Kuutazama Ulimwengu
Maji Hutoa Uhai
Gazeti la Brazili Claudia lasema kwamba bila maji mtu anaweza kufa kwa muda wa saa 48 tu. Wanasayansi wanakadiria kwamba maji hufanyiza asilimia 70 hadi 80 ya uzito wa mwili wa binadamu. Kwa msingi hayo maji yamo katika chembe. Asilimia ndogo zaidi yamo katika umajimaji unaojaza nafasi zilizopo kati ya chembe. Maji hubeba protini, hormoni, mafuta ya mwili, chumvi, na sukari za aina mbalimbali. Kwa hiyo, bila maji, utendaji wa kawaida wa kibiolojia na kikemia hauwezi kutokea. Na zaidi, ukosefu wa maji, kulingana na Claudia, waweza kuharibu vibaya viungo na kufanya damu iwe nzito, ukiwekea moyo mzigo mzito; mafigo huchoka yakijaribu kuondoa umajimaji wenye kujaa sumu, kukitokeza uchovu na kujisikia mgonjwa. Madaktari wanapendekeza kunywa maji lita mbili hadi tatu.
Wanawake Makachero
“Sherlock Holmes [kachero anayependwa katika vitabu] atakayefuata huenda akawa mwanamke,” lasema gazeti la Japani la Asahi Evening News. Katika shule moja mpya katika Tokyo, wanafunzi mia tatu wanazoezwa kuwa makachero, na zaidi ya theluthi tatu yao ni wanawake, wengi wao wakiwa katika miaka ya mapema ya 20 hadi miaka ya mapema ya 40. Ukachero unawapendeza kwa sababu nyingi tofauti-tofauti. Mke mmoja wa nyumbani mwenye umri wa miaka 46 aliripotiwa kuwa alijiorodhesha katika shule hiyo kwa sababu “hakuridhika na mitaala ya kawaida inayofundisha wanawake jinsi ya kupanga maua na jinsi ya kuvaa kimono [vazi] vizuri.” Hata hivyo, kwa wengine somo hilo linakuwa zaidi ya upendezi tu. Zaidi ya nusu ya wake wa nyumbani hawajaeleza waume zao. Baadhi yao wanapata stadi mpya za kuwachunguza wenzi wao ambao si waaminifu.
Miti Yashambuliwa
Uchunguzi wa miti katika nchi 24 za Ulaya wafunua tatizo linalozidi kuwa baya. The European laripoti kwamba mti 1 kati ya 5 umepoteza majani kupita kiasi. Katika nchi zilizo nje ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya, uharibifu mkubwa zaidi umetokea katika Bulgaria, Jamhuri ya Cheki, Slovakia, na Lithuania. Katika nchi za Jumuiya ya Nchi za Ulaya, Ufaransa na Uhispania zina misitu yenye afya zaidi, lakini miti iliyoharibiwa zaidi imo katika Uingereza. Katika 1988 robo ya miti katika nchi hiyo ilionyesha ishara za uharibifu. Kufikia 1991 miti zaidi ya nusu katika nchi hiyo ilikuwa imepoteza asilimia 25 au zaidi ya matawi yayo. Ingawa mvua ya asidi inalaumiwa kote, vipindi mfululizo vya kiangazi chenye ukavu katika Uingereza vimeongezea matatizo ya miti.
Ongezeko la Salmonella
“Kuna visa vipatavyo 60,000 hadi 100,000 vya ambukizo la [ugonjwa wa] salmonella katika Ujerumani kila mwaka, ambao mwisho wa angalau 200 huwa kifo,” laripoti gazeti la kila mwezi Kosmos. Takwimu hizo zilitolewa na Profesa Hans-Dieter Brede wa Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Tibakemili ya Georg-Speyer-Haus katika Frankfurt. Ugonjwa huo umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, sanasana kwa sababu ya ukosefu wa usafi katika sehemu wanyama wanakowekwa au kushughulikiwa. Mayai ambayo hayajapikwa vizuri au nyama ya kuku iliyoambukizwa ugonjwa wa salmonella ni kisababishi kikubwa. “[Vijidudu] vya salmonella hufa katika halijoto isiyopungua digrii 70 sentigredi,” gazeti hilo likaeleza.
Uchovu wa Wafanyakazi
“Usimamizi mbaya ni kisababishi kikubwa zaidi cha uchovu na mazao ya chini ya wafanyakazi,” laripoti The Toronto Star. Msimamizi mbaya “anaweza kuharibu siku yako, na hata kuharibu maisha yako ya binafsi. . . . Usimamizi mbaya ulielekea kutokeza matokeo mabaya kazini kuliko matatizo ya kibinafsi kama vile kifo cha mtu wa ukoo wa karibu au ndoa yenye matatizo,” lasema Star. Unaweza kugharimu kampuni “aksidenti zenye kuongezeka, ukosefu wa kwenda kazini kwa ukawaida na matatizo yanayohusika ya mikazo ya akili.” Kwa upande mwingine, msimamizi mzuri ni mwasilianaji mzuri na mwenye kutia moyo na anayeweza kutokeza “wafanyakazi wenye ubuni na wenye matokeo.” Wastadi wanapendekeza kwamba wasimamizi waweke miradi ya wazi na kuandaa vitu vinavyohitajika vya kufanya kazi hiyo. Wanapaswa kuwa watu wanaoweza kufikiwa, wenye kusikiliza vizuri, wasiopendelea, na wasioogopa kujifunza kutoka kwa wafanyakazi wao.
Mwendo wa Kutenda Vibaya
Karibu nusu ya mashambulizi yote ya kimwili kwa wanawake wazee katika United States yanafanywa na waume zao wenyewe. Katika kipindi cha 1991 “zaidi ya wanawake 700,000 wenye umri wa zaidi ya 50 walipigwa na waume zao,” kulingana na gazeti New Choices for Retirement Living. Idadi kubwa ya waume wenye umri wa miaka ya 50, 60, na hata 70 hupiga wake zao kwa wastani wa mara tatu au nne kwa mwaka. “Kumekuwa sehemu ya desturi ya ndoa,” asema Richard Gelles, mkurugenzi wa Programu ya Utafiti wa Ujeuri wa Familia katika Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Rhode. Mwanamke mmoja alielezea hivi ono lake: “Mambo niliyoona kuwa yenye kudhuru hata zaidi yalikuwa kutendwa vibaya kiakili na kupitia maneno makali. Hayo yalidumu daima.”
Kupokezana Vipuli—Hatari ya Kiafya
“Vipuli vyenye damu vinaweza kuwa chanzo cha ambukizo vikiwa na vijidudu vingi [kutia ndani] virusi vya mchochota-ini aina ya B na vya ukosefu wa kinga mwilini,” wanadai Philip D. Walson na Michael T. Brady, madaktari katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Ohio na Hospitali ya Watoto. Katika barua ya pamoja iliyochapishwa katika jarida la kitiba la Amerika Pediatrics, hangaiko lilionyeshwa kuhusu zoea linaloonekana kuwa limeenea la kupokezana vipuli ambavyo havijaondolewa vijidudu vya magonjwa. Vijana wanaobalehe na vijana wanaokuwa watu wazima wanaweza kuwa wanajua hatari za kiafya zinazohusika na utendaji wa kingono na kupokezana sindano za kujidungia dawa za kulevya—lakini hawatambui hatari za zoea la kupokezana vipuli. Una “uwezekano wa kuambukiza magonjwa yanayopitishwa kwa damu,” madaktari hao wawili wanadai. Wanapendekeza kwamba madaktari “wajaribu kuzuia wagonjwa wao wasiwe na zoea hilo.”
Wakanada Wana Matatizo ya Kupata Usingizi
Karibu 1 kati ya kila watu wazima 4 wa Kanada walikuwa na matatizo ya kupata usingizi katika 1991, kulingana na uchunguzi wa karibuni wa mielekeo ya kijamii uliofanywa na Takwimu za Kanada. Mkazo wa akili ulikuwa ndio kisababishi kikuu. Gazeti The Globe and Mail la Toronto lilisema kwamba “matatizo machungu ya kiafya” yalisababisha matatizo ya kupata usingizi katika asilimia 44 ya wale waliohojiwa. Kwa wanawake waliohojiwa, asilimia 28 walikuwa na matatizo ya kupata usingizi. Kulikuwa na visa vya asilimia 19 miongoni mwa wanaume waliojibu. Akina mama ambao wako peke yao, watu maskini, wazee-wazee, wafanyakazi wa zamu, na wale wanaotafuta kazi walikuwa na kiwango cha juu hasa cha ukosefu wa usingizi. Dakt. Jeffrey Lipsitz, wa Kitovu cha Matatizo ya Usingizi cha Metropolitan Toronto, ambaye kliniki yake inachunguza wagonjwa wapya zaidi ya elfu moja kwa mwaka, alisema kwamba watu wanapohangaika zaidi juu ya kupoteza kazi au fedha, wanaanza kupoteza usingizi.
