Mizingile—Kwa Nini Huvutia Sana?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Uingereza
Mzingile unaweza kuwa na njia zilizozibwa kwenye mwisho mmoja, na njia sahihi, inapogunduliwa, kwa kawaida huongoza kwenye mzingile, ikitokea kwenye njia nyingine.
Mizingile yaweza kuogofya, kutatanisha, au kuvunja moyo wale wanaoiingia. Lakini mizingile ya kale pia inahusishwa na sanaa za jadi za ushirikina. Kwa nini basi, wajenzi wa makanisa ya Jumuiya ya Wakristo hujenga mizingile katika majengo yao? Jibu hutatanisha.
KAZI kubwa zaidi ya ujenzi ya Wamisri wa kale ilikuwa gani? Kulingana na waandishi fulani, haikuwa piramidi, kama inavyoaminiwa kwa ujumla, bali Mzingile wao mkubwa sana. Ulijengwa karibu na Ziwa Moeris, linalojulikana leo kuwa Ziwa Qarun, lililoko magharibi ya Mto Nile, kilometa 80 kusini ya jiji la kisasa la Cairo.
Mnamo karne ya tano K.W.K., mwanahistoria Mgiriki Herodoto aliandika hivi: “Nilizuru mahali hapa [Mzingile] na kuona kwamba hapawezi kufafanuliwa; kwa kuwa ikiwa kazi na gharama za kuta zote na majengo yote makubwa ya Wagiriki zingejumlishwa, haziwezi kufikia za Mzingile huu.” Aliongezea hivi: “Mzingile wazidi piramidi.” Karne nne baadaye, mwanahistoria mwingine Mgiriki, Strabo, aliutaja Mzingile kuwa “kazi iliyotoshana na kujenga Piramidi,” ingawa kufikia wakati huo ulikuwa umechakaa sana.
Mwanahistoria F. Barham Zincke alizuru eneo hilo mwaka wa 1871, na hatimaye mahali hapo pakatambuliwa na mwakiolojia Flinders Petrie mwaka wa 1888. Ni mabaki ya Mzingile yaliyosalia wakati huo, na leo vitabu vya mwongozo haviutaji hata kidogo. Hata hivyo, wakati mmoja, Mzingile huo ulikuwa mashuhuri. Ulikuwaje, na kwa nini ulijengwa?
Maelezo na Kusudi
Mzingile ulijengwa mapema sana katika historia ya Misri, labda hata kabla Waebrania kukaa Misri. (Mwanzo 46:1-27) Ulisemekana kuwa na orofa mbili zenye vyumba 3,000 vyenye ukubwa sawa—orofa moja ilikuwa chini ya ardhi. Ulikuwa na ukubwa wa meta mraba 70,000.
Mfumo wa njia za Mzingile, nyua, vyumba, na safu za nguzo ulikuwa wenye kutatanisha na kukanganya sana hivi kwamba mgeni hangeweza kamwe kuingia au kutoka bila mwongozo fulani. Sehemu kubwa ilikuwa na giza totoro, na wakati baadhi ya milango ilipofunguliwa, ilisemekana kuwa ilitokeza sauti yenye kuogofya, kama ile ya radi. Baada ya kuporomoka kwa Misri ikiwa Serikali ya Ulimwengu, nguzo za matale zenye kuvutia za rangi nyekundu, vibamba vikubwa vya mawe, na mawe ya chokaa yaliyong’arishwa vizuri ya Mzingile huo yaliporwa na kutumiwa tena.
Ijapokuwa inaripotiwa kwamba Mzingile huo ulitumiwa na wafalme wa Misri kuwa kituo cha utawala wa nchi hiyo, kazi yake halisi ilikuwa ya kidini. Ulikuwa jengo la hekalu ambamo dhabihu zilitolewa kwa miungu yote ya Misri. Wageni hawakuruhusiwa kuona vyumba vya ardhini vya Mzingile, vilivyokuwa na maziara ya wafalme na mamba watakatifu.
Umuhimu wa ngano ya Mzingile hueleweka vizuri zaidi kuhusiana na desturi za kidini zilizohusu mungu wa Misri Osiris, ambaye wakati mmoja Wamisri waliamini alikuwa mfalme wa Misri. Osiris alikuwa mungu wa wafu, au mungu wa waovu.
Mithiolojia na Hali ya Kutokufa
Kifo cha Osiris kiliigizwa upya katika Mystery Drama ya Wamisri ambayo hufanywa kila mwaka. Apis, fahali mtakatifu, alichinjwa katika sherehe badala ya Osiris huku kukiwa na kilio kikubwa na kutoa machozi. Kutoa machozi huko kuligeuka kuwa shangwe wakati kuhani aliyekuwa akitumikia rasmi alipowatangazia watu habari za kufurahisha za ufufuo wa Osiris. Matukio hayo ya kimafumbo, yalikuwa jambo kuu kwa Wamisri linalohusu tumaini lao la uhai. Waliamini kwamba kila mtu, wala si mfalme peke yake, alifanana na Osiris alipokufa.
Kitabu The Labyrinth, kilichohaririwa na Profesa S. H. Hooke, kilisema: “Katika Misri ngano ya mapema ya Osiris hudokeza kuwepo kwa kani kadhaa zilizotishia uhai wa mungu-mfalme, akiwa duniani na kwenye maisha ya baadaye.” Hivyo, iliaminiwa kuwa Mzingile wenye mfumo wa njia zenye kutatanisha ulimlinda mungu-mfalme dhidi ya maadui wake katika maisha ya sasa na yale yajayo—hata kutokana na kifo chenyewe.
Halafu, itikadi ya hali ya kutokufa ya binadamu ikaimarika sana katika Misri ya kale na katika ulimwengu wote wa kale. Kwa kweli, fundisho la hali ya kutokufa kwa nafsi ya binadamu lililositawi katika karne zilizofuata punde si punde lilikubaliwa si na wafalme peke yao bali pia na wanadamu wote.
Mzingile wa Krete
Yaelekea mzingile ulioko Knossos, kwenye kisiwa cha Krete, ulijengwa miaka kadhaa baada ya ule wa Misri. Ijapokuwa mahali hapo hapajatambuliwa hasa, rekodi zaonyeshwa kwamba ulifanana na, lakini ni mdogo zaidi ya kiolezo cha Wamisri.a Neno la Kiingereza “labyrinth” labda lahusiana na neno laʹbrys, shoka lenye vichwa viwili vinavyowakilisha pembe mbili za fahali mtakatifu. Fahali huyo alikuwa mashuhuri katika ibada huko Minoa (ya Krete), iliyoathiriwa sana na mithiolojia.
Mzingile wa Krete ulikuwa mashuhuri katika mithiolojia kwa sababu ya mkazi wake aliyeitwa Zimwi la Minos—mtu anayesimuliwa katika ngano mwenye kichwa cha fahali. Pasiphaë, mke wa Minos, mfalme wa Krete, kulingana na hekaya, alikuwa amezaa kiumbe hicho—hivyo kikapewa jina, Zimwi la Minos, linalomaanisha “Fahali wa Minos.” Kulingana na ngano hiyo, jiji la Athene lilishindwa vita na Krete, na watu wake walilazimishwa kutoa vijana 14 kila baada ya miaka tisa—wavulana 7 na wasichana 7—kuwa dhabihu kwa Zimwi la Minos. Vijana hao waliingizwa kwenye mzingile, ambapo walipotea kisha wakadhaniwa kuwa walinyafuliwa na Zimwi la Minos.
Hata hivyo, baada ya muda, kijana mmoja, Theseus, alikubali mgawo huo na kuingia kwenye mzingile ili kuua dubwana hilo linalosimuliwa kwenye ngano. Inasemekana kwamba alipokutana nalo, Theseus aliliua Zimwi la Minos hilo kwa upanga wake. Ili kuponyoka, alirudi nyuma kwa kufuata uzi wa dhahabu, aliokuwa ameuweka chini kutoka kwenye mwingilio wa mzingile. Alikuwa amepewa uzi huo na Ariadne, binti ya Mfalme Minos.
Michael Ayrton, aliyejenga muundo wa kukisia wa mzingile wa Wakrete, alieleza hivi: “Maisha ya kila mtu ni jambo lenye kutatanisha ambapo mwishowe hufikia kifo, hata baada ya kifo yawezekana kwamba hupita mzingile wa mwisho kabla ya kukoma kuwapo.” Katika maana hiyo, Theseus anayesimuliwa katika ngano alipoponyoka kutoka kwenye mzingile huo ulikuwa ufananisho wa kuzaliwa tena, alikwepa kifo. Tena, fundisho la hali ya kutokufa ya binadamu ni dhahiri.
Ugiriki na Roma
Kiolezo cha mzingile bora wa Wakrete huonekana kwenye sarafu zilizopatikana Knossos. Punde si punde kiolezo hicho kiliigwa na milki za Wagiriki na Waroma. Pliny ataja mzingile kwenye kisiwa cha Mediterania cha Samos na mwingine, uliokuwa maarufu kwa umaridadi wake wa nguzo 150, kwenye kisiwa cha Lemnos. Pia arejezea ziara lililopangwa kwa uangalifu la Waetruska ambalo habari zake ziliandikwa mapema na mwandishi, Varro, linalosemekana kuwa lilikuwa na mzingile wa chini ya ardhi.
Jiji la Pompeii, lililoharibiwa na mlipuko wa Mlima Vesuvius mwaka wa 79 W.K., lilikuwa na angalau mizingile miwili iliyorembwa. Mojawapo kati yake, Nyumba ya Mzingile, inajulikana sana kwa sababu ya usanii wake wa mozeiki usio wa kawaida unaoonyesha pambano kati ya Theseus na Zimwi la Minos. Mwandishi Marcel Brion asisitiza kwamba hii ni “istiari ya uhai wa kibinadamu na ya safari ngumu ambazo lazima nafsi ifunge katika ulimwengu huu na ule ujao kabla ya kufikia hali yenye baraka ya kutokufa.”
Katika Roma ya kale watoto walicheza kwenye vigezo vya mzingile vilivyopangwa viwanjani na njiani. Leo kotekote katika Ulaya kuna mabaki mengi sana ya vigezo vya sakafu vilivyojengwa kwa usanii wa mozeiki kwenye nyumba za mashamba zilizochimbuliwa na majengo mengine ya raia Waroma. Lakini mawazo ya mithiolojia yalizidi kuenea hata yakafika ng’ambo.
Hadi Kwenye Nchi Nyingi
Hekalu la Halebid, huko Mysore, India, lina sehemu yenye ukanda wa nakshi unaotia ndani mzingile. Hekalu hilo lililojengwa mnamo karne ya 13 W.K., huonyesha kisa kilicho katika kichapo cha Mahabharata.
Wachina waliamini kwamba roho waovu wangeweza kupuruka tu kwa mstari ulionyooka, kwa hiyo walijenga miingilio ya mzingile sahili ili kuzuia roho waovu wasiingie katika nyumba zao na miji yao.
Katika Skandinavia, kuna mizingile ya mawe zaidi ya 600 kwenye kingo za Bahari ya Baltiki. Inasemekana kwamba mizingile mingi ilijengwa na wavuvi wenyeji waliotembea katikati yake kwa kufuata ushirikina ili kuhakikisha kwamba watavua samaki wengi na kurudi wakiwa salama.
Huko St. Agnes, kisiwa kidogo kutoka pwani ya kusini-magharibi ya Cornwall, Uingereza, kuna mzingile uliojengwa upya mwaka wa 1726 na mlinzi wa mnara wa taa aliyekuwa kwenye sehemu iliyokuwa na kiolezo cha mapema.
Jambo linalopendeza watu wengi ni kwamba mzingile huo umeshirikishwa na makanisa ya Jumuiya ya Wakristo. Fikiria mifano michache.
Mizingile ya Jumuiya ya Wakristo
Kati ya mizingile mingi yenye kutokeza katika majengo ya Jumuiya ya Wakristo, ulio mdogo zaidi ni ule wa karne ya 15 wenye umbo la duara uliotengenezwa kwa mbao na kutiwa nakshi, ulio kwenye paa ya St. Mary Redcliffe, kanisa lililoko Bristol, Uingereza. Limepakwa rangi ya dhahabu na nyeusi, na lina kipenyo cha sentimeta 20 tu. Mzingile mashuhuri zaidi unapatikana kwenye Kanisa Kuu la Chartres la Ufaransa. Ulijengwa mnamo mwaka wa 1235, kwa mawe ya rangi ya buluu na nyeupe, una kipenyo cha meta 10.
Mizingile mikubwa ya sakafuni iliwekwa katika makanisa makuu mengine ya enzi za kati katika Ufaransa na Italia, kutia ndani yale yaliyoko Amiens, Bayeux, Orléans, Ravenna, na Toulouse. Ule mzingile ulioko Reims uliharibiwa miaka 200 iliyopita, na mzingile wa Kanisa Kuu la Mirepoix una Mchoro ulio katikati.
Kichapo kimoja chaandika hivi kuhusu kuwepo kwa mizingile kwenye majengo yenye kutokeza ya kidini: “Mzingile wa wapagani ulianza kutumiwa na kanisa la Kikristo la enzi za kati na kubadilishwa ufae matumizi yake yenyewe kwa kutia ndani ufananisho wa Kikristo katika ubuni huo.” Hivyo, yaelekea mizingile ilitumiwa katika makanisa ya Jumuiya ya Wakristo ili kuwakilisha maisha ya Mkristo, kulingana na mithiolojia iliyoanzishwa na Wamisri wa kale.
Mizingile ya kanisa ilitumiwa pia kuonyesha kwa matendo safari zilizofungwa na washiriki wa vita takatifu kuelekea Yerusalemu. Kufika katikati kulifananisha kufika Yerusalemu na kupata wokovu. Kwa waabudu fulani mzingile ulikuwa njia ya majuto ambayo ingekamilishwa kwa kutembea kwa magoti ili kupata msamaha wa dhambi au kwa kuitembea kupatana na desturi, jambo ambalo lingechukua mahali pa kwenda hija kwenye Bara Takatifu.
Mizingile ya Majani na Udongo
Mizingile iliyochimbwa udongoni, iliyoitwa mizingile ya majani na udongo, ilijengwa katika karne ya 12 na 13, hasa katika Uingereza. Baadaye yaelekea mingine ilitumiwa kwa ajili ya tafrija, lakini kwa kuwa ilifanana na mizingile iliyo katika majengo ya kanisa, watu fulani waliiona kuwa ina maana fulani ya kidini. Mzingile wa pande la majani na udongo ulio mkubwa zaidi ulimwenguni, ambao watu fulani wanaufikiria kuwa umedumu kwa miaka zaidi ya 800, uko katika ardhi ya umma huko Saffron Walden, kwenye jimbo la Essex. Si wa kawaida kwa njia ya kwamba una ngome kubwa nne zilizojitokeza, ambazo zimeinuliwa. Urefu wa njia yake ni takriban kilometa mbili.
W. H. Matthews ahusisha upande wa historia na mithiolojia, akisema kwamba mizingile ya kidini “yaweza kuonwa kuwa ishara ya kishawishi chenye kutatanisha cha maisha ya sasa, kinachoweza kuvukwa tu kwa fadhili ya kimungu, unaofananishwa na uzi aliopewa Theseus na Ariadne.”—Mazes and Labyrinths—Their History and Development.
Je, unashangaa kwamba ijapokuwa mizingile ina chanzo cha kipagani, inashirikishwa na Jumuiya ya Wakristo? Je, Ukristo wa kweli unaweza kupatana na ushirikina wa kipagani?
Je, Inapatana na Imani ya Kikristo?
Hata ingawa historia ya mizingile ni yenye kuvutia sana, itikadi zinazohusiana nayo hazipatani na imani ya Kikristo. Hakuna mahali popote ambapo Biblia hufundisha kwamba nafsi ya binadamu imetenganishwa na mwili na kwamba inaendelea kuishi mtu anapokufa. Badala yake, Biblia hufundisha kwamba nafsi ya binadamu yaweza kufa. Inasema: “Nafsi inayofanya zambi, itakufa.”—Ezekieli 18:4, Zaire Swahili Bible.
Neno la Mungu, Biblia lina nguvu na limelinganishwa na upanga, “upanga wa roho.” Wakristo hutumia silaha hiyo kwa ustadi ili kushinda kiumbe wa roho aliye halisi, mwenye nguvu zipitazo za binadamu, asiyeonekana pamoja na roho waovu wake, si Zimwi linalosimuliwa katika ngano. (Waefeso 6:12, 17) Tokeo ni kwamba, wana imani isiyoshindwa na tumaini hakika la wokovu. Imani hiyo itawasaidia wapite mwisho wa mfumo huu wa mambo hadi kwenye ulimwengu mpya wenye uadilifu—jambo ambalo itikadi katika mithiolojia haziwezi kufanya kamwe.—2 Petro 3:13.
[Maelezo ya Chini]
a Katika karne ya kwanza W.K., Pliny, mtaalamu Mroma wa mambo ya asili, alisema kwamba Wakrete walijenga mzingile wao wenye ukubwa wa sehemu moja kwa mia ya ule wa Misri.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Mizingile ya Kujifurahisha
Mzingile wa aina mpya ulibuniwa miaka mia sita iliyopita. Haukuwa na maana yoyote ya kidini bali ulibuniwa kwa ajili ya madoido. Katika Uingereza kote punde si punde mizingile sahili ya shambani ikawa jambo la kawaida. Hatimaye, mizingile hiyo ilibuniwa ikiwa na njia zenye kutatanisha zaidi, na upande wa ndani wa njia zake uliwekwa mmea unaotokeza mbao ngumu, ambao ungeweza kupunguzwa ukubwa kwa njia nadhifu.
Katika miaka ya karibuni mizingile mingi ya kisasa yenye ubuni wa kutatanisha imetokea ulimwenguni pote. Inapendwa na watoto na watu wazima pia. Inaweza kufurahisha!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
Matumizi ya Jumuiya ya Wakristo ya Mzingile
Hivi karibuni Makao ya Watawa yaliyoko Westminster, London, yalitokeza kitambaa kipya cha madhabahu kilichotiwa nakshi. Ona mzingile ulio katikati unaozungukwa na herufi “Α” (alpha, “MWANZO”) na “Ω” (omega, “MWISHO”). Katikati ya ubuni wa mzingile huu, ona “MIMI NIKO,” linalowakilisha Yehova, “MIMI NIKO” mkuu anayerejezewa kwenye Kutoka 3:14, King James Version. Huo ni mfano wa kisasa wenye kuvutia unaoonyesha uhusiano wa karibu kati ya mzingile na dini leo.
[Hisani]
Picha: David Johnson
[Picha katika ukurasa wa 21]
Sarafu za karne ya nne na ya tano K.W.K. zilizopatikana huko Knossos, Krete. Ona kiolezo cha mzingile na kichwa cha fahali, kinachowakilisha Zimwi la Minos
[Hisani]
Copyright British Museum
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mzingile wa majani na udongo ulio mkubwa zaidi ulimwenguni, huko Saffron Walden, Uingereza
[Hisani]
Courtesy Saffron Walden Tourist Office