Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 1/15 kur. 5-8
  • Furiko Katika Hekaya za Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Furiko Katika Hekaya za Ulimwengu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mambo Yenye Kufanana Sana
  • Hekaya za Kale Kuhusu Furiko
  • Hekaya za Mashariki ya Mbali
  • Katika Nchi za Amerika
  • Pasifiki Kusini na Esia
  • Chanzo Kimoja
  • Simulizi la Noa na Gharika Kuu—Je, Ni Hekaya Tu?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Ulimwengu Ulioharibiwa
    Kuokolewa Kuingia Katika Dunia Mpya
  • Ulimwengu Mzima Waharibiwa!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
  • Ile Gharika—Onyo Kutokana na Wakati Uliopita
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 1/15 kur. 5-8

Furiko Katika Hekaya za Ulimwengu

FURIKO la siku ya Noa lilikuwa msiba mkubwa wenye uharibifu mwingi sana hivi kwamba ainabinadamu isingeweza kamwe kulisahau. Zaidi ya miaka 2,400 baadaye, Yesu Kristo alisema juu yalo likiwa jambo la hakika la historia. (Mathayo 24:37-39) Tukio hilo lenye kutisha sana liliacha kumbukumbu la ajabu lisilofutika akilini mwa jamii ya kibinadamu hivi kwamba kuna hekaya kuhusu hilo kotekote ulimwenguni.

Katika kitabu Myths of Creation, Philip Freund hukadiri kwamba hekaya zaidi ya 500 kuhusu Furiko husimuliwa na makabila na jamii za watu zaidi ya 250. Kama iwezavyo kutazamiwa, karne nyingi zikiwa zimepita, hekaya hizo zimetiwa chumvi sana na matukio na watu wa kuwaziwa tu. Hata hivyo, katika hizo zote, mambo ya msingi yenye kufanana yaweza kupatikana.

Mambo Yenye Kufanana Sana

Watu walipohama kutoka Mesopotamia baada ya Furiko, walichukua masimulizi ya msiba huo mkubwa kuelekea sehemu zote za dunia. Hivyo, wenyeji wa Esia, visiwa vya Pasifiki Kusini, Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati, na Amerika Kusini wana hadithi za tukio hilo lenye kuvutia. Hekaya nyingi kuhusu Furiko zilikuwako muda mrefu kabla ya watu hao kuarifiwa juu ya Biblia. Hata hivyo, hekaya hizo zinashiriki mambo fulani ya msingi pamoja na usimulizi wa Kibiblia kuhusu Gharika.

Hekaya nyingine hutaja kwamba majitu wenye jeuri walikuwa wakiishi duniani kabla ya Furiko. Kwa ulinganifu, Biblia huonyesha kwamba kabla ya Gharika malaika wasiotii walivaa miili ya kimnofu, wakaishi pamoja na wanawake, na kutokeza jamii ya majitu waitwao Wanefili.—Mwanzo 6:1-4; 2 Petro 2:4, 5.

Hekaya kuhusu Furiko kwa kawaida huonyesha kwamba mwanamume mmoja alionywa juu ya kuja kwa furiko lenye chanzo cha kimungu. Kulingana na Biblia, Yehova Mungu alimwonya Noa kwamba Yeye angewaharibu waovu na wale wenye jeuri. Mungu alimwambia Noa hivi: “Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.”—Mwanzo 6:13.

Hekaya kuhusu Furiko kwa kawaida huonyesha kwamba ilisababisha uharibifu wa duniani pote. Vivyo hivyo, Biblia husema hivi: “Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa. Kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu.”—Mwanzo 7:19, 22.

Hekaya kuhusu Furiko zilizo nyingi husema kwamba mwanamume aliokoka Gharika pamoja na mtu mmoja au na watu wawili wengine. Hekaya nyingi husimulia kwamba alipata himaya katika mashua aliyokuwa amejenga, nazo husimulia kwamba ilitua kwenye mlima. Kwa ulinganifu, Maandiko husema kwamba Noa alijenga safina. Yanataarifu hivi pia: “Akabaki Nuhu [Noa, NW] tu, na hao walio pamoja naye katika safina.” (Mwanzo 6:5-8; 7:23) Kulingana na Biblia, baada ya Gharika “safina ikatua juu ya milima ya Ararati,” ambapo Noa na familia yake walitoka. (Mwanzo 8:4, 15-18) Hekaya huonyesha pia kwamba waokokaji wa Furiko walianza kuijaza tena dunia watu, kama Biblia inavyoonyesha kwamba Noa na familia yake walifanya.—Mwanzo 9:1; 10:1.

Hekaya za Kale Kuhusu Furiko

Tunapofikiria mambo hayo yaliyotangulia, acheni tuangalie hekaya fulani kuhusu Furiko. Labda tuanze na Wasumeria, jamii ya watu ya kale iliyokaa Mesopotamia. Usimulizi wayo wa Gharika ulipatikana kwenye bamba la udongo lililofukuliwa katika magofu ya Nippur. Bamba hilo lasema kwamba miungu ya Wasumeria Anu na Enlili waliamua kuiharibu ainabinadamu kwa furiko kubwa. Akiwa ameonywa na mungu Enki, Ziusudra na familia yake waliweza kuokoka katika mashua kubwa sana.

Masimulizi ya Kibabuloni ya Utenzi wa Gilgamesh yana maelezo mengi. Kulingana nayo, Gilgamesh alitembelea babu yake wa kale Utnapishtim aliyekuwa amepewa uhai wa milele baada ya kuokoka Furiko. Katika mazungumzo yaliyofuata, Utnapishtim alieleza kwamba alikuwa ameambiwa ajenge meli na kuchukua ng’ombe, hayawani-mwitu, na familia yake ndani yayo. Alijenga meli hiyo kuwa mchemraba mkubwa mno wa meta 60 kwenye kila upande, ukiwa na orofa sita. Amwambia Gilgamesh kwamba dhoruba hiyo ilichukua muda wa siku sita mchana na usiku, kisha akasema hivi: “Siku ya saba ilipofika, tufani, Gharika, na Mshtuo wa vita ulivunjwa, ambao ulikuwa umepiga kama jeshi. Bahari ilitulia, tufani ilififia, na Gharika ikakoma. Nilitazama bahari na mvumo wa sauti ulikuwa umeisha. Na ainabinadamu wote walikuwa wamegeuka kuwa udongo.”

Chombo hicho kilipotua kwenye Mlima Nisir, Utnapishtim aliachilia njiwa aliyerudia mashua wakati hakupata mahali pa kupumzika. Huyo alifuatwa na mbayuwayu aliyerudi pia. Kunguru kisha akaachiliwa, na alipokosa kurudi, Utnapishtim alijua kwamba maji yalikuwa yamepunguka. Kisha Utnapishtim akawaachilia wanyama na kufanya toleo la dhabihu.

Hekaya hiyo ya zamani sana inafanana kwa njia fulani na usimulizi wa Kibiblia wa Furiko. Hata hivyo, inakosa maelezo madogo madogo ya waziwazi na urahisi wa usimulizi wa Biblia, na haitolei safina vimo vinavyofaa wala haiandai muda wa wakati unaoonyeshwa katika Maandiko. Kwa mfano, Masimulizi ya Utenzi wa Gilgamesh yalisema kwamba dhoruba ilichukua siku sita mchana na usiku, hali Biblia husema kwamba “Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku”—mvua nzito ya kuendelea ambayo hatimaye ilifunikiza dunia yote kwa maji.—Mwanzo 7:12.

Ingawa Biblia hutaja waokokaji wa Furiko wanane, katika hekaya ya Kigiriki ni Deucalion tu na mke wake, Pyrrha, ndio waliookoka. (2 Petro 2:5) Kulingana na hekaya hiyo, kabla ya Furiko dunia ilikaliwa na watu wenye jeuri waitwao wanaume wa shaba nyeusi. Mungu Zeus aliamua kuwaharibu kwa furiko kubwa na akamwambia Deucalion ajenge sanduku kubwa na kuingia ndani yalo. Furiko lilipopunguka, sanduku hilo lilitua kwenye Mlima Parnassus. Deucalion na Pyrrha walishuka mlima huo na kuanza ainabinadamu tena.

Hekaya za Mashariki ya Mbali

Katika India, kuna hekaya kuhusu Furiko ambayo katika hiyo Manu ndiye mwanadamu anayeokoka. Anafanya urafiki na samaki mdogo anayekua kufikia ukubwa sana na ambaye amwonya kuhusu furiko lenye uharibifu mwingi. Manu ajenga mashua, ambayo samaki huyo avuta mpaka inapotua kwenye mlima katika Himalaya. Furiko linapopunguka, Manu ashuka mlima na pamoja na Ida, aliye ufananisho wa dhabihu yake katika umbo la kibinadamu, afanya upya jamii ya kibinadamu.

Kulingana na hekaya ya furiko ya Kichina, mungu wa radi awapa watoto wawili Nuwa na Fusi, jino moja. Yeye awaagiza walipande na kupata himaya katika mumunya utakaomea kutoka jino hilo. Mti wamea haraka kutoka jino hilo na kutokeza mumunya mkubwa sana. Mungu huyo wa radi anaposababisha mvua nyingi sana, watoto hao wanapanda kuingia ndani ya mumunya. Ingawa furiko linalofuata linawazamisha wakaaji wengine wote wa dunia, Nuwa na Fusi wanaokoka na kuijaza tena dunia watu.

Katika Nchi za Amerika

Wahindi wa Amerika Kaskazini wana hekaya mbalimbali zilizo na kichwa kilekile cha furiko linaloharibu watu wote ijapokuwa watu wachache tu. Kwa mfano, Waarikara, watu wa Kaddo, husema kwamba dunia wakati mmoja ilikaliwa na jamii ya watu wenye nguvu sana hivi kwamba waliwadhihaki miungu. Mungu Nesaru aliwaharibu majitu hao kwa njia ya furiko lakini aliwahifadhi watu wake, wanyama, na mahindi katika pango. Wahavasupai husema kwamba mungu Hokomata alisababisha furiko lililoharibu ainabinadamu. Hata hivyo, mwanamume Tochopa alihifadhi binti yake Pukeheh kwa kumficha katika gogo lenye shimo.

