Wanawake Je! Wanastahiwa Nyumbani?
“Wanawake walipatwa na vifo vyenye kuogofya, mmoja baada ya mwingine. . . . Na ijapokuwa namna ya vifo vyao ilitofautiana, hali zilizosababisha hazikutofautiana: Polisi wa Quebec [Canada] wasema kwamba kila mmoja wa wanawake hao aliuawa na aliyekuwa mume au mpenzi wake wa zamani au wa sasa. Kwa ujumla, wanawake 21 wameuawa katika Quebec mwaka huu [1990], wakiuawa katika wimbi la jeuri katika uhusiano wa kindoa.”—Maclean’s, Oktoba 22, 1990.
JEURI ya nyumbani, inayoitwa na wengine “sehemu isiyopendeza ya maisha ya familia,” inatokeza familia zilizofarakana na kutokeza watoto walio na maoni yasiyofaa ya jinsi uhusiano wa ndoa wapaswa kuwa. Watoto hugawanyika katika uaminifu-mshikamanifu wao kwa wazazi wao wanapojaribu kuelewa ni kwa nini baba anampiga mama. (Mara chache swali, ni kwa nini mama anakuwa mkali kwa baba?) Tokeo la jeuri ya nyumbani mara nyingi hutia ndani wana wanaokuja kuwa wapiga wake baadaye. Athari ya baba imewaacha na matatizo makubwa ya kiakili na kiutu.
Kichapo cha UM The World’s Women—1970-1990 chasema: “Mashambulio ya wanaume dhidi ya wanawake nyumbani mwao yanadhaniwa kuwa ndio uhalifu unaoripotiwa mara chache sana—kwa sehemu fulani kwa sababu jeuri hiyo huonekana kuwa tatizo la kijamii, si uhalifu.”
Kutenda wenzi vibaya ni kwingi kadiri gani katika United States? Ripoti ya Bunge iliyonukuliwa katika makala iliyotangulia yasema: “Usemi ‘jeuri ya nyumbani’ waweza kuonekana wenye upole, lakini tabia inayofafanuliwa si yenye upole hata kidogo. Tarakimu zaonyesha hali yenye kuhuzunisha sana ya jinsi kumtenda vibaya mwenzi kulivyo jambo zito—naam hata lenye kufisha. Wanawake kati ya 2,000 na 4,000 hufa kila mwaka kwa sababu ya kutendwa vibaya. . . . Tofauti na uhalifu mwingine wowote, kumtenda vibaya mwenzi ni jeuri ya ‘kudumu’. Ni tisho la kuendelea na kuumizwa kimwili kwa kurudiarudia.”
Gazeti World Health lasema: “Jeuri dhidi ya wanawake hutukia katika kila nchi na katika kila tabaka ya kijamii na kiuchumi. Katika tamaduni nyingi, kupiga mke huonwa kuwa haki ya mwanamume. Mara nyingi, zoea la kupiga na kulalwa kinguvu kwa wanawake na wasichana huonwa kuwa ‘mambo ya faragha’ yasiyowahusu wengine—iwe ni mamlaka za kisheria au wafanyakazi wa hospitali.” Jeuri hii ya nyumbani yaweza kuenea kwa urahisi hadi shuleni.
Hilo lilionyeshwa wazi na yaliyotukia Julai 1991 katika shule moja ya bweni ya wasichana na wavulana katika Kenya. The New York Times liliripoti kwamba “wasichana matineja 71 walilalwa kinguvu na wanafunzi wavulana na wengine 19 wakafa katika usiku wa jeuri ndani ya vyumba vya bweni ambayo yaripotiwa kuwa . . . haikukomeshwa na polisi wala walimu.” Ghasia hiyo ya jeuri ya kingono yaweza kuelezwaje? “Msiba huo umekazia ule upigaji ubwana wa kiume wenye kuchukiza ambao huongoza maisha ya kijamii ya Kenya,” akaandika Hilary Ng’Weno, mhariri mkuu wa gazeti la Kenya linalosomwa na wengi The Weekly Review. “Hali ya wanawake na wasichana wetu ni ya kuombolezewa. . . . Tunalea wavulana wetu wakiwa na staha ndogo au bila staha yoyote kwa wasichana.”
Hicho ndicho kiini hasa cha tatizo lenyewe la ulimwenguni pote—wavulana mara nyingi hulelewa kuwaona wasichana na wanawake kuwa wenye cheo cha chini na viumbe wa kutumiwa vibaya. Wanawake huonwa kuwa dhaifu na wawezao kutawalwa kwa urahisi. Kutoka hapo ni hatua fupi tu ya kuelekea ukosefu wa staha kwa wanawake na upigaji ubwana kikamili wa kiume na hatua fupi vilevile ya kumlala kinguvu mtu wamjuaye au kumlala kinguvu mtu ambaye wamefanya urafiki naye. Na kuhusu kulala kinguvu, isisahaulike kwamba “shambulio laweza kuchukua muda mfupi, lakini lihisiwe kwa muda wote wa maisha.”—Ripoti ya Bunge ya Amerika.
Ijapokuwa wanaume wengi si wenye jeuri kimwili kuelekea wanawake, wanaweza kuelezwa kuwa wachukia wanawake. Badala ya kuwa wajeuri kimwili, wao huwatenda vibaya au kuwaumiza kiakili au kuwapiga. Katika kitabu chake Men Who Hate Women & the Women Who Love Them, Dakt. Susan Forward asema: “Kama vile wenzi wao walivyowafafanua, [wanaume hao] mara nyingi walikuwa wenye urafiki na hata wenye upendo, lakini waliweza kugeuka ghafula kwa tabia ya ukatili, yenye kuchambua, na ya ufidhuli. Tabia yao ilitia ndani nyendo tofauti-tofauti, kuanzia uchokozi wa wazi na vitisho hata kufikia mashambulio yenye hila na ya kisiri zaidi ambayo yalikuwa ya namna ya kushushwa hali daima au uchambuzi wenye kuumiza. Hata mbinu iwe ni ipi, matokeo yalikuwa yaleyale. Mwanamume alipata udhibiti kwa kumkandamiza mwanamke. Wanaume hao pia walikataa kuchukua daraka lolote la jinsi mashambulio yao yalivyowafanya wenzi wao wahisi.”
Yasuko,a mwanamke mdogo Mjapani, ambaye sasa ameolewa kwa miaka 15, aliambia Amkeni! juu ya ono la familia yake: “Baba yangu alikuwa akimpiga na kumtenda vibaya mama yangu kwa ukawaida. Angempiga mateke na ngumi, kumburuta kwa nywele zake, na hata kumrushia mawe. Na unajua ni kwa sababu gani? Kwa sababu alijaribu kumwuliza juu ya uzinzi wake na mwanamke mwingine. Ni hivi, katika utamaduni wa Kijapani, imeonwa kuwa jambo la kawaida kwa wanaume fulani kuweka mwanamke kinyumba. Mama yangu alikuwa na maoni ya ki-siku-hizi na akakataa kukubaliana na hilo. Baada ya miaka 16 ya ndoa na watoto wanne, alipata talaka. Aliachwa na baba yangu bila utegemezo wowote wa kulea watoto.”
Hata hivyo, hata mahali ambapo kupiga mke kumeripotiwa kwa wenye mamlaka, kwa kawaida hakumzuii mwanamume mwenye kisasi kumwua mke wake. Katika pindi nyingi, katika nchi kama vile United States, sheria haijafanya mengi ili kumlinda mwenzi anayetishwa au kudhulumiwa. “Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba zaidi ya nusu ya wanawake wote waliouawa na waume zao, polisi walikuwa wameitwa kwenye makao hayo mara tano katika mwaka uliopita ili kuchunguza lalamiko juu ya jeuri ya nyumbani.” (Ripoti ya Bunge ya Amerika) Katika visa vingine vyenye kupita kiasi, mke ameua mumeye, ili ajiokoe mwenyewe kutokana na kutendwa vibaya zaidi.
Jeuri ya nyumbani, ambayo kwa kawaida mwanamke ndiye huwa mwenye kuumizwa, hujionyesha yenyewe katika njia nyingi tofauti. Katika India idadi inayoripotiwa ya vile viitwavyo eti vifo vya mahari (waume kuua wake zao kwa sababu ya kutotosheka na mahari inayolipwa na familia ya mke) viliongezeka kutoka 2,209 katika 1988 hadi 4,835 katika 1990. Hata hivyo, hesabu hizo si kamili au sahihi, kwa kuwa vifo vingi vya wanawake husemekana tu kuwa aksidenti za nyumbani—mara nyingi kwa kuchomwa kimakusudi na mafuta ya taa. Wenye kuongezewa kwa tarakimu hizo ni ujiuaji mwingi wa wake ambao hawawezi tena kukabili huzuni ya nyumbani.
Wakati Uchaguzi Ni Kati ya Wana au Mabinti
Wanawake hubaguliwa kuanzia kuzaliwa au hata kabla ya kuzaliwa. Yawezekanaje hivyo? Amkeni! lilimhoji Madhu kutoka Bombay, India, kwa jibu moja: “Mwana anapozaliwa katika familia ya Wahindi, kuna shangwe. Matatizo ya mama hayapo tena. Sasa wazazi wana mwana wa kuwatunza uzeeni. ‘Malipo yao ya uzeeni’ yamehakikishwa. Lakini akizaa binti, anaonwa kuwa mpungufu. Ni kana kwamba ameleta mzigo mwingine ulimwenguni. Wazazi watalazimika kutoa mahari ghali sana ili aolewe. Na mama akiendelea kuzaa mabinti, basi yeye anapatwa na hasara.b”
Jarida Indian Express liliripoti hivi kuhusu wasichana katika India: “Kuokoka kwao hakuonwi kuwa kwa maana sana katika kuokoka kwa familia.” Jarida hilohilo lataja uchunguzi katika Bombay “uliofunua kwamba kati ya vijusu 8,000 vinavyohusu kutolewa mimba kufuatia kutambuliwa kwa jinsia ya vijusu hivyo, 7,999 vilikuwa vya kike.”
Elisabeth Bumiller aandika: “Hali ya wanawake wengine wa India ni fukara sana hivi kwamba ikiwa tatizo lao gumu lingetolewa uangalifu ule unaotolewa matatizo ya kikabila na ya rangi katika nchi nyinginezo za ulimwengu, tatizo lao lingeshughulikiwa na vikundi vya kupigania haki za kibinadamu.”—May You Be the Mother of a Hundred Sons.
“Kazi ya Mwanamke Huwa Haifanywi Kamwe”
“Kazi ya mwanamke huwa haifanywi kamwe” waweza kuonekana kuwa msemo usio na maana. Lakini waonyesha ukweli ambao wanaume wengi hupuuza. Mwanamke mwenye watoto hana ratiba ya kazi isiyobadilika, kuanzia saa tatu hadi saa kumi na moja, kama ile ambayo wanaume huwa nayo mara nyingi. Mtoto akilia usiku ni nani anayeelekea kuamka? Ni nani hufanya usafi, kufua, na kupiga pasi? Ni nani hutayarisha na kuandaa chakula mume anaporudi nyumbani kutoka kazini? Ni nani anayesafisha baada ya mlo halafu kutayarisha watoto walale? Na katika nchi nyingi, pamoja na hayo yote, ni nani anayetazamiwa kuchota maji na hata kufanya kazi shambani akiwa na mtoto mgongoni? Mara nyingi ni mama. Ratiba yake si muda wa saa 8 au 9 tu kwa siku; mara nyingi ni saa 12 hadi 14 au zaidi. Hata hivyo, halipwi kwa ajili ya wakati huo wa ziada—na mara nyingi sana hakuna asante!
Kulingana na gazeti World Health, katika Ethiopia “wanawake [wengi] hutazamiwa kufanya kazi muda wa saa 16 hadi 18 kwa siku, [na] kiwango chao cha mapato ni cha chini sana hivi kwamba hawawezi kujitunza wenyewe na familia zao. . . . Njaa ni tukio la kila siku; mara nyingi, [wanawake wakusanyaji kuni na wabebaji mizigo] hupata mlo mmoja tu usiotosheleza kwa siku na mara nyingi hutoka nyumbani mwao bila kiamshakinywa.”
Siu, aliyetoka Hong Kong, ambaye sasa ameolewa kwa miaka 20, alisema: “Katika mazingira ya Kichina, wanaume wamekuwa na mwelekeo wa kuwashusha wanawake wakiwaona kwa upande mmoja kuwa wasaidiaji nyumbani na wazaa watoto au, kwa upande ule mwingine kama visanamu, vibaramwezi, au vyombo vya ngono. Lakini kwa kweli, tunalotaka sisi wanawake ni kutendwa kama viumbe weledi. Tunataka wanaume watusikilize tunapoongea na si kutenda kana kwamba sisi ni vitu.”
Haishangazi kwamba kitabu Men and Women husema hivi: “Kila mahali, hata ikiwa wanawake wanaheshimiwa sana, utendaji wa wanaume huthaminiwa zaidi ya ule wa wanawake. Huwa haidhuru hata kidogo jinsi jamii inavyogawanya madaraka na kazi kati ya watu wa jinsia tofauti; zile za wanaume huonwa kuwa za thamani zaidi machoni pa jumuiya nzima.”
Ukweli wa jambo hilo ni kwamba daraka la mwanamke nyumbani kwa kawaida huchukuliwa kivivi-hivi tu. Hivyo, utangulizi mfupi wa The World’s Women—1970-1990 wasema: “Hali za maisha za wanawake—na kuchangia kwao familia, uchumi na watu wa nyumbani—zimepuuzwa kwa ujumla. Tarakimu nyingi zimefasiliwa kwa njia zinazoonyesha hali za wanaume na michango yao, si zile za wanawake, au zinazopuuza jinsia kwa ujumla. . . . Kazi nyingi wanazofanya wanawake bado hazionwi kuwa zenye thamani ya kiuchumi hata kidogo—na hata hazipimwi.”
Katika 1934, mwandikaji Gerald W. Johnston Mwamerika wa Kaskazini alieleza maoni kuhusu wanawake kazini: “Mwanamke mara nyingi hupata kazi ya mwanamume lakini ni mara chache hulipwa mshahara wa mwanamume. Sababu ni kwamba hakuna aina ya kazi ya kila siku ambayo yaweza kufanywa na mwanamke yeyote vizuri zaidi ya mwanamume. Washonaji mashuhuri na watengenezaji kofia za wanawake ni wanaume . . . Wapishi mashuhuri sikuzote ni wanaume. . .. Hivi sasa ni jambo la hakika kwamba mwajiri-kazi yeyote ananuia kumpa mwanamume pesa nyingi kuliko mwanamke kwa kazi ileile kwa sababu ya kuamini kwamba mwanamume ataifanya vizuri zaidi.” Ingawa maelezo hayo huenda yalitolewa kwa mzaha, yalionyesha upendeleo uliokuwapo wakati huo, na ambao ungalipo katika akili za wanaume wengi leo.
Ukosefu wa Staha—Tatizo la Ulimwenguni Pote
Kila tamaduni imetokeza mitazamo yake, upendeleo, na chuki zisizo na sababu kuhusu daraka la wanawake katika jamii. Lakini swali linalopaswa kujibiwa ni hili, Je! mitazamo hiyo inaonyesha staha ifaayo kwa cheo cha wanawake? Au badala yake, inaonyesha utawala wa kiume wa karne nyingi kwa sababu ya nguvu za kimwili, za mwanamume ambazo kwa kawaida huwa nyingi zaidi? Ikiwa wanawake wanatendwa kama watumwa au kama vitu vya kutumiwa vibaya, basi i wapi staha ya cheo chao? Kwa kadiri kubwa au ndogo, tamaduni nyingi zimeharibu daraka la mwanamke na kushusha kujistahi kwake.
Mfano mmoja kati ya mingi kuzunguka ulimwengu unatoka Afrika: “Wanawake wa Yoruba [Naijeria] ni lazima wajisingizie kuwa wasiojua kitu na kukubali mambo yote bila kuteta waume zao wakiwepo, na wanapowaandalia chakula, wanatakiwa kupiga magoti mbele ya miguu ya waume zao.” (Men and Women) Katika sehemu nyingine za ulimwengu, ujitiisho huo wa kupita kiasi waweza kuonyeshwa katika njia mbalimbali—mke akipaswa kutembea umbali fulani nyuma ya mumewe, au kutembea huku mume akiendesha farasi au punda, au kubeba mizigo huku mume akiwa bila chochote, au kula kando peke yake, na kadhalika.
Katika kitabu chake, The Japanese, Edwin Reischauer, mzalia na mkulia Japani, aliandika: “Mitazamo ya kupiga ubwana kwa wanaume huonekana waziwazi katika Japani. . . . Kiwango maradufu cha kijinsia, ambacho humwacha mwanamume akiwa huru na mwanamke akiwa amezuiwa, lingali jambo la kawaida. . . . Zaidi ya hilo, wanawake walioolewa hutazamiwa kuwa waaminifu sana kuliko wanaume.”
Kama ilivyo katika nchi nyingi, udhia wa kingono ni tatizo pia katika Japani, hasa katika mabehewa ya reli ya chini yaliyojaa pomoni wakati wengi wanaposafiri. Yasuko, kutoka Jiji la Hino, Tokyo, aliambia Amkeni! hivi: “Nikiwa mwanamke kijana nilikuwa nikisafiri kwenda Tokyo. Lilikuwa jambo lenye kuaibisha sana kwa sababu wanaume fulani walitumia pindi hiyo kwa manufaa yao kwa kufinya na kugusa popote walipoweza. Sisi wanawake tungeweza kufanya nini kuhusu hilo? Tulilazimika kuvumilia. Lakini lilikuwa jambo lenye kuaibisha sana. Saa za asubuhi wakati wengi sana husafiri, kulikuwako behewa lililotengewa wanawake, kwa hiyo angalau wengine wangeweza kuepuka aibu hizo.”
Sue, aliyekuwa akiishi Japani, alikuwa na njia yake mwenyewe ya kuepa mambo hayo. Yeye alikuwa akisema kwa sauti kuu “Fuzakenai de kudasai!” linalomaanisha “Acha Ujinga!” Yeye asema: “Hilo lilisikiwa na kuwa na matokeo mara moja. Hakuna aliyetaka kuaibishwa mbele ya wengine wote. Kwa ghafula hakuna mwanamume aliyekuwa akinigusa tena!”
Ukosefu wa staha kwa wanawake nyumbani kwa wazi, ni tatizo la ulimwenguni pote. Lakini vipi daraka la wanawake kazini? Je! wao hustahiwa na kutambuliwa zaidi huko?
[Maelezo ya Chini]
a Wahojiwa waliomba majina yao yasitajwe. Majina ya badala yanatumiwa katika makala hizi.
b Waume karibu sikuzote huwazia kwamba mke ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa kuzaa mabinti. Hawaifikirii sheria ya urithi-tabia. (Ona kisanduku, ukurasa huu.)
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
Jinsia ya Mtoto Huamuliwaje?
“Jinsia ya mtoto asiyezaliwa huamuliwa wakati wa kuchukua mimba, na ni shahawa za baba ambazo huamua. Kila mbegu, au yai, ambalo mwanamke hutoa ni la kike katika maana ya kwamba lina X, au kromosomu (nyuzinyuzi katika kiini cha seli zenye jeni) ya jinsia ya kike. Katika mwanamume, ni nusu tu ya shahawa zilizo na kromosomu X, hali ile nusu nyingine ina Y, ambayo ni kromosomu ya jinsia ya kiume.” Kwa hiyo, ikiwa X mbili zinaungana, matokeo yatakuwa msichana; ikiwa Y ya mwanamume inaungana na X ya mwanamke, mtoto atakuwa mvulana. Hivyo, ikiwa mwanamke atakuwa na wavulana au wasichana hilo huamuliwa na aina ya kromosomu katika shahawa za mwanamume (ABC’s of the Human Body, kichapo cha Reader’s Digest) Ni jambo lisilo la kiakili kwa mwanamume kumlaumu mke wake kwa sababu ya kuzaa wasichana tu. Hakupasi kuwe na lawama lolote kuhusu hilo. Hilo ni jambo la uumbaji lisiloweza kutabirika.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]
Msiba Mkubwa Mno
Katika kitabu chake Feminism Without Illusions, Elizabeth Fox-Genovese aliandika: “Kuna sababu nzuri ya kuamini kwamba wanaume wengi . . . wanaendelea kushawishwa kutumia nguvu [zao] katika hali moja ambayo bado yawapa ushindi rahisi—uhusiano wao binafsi na wanawake. Ikiwa niko sahihi katika kudhania huku, basi tunakabili msiba mkubwa mno.” Na msiba huo mkubwa mno unatia ndani mamilioni ya wanawake wanaoteseka kila siku mikononi mwa waume wenye kudhulumu, baba, au mwanamume yeyote—mwanamume anayekosa “kufuata usawa na haki.”
“Katika majimbo thelathini [ya United States], bado kwa ujumla ni halali kwa waume kuwalala kinguvu wake zao; na ni majimbo kumi tu yaliyo na sheria za kuhukumu vifungo kwa ajili ya jeuri ya nyumbani . . . Wanawake ambao hawana uchaguzi mwingine ila kutoroka hawaoni hilo kuwa suluhisho lifaalo pia. . . . Theluthi moja ya wanawake milioni 1 wanaopigwa ambao hutafuta makao ya dharura kila mwaka hawapati yoyote.”—Utangulizi wa Backlash—The Undeclared War Against American Women, cha Susan Faludi.
[Picha]
Kwa mamilioni, jeuri ya nyumbani ni sehemu isiyopendeza ya maisha ya familia
[Picha katika ukurasa wa 18]
Mamia ya mamilioni huishi bila maji ya mfereji, mifereji ya kuondoshea mbali maji machafu, au stima katika nyumba zao—ikiwa wana nyumba