Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Maradhi ya Figo Ile makala “‘Ni ya Muda Tu!’—Maisha Yangu Nikiwa na Maradhi ya Figo” (Novemba 22, 1996) ilifanikiwa katika kutia moyo mume wangu nami katika wakati mgumu sana. Kama vile mwandikaji wa makala hiyo, mume wangu ameanza tiba ya peritoneal dialysis, na hali imekuwa ngumu. Mara nyingine hali ya kukata tamaa hutuzidi. Lakini makala yenu ilikuwa faraja kubwa sana, ikitukumbusha kwamba kasoro ya figo ni ya muda tu na kwamba karibuni itaondoshwa kabisa na Ufalme wa Mungu, pamoja na magonjwa mengine yote.
V. Q., Italia
Kusoma juu ya mwanamume ambaye alithamini sana familia na ibada yake japo mapambano ya maisha yote na maradhi kulinifanya nibubujike machozi. Mimi ni mweneza-evanjeli wa wakati wote mwenye umri wa miaka 18 na mwenye afya nzuri, na ninatambua ni mara nyingi jinsi gani siichukulii afya yangu kwa uzito. Imani ya Lee Cordaway na mtazamo wake zilikuwa zenye kutia moyo sana kusoma.
J. S., Marekani
Katika 1992, nikiwa na umri wa miaka 11, niligundua kwamba nilikuwa na maradhi ya figo, ambayo hatimaye yalifanya mafigo yashindwe kufanya kazi. Nililazimika kupata tiba ya kuondolewa kwa uchafu katika damu. Ninathamini kwamba mliieleza njia hiyo vizuri sana kwani mara nyingi watu hushangaa jinsi inavyofanya kazi. Ilinitia moyo na pia rafiki zangu kusoma kwamba hali ninayokabili leo haitakuwepo kwa wakati wote.
A. H., Marekani
Tangu niliposoma makala hiyo juu ya Lee Cordaway nimekuwa na donge. Lilikuwa jambo gumu sana kwangu kukubali kwamba alikufa! Mume wangu nami twapenda kutuma salamu zetu za upendo kwa mke wake mpendwa na familia yake. Jambo lililompata linanifanya nitambue kwamba matatizo yangu ni madogo sana kwa kulinganisha na yake. Mwanamume Mkristo aliye mwaminifu na mpendwa kama nini! Ninatiwa moyo sana na kielelezo chake.
F. H., Marekani
Ingawa nina umri wa miaka kumi tu na sina maradhi yoyote, mimi hufurahia makala kama hizo zenye kutia moyo. Natamani Lee Cordaway angeweza kusoma barua hii, lakini ninatambua kwamba hataweza kufanya hivyo hadi atakapofufuliwa katika Paradiso.
E. T., Marekani
Mapilgrimu Ninataka niwaambie jinsi nilivyothamini makala yenu “Wale Mapilgrimu na Kupigania Kwao Uhuru.” (Novemba 22, 1996) Nilipokuwa shuleni, sikusoma historia halisi juu ya mapilgrimu. Lakini nimejifunza mengi sana kutokana na makala zenu!
S. B., Marekani
Roki ya Badala Nina umri wa miaka 18, na ile makala “Vijana Huuliza . . . Roki ya Badala—Je, Inanifaa?” iliandikwa vizuri. (Novemba 22, 1996) Ninapenda roki ya badala, hivyo nilifikiri kwamba makala hiyo ingeniudhi. Lakini nilipoimaliza, nilithamini sana. Nina tatizo la mshuko-moyo, na natambua kwamba chaguo langu la muziki linaweza ama kuzidisha mshuko-moyo wangu au kunisaidia kupambana nao. Nilifurahia jinsi makala hiyo ilivyouliza, ‘Kwa nini usitafute muziki unaokuchangamsha?’ Asanteni kwa shauri hili lenye kutia moyo na lenye kutumika.
J. D., Marekani
Hayo maelezo yalikuwa sahihi sana na yasiyopendelea. Mimi hupata baadhi ya muziki huu kuwa wenye kupendeza. Asanteni kwa kutoa maonyo bila kulaumu kwa ujumla muziki wa roki ya badala.
S. C., Marekani
Hadithi za Wanyama Mimi hupenda kusoma makala mnazochapisha juu ya wanyama. Kwa vile sikuwa nimesikia kamwe juu ya pulatipasi, ile makala “Pulatipasi wa Kifumbo” (Desemba 8, 1996) ilinishangaza sana! Katika toleo hilohilo, ile makala juu ya urafiki wa kufurahisha kati ya mnyama na wanadamu, “Tandala Huyu Alikumbuka,” pia ilinigusa moyo. Ni vizuri kama nini wanadamu waonyeshapo upendo na staha kwa wanyama!
F. A., Brazili