Kwa Nini Wanaume Huwapiga Wanawake?
WATAALAMU fulani wanasema kwamba wanawake wengi wanakabili hatari ya kuuawa na wenzi wao wa kiume kuliko na wahalifu wote wakijumlishwa. Uchunguzi mwingi umefanywa katika jitihada za kukomesha jeuri kati ya wenzi wa ndoa. Ni mwanamume wa aina gani humpiga mke wake? Maisha yake ya utotoni yalikuwaje? Je, alikuwa mwenye jeuri wakati wa uchumba? Mwanamume huyo amefanya maendeleo gani baada ya kutibiwa?
Kulingana na uchunguzi wa wataalamu fulani, wanaume wanaowapiga wanawake hutofautiana. Kuna yule aliye mjeuri mara moja moja. Hatumii silaha wala hana zoea la kumpiga mwenzi wake. Kwake kutenda jeuri si jambo la kawaida na yaelekea huchochewa na watu au mambo yanayomzunguka. Kwa upande mwingine, kuna yule aliye na zoea la kumpiga mwenzi wake. Kwa mtu huyo, jeuri ni jambo la kawaida na hajuti wala kuonyesha dalili za kuacha zoea hilo.
Hata hivyo, uhakika wa kwamba watu wanaopiga wanawake hutofautiana haimaanishi kwamba njia fulani za kuwapiga wanawake si hatari. Kwa hakika, kumtendea mtu vibaya kwa njia yoyote kunaweza kutokeza majeraha—hata kifo. Hivyo, uhakika wa kwamba mtu fulani hatendi jeuri kila wakati au si katili sana haimaanishi kwamba anakubalika. Bila shaka hakuna kupiga “kunakokubalika.” Hata hivyo, ni mambo gani humfanya mwanamume amjeruhi mwanamke ambaye aliahidi kumtunza kwa muda wote wa maisha yake?
Athari ya Familia
Si ajabu kwamba wanaume wengi wanaowapiga wake zao walikulia katika familia zenye jeuri. “Wengi wao walilelewa katika nyumba zilizofanana na maeneo ya vita,” aandika Michael Groetsch, ambaye kwa miaka 20 amefanya utafiti kuhusiana na jeuri kati ya wenzi wa ndoa. “Wakiwa watoto, walikulia katika mazingira hatari ambapo kutendewa vibaya kihisia-moyo na kimwili yalikuwa mambo ya ‘kawaida.’” Kulingana na mtaalamu mmoja, mwanamume aliyekulia mazingira kama hayo “anaweza kuiga chuki ya baba yake kuelekea wanawake akiwa angali mchanga sana. Mvulana huyo anajifunza kwamba ni lazima mwanamume awadhibiti wanawake kwa kuwatisha, kuwaumiza, na kuwadharau. Na wakati huohuo anajifunza kwamba, ili apate kibali cha baba yake ni lazima amwige.”
Biblia inaonyesha wazi kwamba mwenendo wa mzazi unaweza kumwathiri mtoto kwa njia ifaayo au isiyofaa. (Mithali 22:6; Wakolosai 3:21) Bila shaka mazingira ya familia hayampi mtu sababu ya kumpiga mwenzi wake, lakini yanaweza kuonyesha chanzo cha mwenendo huo wenye jeuri.
Athari ya Kitamaduni
Katika nchi fulani kumpiga mwanamke ni jambo linalokubaliwa na hata la kawaida. “Jamii nyingi zinaamini sana kwamba mume ana haki ya kumpiga au kumuumiza mkewe,” yaeleza ripoti moja ya Umoja wa Mataifa.
Hata katika nchi ambazo ukatili wa aina hii haukubaliwi, watu mmoja-mmoja hutenda kwa jeuri. Inashangaza kwamba wanaume fulani wana maoni hayo yasiyo na msingi kuelekea jambo hilo. Kulingana na gazeti la Weekly Mail and Guardian la Afrika Kusini, uchunguzi uliofanywa huko Cape Peninsula, uligundua kwamba wanaume wengi waliodai kutowatendea wake zao kwa ukatili walihisi kwamba kumpiga mwanamke kunakubaliwa na si ujeuri.
Ni wazi kwamba maoni hayo yaliyopotoka yanaanza utotoni. Kwa mfano, kulingana na uchunguzi mmoja huko Uingereza, asilimia 75 ya wavulana wenye umri wa miaka 11 na 12 wanahisi kwamba mwanamume anaweza kumpiga mwanamke anapomkasirisha.
Hakuna Sababu ya Kumpiga Mwenzi wa Ndoa
Mambo yaliyotangulia kutajwa huenda yakasaidia kufafanua visababishi vya ukatili kuelekea mwenzi wa ndoa, lakini hayaonyeshi kuwa ukatili huo unakubaliwa. Kwa ufupi, kumpiga mwenzi wa ndoa ni dhambi nzito machoni pa Mungu. Katika Neno lake Biblia, twasoma: “Waume wapaswa kuwa wakiwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Yeye apendaye mke wake ajipenda mwenyewe, kwa maana hakuna mtu aliyepata wakati wowote kuuchukia mwili wake mwenyewe; bali huulisha na kuutunza sana kama vile Kristo pia alifanyiavyo kutaniko.”—Waefeso 5:28, 29.
Biblia ilitabiri kwamba katika “siku za mwisho” za huu mfumo wa mambo, watu wengi watakuwa “wakatili,” “wasio na shauku ya asili,” na “wakali.” (2 Timotheo 3:1-3; The New English Bible) Kuongezeka kwa ukatili katika ndoa ni mmojawapo wa uthibitisho wa kwamba tunaishi katika kipindi kinachozungumziwa na unabii huo. Lakini wanaotendewa ukatili wanaweza kusaidiwaje? Je, kuna tumaini lolote kwamba wanaowatendea wengine ukatili watabadili mwenendo wao?
[Blabu katika ukurasa wa 5]
“Mtu anayempiga mkewe hatofautiani na mhalifu anayempiga mtu fulani.”—When Men Batter Women
[Sanduki katika ukurasa wa 6]
Jeuri Nyumbani Ni Tatizo Lililoenea Ulimwenguni Pote
Ripoti ifuatayo inaonyesha kwamba “wanaume wenye kiburi, walio na mwelekeo wa ukatili kuelekea wanawake wameongezeka ulimwenguni pote.”
Misri: Uchunguzi wa miezi mitatu uliofanywa huko Aleksandria, ulionyesha kwamba wanawake wengi sana wanajeruhiwa hasa kupitia jeuri nyumbani. Jeuri hiyo inasababisha pia asilimia 27.9 ya wanawake kwenda kutibiwa kwenye vituo vya matibabu ya dharura.—Muhtasari wa 5 wa Mkutano wa Nne Unaohusu Wanawake Ulimwenguni.
Thailand: Asilimia 50 ya wanawake walioolewa hupigwa mara kwa mara katika kitongoji kikubwa zaidi cha Bangkok.—Shirika la Pasifiki la Kutetea Afya ya Wanawake.
Hong Kong: “Idadi ya wanawake wanaoripoti kupigwa na wenzi wao iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 mwaka uliopita.”—Gazeti South China Morning Post la Julai 21, 2000.
Japani: Idadi ya wanawake wanaotafuta makao iliongezeka kutoka 4,843 mwaka wa 1995 kufikia 6,340 mwaka wa 1998. “Karibu theluthi moja walisema kwamba walitafuta makao kwa sababu ya ujeuri wa waume zao.”—Gazeti The Japan Times la Septemba 10, 2000.
Uingereza: “Kila sekunde sita, mwanamke hubakwa, hupigwa, au hushambuliwa kwa kisu katika nyumba fulani kotekote Uingereza.” Kulingana na ripoti moja ya Idara ya Uingereza ya Upelelezi wa Jinai, “kila siku polisi hupokea simu 1,300 kutoka kwa wale wanaotendewa jeuri nyumbani, yaani wanapokea zaidi ya simu 570,000 kwa mwaka. Asilimia 81 ni wanawake walioshambuliwa na wanaume.”—Gazeti The Times, la Oktoba 25, 2000.
Peru: Asilimia 70 ya visa vyote vya uhalifu vinavyoripotiwa kwa polisi vinahusu wanawake waliopigwa na waume zao. —Shirika la Pasifiki la Kutetea Afya ya Wanawake.
Urusi: “Katika mwaka mmoja, wanawake Warusi 14,500 waliuawa na waume zao, na wengine 56,400 walilemazwa au kujeruhiwa vibaya katika mashambulizi ya nyumbani.”—The Guardian.
China: “Ni tatizo jipya linaloongezeka upesi hasa katika miji mikubwa,” asema Profesa Chen Yiyun, Mkurugenzi wa Kituo cha Familia cha Jinglun. “Hata uvutano wa majirani hauzuii jeuri nyumbani.”—The Guardian.
Nikaragua: “Jeuri dhidi ya wanawake inazidi kuongezeka. Uchunguzi mmoja ulidai kwamba mwaka uliopita pekee, asilimia 52 ya wanawake wa Nikaragua waliteseka kutokana na jeuri iliyosababishwa na waume zao.”—Shirika la Habari la Uingereza.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Visababishi vya Jeuri Nyumbani
Kulingana na uchunguzi uliosimamiwa na Richard J. Gelles katika Chuo Kikuu cha Rhode Island, Marekani, vifuatavyo ni visababishi vya kutendewa vibaya kimwili na kihisia-moyo nyumbani.
1. Mwanamume huyo alihusika katika jeuri nyumbani hapo awali.
2. Hana kazi ya kuajiriwa.
3. Anatumia dawa haramu za kulevya angalau mara moja kwa mwaka.
4. Alipoishi na wazazi wake, aliona baba akimpiga mama yake.
5. Wenzi hawa hawajafunga ndoa; wanaishi pamoja tu.
6. Iwapo ameajiriwa, ana mapato ya chini.
7. Hakupata elimu ya kutosha.
8. Ana umri wa kati ya miaka 18 na 30.
9. Huenda mmoja wao au wote wawili huwatendea watoto wao kwa jeuri.
10. Ni maskini hohehahe.
11. Mwanamume na mwanamke huyo wanatoka katika tamaduni mbalimbali.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Jeuri ya nyumbani inaweza kuathiri watoto vibaya