Ni Nini Husababisha Jeuri ya Nyumbani?
“Badala ya kuwa kimbilio kutoka kwenye mikazo, shida, vitendo visivyo vya kiakili vya jamii iliyo nje, familia mara nyingi huonekana ikionyesha au hata kukuza shida hizo.”—The Intimate Environment—Exploring Marriage and the Family.
UTAFITI juu ya jeuri ya familia ni jitihada ya karibuni kwa kulinganisha. Uchunguzi mwingi umefanywa tu wakati wa miongo ya karibuni. Matokeo ya uchunguzi huo mwingi huenda yasipatane sikuzote, lakini mambo fulani ya msingi yenye kuchangia jeuri ya nyumbani yamegunduliwa. Acheni tufikirie baadhi yayo.
Historia ya Familia Huwa na Fungu Gani?
Idadi fulani ya watafiti walisema hivi kuhusu mambo waliyogundua: “Kadiri wenzi wa ndoa waliohojiwa walivyo wajeuri zaidi kwa mmoja na mwenzake, ndivyo watoto wao walivyo wajeuri zaidi kwa mmoja na mwenzake, na kwa wazazi wao.”
Kuona tu jeuri ya familia kuna matokeo makubwa kwa mtoto. “Mtoto aonaye mama yake akipigwa ni sawa na mtoto kupigwa,” asema daktari wa tiba ya therapia John Bradshaw. Kijana mmoja aitwaye Ed alichukia kuona baba yake akimpiga mama yake. Hata hivyo, ijapokuwa huenda akawa hakujua hivyo, alikuwa akifunzwa kuamini kwamba wanaume hudhibiti wanawake na kwamba ili kufanya hivyo, wanaume lazima wawaogopeshe, wawaumize, na kuwavunjia heshima. Alipopata kuwa mtu mzima, Ed alitumia mbinu hizo za jeuri, za kumtenda vibaya mke wake.
Baadhi ya wazazi hukataza watoto wao kwa tahadhari wasitazame jeuri katika televisheni, na hilo ni jambo zuri. Lakini wazazi wapaswa kuwa wenye tahadhari hata zaidi inapohusu kuangalia tabia yao wenyewe wakiwa violezo vya kuigwa na watoto wao wenye kuathiriwa na mambo hayo kwa urahisi sana.
Mkazo Huwa na Fungu Gani?
Uchukuaji mimba, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, kifo cha mzazi, kuhama, ugonjwa, na matatizo ya kifedha huleta mkazo, kama yafanyavyo mambo mengine. Watu wengi zaidi hushughulikia mkazo bila kufanya jeuri. Hata hivyo, kwa wengine, mkazo waweza kutokeza jeuri, hasa ukichanganywa na mambo mengine. Kwa mfano, kutunza mzazi mwenye umri mkubwa—hasa mzazi akiwa mgonjwa—mara nyingi kumeongoza kwenye kumtenda vibaya wakati mtunzaji amelemewa na madaraka mengine ya familia.
Kulea watoto hutokeza mkazo. Kama tokeo, uwezekano wa kumtenda mtoto vibaya huongezeka kadiri familia izidivyo kuwa kubwa. Watoto huenda wakaleta ongezeko la kutendwa vibaya kwa mwenzi wa ndoa pia, maana “kutopatana juu ya watoto ndiko huonekana zaidi kukifanya wenzi wa ndoa waanze kupigana,” laripoti Behind Closed Doors.
Maoni Yasiofaa Juu ya Jinsia Tofauti
Dan Bajorek ambaye husimamia kikundi cha kushauri katika Kanada, husema kwamba wanaume wenye kutumia jeuri juu ya wanawake huwa na maoni mabaya juu ya wanawake: “Hata wawe watoka utamaduni gani, wamelelewa kuamini kwamba wanaume ni Namba 1.” Hamish Sinclair, ambaye husimamia programu ya tiba kwa ajili ya wanaume wenye kutumia jeuri juu ya wanawake, husema kwamba wanaume wamezoezwa kuamini kwamba wao ni bora kuliko wanawake na kwamba ni haki yao “kuwaadhibu, kuwatia nidhamu au kuwaogopesha.”
Katika mabara mengi mwanamume huonwa kuwa ana haki ya kumtendea mke wake kama kitu tu, kama kisehemu kingine cha mali yake. Udhibiti na utawala wake juu ya mke wake humfanya aonwe kuwa mwanamume na aheshimiwe. Mara nyingi wake hupigwa vibaya sana na kutendwa vibaya vinginevyo, na mifumo ya kisheria haifanyi lolote hata kidogo juu ya jambo hilo kwa sababu hiyo ndiyo sheria katika mabara hayo. Mwanamume ni bora, na mwanamke ni wa chini; lazima atoe utii kamili kwake bila kujali kama yeye ni mwenye kudharaulika, mjeuri, mpotovu, au mwenye ubinafsi kadiri gani.
Morley Safer ripota wa televisheni ya CBS aliripoti juu ya nchi moja ya Amerika Kusini: “Hakuna mahali katika Latini Amerika ambapo ibada ya kujivunia nguvu za kiume huonekana wazi zaidi . . . Huienea jamii yote, kutia na mahakama ambamo katika kutetea heshima yake ya kiume aweza hata kuua kimakusudi bila hofu ya kuadhibiwa, hasa ikiwa mwenye kuuawa ni mke au kimada wake.” Alishikilia kwamba “hakuna mahali duniani ambapo wanawake huvunjiwa heshima” kama ifanywavyo katika nchi hiyo. Lakini utawala wa wanaume juu ya wanawake na kuvunjia heshima wanawake ni mambo ambayo yameenea pote. Si jambo la bara moja, hata liwe baya kadiri gani humo.
Minna Schulman, mkurugenzi wa idara ya jeuri ya nyumbani na kufikiliza sheria katika New York, alitaarifu kwamba jeuri ni chombo ambacho wanaume hutumia ili kudumisha udhibiti na kuonyesha nguvu na mamlaka yao juu ya wanawake. Aliongeza hivi: “Sisi huona jeuri ya nyumbani kuwa matumizi mabaya ya nguvu na udhibiti.”
Baadhi ya wapiga wake husumbuliwa na hali ya kutojiheshimu, tabia ileile ambayo wao hutia katika wale wapigao. Wakifanya hivyo basi kujiheshimu kwao kutatoshelezwa, nao watahisi kadiri fulani ya kuwa bora na kuwa na udhibiti juu ya binadamu mwingine. Wao huhisi kwamba wanathibitisha uanaume wao kwa njia hiyo. Hata hivyo, je, kweli wafanya hivyo? Kwa kuwa wao hufanya jeuri yao juu ya mwanamke aliye dhaifu zaidi, je, hilo lathibitisha kwamba kwelikweli wao wana nguvu, au badala ya hivyo, halithibitishi kwamba wao hawatumii akili? Je! kweli ni jambo la kiume kwa mwanamume mwenye nguvu zaidi kumpiga mwanamke dhaifu zaidi, asiye na nguvu zaidi? Mwanamume wa tabia yenye nguvu zaidi ya kiadili angeonyesha ufikirio na huruma kwa yule aliye dhaifu zaidi na asiye na nguvu zaidi, si kumtumia isivyo haki kwa manufaa yake mwenyewe.
Wonyesho mwingine wa kufikiri kusiko kwa akili kwa mtumiaji jeuri juu ya wanawake ni uhakika wa kwamba mara nyingi yeye humlaumu mke wake kwa kuchochea mapigo hayo. Huenda akadokeza, au hata akamwambia, mambo kama vile: ‘Hukufanya hili vizuri. Ndiyo sababu ninakupiga.’ Au: ‘Chakula kilichelewa, hivyo wapata tu ustahilicho.’ Katika akili ya mfanya jeuri, ni kosa la mwanamke. Hata hivyo, hakuna kosa la mwanamke linalostahilisha pigo.
Je! Kileo Huleta Tofauti?
Kwa kuwa kileo hupunguza kujidhibiti na huzidisha uwezekano wa kutenda bila kufikiri, haishangazi kwamba wengine huhisi kwamba kinaweza kutokeza utumiaji wa jeuri. Mara nyingi mtu huweza kudumisha udhibiti juu ya hisia zenye jeuri wakati amelevuka, lakini baada ya vinywaji vichache vyenye kileo, huwa mwenye kutumia jeuri. Kileo kimepunguza uwezo wake mbalimbali wa kiakili na kupunguza uwezo wake wa kudhibiti hasira.
Hata hivyo, wengine hudai kwamba tatizo hutokezwa sana-sana na mkazo wala si kileo chenyewe. Wao husema kwamba mtu atumiaye kileo ili kuuweza mkazo ni mtu wa aina ileile ambayo ingeweza kutumia jeuri kwa kusudi hilo. Hilo lamaanisha kwamba mnywaji aweza kuwa mwenye kutumia jeuri akiwa amelevuka kama vile wakati amelewa. Vyovyote iwavyo, hata sababu iwe nini kwa habari hii, hakika kileo hakisaidii kudhibiti hisia za mtu bali kwa kawaida kitafanya jambo lililo kinyume.
Jinsi Vyombo vya Habari Huathiri Vitendo vya Watu
Wengine hudai kwamba televisheni pamoja na sinema hutia moyo maoni ya kujivunia nguvu za kiume na hufundisha kwamba jeuri ni njia halali ya kushughulikia matatizo na hasira. “Mimi nilivutiwa na itikio langu mwenyewe lenye nguvu kwa sinema Rambo,” akiri mshauri mmoja wa familia. “Ingawa katika akili na hisia zangu za mtu mzima ninagutushwa na mauaji mengi ya Rambo, hisia zangu za kitoto humtia moyo aendelee kuua.”
Kwa kuwa watoto wengi wanatumia maelfu ya saa wakitazama televisheni kukiwa na vitendo visivyohesabika vya jeuri, kunajisiwa, na kuvunjiwa heshima kwa wanadamu wengine, hasa wanawake, si ajabu kwamba wengi hukua na kutenda wengine vitendo hivyohivyo vyenye kudhuru kijamii. Na si watoto peke yao wanaoathiriwa bali hata watu wazima pia.
Pia, hasa katika miaka ya karibuni, kiwango kimeongezeka sana cha vitendo vilivyo wazi sana vya jeuri, vya ukosefu wa adili kingono, na vya kuvunjia heshima wanawake kama vionyeshwavyo katika televisheni na sinema. Hakika hilo lazima lifanye tamasha ya jeuri ya nyumbani kuwa mbaya zaidi. Kama vile kikundi kimoja cha uchunguzi kilivyoona, kuna “uhusiano . . . ulio wazi kati ya kutazama televisheni na sinema na mwenendo wenye jeuri.”
Matokeo ya Upweke
Kwa wengi leo maisha hayahusishi watu wengine na ni yenye upweke. Maduka makubwa-makubwa yamechukuwa mahali pa maduka ya ujirani ambayo wenyewe walijua wateja wao kwa majina na walikuwa wenye urafiki kwao. Programu za kujenga upya majengo duni ya viungani, matatizo ya kiuchumi, na ukosefu wa kazi za kuajiriwa hulazimisha familia kuwa zenye kuhama-hama. Kadiri kubwa ya jeuri ya nyumbani huonekana miongoni mwa wale wasio na mawasiliano yenye nguvu ya kijamii.
James C. Coleman, katika kitabu chake Intimate Relationships, Marriage, and the Family, aeleza kwa nini yeye afikiri ndivyo ilivyo. Yeye ahisi kwamba kuwa mpweke hupunguza mazungumzo yenye maana na hufanya iwe vigumu kwa mtumiaji jeuri kuona hali yake ifaavyo na kutafuta msaada kutoka kwa rafiki mwenye kutumainiwa. Kwa kutokuwa na marafiki na jamaa za karibu wawezao kutenda kama nguvu ya kupunguza jeuri humwezesha mtu kuonyesha ubinafsi wake kwa urahisi zaidi, kwa kuwa kufikiri kwake kwenye makosa hakuzuiwi kila siku na wengine walio karibu naye. Ni kama vile Mithali 18:1 isemavyo: “Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; hushindana na kila shauri jema.”
Msaada kwa Familia Yenye Jeuri
Tumezungumzia kisehemu tu cha maelezo yatolewayo kwa sababu za jeuri ya nyumbani. Kuna mengine. Tukiisha kutambua baadhi ya visababishi, sasa twahitaji kuchunguza utatuzi. Ikiwa mtu yumo katika familia yenye jeuri, kigezo cha jeuri chaweza kukomeshwaje? Ni nini maoni ya Biblia? Je! jeuri ya familia itakwisha wakati wowote? Makala ifuatayo kwenye ukurasa wa 10 itazungumzia maswali hayo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Jeuri ya Kihisiamoyo—Kupiga Sana kwa Maneno
KATIKA jeuri ya kutumia nguvu za mwili shambulio hufanywa kwa ngumi; katika jeuri ya kihisiamoyo shambulio hufanywa kwa maneno. Tofauti pekee ni chaguo la silaha. Ni kama Mithali 12:18 isemavyo: “Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; bali ulimi wa mwenye haki ni afya.”
Jeuri ya kihisiamoyo ni yenye hatari kadiri gani, kutia huko “kuchoma kwa upanga”? Dakt. Susan Forward aandika hivi: “Matokeo ni yaleyale [kama ya jeuri ya kutumia nguvu za mwili]. Unaogopa jinsi ileile, unahisi kuwa hoi jinsi ileile, na hupatwa na maumivu jinsi ileile,” kunena kihisiamoyo.
Jeuri ya kihisiamoyo kuelekea mwenzi wa ndoa: “Jeuri ya kindoa si ya kutumia nguvu za mwili tu. Sehemu kubwa, labda iliyo kubwa zaidi, ni ya maneno na kihisiamoyo,” akasema mwanamke mmoja aliyefanyiwa jeuri kwa muda mrefu. Jeuri hiyo huenda ikatia ndani kuita mtu majina mabaya, kupiga kelele, kuchambua daima, matukano yenye kumvunjia mtu heshima, na vitisho vya kufanyiwa jeuri ya kutumia nguvu za mwili.
Maneno yenye kuumiza ambayo humfanya mtu ajione kuwa si wa maana, yenye kushusha, au kuogopesha yaweza kufanya madhara makubwa. Kama maji yenye kutona-tona juu ya mwamba, huenda mwanzoni maneno yenye kumvunjia mtu heshima yakaonekana kuwa bila madhara. Lakini upesi hali ya mtu ya kujiheshimu huharibiwa polepole. “Kama ningelazimika kuchagua kati ya jeuri ya kutumia nguvu za mwili na ya kutumia maneno, ningependelea kupigwa wakati wowote,” akasema mwanamke mmoja. “Waweza kuona alama,” akaeleza, “hivyo angalau watu wakusikitikia. Jeuri ya kutumia maneno hukuudhi tu kupita kiasi. Makovu hayaonekani. Hakuna anayejali.”
Jeuri ya kihisiamoyo kuelekea mtoto: Huenda hiyo ikatia ndani kuchambua daima na kudharau sura, akili, uwezo wa kufanya mambo, au thamani ya mtoto akiwa mtu. Hasa maneno yenye kuumiza ni yenye kudhuru sana. Mara nyingi watoto huyaelewa maneno yenye kuumiza jinsi yalivyo, bila kupambanua kati ya yale yasemwayo kwa uzito na yale yasemwayo kwa “ucheshi.” Daktari wa tiba ya therapia Sean Hogan-Downey asema hivi: “Mtoto huhisi akiumia, lakini kila mtu anacheka, hivyo hujifunza kutotumaini hisia zake.”
Hivyo, katika visa vingi zaidi, kuna kweli katika yale ambayo mwanahistoria na mtungaji wa insha Mskotlandi Thomas Carlyle alisema wakati mmoja: “Sasa naona maneno yenye kuumiza kuwa, kwa ujumla, lugha ya Ibilisi; kwa sababu hiyo, tangu muda mrefu, nimeikataa kabisa.”
Joy Byers, mtaalamu wa kutibu watoto waliofanyiwa jeuri, asema hivi: “Jeuri ya kutumia nguvu za mwili huenda ikamuua mtoto, lakini waweza pia kuua roho [tabia na nia ya mtoto], na hivyo ndivyo kigezo cha daima cha maneno ya mzazi yenye kuvunja moyo yawezavyo kufanya.” Gazeti FLEducator hutoa maelezo haya: “Tofauti na machubuko ambayo yaweza kutambulikana na kwisha, jeuri ya kihisiamoyo hutokeza mabadiliko yasiyoonekana katika akili na utu wa mtoto ambayo hubadili kwa njia yenye kudumu hali yake ya kuona jinsi mambo yalivyo kikweli na uhusiano wake na wengine.”
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuona jeuri kuna matokeo yenye nguvu juu ya mwenendo wa baadaye wa mtoto