Usalama wa Kweli—Mradi Ulio Mgumu Kufikia
ARNOLD alikuwa mtoto ambaye alipenda kichezeo chake cha simbamarara kilichojazwa sufu. Kila alipokwenda, alikiburuta—wakati wa kucheza, wakati wa kula, hadi kitandani mwake. Kwake, simbamarara huyo aliandaa faraja, usalama. Siku moja, kulikuwa na tatizo. Simbamarara alipotea!
Arnold alipokuwa akilia, mama, baba, na ndugu zake wakubwa watatu walipekua-pekua nyumba yao kubwa ili kumpata simbamarara. Hatimaye mmoja wao aligundua alimokuwa, katika kisanduku cha meza. Kwa wazi, Arnold alikuwa amemweka hapo na kusahau mara hiyo mahali alipokuwa. Simbamarara alirudishwa, Arnold akaacha kulia. Alihisi furaha na salama tena.
Ingekuwa vizuri kama nini ikiwa matatizo yote yangeweza kutatuliwa kwa urahisi hivyo—kwa urahisi kama tu kupata simbamarara wa kichezeo katika kisanduku cha meza! Hata hivyo, kwa watu wengi, masuala ya usalama ni yenye uzito zaidi na tata kuliko hilo. Karibu kila mahali, watu wanajiuliza, ‘Je, nitakuwa mhasiriwa wa uhalifu au jeuri? Je, nimo hatarini mwa kupoteza kazi yangu? Je, familia yangu ina uhakika wa kuwa na chakula cha kutosha? Je, wengine wataniepuka kwa sababu ya dini yangu au malezi yangu ya kikabila?’
Idadi ya watu wanaokosa usalama ni kubwa sana. Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu watu bilioni tatu hawakosi tu fursa ya kupata matibabu ya maradhi ya kawaida bali pia hukosa dawa muhimu. Zaidi ya watu bilioni moja huishi katika umaskini wa kupindukia. Karibu bilioni moja, ingawa wanaweza kufanya kazi, wana kazi isiyo ya wakati wote. Idadi ya wakimbizi inaongezeka. Kufikia mwishoni mwa 1994, 1 hivi kati ya kila watu 115 duniani alikuwa amelazimika kutoroka makwao. Mamilioni ya uhai yanaharibiwa kwa sababu ya ulanguzi wa dawa za kulevya ambao kila mwaka huchuma dola bilioni 500 na kutokeza vitendo visivyohesabika vya uhalifu na jeuri. Vita huharibu maisha za mamilioni. Katika 1993 pekee, nchi 42 zilijihusisha katika vita kubwa, huku nyinginezo 37 zikipatwa na jeuri ya kisiasa.
Vita, umaskini, uhalifu, na matisho mengine kwa usalama wa binadamu yanahusiana, nayo yanaongezeka. Hakuna masuluhisho rahisi kwa matatizo hayo. Kwa hakika, binadamu hawatayatatua kamwe.
“Msiwatumainie wakuu, wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake,” latahadharisha Neno la Mungu, Biblia. Basi, tumtumaini nani? Andiko hilo huendelea hivi: “Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, na tumaini lake ni kwa BWANA, Mungu wake, aliyezifanya mbingu na nchi, bahari na vitu vyote vilivyomo.”—Zaburi 146:3-6.
Kwa nini twaweza kumtumaini Yehova kuleta usalama kwenye dunia hii? Je, yawezekana kufurahia maisha salama, zenye furaha sasa? Mungu ataondoaje vizuizi vya usalama wa binadamu?