiwa amejikunyata chini lakini hakusongea ili kushambulia. Baada ya dakika kadhaa zilizoonekana kuwa muda mrefu sana, Dakt. McDougal alichukua hatua chache kurudi nyuma. ‘Kisha,’ asema, ‘Niligeuka tu na kurudi kule nilikotoka.’

Mwanzoni mwa karne hii, kulikuwa na simbamarara 100,000 katika makao yao ya Asia, kutia ndani 40,000 hivi katika India. Kufikia 1973 idadi ya ulimwenguni ya viumbe hawa wenye fahari ilikuwa imepunguzwa hadi kufikia chini ya 4,000, hasa kwa sababu ya kuwindwa. Simbamarara, paka mkubwa zaidi duniani, alikuja kutishwa kutoweshwa na mwanadamu. Lakini je, simbamarara ni tisho kwa wanadamu? Paka huyu mkuu yukoje hasa? Je, jitihada za kumwokoa asitoweke zimefanikiwa?

Maisha ya Familia ya Simbamarara

Miaka mingi ya utazamaji wenye subira imeelewesha zaidi wataalamu wa maumbile ya asili juu ya maisha ya simbamarara. Ebu tuwazie kwamba tunatazama familia ya kawaida ya simbamarara katika misitu yenye kupendeza ya Ranthambhore, kaskazini mwa India. Dume ana karibu urefu wa meta tatu kutoka pua yake hadi ncha ya mkia wake na ana uzani wa kilogramu 200 hivi. Mwenzi wake ana urefu wa meta 2.7 hivi na uzani wa kilogramu 140 hivi.a Kuna watoto watatu, mmoja wa kiume na wawili wa kike.

Halijoto katika misitu hii yaweza kuzidi digrii 45 Selsiasi, lakini familia ya simbamarara hupata kivuli chini ya miti yenye majani mengi. Nao waweza sikuzote kufurahia kuogelea katika maji baridi ya ziwa lililoko karibu. Paka waogeleao? Ndiyo, simbamarara hupenda maji! Kwa hakika, wamejulikana kuogelea kwa zaidi ya kilometa tano bila kusimama.

Nuru ya jua yapenya katikati ya miti hadi kwenye manyoya ya simbamarara ya rangi ya machungwa yenye kung’aa, ikiyafanya yaonekane kama kwamba yanawaka. Ile mistari myeusi humetameta, na mapaku meupe juu ya macho yenye rangi ya manjano-machungwa humweka kwa wangavu. Baada ya kuwatazama watoto watatu kwa muda fulani, inakuwa rahisi kwetu kutofautisha mmoja na mwenzake kwa alama tofauti za mistari na za uso.

Kukua Wakiwa Simbamarara

Mama simbamarara alipokuwa akitarajia watoto wake, alitafuta pango lifaalo, lililofichwa vizuri na mimea. Kutoka hapo, familia hiyo sasa hufurahia kutazama uwanda wakiwa juu pamoja na kisima ambacho huwavutia wanyama wengine. Simbamarara huyo wa kike alichagua mahali hapa ili aweze kuwinda chakula bila ya kuwa mbali na watoto wake.

Tangu kuzaliwa, watoto hao walipata uangalifu mwingi sana. Utotoni mwao wote mama yao aliwakumbatia katikati ya miguu yake, kuwagusagusa kwa pua, na kuwalamba, huku akiwanong’onezea kwa wororo. Watoto hao walipokuwa wakubwa, walianza kucheza mchezo wa kujificha na kutafutana na kupigana kimchezo. Ingawa watoto wa simbamarara hawawezi kukoroma, kuanzia umri wa mwaka mmoja hivi, wao hupumua nje kwa mianguo mikubwa, ya sauti kuu wakati mama yao anaporudi baada ya kutowepo.

Watoto hao hupenda kuogelea na kucheza katika maji, pamoja na mama yao. Ona akilini simbamarara wa kike akiwa ameketi kwenye ukingo wa ziwa mkia wake ukiwa majini. Mara kwa mara, yeye arusha mkia wake ili kuurushia mwili wake wenye ujoto maji baridi. Na kwa habari ya mikia, watoto hawachoki kamwe kuushika mkia wa mama yao anapoutikisa kutoka upande mmoja hadi mwingine. Kwa kufanya hivi, simbamarara huyo wa kike hachezi tu na watoto wake; bali pia anawafundisha ustadi wa kurukia, ambao watautumia baadaye, wanapoanza kuwinda. Watoto hao pia hupenda kupanda miti. Lakini kufikia umri wa miezi 15, wamekuwa wakubwa na wazito sana kuweza kupanda miti kwa urahisi.