Walaji wa Sarafu
Kila mwaka makumi ya maelfu ya watoto wadogo hupelekwa kwenye vyumba vya matibabu ya dharura vya hospitali ili wafanyiwe eksirei zenye kugharimu sana baada ya wao kumeza sarafu. Nyingi za sarafu hizo hupita mwilini bila matatizo, lakini mara kwa mara sarafu hukwama katika umio, ikisababisha kutokwa damu kindani, maambukizo, na nyakati nyingine kifo inapotoboa umio. Kichunguzio sahili na ambacho ni salama kabisa kinachoshikwa mkononi, kilicho sawa na vile ambavyo nyakati nyingine hutumiwa na maofisa wa usalama wa viwanja-ndege, kimebuniwa ili madaktari wa watoto waweze kupata mahali palipo sarafu iliyomezwa. Dakt. Simon Ros, mkurugenzi wa dawa ya dharura ya watoto katika Illinois na ambaye ni mmoja wa wale waliovumbua njia hiyo, anasema kwamba chombo hicho kinaweza kuondoa ziara ya kwenda kwenye chumba cha matibabu ya dharura, “ambapo kupata mahali sarafu ilipo kunaweza kugharimu zaidi ya dola $300.” Njia hiyo, iliyoripotiwa katika Journal of Pediatrics and Pediatric Emergency Care, inaelekea itatumiwa kote karibuni kwa sababu ya matokeo yayo mazuri na gharama yayo ya chini.
Vijana Wenye Matatizo
Ongezeko la hesabu ya kujiua katika Hong Kong ‘limeshtua, limeshangaza, na kuogofya’ maofisa, laripoti The Toronto Star. Watoto wenye umri kati ya 8 na 15 wanaruka nje ya majengo na kufa. Ni nini kinachowatatiza vijana hawa? Wengine wanalaumu mfumo wa elimu. Thomas Mulvey, mkurugenzi wa Shirika la Hali Njema ya Familia la Hong Kong, asema hivi: “Katika Hong Kong, shule zimeelezwa kuwa hatari ya kiafya kwa watoto, zikifanya madai yasiyo na kiasi kwa wanafunzi na kukosa kuhisi mahitaji yao.” Wazazi pia “hutia thamani kubwa juu ya mafanikio ya elimu” na “kutojali hisia za watoto wao,” aeleza Mulvey. Watoto “wanahisi wametengwa kihisia-moyo, wapweke na wenye kupuuzwa.” Gazeti Star laripoti kwamba maofisa wa serikali wamesadikishwa kwamba “chanzo cha matatizo mengi kimo nyumbani.”
Utoaji-Mimba Katika Kolombia
Katika Kolombia, karibu wanawake milioni moja na nusu wametoa mimba angalau mara moja. Hiyo ni karibu na asillimia 20 ya wanawake wote wenye umri wa kuweza kuzaa katika nchi hiyo. Wanawake wengi wanakufa kwa sababu ya matatizo yanayotokana na utoaji-mimba. Gazeti la Kolombia Semana laripoti kwamba katika “Taasisi ya Akina Mama na Watoto ya Bogotá, utoaji-mimba hutokeza idadi kubwa zaidi ya vifo vya akina mama.” Inakadiriwa kwamba karibu utoaji-mimba 400,000 hufanywa kila mwaka katika Kolombia. Hiyo ni wastani wa karibu utoaji-mimba 45 kila muda wa saa moja.
Kitumbuizo Kinachodhuru
“Aibu kwa Hollywood [kwa watengeneza sinema] kwa ajili ya mfululizo wa sinema zinazojaa uchafu, uchi, ngono, jeuri, na mauaji.” Taarifa hiyo ilikuwa sehemu ya tangazo la ukurasa mzima lililochapwa karibuni katika gazeti la habari USA Today. Kulingana na tangazo moja, kampuni moja kubwa ya televisheni imeruhusu programu moja “inayopendwa na vijana iwe na maonyesho ya kupiga punyeto, watu wenye kushughulikia maiti wakifanya ngono na wafu,” na mambo mengine mabaya. Tangazo hilo lilitaja kwamba kwa kutazama programu za televisheni, “mtoto wa wastani mwenye umri wa miaka 16 [ameona] vitendo zaidi ya 200,000 vya ujeuri na mauaji 33,000.”