Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 12/22 kur. 17-19
  • Je, Napaswa Kuchukua Kadi ya Mkopo?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Napaswa Kuchukua Kadi ya Mkopo?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuhesabu Gharama
  • Kutumia Kadi ya Mkopo kwa Busara
  • Kufurahia Manufaa
  • Kadi za Mkopo—Je, Zitakutumikia au Zitakutumikisha?
    Amkeni!—1996
  • “Tupeleke Kadi”
    Amkeni!—1993
  • Uandalizi Mpya wa Kutusaidia Kujiepusha na Damu
    Huduma ya Ufalme—2006
  • Je, Unatumia Vizuri Kadi za Mawasiliano za JW.ORG?
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo (2016)
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 12/22 kur. 17-19

Vijana Huuliza . . .

Je, Napaswa Kuchukua Kadi ya Mkopo?

“Nilipokea ombi la kadi ya mkopo mara ya kwanza nilipokuwa na umri wa miaka 16. . . . Nilipofikia umri wa miaka 18, nilikuwa na deni kubwa la takriban dola 60,000 za Marekani.”—Kristin.

MWANZONI, Kristin alipanga kutumia kadi yake ya mkopo hasa kwa hali za dharura—na labda kwa ununuzi wa kitu kimoja-kimoja alichohitaji asichoweza kulipia kwa pesa taslimu. Punde si punde mambo yakaenda mrama. “Nilianza kununua vitu ovyoovyo huku nikiagiza kwa shauku nyingi vitu vilivyoorodheshwa,” akiri Kristin. “Hata nilinunua vitu nisivyopenda.” Sasa Kristin ana maoni tofauti kuhusu kadi za mkopo. “Sikujua kamwe namna ambavyo kadi hiyo ndogo ya plastiki ingevuruga maisha yangu,” yeye asema.—gazeti la Teen.

Jambo lililompata Kristin ni la kawaida. Idadi inayoongezeka ya vijana wanajitumbukiza katika hatari ya kifedha kwa sababu ya kipande hicho cha plastiki, kadi ya mkopo. Baadhi ya makampuni yanawalenga sana vijana. Yaelekea wanajua kwamba kadi za mkopo zaweza kuwa, kile kilichoitwa na mshauri wa kifedha Jane Bryant Quin, “dawa ya kulevya ya kifedha” kwa wale wanaopenda kutumia fedha. “Kadiri unavyozitumia,” yeye asema, “ndivyo inavyokuwa vigumu kuacha.”

Kwa kweli, kuwa na kadi ya mkopo kwaweza kunufaisha—kwa mfano, hali ya dharura inapozuka au inapokuwa hatari kubeba pesa taslimu. Hiyo ni sababu moja inayofanya kadi za mkopo zipendwe na wengi Marekani na katika nchi nyingine pia. Hata hivyo, kadi ya mkopo isipotumiwa kwa busara, inaweza kumletea mtumiaji deni kubwa sana asiloweza kulipa kwa urahisi. Hivyo, ripoti moja iliyochapishwa katika gazeti la Globe and Mail la Toronto ilionyesha ongezeko la zaidi ya mara tatu “la idadi ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 23 wenye madeni chungu nzima wanaotafuta msaada katika Idara ya Kutoa Mashauri Kuhusu Madeni huko Toronto.” Ripoti hiyo ilisema kwamba wengi wao walikuwa na deni la dola zipatazo 25,000 za Kanada, na mojawapo ya kisababishi kikuu cha madeni hayo kilikuwa ni gharama zilizosababishwa na kadi ya mkopo.

Je, wapaswa kuchukua kadi ya mkopo? Hilo lapasa kuamuliwa na wazazi wako. Ikiwa wanaona kwamba unahitaji kungoja, uwe mwenye subira. Ukitumia fedha kwa busara, punde si punde huenda wakakupa madaraka makubwa zaidi ya kifedha. (Linganisha Luka 16:10.) Kwa sasa, wapaswa kujua kwamba kutumia kadi ya mkopo—sawa na kuendesha gari—kuna manufaa na hatari.

Kuhesabu Gharama

Kwa kweli kununua vitu kwa kutumia kadi ya mkopo ni sawa na kukopa fedha. Na kama ilivyo na kukopa kokote, ni lazima ulipe unachokopa. (Mithali 22:7) Lakini unalipiaje vitu unavyonunua kwa kadi ya mkopo?

Kwa kawaida, karibu mwisho wa kila mwezi unapokea taarifa iliyochapishwa ya malipo, inayoonyesha vitu vilivyonunuliwa kwa kadi hiyo na vilevile jumla ya fedha unazodaiwa. Taarifa hiyo huonyesha pia kiasi unachotarajiwa kulipa mara moja. Kwa kawaida, kiasi hicho huwa kidogo sana. Kama tokeo, huenda ukafikiri, ‘Si jambo baya sana. Endapo nitalipa kiasi kidogo wanachohitaji kila mwezi, baada ya muda nitakamilisha deni langu.’ Hata hivyo, tatizo ni kwamba muda wa nyongeza wa kulipa unapopita, utaanza kutozwa ada ya kifedha—riba—kwa kiasi kinachosalia unachodaiwa. Na malipo ya riba kwa kadi za mkopo yaweza kuwa juu sana.a

Fikiria Joseph, aliyedaiwa kiasi cha takriban dola 1,000 za Marekani kwenye taarifa ya malipo ya mwezi mmoja. Bila shaka, Joseph alihitaji kulipa tu kiasi kidogo kilichoombwa, kiasi cha dola 20 za Marekani. Lakini Joseph alipochunguza kwa uangalifu taarifa yake ya malipo, aligundua kwamba alikuwa ametozwa ada ya takriban dola 17 kuongezea kiasi alichodaiwa mwezi huo! Hilo lilimaanisha kwamba hata kama Joseph angelipa kiasi kidogo cha dola 20, angekuwa amepunguza deni lake la dola 1,000 kwa dola 3 tu!

Ikiwa utalipa tu kiasi kidogo kinachodaiwa, itakuchukua muda gani kulipia deni la kadi ya mkopo? Kikitoa mfano wa kukisiwa, kijitabu kilichochapishwa na Federal Trade Commission na Shirika la American Express kinasema: “Ikiwa utalipa kiasi kidogo tu kila mwezi kwa ajili ya deni lililosalia la dola 2,000 za Marekani na kutozwa riba ya asilimia 18.5, utalipia deni hilo kwa zaidi ya miaka 11 na itakugharimu dola 1,934 zaidi za riba tu, kiasi ambacho chakaribia kuwa maradufu ya bei ya kawaida.”

Kama uwezavyo kuona, usipokuwa mwangalifu, unaweza kujitumbukiza katika matatizo makubwa ya kifedha kwa kutumia kadi ya mkopo. “Kwa kweli nilikuwa nikilipa karibu maradufu kwa kila kitu,” asema Kristin. “Nilipochelewa kulipa, wakopeshaji walinitoza ada ya kuchelewa kulipa. Sikujua la kufanya.”

Kutumia Kadi ya Mkopo kwa Busara

Kristin alijifunza kupitia magumu kwamba zoea la “kuchukua sasa, na kulipa baadaye” unaponunua vitu laweza kuwa hatari. Madeni yaweza kurundamana, na punde si punde utapata kwamba kiasi kidogo unacholipa kinagharimia tu ada za kifedha unazotozwa. Watumiaji wenye busara wa kadi za mkopo huepukaje mtego huo wa kifedha?

● Wao huzingatia ununuzi wao na kuchunguza kwa uangalifu taarifa zao za malipo ya kila mwezi ili kuhakikisha kwamba wanatozwa tu kiasi kinacholingana na ununuzi wao.

● Wao hulipa madeni yao pasipo kukawia, wakitambua kwamba rekodi nzuri ya ukopaji itawasaidia baadaye—labda wanapoomba kazi au bima au wanaponunua gari au nyumba.

● Wao hulipa kiasi kamili wanachodaiwa iwezekanapo ili waweze kuepuka kutozwa riba ya juu kwa kiasi kinachosalia.

● Hawataji nambari na tarehe ya mwisho ya kadi yao ya mkopo kupitia simu isipokuwa wawe wanamjua mtu au kampuni wanayoshughulika nayo.

● Hawampi kamwe mtu yeyote kadi yao ya mkopo, hata akiwa rafiki. Kwa vyovyote vile, ikiwa kadi hiyo itatumiwa isivyofaa ni rekodi ya ukopaji ya mmiliki wa kadi itakayoathiriwa.

● Wao huepuka kutumia kadi yao ya mkopo kuwa njia nyepesi ya kupata pesa taslimu, kana kwamba ni kadi ya benki. Kumbuka kwamba, kwa kawaida deni la pesa taslimu hutozwa riba ya juu kuliko la ununuzi.

● Wao hawajazi na kupeleka kila ombi la kadi ya mkopo wanalopokea. Kwa vijana wengi, kadi moja yatosha.

● Wao hutumia kadi yao ya mkopo kwa busara, wakitambua kabisa kwamba wanaponunua kitu nayo, wangali wanatumia fedha halisi, hata ingawa hawatumii noti au sarafu.

Kufurahia Manufaa

ahamu kabisa manufaa na hatari za kadi ya mkopo, uwe unayo sasa au iwapo unafikiria kuchukua moja hivi karibuni. Jiulize maswali yafuatayo: Kwa nini nahitaji kadi ya mkopo? Je, ni kwa sababu tu nataka kununua vitu vya kimwili, kuwa na vitu vya mtindo wa kisasa, ili niwapendeze marafiki wangu? Je, nahitaji kujifunza kuwa mwenye kuridhika zaidi na vitu vya lazima, vile vilivyoitwa na mtume Mkristo Paulo “riziki na cha kujifunika”? (1 Timotheo 6:8) Je, madeni yaletwayo na kadi za mkopo yatatokeza matatizo ya kifedha yenye kulemea yatakayonizuia nisikazie mambo ya maana zaidi maishani?—Mathayo 6:33; Wafilipi 1:8-11.

Yafikirie maswali hayo kwa uzito, na uyazungumzie na wazazi wako. Ukifanya hivyo, basi uwe una kadi ya mkopo au la, utaepuka mkazo wa kifedha ambao watu wengi wamejiletea.—Mithali 22:3.

[Maelezo ya Chini]

a Unaweza kujua riba inayotozwa na kampuni mahususi ya kadi za mikopo kwa kuchunguza asilimia ya malipo ya kila mwaka (APR) yaliyoandikwa kwenye ombi au kwenye taarifa ya kila mwezi ya malipo.

[Sanduku katika ukurasa wa 19]

Umuhimu wa Kupata Kibali cha Wazazi

Vijana wengi hupata fursa ya kumiliki kadi ya mkopo kwa mara ya kwanza wanapopokea ombi katika sanduku lao la barua. Kwa kweli, baada ya muda fulani baadhi yao hupokea maombi kadhaa. “Makampuni yanayotoa kadi za mikopo yanashindana sana kuwapa vijana kadi hizo,” aeleza Jane Bryant Quinn, “kwa sababu uchunguzi unaonyesha kwamba sisi huelekea kuhifadhi kadi ya mkopo tunayopata kwanza.”

Kwa kawaida ni lazima mzazi au mtu mwingine mzima mwenye rekodi nzuri ya kutumia kadi ya mkopo atie sahihi ombi hilo la kadi ya mkopo ili kuhakikishia kampuni inayotoa kadi ya mkopo kwamba vitu vyote vinavyochukuliwa vitagharimiwa. Kwa kusikitisha, vijana wengi hutumia udanganyifu ili kuepuka hatua hiyo. Kijana mmoja aliandika jina la nyanya kuwa mwombaji mkuu pasipo kibali chake na jina lake kuwa mwombaji mshirika. Wazia mshangao wa nyanya alipogundua kwamba alikuwa na deni la makumi elfu ya dola!

Kuiga kwa udanganyifu sahihi ya mzazi au ya mtu mwingine mzima kwenye ombi la kadi ya mkopo ni ukosefu wa haki, na ukosefu wa haki hushutumiwa na Mungu. (Mithali 11:1; Waebrania 13:18) Kwa hiyo iwapo unataka kadi ya mkopo, zungumza na wazazi wako kuhusu jambo hilo. Kupata kibali chao kutakufaidi hatimaye. Kumbuka kwamba, yaelekea wazazi wako wana uzoefu wa kulipa madeni, na wanaweza kukupa shauri linalofaa. Kwa hiyo zungumza nao, na usitumie kamwe ukosefu wa haki ili kupokea kadi ya mkopo.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kutumia kadi ya mkopo kiholelaholela kwaweza kutokeza matatizo makubwa ya kifedhayy

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki