Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 12/8 kur. 23-25
  • Madubwana Wenye Kuvutia wa Kaskazini mwa Kanada

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Madubwana Wenye Kuvutia wa Kaskazini mwa Kanada
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kujamiiana na Kuishi Katika Pango
  • Tabia Zao Nyinginezo
  • Kuzuru Dubu-Barafu
  • Dubu-Jike Hulala Fofofo Wakati wa Majira ya Baridi Kali
    Amkeni!—2002
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2003
  • Chui—Paka Mwenye Usiri
    Amkeni!—1995
  • Jinsi Wanyama Wanavyowalisha na Kuwatunza Watoto Wao
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 12/8 kur. 23-25

Madubwana Wenye Kuvutia wa Kaskazini mwa Kanada

Na mleta habari za Amkeni! katika Kanada

“MFALME wa Kaskazini” na “Mabwana wa Aktiki” ni majina yanayovutia ambayo hutumiwa kwa dubu-barafu wapatao 30,000 ambao huzurura-zurura katika sehemu zote za Eneo la Barafu la Kaskazini.

Kuna aina kadhaa tofauti-tofauti za dubu-barafu. Kikundi kimoja kimechagua pwani ya kusini-magharibi ya Ghuba ya Hudson ya Kanada, kutoka Kisiwa cha Akimski katika Ghuba ya James hadi Hori ya Chesterfield, kuelekea kaskazini, kuwa eneo lao. Hivyo, mji Churchill, katika Manitoba, ambao upo kati ya sehemu hizo mbili, umeitwa “mji mkuu wa dubu-barafu ulimwenguni pote.”

Dubu-barafu wa kiume huzurura-zurura katika eneo lake kwa udadisi bila kuchoka. Jambo hilo limefanya apewe jina la kishairi la lugha ya Kiinuit Pihoqahiak, yaani “yule atangatangaye daima.”

Wavumbuzi wa nchi wa mapema wa sehemu za kaskazini walishangazwa na dubu-barafu. John Muir, mpenda-asili Mwamerika, alimfafanua kuwa ‘mnyama mwenye fahari na nguvu nyingi sana, aishiye kwa ujasiri na kwa ujoto kati ya barafu ya daima.’

Ingawa wana uzito wa kutoka kilo 450 hadi 640, wao ni wepesi karibu kama paka. Mwanabiolojia mmoja alisema hivi: “Wao ni kama paka wakubwa. Huwezi kuamini kabisa jinsi walivyo wepesi—wao huenda kwa kasi wee.”

Kujamiiana na Kuishi Katika Pango

Dubu wa kiume ‘hapendi maisha ya familia.’ Baada ya kujamiiana, yeye huacha jike abaki peke yake na mzigo wote wa kulea watoto. Yai lililotungwa ndani ya jike hujigawanya mara kadhaa, kisha labaki katika hali iyo hiyo bila utendaji wowote kwa miezi minne au mitano ijayo.

Uhai uanzapo na ukuzi kuanza, dubu jike huchimba pango katika theluji katika bonde lenye kina zaidi awezalo kupata au pango katika mchanga kwenye ukingo wa ziwa. Huko atakaa bila chakula, bila kukojoa wala kunya mpaka mwisho wa mwezi wa Machi.

Pango hilo limefanyizwa kwa uhandisi mkubwa. Kutokea kiingilio shimo refu lainuka kuelekea juu kwa meta mbili hivi kufikia chumba chenye ukubwa wa kutosha. Joto la mwili wake hunaswa humo ndani hivi kwamba pango hilo mara nyingi huwa na joto la digrii za Sentigrade 20 kuliko halijoto ya nje. Tundu ndogo kwenye dari ya pango hutoa hewa chafu. Tandiko jipya la sakafu hufanywa kulingana na uhitaji kwa kukanyaga-kanyaga chini theluji iliyotolewa juu ya pango.

Ungetazamia kwamba dubu mkubwa kama huyo angezaa watoto wakubwa kama yeye. Lakini watoto waliotoka tu kuzaliwa huwa na uzito upatao nusu-kilo pekee! Mara nyingi wao huzaliwa wakati fulani katika Desemba au mapema katika Januari.

Watoto hao huzaliwa vipofu na viziwi, nao hufunikwa kwa sufu za nyuzinyuzi ila tu kwenye mafumba ya miguu yao na pua zao. Wakitumia makucha yao yaliyo kama mundu, wao hupanda manyoya ya mama yao ili wanyonye maziwa yake yenye lishe bora, yaliyo na mtindi na ladha ya mafuta ya samaki.

Mara nyingi dubu wa kike huzaa mapacha kwa kila miaka mitatu katika maeneo mengi ya Kaskazini. Lakini, nyakati nyingine wale dubu wa eneo la Ghuba ya Hudson huzaa watoto watatu, na mara moja-moja watoto wanne, katika kila mwaka wa pili. Watoto hao hukua haraka. Baada ya siku zipatazo 26, wao husikia sauti zao za kwanza. Siku saba baadaye, macho yao hufunguka. Manyoya ya utotoni hugeuka kuwa manyoya halisi, ambayo humea kwa wingi zaidi.

Kuelekea mwisho wa mwezi wa Machi, familia hutoka kwenye pango na kuingia kwenye jua la masika ya Aktiki. Kukiwa na theluji nyingi kila mahali, watoto hao huruka-ruka na kujivingirisha-vingirisha. Wakipata mteremko wa kilima kilichoinuka sana, wao huteleza kuelekea chini kwa matumbo yao madogo yaliyonenepa, miguu ya mbele na ya nyuma ikiwa imenyooshwa, na kwenda moja kwa moja hadi kwenye mikono ya mama anayengojea kule chini.

Nyakati nyingine inakuwa vigumu kwa watoto kufuata nyayo za mama kupitia theluji yenye kina. Suluhisho lao ni nini? Kupanda mgongo wa mama! Pindi moja mpiga-picha mmoja aliona dubu wa kike, waliokuwa wamesumbuliwa na helikopta, wakitoroka huku watoto wao wakiwa mgongoni mwao “kama wapandaji farasi wadogo wenye hofu.”

Mama huwazoeza kwa uangalifu kwa miaka miwili na nusu hivi. Kisha huwaacha. Sasa dubu hao wachanga hujitegemea.

Tabia Zao Nyinginezo

Kulingana na makala moja katika gazeti Life, “dubu-barafu ni waogeleaji wenye nguvu zaidi ya wanyama wote wenye miguu minne ulimwenguni.” Wao waweza kuogelea miongoni mwa barafu zinazoelea na kuvuka ghuba zilizo kubwa. Na kwa kuwa wala maji wala vijipande vya barafu haviwezi kushika manyoya yao yenye mafuta, wao hujitikisa kwa nguvu na kuondoa umajimaji mwingi. Kujiviringisha katika theluji iliyokauka huondoa unyevu wowote ambao umebaki, na manyoya yake hukauka baada ya dakika chache tu.

Wanasayansi wamejifunza hivi karibuni tu juu ya siri za kustaajabisha za manyoya ya dubu. Jinsi ambavyo manyoya hayo hufyonza nuru na kuiangaza husaidia mwili ubaki katika hali ya joto na vilevile hufanya manyoya yaangaze kwa weupe sana.a

Lakini ni kwa nini wao hawapotei katika mandhari ya Aktiki ibadilikayo daima ambayo ina ishara chache sana za kudumu, ikiwa ziko, ziwezazo kuwasaidia wasipotee njia? Kulingana na kitabu Arctic Dreams, ni lazima dubu “awe na ramani akilini mwake . . . Kumbukumbu haliwezi kumsaidia. Jinsi ambavyo dubu hufanyiza na kutumia ramani hizo ni mojayapo maswali yatatanishayo zaidi juu yao.” Wao waweza kutanga-tanga kwa majuma bila kupotea.

Ingawa ni nadra sana kwa dubu kushambulia wanadamu, wageni wahitaji kustahi nguvu zao nyingi na wepesi wao mkubwa. Kitabu icho hicho kilisema hivi: “Dubu-barafu ni wenye haya kidogo na ni wapole, hasa ukiwalinganisha na dubu-mkuu.” Lakini wao waweza kukushtua kwa sababu miguu yao yenye manyoya mengi huwafanya watembee bila kutokeza sauti.

Kuzuru Dubu-Barafu

Twaweza kuzuruje viumbe hivi vyenye kupendeza? Wanasayansi wamejenga minara ya vyuma yenye kimo cha meta 14 kando-kando ya pwani ya Ghuba ya Hudson ambako dubu-barafu huchunguzwa.

Magari yaitwayo Tundra Buggies hupatikana kwa watalii katika mji wa Churchill. Hayo ni magari makubwa yenye vyuma yawezayo kubeba abiria kadhaa wanaotembezwa. Nyakati nyingine waweza kuona dubu kwa ukaribu wakati aegemeapo vyuma vya gari au kuvipiga kwa fumba ili aelekezewe fikira au akitaka apewe chakula.

Twatumaini kwamba umefurahia ziara hii ya dubu wakubwa wa Kaskazini, ambao wanaripotiwa kuwa miongoni mwa wanyama kumi “wapendwao zaidi” wa ulimwengu. Kwa kweli, wao ni viumbe vyenye urembo, kazi za Muumba mwenye hekima yote, aliyewapa uwezo wa kujipatanisha na sehemu za dunia zenye barafu za Eneo la Barafu la Kaskazini.

[Maelezo ya Chini]

a Ona “Uhandisi Mkubwa wa Dubu-Barafu” katika toleo la Amkeni! la Mei 22, 1991, Kiingereza.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mama azoeza watoto wake kwa muda wa miaka miwili hivi

[Picha katika ukurasa wa 25]

Ndume wachanga wafurahia kupigana kimchezo, na kisha wajipoeza kwenye theluji

[Hisani]

Picha zote: Mike Beedell/Adventure Canada

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki