Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Carnival Asanteni kwa makala “Maoni ya Biblia: Misherehekeo ya Carnival—Je, Yafaa au Haifai?” (Juni 8, 1996) Naishi Brazili, na carnival ni pindi yenye kusisimua sana hapa. Sikuzote nilikuwa nashawishika kujiunga na sherehe hizo. Nilijua si vizuri, lakini sikuelewa ni kwa nini. Hata hivyo, makala hii ilionyesha wazi kwamba carnival hutia ndani karamu za ulevi na kwamba Mungu huona sherehe kama hizo kuwa “matendo ya giza.”—Warumi 13:12 (Union Version).
F. M. M., Brazili
Likizo Asanteni sana kwa mfululizo wa makala “Je, Waenda Likizoni?—Kile Upaswacho Kujua.” (Juni 22, 1996) Ulikuja kwa wakati ufaao kabisa kwa sababu siku chache tu baadaye, tulienda likizo. Madokezo yaliyotolewa yalikuwa yenye msaada sana. Asanteni tena.
L. J., Marekani
Maradhi ya Lyme Asanteni kwa makala “Maradhi ya Lyme—Je, Umo Hatarini?” (Juni 22, 1996) Nikiwa tabibu, majuzi nimeona wagonjwa wachache wenye maradhi haya, nami naweza kuthibitisha tahadhari mlizotaja. Katika visa vingi wagonjwa hawachukuliwi kwa uzito nao huugua kwa muda mrefu. Amkeni! lilishughulikia maradhi ya Lyme ya aina ya yabisi-baridi, ambayo imeenea Marekani. Aina nyingine mbili zimegunduliwa Ulaya, na majaribu ya maabara ya kawaida hayawezi kuzitambua. Dawa za viuavijasumu vinafanya vizuri kwa maradhi ya Lyme katika hatua za mapema na mara nyingi hazifaulu baadaye.
I. S., Ujerumani
Nikiwa naugua maradhi ya Lyme, niliona makala hii kuwa yenye kutia moyo sana. Natumaini wote wanaoisoma watachukua ugonjwa huu kwa uzito na kuchukua tahadhari zote ziwezekanazo.
D. P., Marekani
Matatizo ya Kujifunza Nilithamini sana makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Siwezi Kujifunza?” (Juni 22, 1996) Ninang’ang’ana shuleni kwa sababu ya baadhi ya sababu zilizotajwa katika makala hiyo. Nitatumia madokezo yenu. Asanteni sana.
R. C., Marekani
Nilikuwa napoteza kabisa hamu ya kujifunza na sikuwa nikikaza fikira shuleni. Kwa kutumia madokezo yaliyotolewa katika makala hiyo, natumaini kuboresha tabia yangu ya kusoma.
M. E. O., Uganda
Mimi sina matatizo ya kujifunza, lakini sipendi kusoma. Pia nina matatizo ya kukumbuka njia za kufanya hesabu. Makala hiyo ilitaja kurudia-rudia na kutamka maneno kuwa msaada kwa matatizo ya kutokumbuka jambo upesi. Mara ya kwanza nilidhani ingekuwa upumbavu kujisomea kwa sauti, lakini nilipojaribu, nilifurahi sana!
N. I., Japani
Mhalifu Asanteni kwa kuchapisha maono ya Franck Mannino, yenye kichwa “Nilikuwa Mhalifu.” (Juni 22, 1996) Ilinigusa moyo na kunifanya nielewe jinsi Yehova, Muumba wetu mwenye upendo, alivyo na nguvu. Nimemtumikia kwa miaka 30, na maono hayo yamenitia moyo kufanya kadiri niwezayo katika kazi ya kuhubiri maadamu niko huru kufanya hivyo.
E. B., Italia
Makala hiyo ilinisaidia kuthamini pendeleo la kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Kutoweza kujipangia mambo vizuri kumenifanya nichelewe daima kwenye mikutano. Franck Mannino hakuwa na uhuru alipokuwa gerezani, lakini maisha yake yalikuwa yenye matokeo sana.
D. W., Marekani
Niliguswa moyo na bidii ambayo Franck Mannino alionyesha, hata alipokuwa katika gereza. Ingawa maisha yake yalianza vibaya, sasa yeye ni kielelezo bora kabisa.
C. R., Marekani