Fungu la Baba

Hadi hivi majuzi, wengi waliamini kwamba mama simbamarara aliwalea watoto peke yake na kwamba yule wa kiume angewaua watoto akipata fursa. Hata hivyo, sivyo ilivyo kuhusu simbamarara wengi. Baba simbamarara hutokomea msituni kwa vipindi virefu, akizurura katika eneo lake la zaidi ya kilometa 50 za mraba. Lakini pia huzuru familia yake. Anapofanya hivyo, huenda akajiunga na simbamarara wa kike na watoto katika uwindaji, hata kushiriki windo pamoja nao. Mtoto wa kiume mwenye ugomvi zaidi aweza kuchukua zamu yake ya kula kwanza. Ingawa hivyo, akiwazuia dada zake kwa pupa kwa muda mrefu, mama yake humdukua au hata kumchapa kofi kwa mguu wake ili kuruhusu watoto wa kike wapate sehemu yao ya karamu hiyo.

Watoto hao hufurahia kucheza na baba yao mkubwa sana. Mahali papendwapo sana kwa jambo hilo ni mahali pa kunywa maji palipo karibu. Baba simbamarara hujiachilia kinyume-nyume kuingia majini azame hadi kufikia kichwani. (Simbamarara hawapendi maji yarukie macho yao!) Kisha yeye huwaruhusu watoto wake wamguseguse kwa pua huku akiwalamba nyuso zao. Kwa wazi, kuna kifungo chenye nguvu cha familia.

Wala-Watu?

Vitabu na filamu mara nyingi huwaonyesha simbamarara kuwa viumbe wakali na washambulizi, wenye kunyemelea na kushambulia wanadamu, wakiwaparuza na kuwala. Hiyo si kweli hata kidogo. Simbamarara si wala-watu kamwe. Kwa kawaida, simbamarara amwonapo mtu msituni, yeye hupendelea kwenda zake kimya-kimya. Kwa kupendeza, simbamarara hawawezi kutambua harufu ya binadamu.

Hata hivyo, chini ya hali fulani simbamarara mwenye njaa aweza kuwa hatari sana. Akipoteza meno kwa sababu ya uzee au ameumizwa na wanadamu, huenda akashindwa kuwinda kwa njia ya kawaida. Vivyo hivyo, ikiwa makao ya wanadamu yanaingia hadi kwenye makao ya simbamarara, mawindo ya kiasili ya simbamarara huenda yakapungua. Kwa sababu kama hizi, watu 50 hivi kila mwaka huuawa na simbamarara katika India, ingawa idadi hii ni chache zaidi mara mia moja kuliko idadi inayouawa na nyoka. Mashambulio ya simbamarara hutukia hasa katika mabwawa ya mahali ambapo mto Ganges hugawanyika.

Kulingana na Dakt. McDougal, simbamarara si hatari sana kama vile watu fulani hufikiri. Ingawa kumshtua simbamarara kwa karibu sana kwaweza kusababisha shambulizi, “simbamarara ni mnyama mtulivu sana na mpole,” yeye asema. “Kwa kawaida, ukikutana na simbamarara—hata akiwa karibu sana—yeye hatashambulia.”

Miongoni mwa simbamarara ugomvi ni nadra sana. Kwa mfano, simbamarara mchanga aweza kuzurura kuingia katika eneo la simbamarara mwingine na kukutana na dume wa hapo. Kitakachotokea ni mingurumo yenye kuogofya, na kutoa ukali wakiwa wamekabiliana pua kwa pua. Lakini dume mwenye umri mkubwa zaidi anapoonyesha ukuu wake, yule mchanga kwa kawaida atajibiringisha na kulala chali kama ishara ya ujitiisho, na mkabala huo waisha.

Wakati Ujao wa Paka Huyo Mkuu

Badala ya kuwa hatarini kwa sababu ya simbamarara, mwanadamu amethibitika kuwa hatari pekee ya kweli kwa simbamarara. Kwa wakati huu, jitihada zafanywa ili kumwokoa simbamarara asitoweke. Nchi kadhaa za Asia zimeanzisha hifadhi za simbamarara. Katika 1973, mradi wa kipekee uitwao Mradi wa Simbamarara ulianzishwa katika Hifadhi ya Kitaifa ya Corbett, katika India kaskazini. Fedha na vifaa kwa ajili ya Mradi wa Simbamarara viliwasili kutoka kotekote ulimwenguni. Hatimaye, hifadhi 18 za simbamarara zilianzishwa katika India, zikiwa na eneo la jumla la zaidi ya kilometa za mraba 28,000. Kufikia 1978, simbamarara pia waliwekwa katika orodha ya spishi zilizo hatarini mwa kutoweka. Kulikuwa na matokeo yenye kushangaza! Kabla ya uwindaji wa simbamarara kupigwa marufuku, simbamarara walikuja kuwa wahepaji na kutokea hasa usiku kwa sababu ya kuhofu mwanadamu. Lakini baada ya miaka fulani ya ulinzi, simbamarara walianza kutembea-tembea katika hifadhi na kuwinda mchana!

Hata hivyo, kuna tisho lenye kuendelea kwa simbamarara: uhitaji wa kimataifa wa dawa za Kiasia za kitamaduni zitengenezwazo kutokana na sehemu za mwili wa simbamarara. Kwa kielelezo, mfuko mmoja wa mifupa ya simbamarara, waweza kuleta zaidi ya dola 500 katika India; na kufikia wakati mifupa inapotayarishwa na kufikia masoko ya Mashariki ya Mbali, thamani imeongezeka hadi zaidi ya dola 25,000. Kukiwa na fedha hizi nyingi ziwezazo kupatikana, wanakijiji maskini wanashawishiwa kushirikiana na wawindaji-haramu wa simbamarara katika kushindana na walinzi wa misitu. Mwanzoni, jitihada za kumwokoa simbamarara zilionwa kuwa zinafaulu. Lakini tangu 1988, hali imegeuka kuwa mbaya. Leo, ni simbamarara 27 hivi tu wanaozunguka-zunguka Ranthambhore, wakilinganishwa na 40 ambao walikuwapo miaka 20 iliyopita. Na idadi ya ulimwenguni ya simbamarara yaweza kuwa chini sana kama 5,000!

Hadi kufikia mwishoni mwa karne iliyopita, simbamarara na wanadamu wameishi pamoja katika India kwa upatano wa kadiri. Je, wataweza kufanya hivyo tena? Kwa sasa, mwito wenye msisimko “Simbamarara! Simbamarara!” waweza bado kumaanisha kuonekana kwa paka mkubwa zaidi ulimwenguni. Iwe programu za hifadhi zitaweza kuhakikisha usalama wa simbamarara wakati ujao au la haijulikani. Lakini Biblia hutuhakikishia kwamba siku moja dunia yote itakuwa paradiso kama Bustani ya Edeni. Kisha mwanadamu na viumbe wa porini kama vile simbamarara watashiriki dunia kwa amani.—Isaya 11:6-9.

[Maelezo ya Chini]

a Simbamarara wa Siberia, spishi-ndogo kubwa zaidi, aweza kuwa na uzani wa kilogramu 320 na kufikia urefu wa meta nne.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa17]

Simbamarara Mweupe

Akiwa hazina ya kitaifa katika India, simbamarara mweupe aliye nadra ni tokeo la jeni-mgeuko iliyo fifi. Katika 1951 mtoto mweupe wa kiume alikamatwa katika Msitu wa Rewa wa India. Alipojamiiana na simbamarara wa kike wa rangi ya kawaida, watoto wa kawaida walizaliwa. Hata hivyo, wakati jike kutoka mmojapo watoto hao alipojamiiana na yule dume mweupe, alizaa watoto wanne weupe. Uzalishaji wenye uangalifu umefanya iwezekane kwa watu katika mahali pengi kuona mnyama huyo mwenye kuvutia aliye nadra katika hifadhi zao za wanyama.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Paka waogeleao? Ndiyo!

[Picha katika ukurasa wa 17]

Simbamarara si hatari sana kama vile watu wengi hufikiri

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki