Sura 3
Nyuzi Zile Zile Katika Ngano
1-3 (a) Kwa nini tupendezwe na ngano? (b) Tutazungumzia nini katika sura hii?
KWA nini tuchunguze ngano? Je! hizo si ubuni wa wakati mrefu uliopita tu? Ingawa ni kweli kwamba nyingi zazo hutegemea ubuni, nyingine zategemea jambo la hakika. Kielelezo ni ngano na hekaya zinazopatikana ulimwenguni pote ambazo hutegemea uhakika wa Gharika ya ulimwengu, au Furiko, ambalo Biblia husimulia.
2 Sababu moja ya kuchunguza ngano ni kwamba ndizo msingi wa imani na desturi ambazo zingali zapatikana katika dini leo. Kwa kielelezo, imani katika nafsi isiyoweza kufa yaweza kufuatishwa mpaka kwenye ngano za Waashuri-Wababuloni wa kale kupitia ngano za Kimisri, Kigiriki, na Kiroma mpaka kwenye Jumuiya ya Wakristo, ambako zimekuwa itikadi iliyo na msingi katika theolojia yake. Ngano ni uthibitisho wa kwamba mtu wa kale alifanya jitihada ya kutafuta vijimungu, na pia maana ya uzima. Katika sura hii tutazungumza kifupi baadhi ya habari za kawaida zinazotokana na ngano za tamaduni kubwa-kubwa za ulimwengu. Tupitiapo ngano hizo, tutaona jinsi uumbaji, Furiko, vijimungu vya bandia na vijimungu-nusu, nafsi isiyoweza kufa, na ibada ya jua zinavyojitokeza kwa ukawaida kuwa nyuzi zile zile katika visehemu-sehemu vya ngano. Lakini kwa nini iwe hivyo?
3 Pindi nyingi sana kuna kiini cha uhakika wa kihistoria, mtu fulani, au tukio fulani ambalo baadaye limetiwa chumvi au likapotolewa ili kufanya iwe ngano hiyo. Moja la mambo hakika hayo ya kihistoria ni maandishi ya Biblia ya uumbaji.a
Uhakika na Hadithi ya Kubuni Juu ya Uumbaji
4, 5. Ni zipi zilizokuwa baadhi ya itikadi za ngano za Kigiriki?
4 Ngano juu ya uumbaji ni tele, lakini hakuna yoyote inayoeleza kwa njia rahisi ya kiakili kama maandishi ya Biblia juu ya uumbaji. (Mwanzo, sura 1, 2) Kwa kielelezo, simulizi litolewalo katika ngano za Kigiriki lasikika kuwa la kishenzi. Mgiriki wa kwanza kuandika ngano katika njia ya utaratibu alikuwa Hesiod, aliyeandika Theogony chake katika karne ya nane K.W.K. Yeye afafanua jinsi vijimungu na ulimwengu vilivyoanza. Aanza na Gaea, au Gaia (Dunia), anayemzaa Zohari (Mbingu). Mambo yanayofuatwa yamefafanuliwa na msomi Jasper Griffin katika The Oxford History of the Classical World:
5 “Hesiod asimulia hadithi, inayojulikana na Homer, juu ya mfuatano wa vijimungu vya anga. Kwanza Zohari ndiye mkuu zaidi, lakini alikandamiza watoto wake, na Gaia alimtia moyo mwana wake Kronosi amhasi. Kronosi naye akawala watoto wake mwenyewe, mpaka Rhea mke wake akampa jiwe ale badala ya Zeu; mtoto Zeu alilelewa Krete, akamlazimisha baba yake atapike ndugu zake, akiwa pamoja nao na msaada mwingine wakamshinda Kronosi na Matitani wake na kuwatupa chini ndani ya Tartaro.”
6. Kulingana na Jasper Griffin, ni nini kinachoelekea kuwa ndicho chanzo cha ngano nyingi za Kigiriki?
6 Wagiriki walipata kutoka chanzo gani ngano hizi za kiajabu? Mtungaji uyo huyo ajibu: “Asili yazo ya kwanza yaelekea kuwa ilikuwa ya Kisumeri. Katika hadithi hizi za mashariki twaona mfufulizo wa vijimungu, na taswira za kuhasiwa, za kumeza, na za jiwe moja likirudi katika njia ambazo, ijapokuwa zenye kutofautiana, zaonyesha kwamba ufanani na Hesiod si sadifu tu.” Tunalazimika kuangalia Mesopotamia na Babuloni za kale kuwa ndizo chanzo cha ngano nyingi zilizoenea katika tamaduni nyinginezo.
7. (a) Kwa nini si rahisi kupata habari juu ya ngano za kale za Uchina? (b) Ngano moja ya Kichina yafafanuaje uumbaji wa dunia na binadamu? (Linganisha Mwanzo 1:27; 2:7.)
7 Ngano za kale za dini ya wenyeji Wachina si rahisi nyakati zote kufafanua, kwani maandishi mengi ya kale yaliharibiwa katika kipindi cha 213-191 K.W.K.b Hata hivyo, ngano fulani zimesalia, kama ile inayosimulia jinsi dunia ilivyofanyizwa. Profesa mmoja wa sanaa ya Mashariki, Anthony Christie, aandika hivi: “Twajifunza Kaosi alikuwa kama yai la kuku. Wala Mbingu wala Dunia havikuwapo. Kutoka kwa yai P’an-ku akazaliwa, kutoka kwa elementi zalo nzito Dunia ikafanyizwa na Anga kutoka kwa elementi nyepesi. P’an-ku huwakilishwa na mbilikimo, aliyevaa ngozi ya dubu au shela ya majani. Kwa miaka 18,000 umbali kati ya Dunia na Anga uliongezeka kila siku kwa futi 10, na P’an-ku akakua kwa kimo icho hicho hivi kwamba mwili wake ukajaza pengo hilo. Alipokufa, sehemu tofauti-tofauti za mwili wake zikawa elementi mbalimbali za asili. . . . Viroboto vya mwili wake vikawa ndiyo jamii ya kibinadamu.”
8. Kulingana na ngano za Wainka, lugha zilitokeaje?
8 Kutoka Amerika ya Kusini hekaya ya Inka yafafanua jinsi muumba anayesimuliwa katika ngano alivyolipa kila taifa usemi. “Yeye alilipa kila taifa lugha ambayo lingeisema . . . Yeye alimpa kila mmoja mwili na pia wanaume na wanawake hali ya kuwapo na nafsi, akaliamuru kila taifa lizame chini ya dunia. Basi kila taifa likapita chini ya ardhi na likatokea katika sehemu ambazo yeye aliligawia.” (The Fables and Rites of the Yncas, cha Cristóbal de Molina wa Cuzco, kilichonukuliwa katika South American Mythology) Katika kisa hiki yaonekana kwamba simulizi la Biblia la kuvurugwa kwa lugha kule Babeli ndilo kiini cha uhakika wa ngano hii ya Inka. (Mwanzo 11:1-9) Lakini sasa acheni tugeuze uangalifu kwenye Gharika inayosimuliwa katika Biblia kwenye Mwanzo 7:17-24.
Furiko—Jambo la Hakika au Ngano?
9. (a) Biblia yatuambia nini juu ya hali duniani kabla ya Furiko? (b) Nuhu na familia yake walipaswa kufanya nini ili waokolewe kutoka Furiko hilo?
9 Ikiturudisha nyuma miaka ipatayo 4,500 iliyopita, karibu na 2,500 K.W.K., Biblia hutuambia kwamba wana wa roho wa Mungu walioasi walitwaa miili ya kibinadamu “wakajitwalia wake wo wote waliojichagulia.” Uzazi-mchanganyiko huu usio wa asili ulitokeza Wanefili wenye kufanya jeuri, “waliokuwa watu hodari wa zamani.” Mwenendo wao wa kuhalifu sheria uliathiri ulimwengu wa kabla ya Furiko kufikia hatua ya kwamba Yehova akasema: “Nitamfutilia mbali binadamu niliyemwumba usoni pa nchi . . . kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA [Yehova].” Halafu simulizi hilo laendelea kusema juu ya hatua kamili na zenye vitendo ambazo Nuhu alipaswa kuchukua ili ajiokoe mwenyewe na Furiko hilo, na pia familia yake na aina mbalimbali za wanyama.—Mwanzo 6:1-8, 13–8:22; 1 Petro 3:19, 20; 2 Petro 2:4; Yuda 6.
10. Kwa nini simulizi la Biblia juu ya Furiko halipasi kuonwa kuwa ngano?
10 Wahakiki wa ki-siku-hizi husema maandishi ya matukio ya kabla ya Gharika yanayosimuliwa katika Mwanzo ni ngano. Hata hivyo, historia ya Nuhu ilipokewa na kuaminiwa na wanaume waaminifu, kama vile Isaya, Ezekieli, Yesu Kristo, na mitume Petro na Paulo. Pia inaungwa mkono na uhakika wa kwamba inawakilishwa katika ngano nyingi mno ulimwenguni pote, kutia Utenzi wa Gilgameshi wa kale na pia ngano za China na za Waazteki, Wainka, na Wamaya. Tukiwa tunazingatia akilini maandishi ya Biblia, acheni sasa tufikirie ngano za Waashuri-Wababuloni na marejezo yazo kwenye furiko fulani.c—Isaya 54:9; Ezekieli 14:20; Mathayo 24:37; Waebrania 11:7.
Furiko na Gilgameshi Binadamu-Kijimungu
11. Maarifa yetu juu ya Utenzi wa Gilgameshi yategemea nini?
11 Tukirudi nyuma katika historia miaka zaidi ya 3,000, twakuta ngano ya Kiakadia iliyo maarufu sana iitwayo Utenzi wa Gilgameshi. Maarifa yetu juu ya hilo yategemea hasa maandishi-awali ya maandishi-kabari yaliyotoka kwenye maktaba ya Ashurbanipali, aliyetawala katika Ninawi la kale.
12. Gilgameshi alikuwa nani, na kwa nini yeye hakupendwa na wengi? (Linganisha Mwanzo 6:1, 2.)
12 Hiyo ni hadithi ya matendo hodari ya Gilgameshi, anayesimuliwa kuwa theluthi mbili kijimungu na theluthi moja binadamu, binadamu-kijimungu. Aina moja ya utenzi huo yaeleza hivi: “Katika Uruki alijenga kuta, boma kubwa, na hekalu la mbarikiwa Eanna kwa ajili ya kijimungu Anu cha anga, na kwa ajili ya Ishtari kijimungu-kike cha upendo . . . , bibi yetu wa upendo na vita.” (Ona kisanduku, ukurasa 45, kwa ajili ya orodhesho la vijimungu na vijimungu-vike vya Waashuri-Wababuloni.) Hata hivyo, Gilgameshi hakuwa hasa kiumbe mzuri kukaribiwa. Wakaaji wa Uruki walilalamikia vijimungu hivi: “Ashiki yake haiachii bikira mpenzi wake, wala binti ya shujaa wala mke wa sharifu.”
13. (a) Vijimungu vilichukua hatua gani, na Gilgameshi alifanya nini? (b) Utnapishtimu alikuwa nani?
13 Vijimungu hivyo vilichukua hatua gani kwa kuitikia uteti wa watu? Kijimungu-kike Aruru kiliumba Enkidu awe mshindani binadamu wa Gilgameshi. Hata hivyo, badala ya kuwa maadui, wakawa marafiki wa karibu. Utenzi huo ulipoendelea, Enkidu akafa. Kwa majonzi mengi, Gilgameshi alilia hivi: “Nifapo, je! sitakuwa kama Enkidu? Ole umeingia tumboni mwangu. Kwa kuhofu kifo, natanga-tanga uwandani.” Yeye alitaka siri ya kutokufa basi akafunga safari akamtafute Utnapishtimu, mwokokaji wa gharika aliyekuwa amekabidhiwa na vijimungu hali ya kutoweza kufa.
14. (a) Utnapishtimu aliambiwa afanye nini? (Linganisha Mwanzo 6:13-16.) (b) Safari ya Gilgameshi inayotajwa na utenzi ikawaje?
14 Hatimaye Gilgameshi ampata Utnapishtimu, ambaye amsimulia hadithi ya furiko. Kama inavyoonekana katika bamba la Utenzi wa 11, liitwalo Bamba la Furiko, Utnapishtimu amsimulia maagizo aliyopewa kuhusu furiko: “Bomoa nyumba (hii), jenga merikebu! Acha mali, tafuta uhai. . . . Ndani ya merikebu ingiza mbegu yako ya vitu vyote vilivyo hai.” Je! hili halisikiki kidogo kufanana na mrejezo wa Biblia kuhusu Nuhu na Furiko? Lakini Utnapishtimu hawezi kumtuza Gilgameshi hali ya kutoweza kufa. Gilgameshi, akiwa amekata tamaa, arudi nyumbani Uruki. Simulizi lamalizika kwa kifo chake. Jumla ya ujumbe wa utenzi huo ni huzuni na fadhaa ya kifo na maisha ya baadaye. Watu hao wa kale hawakumpata Mungu wa ukweli na tumaini. Hata hivyo, kiunganishi cha utenzi huo na simulizi rahisi la Biblia la muhula kabla ya Furiko ni wazi kabisa. Sasa na tugeukie simulizi la Furiko kama linavyoelezwa na hekaya nyingine.
Hekaya ya Furiko katika Tamaduni Nyingine
15. Kwa nini tupendezwe na hekaya ya Kisumeri juu ya furiko?
15 Hata mapema zaidi ya Utenzi wa Kale wa Gilgameshi ni ngano ya Kisumeri inayotaja “Ziusudra, kifani cha Nuhu wa kibiblia, ambaye anaelezwa kuwa mfalme mwogopa-mungu, mwenye kuhofu kijimungu, daima akitafuta-tafuta ufunuo wa kimungu katika ndoto au tabano.” (Ancient Near Eastern Texts Relating to the Old Testament) Kulingana na chanzo icho hicho, ngano hii “yatoa ulinganifu wa karibu zaidi na wenye kutokeza zaidi kwa habari ya kibiblia isiyopata kuchimbuliwa bado katika fasihi ya Kisumeri.” Staarabu za Wababuloni na Waashuri, zilizofuata baadaye, ziliathiriwa na ule wa Kisumeri.
16. Hekaya za Kichina juu ya furiko zingaliweza kuwa zilitokana na chanzo gani?
16 Kitabu China—A History in Art chatuambia kwamba mmoja wa watawala wa kale wa China alikuwa Yü, “mshinda Furiko Kubwa. Yü alielekeza maji ya furiko kwa njia ya mfereji kwenye mito na bahari ili awape makao tena watu wake.” Mtaalamu wa ngano Joseph Campbell aliandika juu ya “Kipindi cha Wakubwa Kumi” cha Uchina, akisema: “Kwa enzi hii ya maana, inayofikia ukomo katika Gharika, maliki kumi walipewa mgawo katika ngano za mapema za wakati wa Chou. Kwa sababu hiyo, inaonekana kwamba huenda tunachotazama hapa ni badiliko la kimahali la mfululizo wa orodha ya kale ya mfalme wa Sumeri.” Halafu Campbell alitaja visehemu fulani kutoka hekaya hizi za Kichina zilizoelekea “kukazia ile hoja kwa ajili ya chanzo kuwa cha Kimesopotamia.” Hiyo inaturudisha nyuma kwenye chanzo kile kile kilicho kiini cha ngano nyingi. Hata hivyo, hadithi za Furiko zaonekana pia katika mabara ya Amerika, kwa kielelezi, katika Meksiko wakati wa kipindi cha Waazteki katika karne za 15 na 16 W.K.
17. Waazteki walikuwa na hekaya gani?
17 Ngano za Kiazteki zilisema juu ya enzi nne zilizotangulia, wakati wa ile ya kwanza dunia ilikaliwa na majitu. (Hicho ni kikumbusho kingine juu ya Wanefili, majitu wanaorejezewa kwenye Biblia katika Mwanzo 6:4.) Zilitia ndani hekaya ya zamani za kabla ya furiko ambayo katika hiyo “maji yaliyo juu yaungana na yale yaliyo chini, yakifuta kabisa peo za macho na kufanya kila kitu kuwa bahari isiyo na mwisho ya ulimwengu mzima.” Kijimungu chenye kuongoza mvua na maji kilikuwa Tlaloki. Hata hivyo, mvua yacho haikupatikana kwa bei nafuu bali ilitolewa “kwa kubadilishana na damu ya wahanga waliotolewa dhabihu ambao machozi yao yenye kutiririka yangekuwa kama mvua na kwa hiyo kuchochea mtiririko wa mvua.” (Mythology—An Illustrated Encyclopedia) Hekaya nyingine yaeleza kwamba muhula wa nne ulitawalwa na Chalchiuhtlicue, kijimungu-kike cha maji, ambacho ulimwengu wacho uliangamia katika furiko. Watu waliokolewa kwa kuwa samaki!
18. Ni masimulizi gani yametapakaa katika ngano za Amerika Kusini? (Linganisha Mwanzo 6:7, 8; 2 Petro 2:5.)
18 Hali moja na hiyo, Wainka walikuwa na hekaya zao juu ya Furiko. Mwandikaji Mwingereza Harold Osborne aeleza hivi: “Labda sehemu katika ngano za Amerika ya Kusini zilizoenea zaidi kotekote ni zile hadithi za gharika . . . Ngano za gharika zimeenea sana kati ya vikundi vya watu wa nyanda za juu na makabila ya nyanda za chini. Gharika kwa ujumla hukamatanishwa na uumbaji na Epifani [udhihirisho] ya kijimungu-muumba. . . Nyakati nyingine huonwa kuwa adhabu ya kimungu ikifutilia mbali aina ya kibinadamu katika kufanya tayarisho la kutokeza jamii mpya.”
19. Eleza juu ya hekaya ya Maya inayohusu furiko.
19 Vivyo hivyo, Wamaya katika Meksiko na Amerika ya Kati walikuwa na hekaya yao juu ya Furiko iliyohusisha gharika ya ulimwengu wote, au haiyococab, maana yake “maji juu ya uso wa dunia.” Askofu Mkatoliki Las Casas aliandika kwamba Wahindi Waguatemala waliiita Butic, ambalo ndilo neno linalomaanisha furiko la maji mengi na humaanisha hukumu ya mwisho, na kwa hiyo wao waamini kwamba Butic nyingine iko karibu, ambayo ni furiko na hukumu nyingine, si la maji, bali la moto.” Hekaya nyingine nyingi kuhusu furiko zipo ulimwenguni pote, lakini zile chache zilizokwisha kunukuliwa zathibitisha kiini cha hekaya hiyo, lile tukio la kihistoria linalosimuliwa katika kitabu cha Mwanzo.
Imani Iliyotapakaa Kotekote ya Nafsi Isiyoweza Kufa
20. Imani ya Kiashuri-Kibabuloni ilikuwa nini kuhusu maisha baada ya kufa?
20 Hata hivyo, si ngano zote zinazotegemea jambo la hakika au Biblia. Katika jitihada ya kumtafuta Mungu, binadamu ameshika hewa, akidanganywa na dhana ya kutokufa. Kama tutakavyoona katika kitabu hiki chote, imani ya nafsi isiyoweza kufa au unamna-namna wayo ni urithi ambao umetufikia sisi kupitia maelfu mengi ya miaka. Watu wa utamaduni wa kale wa Kiashuri-Kibabuloni waliamini uzima baada ya kifo. New Larousse Encyclopedia of Mythology chaeleza hivi: “Chini ya dunia, ng’ambo ya abiso ya Apsu [yenye kujaa maji matamu na yenye kuizunguka dunia], mlikuwa makao yenye moto ambamo watu walishuka baada ya kifo. Ilikuwa ‘Nchi ya kutobanduka’ . . . Katika sehemu hizi za giza la milele nafsi za wafu—edimmu—‘zikiwa zimevikwa, kama ndege, vazi la mabawa’ zote zimeborongwa pamoja.” Kulingana na ngano hiyo, ulimwengu huu wa chini ya ardhi ulitawalwa na kijimungu-kike Ereshkigali, “Binti-mfalme wa dunia kubwa.”
21. Kulingana na imani ya Kimisri, wafu walipatwa na nini?
21 Vivyo hivyo Wamisri walikuwa na wazo lao juu ya nafsi isiyoweza kufa. Kabla ya nafsi kuweza kufikia kituo salama, ililazimika kupimanishwa na Maat, kijimungu-kike cha ukweli na haki, kilichofananishwa na unyoya wa ukweli. Ama Anubisi, kijimungu chenye kichwa cha mbweha, au Horasi, ndege-kipanga, kilisaidia katika taratibu hiyo. Kama ikiidhinishwa na Osirisi, nafsi hiyo ingeenda kushiriki raha pamoja na vijimungu. (Ona mfano, ukurasa 50.) Kama ilivyo mara nyingi, hapa tunaona uzi ule ule wa Kibabuloni unaotoa wazo la nafsi isiyoweza kufa lenye kuongoza dini, maisha, na vitendo vya watu.
22. Wazo la Wachina kuhusu wafu lilikuwa nini, na ni nini kilichofanywa ili kuwasaidia?
22 Ngano za Kichina za kale zilihusisha imani ya kuendelea kuishi baada ya kifo na uhitaji wa kufurahisha wazazi wa kale waliokufa. Wazazi wa kale waliokufa “walidhaniwa kuwa roho zilizo hai na zenye nguvu, wote wakiwa wanahangaikia sana hali njema ya wazao wao walio hai, lakini wakiwa wanaweza kuadhibu kwa hasira kama hawapendezwi.” Wafu walipaswa kupewa kila ya msaada, kutia ndani waandamani katika kifo. Kwa hiyo, “wafalme fulani wa Shang . . . walizikwa pamoja na wahanga wa kibinadamu kuanzia mia moja mpaka mia tatu, ambao wangekuwa wahudumu wake katika ulimwengu mwingine. (Zoea hilo linahusianisha Uchina wa kale na Misri, Afrika, Japan, na sehemu nyinginezo, ambako dhabihu hizo zilitolewa.)” (Man’s Religions, cha John B. Noss) Katika visa hivyo imani ya nafsi isiyoweza kufa iliongoza kwenye kutolewa kwa wanadamu kuwa dhabihu.—Tofautisha na Mhubiri 9:5, 10; Isaya 38:18, 19.
23. (a) Katika ngano za Kigiriki, Hadesi ilikuwa nani na nini? (b) Kulingana na Biblia, Hadesi ni nini?
23 Wagiriki, wakiwa wamebuni vijimungu vingi katika ngano zao, pia walihangaikia wafu na mahali walikoelekea. Kulingana na ngano hizo, aliyepewa mamlaka ya makao hayo ya giza nene alikuwa mwana wa Kronosi aliye ndugu ya vijimungu Zeu na Poseidoni. Jina lake lilikuwa Hadesi, na makao yake yaliitwa kwa jina lake. Nafsi za wafu zilifikaje Hadesi?d
24. (a) Kulingana na ngano za Kigiriki, kulitukia nini katika ulimwengu wa chini ya ardhi? (b) Kulikuwako ufanani gani kati ya Utenzi wa Gilgameshi na ngano za Kigiriki?
24 Mwandikaji Ellen Switzer afafanua hivi: “Kulikuwako . . . viumbe vyenye kuogopesha katika ulimwengu wa chini. Alikuwako Charoni, aliyeendesha kivushio kilichosafirisha wale waliokuwa wamekufa juzi wakatoka kwenye nchi ya walio hai wakaenda kwenye ulimwengu wa chini. Charoni alitaka malipo kwa ajili ya huduma yake ya kivushio [kuvuka mto Styx], na Wagiriki mara nyingi walizika wafu wao wakiweka sarafu chini ya ulimi wao ili kuhakikisha kwamba wana nauli ya kutosha. Nafsi zilizokufa ambazo hazingeweza kulipa ziliwekwa ng’ambo nyingine ya mto isiyofaa, na katika nchi kama ya ukiwa, na wangeweza kurudi kusumbua walio hai.”e
25. Ni nani waliovutwa na kuwaza kwa Kigiriki juu ya nafsi?
25 Ngano za Kigiriki juu ya nafsi zilivuta wazo la Kiroma, na la wanafalsafa Wagiriki, kama vile Plato (yapata 427-347 K.W.K.), walikuwa na uvutano mkubwa juu ya waasi-imani Wakristo wa kwanza wenye falsafa ambao walipokea fundisho la nafsi isiyoweza kufa liingie katika fundisho lao, hata ingawa halikuwa na msingi wa Kibiblia.
26, 27. Waazteki, Wainka, na Wamaya walikuwa na maoni gani juu ya kifo?
26 Waazteki, Wainka, na Wamaya pia waliamini nafsi isiyoweza kufa. Kifo kilikuwa fumbo kwao sawa na kilivyokuwa kwa staarabu nyinginezo. Walikuwa na sherehe na imani zao za kuwasaidia wajipatanishe nacho. Ni kama mwanahistoria wa akiolojia, Victor W. von Hagen anavyoeleza katika kitabu chake The Ancient Sun Kingdoms of the Americas: “Wafu walikuwa wanaishi hasa: walikuwa wamepita tu toka hatua moja mpaka ile nyingine; walikuwa wasioonekana, wasiohisika, wasiodhurika. Wafu . . . walikuwa wamekuwa washiriki wasioonekana wa ukoo.”—Tofautisha na Waamuzi 16:30; Ezekieli 18:4, 20.
27 Chanzo icho hicho chatuambia kwamba “Mhindi [Mwinka] aliamini kutokufa; kwa kweli yeye aliamini mtu hakupata kufa kamwe, . . . maiti ilipata tu kutoka kifoni na kutwaa mavutano ya nguvu zisizoonekana.” Wamaya pia waliamini nafsi na mbingu 13 na helo 9 (mahali pa moto wa mateso). Kwa hiyo, kokote tunakogeukia, watu wametaka kukanusha uhalisi wa kifo, na nafsi isiyoweza kufa imekuwa kiegemeo chao.—Isaya 38:18; Matendo 3:23.
28. Ni baadhi ya imani zipi ambazo zimetapakaa katika Afrika?
28 Ngano za hekaya za Afrika vilevile ni kutia ndani marejezo ya nafsi inayoendelea kuishi baada ya kifo. Waafrika wengi wanaishi kwa kuhofu sana nafsi za wafu. New Larousse Encyclopedia of Mythology chaeleza hivi: “Imani hii imefungamanishwa na nyingine—kuendelea kuishi kwa nafsi baada ya kifo. Wafanya mizungu waweza kuziomba nafsi ziimarishe nguvu zao. Nafsi za wafu mara nyingi zinahamia kwenye miili ya wanyama, au huenda zikabadilishwa umbo kuwa mimea.” Kwa sababu hiyo, Wazulu hawasubutu kuua nyoka fulani ambao wao huamini ni roho za watu wa ukoo.
29. Fafanua hekaya fulani za baadhi ya makabila ya kusini mwa Afrika. (Linganisha Mwanzo 2:15-17; 3:1-5.)
29 Wamaasai wa Afrika ya kusini-mashariki huamini muumba aitwaye ’Ng ai, ambaye huwekea kila Maasai malaika wa kumlinda. Dakika ile ya kufa, malaika huyo hutwaa nafsi ya shujaa huyo mpaka kwenye maisha yanayofuata. Larousse kilichonukuliwa chatoa hekaya ya Wazulu juu ya kifo inayohusu mtu wa kwanza, Unkulunkulu, ambaye kwa ngano hii alikuwa amekuwa ndiye mkuu zaidi. Yeye alituma kinyonga akaambie ainabinadamu, “Watu hawatakufa!” Kinyonga huyo alikwenda polepole na akakengeushwa njiani. Kwa hiyo Unkulunkulu akapeleka ujumbe tofauti kupitia mjusi, akisema “Watu watakufa!” Mjusi huyo akafika kwanza, “na tangu wakati huo hakuna binadamu ambaye ameponyoka kifo.” Ikiwa yenye unamna-namna, hekaya ii hii inapatikana kati ya makabila ya Wabechuana, Wabasuto, na Wabaronga.
30. Katika kitabu hiki tutaona nini zaidi juu ya nafsi?
30 Tufuatiapo uchunguzi juu ya jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu, tutaona hata zaidi jinsi ngano inayohusu nafsi isiyoweza kufa imekuwa na ingali yenye maana kwa ainabinadamu.
Ibada ya Jua na Dhabihu za Kutoa Wanadamu
31. (a) Wamisri waliamini nini juu ya kijimungu-jua Ra? (b) Hayo yatofautianaje na yale ambayo Biblia husema? (Zaburi 19:4-6)
31 Ngano za Misri zinahusisha jamii pana ya vijimungu na vijimungu-vike. Kama ilivyo katika jumuiya nyingi za kale, Wamisri walipokuwa wakifanya jitihada ya kutafuta Mungu, walivutwa kuelekea kuabudu kile ambacho kilitegemeza maisha yao ya kila siku—jua. Kwa hiyo, chini ya jina Ra (Amon-Ra), wao waliheshimu sana bwana mwenye enzi kuu ya anga, aliyepanda mashua kila siku akienda kutoka mashariki mpaka magharibi. Usiku ulipoingia, alifuata njia yenye hatari katika ulimwengu wa chini.
32. Eleza juu ya mojapo sikukuu za kusherehekea kijimungu-moto Xiuhtecutli (Huehueteotl).
32 Dhabihu za kutoa wanadamu zilikuwa sehemu ya watu wote katika dini ya kuabudu jua ya Waazteki, Wainka, na Wamaya. Waazteki walisherehekea mrudio wenye kudumu wa sikukuu za kidini, wakitoa wanadamu dhabihu kwa vijimungu vyao mbalimbali, hasa katika kuabudu kijimungu-jua Tezcatlipoca. Pia katika sikukuu ya kijimungu-moto Xiuhtecutli (Huehueteotl), “wafungwa wa vita walicheza ngoma pamoja na waliowateka na . . . walizungushwa-zungushwa kwenye moto wenye kung’ara na kisha wakatupwa ndani ya makaa, na kuondolewa wakiwa wangali hai ili mioyo yenye kupwitapwita bado iondolewe kwa kukatwa itolewe kwa vijimungu.”—The Ancient Sun Kingdoms of the Americas.
33. (a) Ibada ya Wainka ilihusisha nini? (b) Biblia yasema nini juu ya dhabihu za kutoa wanadamu? (Linganisha 2 Wafalme 23:5, 11; Yeremia 32:35; Ezekieli 8:16.)
33 Kusini zaidi, dini ya Wainka ilikuwa na dhabihu zayo na ngano. Katika ibada ya kale ya Wainka, watoto na wanyama walitolewa kwa kijimungu-jua na kwa Viracocha, aliye muumba.
Vijimungu na Vijimungu-vike Visimuliwavyo Katika Ngano
34. Ni nani waliokuwa sehemu ya utatu-utatu wa vijimungu maarufu zaidi vya Kimisri, nao walitimiza majukumu gani?
34 Ulio maarufu zaidi kati ya utatu-utatu wa vijimungu vya Kimisri ni ule ulio sehemu ya Isisi, alama ya umama wa kimungu; Osirisi, nduguye na mwandamizi wake; na Horasi, mwana wao, ambaye kwa kawaida huwakilishwa na ndege-kipanga. Isisi huonyeshwa nyakati nyingine katika sanamu za Kimisri akimpa mtoto wake titi lake kwa namna inayofanana sana na sanamu na taswira za Jumuiya ya Wakristo za bikira na mwana, zilizotokea baadaye miaka zaidi ya elfu mbili. Baada ya wakati kupita, Osirisi, mume wake Isisi, alipata umaarufu kuwa kijimungu cha wafu kwa sababu kilizitolea tumaini la uzima wa milele wenye furaha nafsi za wafu katika maisha ya baadaye.
35. Hathori alikuwa nani, na sherehe yake kuu ya kila mwaka ilikuwa ipi?
35 Hathori Mmisri alikuwa kijimungu-kike cha upendo na shangwe, muziki na dansi. Akaja kuwa malkia wa wafu, akiwasaidia kwa ngazi wafike mbinguni. Kama kifafanuavyo New Larousse Encyclopedia of Mythology, yeye alisherehekewa kwa miadhimisho iliyo mikubwa, “zaidi ya yote mnamo Siku ya Mwaka Mpya, iliyokuwa mwadhimisho wa kuzaliwa kwake. Kabla ya kupambazuka kuhani-mke alikuwa akileta mfano wa Hathori nje kwenye ua ili upigwe na miale ya jua lenye kuchomoza. Kushangilia kulikofuata kulikuwa kisingizio cha kufanya sherehe halisi, na hiyo siku ilimalizikia katika kuimba na kulewa.” Je! kumekuwako mabadiliko makubwa katika misherehekeo ya Mwaka Mpya maelfu ya miaka baadaye?
36. (a) Israeli ilikuwa katika hali gani ya kidini katika karne ya 16 K.W.K.? (b) Yale Mapigo Kumi yalikuwa na umaana gani maalumu?
36 Pia Wamisri walikuwa na vijimungu na vijimungu-vike vingi vilivyo wanyama katika vikundi vyao vya vijimungu, kama vile Apisi fahali, Banadedi kondoo-ndume, Hekti chura, Hathori ng’ombe, na Sebeki mamba. (Warumi 1:21-23) Waisraeli walijikuta katika hali hii ya kidini wakiwa watumwa waliotekwa katika karne ya 16 K.W.K. Ili kuwaweka huru na kizuizi cha Farao mwenye kichwa kigumu, Yehova, Mungu wa Israeli, alipeleka mapigo kumi tofauti-tofauti juu ya Misri. (Kutoka 7:14–12:36) Matokeo yaliyokusudiwa kwa mapigo hayo yalikuwa ni kuvunjia heshima vijimungu vya Misri vinavyosimuliwa katika ngano.—Ona kisanduku, ukurasa 62.
37. (a) Baadhi ya vijimungu vya Waroma vilikuwa na sifa za aina gani? (b) Mwenendo wa vijimungu hivyo uliathirije wafuasi wavyo? (c) Paulo na Barnaba walipatwa na nini katika Listra?
37 Sasa na tusonge kwenye vijimungu vya Ugiriki na Roma za kale. Roma ilikopa vijimungu vingi kutoka Ugiriki ya kale, pamoja na mema na maovu yavyo. (Ona visanduku, kurasa 43 na 66.) Kwa kielelezo, Zuhura na Flora walikuwa malaya wasio na haya; Bakasi alikuwa mlevi na mla karamu za ulevi na ulafi; Zebaki alikuwa mnyang’anyi wa barabarani; na Apolo alikuwa mtongoza wanawake. Yaripotiwa kwamba Sumbula, baba ya vijimungu, alifanya uzinzi au ngono za kiukoo na wanawake wapata 59! (Jinsi inavyokumbusha juu ya malaika waasi walioishi kiunyumba pamoja na wanawake kabla ya Furiko!) Kwa kuwa waabudu huelekea kuonyesha mwenendo wa vijimungu vyao, je! inashangaza kwamba wamaliki Waroma kama vile Tiberio, Nero, na Kaligula waliishi maisha mapujufu wakiwa wazinzi, waasherati, na wauaji wa kukusudia?
38. (a) Eleza juu ya aina ya ibada iliyozoewa katika Roma. (b) Dini iliathirije askari-jeshi Mroma?
38 Waroma walichanganya katika dini yao vijimungu kutoka mila nyingi. Kwa kielelezo, walipokea kwa shauku ibada ya Mithrasi, kijimungu cha nuru cha Kiajemi, kilichokuja kuwa kijimungu-jua chao (ona kisanduku, kurasa 60-1), na kijimungu-kike cha Kishami, Atargatis (Ishtari). Waligeuza Artemi cha Ugiriki kilichokuwa mwindaji wa kike kikawa Diana na walikuwa na unamna-namna wao wa Isisi cha Kimisri. Pia walikopa vijimungu-vike vitatu vya Kiselti vya uzaaji.—Matendo 19:23-28.
39. (a) Ni nani aliyetawala ukuhani wa Kiroma? (b) Eleza juu ya mojawapo sherehe za kidini za Kiroma.
39 Kwa ajili ya zoea lao la viibada vya umma kwenye mamia ya vihekalu na mahekalu, walikuwa na unamna-namna wa makuhani, wote wakiwa “chini ya mamlaka ya Pontifex Maximus [Askofu Mkuu], ambaye alikuwa kiongozi wa dini ya serikali.” (Atlas of the Roman World) Atlasi iyo hiyo yaeleza kwamba moja ya sherehe za Kiroma ilikuwa toroboliamu, ambayo katika hiyo “mwabudu alisimama ndani ya shimo na kuogeshwa katika damu ya fahali aliyetolewa dhabihu juu yake. Aliibuka katika sherehe hii ya ibada akiwa na hali ya utakaso usio na hatia.”
Ngano na Hekaya za Kikristo?
40. Wasomi wengi wana maoni gani juu ya matukio ya Ukristo wa mapema?
40 Kulingana na wahakiki fulani wa kisasa, Ukristo pia umepokea na kufuata ngano na hekaya. Je! ndivyo ilivyo? Wasomi wengi hukataa na kusema kuzaliwa kwa Yesu na bikira, miujiza yake, na ufufuo wake ni ngano tu. Wengine hata husema hakuwako kamwe bali kwamba ngano juu yake ilipokezwa kutoka mfumo wa ngano ulio wa kale zaidi na ibada ya jua. Ni kama alivyoandika Joseph Campbell mtaalamu wa ngano: “Kwa hiyo, wasomi kadhaa wamedokeza kwamba hakuwako kamwe Yohana [Mbatizaji] wala Yesu, bali kijimungu-maji na kijimungu-jua tu.” Lakini twahitaji kukumbuka kwamba wengi wa wasomi hao ni waatheisti (hawadai dini yoyote) na kwa hiyo wanakataa katakata imani yoyote katika Mungu.
41, 42. Kuna uthibitisho gani wa kuunga mkono uhakika wa kihistoria wa Ukristo wa mapema?
41 Hata hivyo, maoni hayo ya kitashwishi hupuuza uthibitisho wa kihistoria. Kwa kielelezo, mwanahistoria Myahudi, Yosefo (c.37-c.100 W.K.) aliandika hivi: “Kwa baadhi ya Wayahudi uharibifu wa jeshi la Herode ulionekana kuwa kisasi cha kimungu, na bila shaka kisasi cha haki, kwa ajili ya alivyomtenda Yohana, aitwaye Mbatizaji. Kwa maana Herode alikuwa ameagiza auawe, ijapokuwa alikuwa mtu mwema.”—Marko 1:14; 6:14-29.
42 Mwanahistoria uyo huyo alishuhudia pia kuwapo kwa kihistoria kwa Yesu Kristo, alipoandika kwamba kulitokea “Yesu fulani, binadamu mwenye akili sana, iwapo kweli kweli aweza kuitwa binadamu . . . ambaye wanafunzi wake humwita mwana wa Mungu.” Aliendelea kwa kusema kwamba “Pilato alikuwa amepasisha juu yake hukumu . . . Na hata sasa jamii ya wale wanaoitwa kwa kufuata jina lake ‘Wamesiya’ haijatoweka.”f—Marko 15:1-5, 22-26; Matendo 11:26.
43. Mtume Petro alikuwa na msingi gani wa kuamini Kristo?
43 Kwa hiyo, mtume Petro Mkristo angeweza kuandika kwa usadikisho kamili akiwa shahidi aliyejionea kutukuzwa kwa sura ya Yesu, akisema: “Maana hatukufuata hadithi [bandia, NW; Kigiriki, mýthos] zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.”—2 Petro 1:16-18.g
44. Ni kanuni gani ya Biblia yapasa kuongoza katika mgongano wowote kati ya kauli ya binadamu na Neno la Mungu?
44 Katika mgongano huo kati ya kauli ya binadamu ya “kitaalamu” na Neno la Mungu, twapaswa kutumia kanuni iliyotolewa taarifa mapema: “Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! kutokuamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu? Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa. Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, ukashinde uingiapo katika hukumu.”—Warumi 3:3, 4.
Nyuzi Zile Zile
45. Ni zipi baadhi ya nyuzi zile zile zinazopatikana katika mfumo wa ngano za kilimwengu?
45 Mapitio hayo mafupi ya baadhi ya mifumo ya ngano za ulimwengu yameonyesha mambo fulani yanayofanana, mengi yayo yakiwa yaweza kufuatishwa kurudi nyuma mpaka Babuloni, kitovu cha Mesopotamia cha dini zilizo nyingi. Kuna nyuzi zile zile, ziwe ni kuhusu mambo ya hakika ya uumbaji, au katika masimulizi juu ya kipindi wakati vijimungu-nusu na majitu yalipokaa katika bara na gharika ikaangamiza waovu, au katika mawazo ya msingi ya kidini ya ibada ya jua na ya nafsi isiyoweza kufa.
46, 47. (a) Twaweza kutoa ufafanuzi gani wa Kibiblia juu ya asili na nyuzi zile zile za ngano? (b) Tutazungumzia sehemu gani zaidi za ibada ya kale?
46 Kwa maoni ya Biblia, twaweza kueleza nyuzi hizi za kijumla tukumbukapo kwamba baada ya Furiko, kwa amri ya Mungu ainabinadamu ilitawanyika kutoka Babeli katika Mesopotamia zaidi ya miaka 4,200 iliyopita. Ingawa waliachana, wakiunda familia na makabila yenye lugha tofauti-tofauti, walianza na uelewevu wa kimsingi ule ule wa historia na mawazo ya kidini yaliyotangulia. (Mwanzo 11:1-9) Karne zilivyopita, uelewevu huo ulipotolewa ukatiwa mapambo katika kila utamaduni, matokeo yakawa ni hadithi za kubuni, hekaya, na ngano ambazo zimetufikia sisi leo. Ngano hizo, zisizo na ukweli wa Biblia, zilishindwa kuleta ainabinadamu karibu zaidi na Mungu wa kweli.
47 Hata hivyo, wanadamu pia wameonyesha hisi zao za kidini katika njia nyingine mbalimbali—uasiliani-roho, ushamani, mizungu, kuabudu wazazi wa kale waliokufa, na kadhalika. Je! hizo zatuambia chochote juu ya jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu?
[Maelezo ya Chini]
a Kwa mazungumzo marefu ya uumbaji, ona kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation?, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society.
b Ngano za China zilizo za karibuni zaidi, ambazo ni matokeo ya Dini ya Buddha, Dini ya Tao, na Dini ya Confucius, zitazungumzwa katika Sura za 6 na 7.
c Kwa mazungumzo ya kirefu zaidi juu ya vithibitisho vya Furiko kuwa historia, ona Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 327-8, 609-12, kilichotangazwa na Watchtower Society.
d “Hadesi” huonekana katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo mara kumi, si akiwa mtu fulani anayetajwa katika ngano, bali kuwa kaburi la ainabinadamu yote. Ndilo neno la Kigiriki linalolingana na lile la Kiebrania she’ohlʹ.—Linganisha Zaburi 16:10; Matendo 2:27, Kingdom Interlinear.—Ona Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 1015-16, kilichotangazwa na Watchtower Society.
e Yapendeza kwamba Utnaphishtimu, shujaa wa Utenzi wa Gilgameshi, alimwagiza Urshanabi, mwendesha kivushio wake, aliyemvusha Gilgameshi maji ya kifo akakutane na mwokokaji wa furiko.
f Kulingana na maandishi ya kimapokeo ya Yosefo, kielezi-chini, ukurasa 48 ya hariri ya Harvard University Press, Buku 9.
g Kwa habari zaidi juu ya Ukristo, ona Sura 10.
[Sanduku katika ukurasa wa 43]
Miungu ya Kigiriki na Kiroma
Vijimungu na vijimungu-vike vingi vya ngano za Kigiriki vilikuwa na vyeo vile vile katika ngano za Kiroma. Jedwali iliyo chini yaorodhesha baadhi yavyo.
Kigiriki Kiroma Jukumu
Afrodito Zuhura Kijimungu-kike cha upendo
Apolo Apolo Kijimungu cha nuru, tiba, na mashairi
Aresi Mihiri Kijimungu cha vita
Artemi Diana Kijimungu-kike cha uwindaji na uzaaji-watoto
Asklepio Aeskulapio Kijimungu cha maponyo
Athena Minerva Kijimungu cha sanaa, vita, na hekima
Kronasi Sarateni Kwa Wagiriki, mtawala wa Matitani na
baba ya Zeu. Katika ngano za Kiroma,
pia kijimungu cha kilimo
Demeteri Seresi Kijimungu-kike cha vimeaji
Dionisio Bakasi Kijimungu cha divai, mrutubisho, na
tabia ya utukutu
Erosi Kiupidi Kijimungu cha upendo
Gaea Terra Alama ya dunia, na mama na
mke wa Zohari
Hifestasi Valkani Mhunzi wa vijimungu na kijimungu cha
moto na kazi ya vyuma
Hera Juno Mlinda ndoa na wanawake.
Kwa Wagiriki, ni dada na mke wa Zeu;
kwa Waroma, mke wake Sumbula
Herme Zebaki Tarishi wa vijimungu; kijimungu cha
biashara na sayansi; na cha kulinda
wasafiri, wezi, na watanga-tanga
Hestia Vesta Kijimungu-kike cha mekoni
Haipnosi Somnasi Kijimungu cha usingizi
Utaridi,Hadesi Utaridi Kijimungu cha ulimwengu wa chini
Poseidoni Kausi Kijimungu cha bahari. Katika ngano za Kigiriki,
pia kijimungu cha matetemeko ya dunia na cha farasi
Rea Opsi Mke na dada ya Kronosi
Zohari Zohari Mwana na mume wa Gaea na baba
ya Matitani
Zeu Sumbula Mtawala wa vijimungu
Imetegemea The World Book Encyclopedia, 1987, Buku 13.
[Sanduku katika ukurasa wa 45]
Vijimungu na Vijimungu-Vike vya Waashuri-Wababuloni
Anu—kijimungu kikuu, kinachotawala mbingu; baba ya Ishtari
Ashuri—kijimungu-shujaa cha kitaifa cha Waashuri; pia kijimungu cha mrutubisho
Ea—kijimungu cha maji. Baba ya Marduki. Kilionya Utnapishtimu juu ya furiko
Enlili (Beli)—bwana wa hewa; baadaye kikafanywa sambamba na Zeu katika ngano za Kigiriki. Kilifanywa na Wababuloni kuwa Marduki (Beli)
Ishtari—nafsi ya kijimungu cha sayari Zuhura; umalaya mtakatifu sehemu ya kiibada chake. Kilikuwa Astarte katika Foinike, Atargatisi katika Shamu, Ashtorethi katika Biblia (1 Wafalme 11:5, 33), Afrodito katika Ugiriki, Zuhura katika Roma
Marduki—cha kwanza kati ya vijimungu vya Kibabuloni; “kiliunganisha vijimungu vingine vyote kikatwaa kazi zavyo zote mbalimbali.” Kiliitwa Merodaki na Waisraeli
Shamashi—kijimungu-jua cha nuru na haki. Kitangulizi cha Apolo cha Wagiriki
Sini—kijimungu-mwezi, kishiriki cha utatu uliotia ndani Shamashi (jua) na Ishtari (sayari Zuhura)
Tamuzi (Dumuzi)—kijimungu cha mavuno. Mpenziye Ishtari
(Imetegemea New Larousse Encyclopedia of Mythology)
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 60, 61]
Vijimungu vya Askari-Jeshi Mroma
Roma ilikuwa maarufu kwa ajili ya jeshi lenye nidhamu. Muungano wa milki yayo ulitegemea hamasa na ufanisi kwa malejioni ya kivita. Je! dini ilihusika? Ndiyo, na kwa matokeo mazuri, Waroma walituachia uthibitisho wazi wa kazi yao kwa namna ya barabara, ngome, mitaro ya maji, majumba ya michezo, na mahekalu. Kwa kielelezo, katika Northumbria, kaskazini mwa Uingereza, kuna ule Ukuta wa Hadrian ujulikanao sana, uliojengwa wapata mwaka 122 W.K. Machimbuzi yamefunua nini juu ya utendaji wa vituo vya jeshi la Kiroma na jukumu la dini?
Katika Housesteads Museum, lililo karibu na mabomoko yaliyochimbuliwa ya kituo cha jeshi la Roma kwenye Ukuta wa Hadrian, kithibitisho kimoja chatoa taarifa hii: “Maisha ya kidini ya askari-jeshi wa Kiroma yaligawanywa sehemu tatu. Kwanza . . . kiibada cha Wamaliki waliofanywa Viabudiwa na ibada ya vijimiungu vilindavyo vya Roma kama Sumbula, Viktori na Mihiri. Madhabahu iliwekwa wakfu kwa Sumbula kila mwaka kwenye uwanja wa gwaride wa kila ngome. Askari-jeshi wote walitazamiwa washiriki katika misherehekeo ya kuadhimisha siku za kuzaliwa, siku za kutawazwa na ushindi wa Wamaliki waliofanywa Viabudiwa.” Jinsi inavyofanana na desturi za majeshi ya leo, ambazo katika hizo makasisi wa jeshi, madhabahu, na bendera ni sehemu ya kawaida ya ibada ya jeshi.
Lakini sehemu ya pili ya maisha ya kidini ya askari-jeshi Mroma ilikuwa nini? Ilikuwa ibada ya vijimungu vilindavyo na roho yenye utunzi ya kikosi chao hasa “na pia vijimungu vilivyoletwa kutoka nchi walikozaliwa.”
“Mwishowe kulikuwako viibada vilivyofuatwa na mtu mwenyewe. Ilimradi askari-jeshi alitimiza madaraka yake kuelekea viibada rasmi yeye alikuwa huru kuabudu kijimungu chochote alichopenda kuabudu.” Hilo lasikika kama kwamba ni hali yenye uhuru mkubwa wa ibada, lakini “zisizokubaliwa zilikuwa dini zile, miongoni mwazo ni Udruidi, ambazo mazoea yazo yalionwa kuwa ya kikatili, na zile ambazo ushikamanifu wazo kwa Serikali ulitiliwa shaka, kwa kielelezo Ukristo.”—Linganisha Luka 20:21-25; 23:1, 2; Matendo 10:1, 2, 22.
Yapendeza kujua kwamba, katika 1949 hekalu moja la Mithrasi lilivumbuliwa katika ziwa la matope kule Carrawburgh, karibu sana na Ukuta wa Hadrian. (Ona picha.) Waakiolojia wakadiria kwamba lilijengwa yapata mwaka 205 W.K. Lina mfano wa kijimungu-jua, madhabahu, na maandishi-mchoro ya Kilatini yanayosema, kwa sehemu, “Kwa Mithrasi kijimungu kisichoshindika.”
[Sanduku katika ukurasa wa 62]
Vijimungu vya Misri na Yale Mapigo Kumi
Yehova alitekeleza hukumu juu ya vijimungu vinyonge vya Misri kwa njia ya yale Mapigo Kumi.—Kutoka 7:14–12:32.
Pigo Maelezo
1 Naili na maji mengine yageuzwa kuwa damu. Kijimungu-Naili
Hapi chaaibishwa
2 Vyura. Kijimungu-kike-chura Hekti hakina nguvu ya kuzuia hilo
3 Mavumbi yageuzwa kuwa chawa. Thothi, bwana wa mizungu, hakikuweza
kuwasaidia wafanya mizungu wa Kimisri
4 Nzi-Waumao katika Misri yote isipokuwa Gosheni ambako Waisraeli walikaa.
Hakuna kijimungu kilichoweza kuzuia hilo—hata Ptah,
muumba ulimwengu wote mzima, wala Thothi, bwana wa mizungu
5 Tauni juu ya mifugo. Wala kijimungu-kike-ng’ombe mtakatifu
wala Apisi fahali hakingeweza kuzuia pigo hilo
6 Majipu. Viabudiwa viponyaji Thothi, Isisi, na Ptah havina uwezo wa kusaidia
7 Radi na mvua ya mawe. Ilifichua unyonge
wa Reshpu, chenye kuongoza umeme, na Thothi,
kijimungu cha mvua na radi
8 Nzige. Hili lilikuwa pigo kwa Mini
kijimungu-kirutubishaji, kilicholinda mazao
9 Siku tatu za giza. Ra, kijimungu-jua mashuhuri, na
Horasi, kijimungu kihusikacho na mambo ya jua, vyaaibishwa
10 Kifo cha wazaliwa wa kwanza kutia ndani wa Farao,
aliyefikiriwa kuwa kijimungu chenye umbo-mwili. Ra (Amon-Ra),
kijimungu-jua na nyakati nyingine kiliwakilishwa
kondoo-ndume, hakikuwa na uwezo wa kulizuia
[Sanduku katika ukurasa wa 66]
Ngano na Ukristo
Ibada ya vijimungu vya Ugiriki na Roma za kale vinavyosimuliwa na ngano ilikuwa imesitawi sana wakati Ukristo ulipotokea karibu miaka elfu mbili iliyopita. Katika Asia Ndogo majina ya Kigiriki yangali yalisambaa, hiyo ikieleza ni kwa nini watu wa Listra (katika Uturuki ya kisasa) waliwaita waponyaji Wakristo Paulo na Barnaba “miungu,” wakirejeza kwao mmoja akiitwa Herme na mwingine Zeu, badala ya Zebaki na Sumbula wa Kiroma. Simulizi hilo lasema kwamba “kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, alileta fahali na shada za maua kwenye malango na alitamani kutoa dhabihu pamoja na umati.” (Matendo 14:8-18) Ni pamoja na magumu tu kwamba Paulo na Barnaba wakausadikisha umati huo usiwatolee dhabihu. Hilo latoa kielezi jinsi zamani hizo watu hao walivyochukua kwa uzito ngano zao.
[Picha katika ukurasa wa 42]
Mlima Olimpasi, Ugiriki, uliodhaniwa kuwa makao ya vijimungu
[Picha katika ukurasa wa 47]
Bamba la udongo la mwandiko wa maandishi-kabari linaloeleza sehemu ya Utenzi wa Gilgameshi
[Picha katika ukurasa wa 50]
Anubisi, kijimungu chenye kichwa cha mbweha, chapima nafsi-moyo, kwenye mizani ya kushoto, kwa kulinganisha na Maat, kijimungu-kike cha ukweli na haki, alama yacho ikiwa unyoya; Thothi chaandika matokeo kwenye bamba kabla ya kuyatangaza kwake Osirisi
[Picha katika ukurasa wa 55]
Chalchiuhtlicue, kijimungu-kike cha Azteki cha maji matamu; chombo chenye umbo la bundi chenye shimo ambamo iliaminiwa iliwekwa mioyo iliyotolewa dhabihu
[Picha katika ukurasa wa 57]
Utatu wa Kimisri: kutoka kushoto, Horasi, Osirisi, na Isisi
[Picha katika ukurasa wa 58]
Ibada ya jua ya Wainka ilizoewa katika Machu Picchu, Peru
Intihuatana, kisimiko, “nguzo ya kufungia” ya jua, labda ilitumiwa kuhusiana na ibada ya jua katika Machu Picchu
[Picha katika ukurasa wa 63]
Viwakilisho vya Horasi ndege-kipanga, Apisi fahali, na Hekti chura. Vijimungu vya Kimisri havikuwa na uwezo wa kuzuia mapigo yaliyopelekwa na Yehova, kutia kugeuza Naili kuwa damu
[Picha katika ukurasa wa 64]
Viabudiwa vya Kigiriki, kutoka kushoto, Afrodito; Zeu kimembeba Ganimede, mnyweshaji wa vijimungu; na Artemiy