Jeuri Iathiripo Nyumbani
“Jeuri ya kibinadamu—iwe ni kuchapwa kofi au kusukumwa,kudungwa kisu au kupigwa risasi—hutukia mara nyingi zaidi miongoni mwa washiriki wa familia kuliko mahali penginepo katika jamii yetu.”—Behind Closed Doors.
TEMBEA katika barabara yoyote katika Amerika. Katika kila nyumba moja kati ya mbili, namna fulani ya jeuri ya nyumbani itatukia angalau mara moja mwaka huu. Na katika nyumba 1 kati ya 4, itatukia mara nyingi. Kwa kushangaza, wengi ambao huogopa kutembea barabarani usiku wamo katika hatari kubwa zaidi wawasilipo nyumbani.
Lakini jeuri ya nyumbani haitukii katika Amerika peke yake. Inatukia ulimwenguni kote. Kwa mfano, katika Denmarki mauaji ya kimakusudi 2 kati ya 3 hutukia katika familia. Utafiti katika Afrika huonyesha kwamba mauaji yote ya kimakusudi yale yatukiayo ndani ya familia hutofautiana kati ya asilimia 22 hadi 63, ikitegemea nchi. Na katika Latini Amerika watu wengi, hasa wanawake, hushushiwa heshima, hupigwa, au kuuawa na wanaume wajivuniao nguvu zao za kiume.
Katika Kanada wanawake wapatao mia moja huuawa na waume zao au wanaume waishio nao. Katika United States, ikiwa na watu karibu mara kumi ya idadi ya watu wa kanada, kila mwaka wanawake wapatao 4,000 huuawa na waume au wanaume rafiki zao. Zaidi ya hilo, kila mwaka watoto wapatao 2,000 huuawa na wazazi wao, na idadi hiyohiyo ya wazazi huuawa na watoto wao.
Hivyo, ulimwenguni kote, waume hupiga wake zao, wake hugonga waume zao, wazazi huchapa watoto wao, watoto hushambulia wazazi wao, na watoto ni wenye jeuri kuelekeana. Hasira na jeuri iliyo nyingi zaidi ambayo huwapata watu wazima katika maisha zao ni kutoka au kuelekea watu wenye uhusiano wa damu,” chashikilia kitabu When Families Fight, “na hasira hiyo ni kali zaidi ya ipatwayo katika uhusiano mwingine wowote.”
Familia Yapigana
Kumtendea vibaya mwenzi wa ndoa: Mara nyingi mno, waume hukiona cheti cha ndoa kuwa cheti cha ruhusa ya kupiga wake zao. Ingawa wanawake hupiga wanaume, dhara kwa kawaida si kubwa kama lile liwapatalo wanawake wakati wanaume wanapowapiga wake zao. Gazeti Parents huripoti hivi: “Zaidi ya asilimia 95 ya visa viripotiwavyo vya kutendwa vibaya [sana] kwa mwenzi wa ndoa huhusisha mwanamume akimpiga mwanamke.”
Mwanasheria wa wilaya katika New York ataarifu hivi: “Jeuri dhidi ya wanawake inaenea kwa kadiri kubwa katika jamii ya Kiamerika. FBI [Shirika la Upelelezi] limekadiria kwamba . . . wanawake wengi kama milioni 6 hupigwa kila mwaka.” Ingawa idadi ya visa hutofautiana nchi na nchi, ripoti huonyesha kwamba kupigwa kwa wanawake na wanaume huenea pote katika mabara mengi ikiwa si yale mengi zaidi.
Katika United States, inakadiriwa kwamba “mmoja kati ya wanawake 10 atashambuliwa vikali (apigwe, apigwe mateke, aumwe au atendwe jambo baya zaidi) na mume wake wakati fulani katika wakati wa ndoa yake.” Visa visivyo vibaya kama hivyo vitiwapo ndani, gazeti Family Relations hutaarifu, “mmoja kati ya wanawake wawili katika United States atapatwa na jeuri ya nyumbani.”
Kwa kweli, mwanasheria mmoja wa wilaya katika New York asema kwamba imeonyeshwa kwamba kupiga wake husababisha kwa wanawake majeraha mengi zaidi yenye kutaka walazwe hospitalini kuliko visa vyote vya kunajisiwa, kushambuliwa na wakora na aksidenti za magari vikijumlishwa pamoja.”
Dakt. Lois G. Livezey aandika hivi: “Ni wazi kwamba jeuri dhidi ya wanawake na jeuri ndani ya familia iko kila mahali, na kwamba watendaji . . . ni watu wa kawaida. . . . Ni tatizo zito miongoni mwa tabaka zote na jamii zote na idadi zote za watu.”
Nyakati nyingine watendwa vibaya hujilaumu wenyewe kwa kutendwa vibaya, ikitokeza hali ya kutojiheshimu sana. Gazeti Parents hueleza hivi: “Mwanamke akosaye kujitumaini na ambaye hajiheshimu sana hujifanya awe lengo la kutendwa vibaya. . . . Mfano wa mwanamke aliyetendwa vibaya ni yeye ambaye huhofu kupanga na kutenda kwa manufaa yake mwenyewe.”
Jeuri ya kindoa huwa pia na matokeo mabaya kwa watoto. Wao hujifunza kwamba jeuri yaweza kutumiwa ili kutumia wengine kujifaidi. Baadhi ya akina mama hata huripoti kwamba watoto wao hutumia vitisho dhidi yao, kama vile “Nitamwambia baba akupige,” ili kupata watakayo.
Kuwatenda watoto vibaya: Kila mwaka mamilioni ya watoto hukabili adhabu ya kimwili yenye kupita kiasi ambayo ingeweza kuwajeruhi, kuwalemaza, au kuwaua. Inakadiriwa kwamba kwa kila kisa cha kutendwa vibaya kiripotiwacho, visa 200 haviripotiwi. “Kwa watoto, mara nyingi nyumbani ndipo mahali hatari kupita pengine pote pa kuwa,” chadai kitabu Sociology of Marriage and the Family.
Profesa wa chuo kikuu John E. Bates asema kwamba kutendwa vibaya ndio uvutano wenye nguvu zaidi wa nyumbani uathirio jinsi mtoto atakavyojiendesha baadaye maishani. Dakt. Susan Forward asema hivi: “Mimi nimeona kwamba hakuna tukio jingine maishani ambalo hutia makovu sana hali ya kujiheshimu kwa watu au kuwafanya waelekee kuwa na magumu makubwa ya kihisiamoyo katika utu mzima.” Ishara za tabia ya jeuri katika hali ngumu zaweza kuonekana hata katika watoto kuanzia umri wa miaka minne hadi mitano. Kadiri wakuavyo, watoto hao huwa na viwango vya juu zaidi vya kutumia vibaya dawa za kulevya, kutumia vibaya kileo, tabia ya uhalifu, masumbufu ya kiakili, na ukuzi uliokawia.
Kwa kueleweka, watoto wengi waliotendwa vibaya huwa na hasira kuelekea awatendaye vibaya, lakini mara nyingi huwa na hasira pia ku-elekea yule mzazi asiyewatenda vibaya kwa kuruhusu jeuri iendelee. Katika akili ya mtoto, yule mzazi aonaye akitendwa vibaya asizuie huenda akaonwa kuwa mshiriki wa kutenda vibaya.
Kuwatenda vibaya watu wa umri mkubwa: Ikadiriwayo kuwa asilimia 15 ya watu wenye umri mkubwa wa Kanada hutendwa vibaya kimwili na kiakili na watoto wao walio watu wazima. Daktari mmoja atabiri kwamba “hali itazidi tu kuwa mbaya huku idadi kubwa zaidi ya watu iwapo yenye umri mkubwa zaidi, na mizigo yenye kulemea kifedha na kihisiamoyo kwa watoto wao iongezekavyo.” Hofu kama hizo huhisiwa ulimwenguni pote.
Mara nyingi, wenye umri mkubwa huwa hawana nia ya kuripoti kutendwa vibaya. Huenda wakawa wanamtegemea mwenye kuwatenda vibaya na hivyo wakachagua kuendelea kuishi chini ya hali mbaya. “Wakati mwingine” ndilo jibu alilotoa daima mwanamke mwenye umri mkubwa alipoulizwa angewaripoti mwana na binti mkwe wake wakati gani kwa wenye mamlaka. Walikuwa wamempiga vibaya sana hivi kwamba alilazwa hospitalini kwa mwezi mmoja.
Kutendeana vibaya kwa watoto: Hii ni namna ya jeuri ya nyumbani yenye kuenea sana. Baadhi ya watu huifanya kuwa jambo dogo, wakisema, “Hiyo ni kawaida ya wavulana.” Hata hivyo, zaidi ya nusu ya watoto waliokuwa katika uchunguzi mmoja walikuwa wametenda vitendo vilivyokuwa vibaya sana kiasi cha kutosha kushtakiwa kwa uhalifu kama vitendo hivyo vingalikuwa vimeelekezwa dhidi ya mtu fulani nje ya familia.
Wengi huhisi kwamba kutendeana vibaya kwa watoto hutokeza kigezo ambacho huendelezwa hadi utu mzima. Kwa wengine hiyo huenda hata ikawa sababu ya kutenda vibaya mwenzi wa ndoa baadaye badala ya kuwa kwamba wameona jeuri kati ya wazazi wao.
Mahali Hatari pa Vita
Mchunguzi mmoja wa kisheria alikadiria wakati mmoja kwamba polisi waliitwa washughulikie mapambano ya familia mara nyingi zaidi ya visa vyote vingine vya uhalifu vikijumlishwa pamoja. Alidai pia kwamba polisi wengi zaidi waliuawa walipokuwa wameenda kushughulikia tatizo la kinyumbani kuliko wakati walipokuwa wakishughulikia ombi la namna nyingine yoyote. “Angalau kwa habari ya wizi wa kutumia nguvu unajua la kutazamia,” akasema polisi mmoja. “Lakini ingia ndani ya nyumba ya mtu fulani . . . hujui litakalotukia.”
Baada ya uchunguzi mwingi wa jeuri ya nyumbani, kikundi kimoja cha uchunguzi katika Amerika kilifikia mkataa kwamba, familia ilikuwa ndicho kikundi cha kijamii chenye jeuri zaidi, isipokuwa tu jeshi katika wakati wa vita.
Ni nini hutokeza jeuri ya familia? Je! itakwisha wakati wowote? Je! Kuna wakati wowote inapostahili? Makala ifuatayo itachunguza maswali hayo.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Jeuri dhidi ya wanawake inaenea kwa kadiri kubwa katika jamii ya Kiamerika.”—Mwanasheria wa wilaya
[Blabu katika ukurasa wa 5]
“Kwa watoto, mara nyingi nyumbani ndipo mahali hatari kupita pengine pote pa kuwa.”—Sociology of Marriage and the Family