Maradhi ya lyme—Je, Umo Hatarini?
WAKATI UKIMWI unapotangazwa sana, maradhi ya Lyme hata hayatajwi. Lakini, maradhi ya Lyme yanaenea kwa kasi. Hata miaka michache iliyopita, The New York Times Magazine liliyaita “maradhi yenye kuambukiza yaeneayo kwa kasi zaidi [Marekani] kufuata UKIMWI.” Ripoti kutoka nchi nyinginezo zaonyesha kwamba hayo maradhi yanaenea katika Asia, Ulaya, na Amerika Kusini vilevile.
Maradhi ya Lyme ni nini? Yanaeneaje? Je, umo hatarini?
Kupe, Dia, na Wewe
Miaka ipatayo 20 iliyopita, ongezeko la kushangaza la visa vya ugonjwa wa yabisi-kavu lilitukia ndani na viunga vya mji wa Lyme, Connecticut, ambao upo kaskazini-mashariki mwa Marekani. Wengi wa wenye kuugua walikuwa watoto. Ugonjwa wao wa yabisi-kavu ulianza kwa vipele, maumivu ya kichwa, na maumivu ya vifundo. Mkazi mmoja alisema kwamba upesi “mume [wake] na watoto wawili walianza kutumia mikongojo.” Baada ya muda mfupi, zaidi ya watu 50 katika eneo hilo walikuwa wameambukizwa, na baada ya miaka kadhaa, maelfu ya watu yalikuwa yakiugua dalili zizo hizo zenye maumivu.
Watafiti, wakitambua kwamba ugonjwa huu ulikuwa tofauti na maradhi mengine, waliyaita maradhi ya Lyme. Chanzo chayo? Bakteria aina ya Borrelia burgdorferi—ambayo ina umbo-mpindo na kuishi katika kupe. Hiyo huenezwaje? Kwa kutembea polepole penye miti mingi kupe aliyeambukizwa aweza kujishikanisha kwa mtu. Kupe huyo huuma ngozi ya mtu na kuingiza bakteria hiyo yenye kusababisha maradhi ndani ya mtembeaji huyo maskini. Kwa kuwa kupe hao wenye maradhi hupanda, hujilisha, na kujamiiana kwenye mnyama aitwaye dia na kwa kuwa watu wengi zaidi wanaanza kuishi maeneo ya mashambani ambako kuna dia wengi, si ajabu kwamba kumekuwa na ongezeko la maradhi ya Lyme.
Dalili na Matatizo
Dalili ya kwanza ya maradhi ya Lyme kwa kawaida ni kipele cha ngozi (ambacho huitwa erythema migrans, au EM) ambacho huanza na doa dogo jekundu. Kwa kipindi cha siku fulani au majuma, doa hilo la dalili huanza kupanuka kuwa kipele chenye umbo duara, pembe-tatu, au umbo-yai ambacho chaweza kufikia ukubwa wa sarafu au kuenea mgongoni mwote mwa mtu. Homa, maumivu ya kichwa, mavune ya shingo, maumivu ya mwili, na uchovu huandamana na vipele. Wasipotibiwa mapema, zaidi ya nusu ya wanaougua hupatwa na maumivu na kufura kwa vifundo, ambayo yaweza kudumu kwa miezi kadhaa. Kufikia karibu asilimia 20 ya wagonjwa wasiotibiwa hatimaye hupata yabisi-kavu ya kudumu. Ingawa si ya kawaida sana, maradhi hayo yaweza pia kuathiri mfumo wa neva na kusababisha matatizo ya moyo.—Ona sanduku linaloandama.
Wastadi wengi huona maradhi ya Lyme kuwa magumu kugundua kwa sababu dalili zayo za kwanza kama mafua hufanana na dalili za maambukizo mengine. Kwa kuongezea, mtu 1 kati ya kila 4 walioambukizwa hatokwi na vipele—jambo kuu la pekee linalopatikana kwa maradhi ya Lyme—na wagonjwa wengi hawawezi kukumbuka ikiwa waliumwa na kupe kwa sababu umo lake mara nyingi halina maumivu.
Ugunduzi wa maradhi hayo huzuiwa hata zaidi kwa sababu uchunguzi wa damu wa kutafuta fingo (viua bakteria mwilini) unaopatikana wakati huu hautegemeki. Fingo zilizo katika damu ya mgonjwa huonyesha kwamba mfumo wa kinga wa mwili umegundua vivamizi, lakini uchunguzi mwingine hauwezi kujua ikiwa vivamizi hivyo ni bakteria za maradhi ya Lyme. Hivyo mgonjwa aweza kugunduliwa kuwa ana maradhi ya Lyme kumbe dalili zake ni za maambukizo mengine ya bakteria. Kwa hiyo, Taasisi za Kitaifa za Afya Marekani (NIH) hushauri matabibu wategemeze ugunduzi wao kwa umo la kupe, dalili za huyo mgonjwa, na kuondolewa kabisa kwa maradhi mengine ambayo huenda yangetokeza dalili hizo.
Tiba na Kuzuia
Yakigunduliwa mapema, wengi wa wagonjwa waweza kutibiwa kwa mafanikio kwa dawa za viuavijasumu. Kadiri tiba ianzavyo mapema, ndivyo mgonjwa aponavyo kwa haraka na kwa ukamili zaidi. Kwa miezi kadhaa baada ya kutibiwa, uchovu na maumivu huenda yakadumu, lakini dalili hizo zaweza kupunguka bila uhitaji wa tiba zaidi ya dawa za viuavijasumu. Hata hivyo, NIH yaonya, “kupatwa na maradhi ya Lyme haimaanishi kwamba ugonjwa huo utazuiliwa wakati ujao.”
Je, hali hiyo isiyo nzuri itapata kubadilika wakati wowote? Taarifa moja ya habari kutoka Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Yale katika Marekani ilitangaza kwamba watafiti wametengeneza dawa ya chanjo inayojaribiwa ambayo huenda ikaweza kuzuia maradhi ya Lyme. Dawa hiyo ya chanjo yenye “kufanya kazi mara mbili” huchochea mfumo wa kinga wa binadamu kutokeza fingo ambazo hushambulia na kuua bakteria ya Lyme zenye kushambulia. Wakati uo huo pia, inaua bakteria zinazoishi katika kupe wanaouma mtu aliyechanjwa dawa hiyo.
“Kujaribu dawa hii ya chanjo,” asema Dakt. Stephen E. Malawista, ambaye ni mmoja wa watafiti waliogundua maradhi ya Lyme 1975, “ni maendeleo makubwa katika jitihada zetu za kulinda watu dhidi ya matokeo mabaya sana ya maradhi ya Lyme.” Wanasayansi wanatumaini, lasema The New York Times, kwamba katika maeneo ambako maradhi hayo yamezuia watu wasitoke nje, “dawa hiyo ya chanjo itawawezesha wanadamu watembee porini bila kuogopa kupe.”
Hata hivyo, kwa wakati uo huo unaweza kuchukua hatua zako mwenyewe za kuyakinza hayo maradhi. NIH yapendekeza: Ikiwa unatembea katika maeneo yaliyojaa kupe, tembea katikati ya njia. Vaa suruali ndefu, shati lenye mikono mirefu, na kofia. Ingiza miguu ya suruali ndefu ndani ya soksi, na uvae viatu ambavyo haviachi sehemu fulani ya miguu ikiwa wazi. Kuvaa nguo zenye rangi nyangavu hufanya iwe rahisi kuona kupe. Vikinza-wadudu vinavyopakwa kwa nguo au ngozi hutumika, lakini vyaweza kutokeza athari mbaya hasa kwa watoto. “Wanawake waja wazito hasa wanahitaji kuwa waangalifu ili kuepuka kupe katika maeneo ya maradhi ya Lyme,” yatahadharisha NIH, “kwa sababu ambukizo laweza kuingizwa kwa mtoto ambaye hajazaliwa” nalo laweza kuongeza uwezekano wa mimba kuharibika au kuzaa mtoto akiwa amekufa.
Mara ufikapo nyumbani, jichunguze na uchunguze watoto wako ikiwa wana kupe, hasa katika sehemu za mwili zenye nywele. Chunguza kwa uangalifu kwa sababu kupe ambao hawajakomaa ni wadogo kama nukta inayokamilisha sentensi hii nawe kwa urahisi waweza kudhani hao ni uchafu fulani. Ikiwa una wanyama-vipenzi, uwachunguze kabla ya wao kuingia ndani ya nyumba—wao pia waweza kushikwa na maradhi ya Lyme.
Unaondoaje kupe? Si kwa vidole vyako bali kwa kibano kisicho na ncha kali. Vuta kwa upole lakini kwa uthabiti karibu na kichwa cha kupe mpaka aachilie ngozi, lakini usimfinye mwili. Kisha pangusa sana mahali ulipoumwa kwa dawa ya kiuaviini. Kuondoa kupe kwa muda wa saa 24, asema Dakt. Gary Wormser, mtaalamu wa maradhi ya kuambukizwa wa Marekani, kwaweza kukuokoa na maradhi ya Lyme.
Ni kweli kwamba hata katika maeneo yenye kupe wengi sana, uwezekano wa kupatwa na maradhi ya Lyme ni kidogo. Lakini, kuzingatia tahadhari hizo sahili kutafanya uwezekano huo uwe kidogo hata zaidi. Je, inastahili kuzingatia tahadhari hizo? Uliza mtu yeyote ambaye anaugua maradhi ya Lyme.
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Ishara za Maradhi ya Lyme
Maambukizo ya Mapema:
○ Vipele
○ Maumivu ya misuli na vifundo
○ Maumivu ya kichwa
○ Mavune ya shingo
○ Uchovu mkubwa
○ Homa
○ Kupooza-uso
○ Utando wa ubongo
○ Vipindi vifupi vya maumivu na kufura kwa vifundo
Yasiyo ya kawaida sana:
○ Kuwasha kwa macho
○ Kizunguzungu
○ Kuishiwa pumzi
Maambukizo ya Baadaye:
○ Yabisi-kavu, ya vipindi au ya kudumu
Yasiyo ya kawaida sana:
○ Kupoteza kumbukumbu
○ Ugumu wa kukaza fikira
○ Badiliko la tabia au la kawaida ya usingizi
Moja au zaidi ya dalili hizo zaweza kuonekana katika nyakati tofauti-tofauti wakati wa kuambukizwa.—Lyme Disease—The Facts, the Challenge, kilichotangazwa na Taasisi za Kitaifa za Afya.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kutembea polepole penye miti mingi kwaweza kukuhatarisha
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kupe (akiwa ameongezwa ukubwa sana)
[Hisani]
Yale School of Medicine
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kupe (ukubwa wake halisi)