Wahindi katika Amerika za Kati na Kusini wana hekaya zenye mambo ya msingi yanayofanana. Wamaya wa Amerika ya Kati waliamini kwamba nyoka mkubwa wa mvua aliharibu dunia kwa maji mengi sana. Katika Meksiko usimulizi wa Wachimalpopoka husema kwamba furiko liliifunikiza milima. Mungu Tezkatlipoka alimwonya mwanadamu Nata aliyechimba shimo katika gogo ambamo yeye na mke wake, Nena, walipata himaya mpaka maji yalipopunguka.

Katika Peru Wachincha wana hekaya kuhusu furiko la siku tano lililoharibu wanadamu wote ijapokuwa mmoja ambaye aliongozwa kwenye usalama juu ya mlima na mnyama Ilama asemaye. Waaymara wa Peru na Bolivia husema kwamba mungu Virakocha alitoka katika Ziwa Titikaka na kuuumba ulimwengu na wanaume wakubwa na wenye nguvu isiyo ya kawaida. Kwa sababu jamii hii ya kwanza ilimkasirisha, Virakocha aliwaharibu kwa furiko.

Wahindi Watupinamba wa Brazili walisema kuhusu wakati ambao furiko kubwa liliwazamisha mababu wao wote wa kale ijapokuwa wale waliookoka katika mitumbwi au katika miti mirefu. Wakashinaua wa Brazili, Wamakushi wa Guyana, Wakaribi wa Amerika ya Kati, na Waona na Wayagan wa Tierra del Fuego katika Amerika Kusini wamo miongoni mwa makabila mengi walio na hekaya kuhusu furiko.

Pasifiki Kusini na Esia

Kotekote katika Pasifiki Kusini, hekaya kuhusu furiko kukiwa na wachache wakiokoka ni za kawaida. Kwa mfano, katika Samoa, kuna hekaya kuhusu furiko katika nyakati za mapema lililoharibu kila mtu isipokuwa Pili na mke wake. Walipata himaya katika mwamba, na baada ya furiko walijaza tena dunia watu. Katika visiwa vya Hawaii, mungu Kane alikasirikia wanadamu akapeleka furiko liwaharibu. Ni Nu’u tu aliyeokoka katika mashua kubwa sana iliyotua mlimani hatimaye.

Kwenye Mindanao, katika Ufilipino, Waata husema kwamba dunia wakati mmoja ilifunikizwa kwa maji yaliyoharibu kila mtu isipokuwa wanaume wawili na mwanamke mmoja. Waibani wa Sarawaki, Borneo, husema kwamba ni watu wachache tu waliookoka furiko kwa kukimbia juu ya vilima vyenye kimo cha juu zaidi. Katika hekaya ya Waigoroti wa Ufilipino, ni ndugu na dada tu ndio waliookoka kwa kupata himaya kwenye Mlima Pokis.

Wasoyoti wa Siberia, Urusi, husema kwamba chura mkubwa mno, aliyekuwa akiitegemeza dunia, alisonga na kusababisha dunia yote igharikishwe. Mwanamume mzee pamoja na familia yake waliokoka kwenye chelezo cha mbao alichofanya. Maji yalipopunguka, chelezo hicho kilitua kwenye mlima wenye kimo cha juu. Waugriani wa magharibi mwa Siberia na Hangari husema pia kwamba waokokaji wa furiko walitumia vyelezo vya mbao lakini wakachukuliwa sehemu tofauti-tofauti za duniani.

Chanzo Kimoja

Twaweza kukata maneno vipi kutokana na hekaya hizo nyingi kuhusu furiko? Ingawa zinatofautiana sana katika maelezo yazo, zina mambo fulani yanayofanana. Hayo yanaonyesha chanzo kimoja katika msiba mkubwa sana usiosahaulika. Zijapokuwa tofauti nyingi katika hekaya hizo muda wa karne zilizopita, kichwa chazo cha msingi ni kama uzi unaozifungamanisha na tukio kubwa moja—usimulizi wa Biblia kuhusu Gharika ya duniani pote ulio sahili, usiotiwa chumvi.

Kwa kuwa hekaya kuhusu Furiko zapatikana kwa kawaida miongoni mwa watu ambao hawakupata kuarifiwa juu ya Biblia mpaka karne za hivi karibuni, ingekuwa kosa kushikilia kauli kwamba walivutwa na usimulizi wa Kimaandiko. Isitoshe, The International Standard Bible Encyclopedia husema hivi: “Mweneo ulimwenguni pote wa masimulizi kuhusu furiko huchukuliwa kwa kawaida kuwa ushuhuda wa uharibifu wa binadamu wenye kuenea ulimwengu wote mzima kwa furiko . . . Isitoshe, mengine ya masimulizi hayo ya kale yaliandikwa na watu waliopinga sana mapokeo ya Ukristo wa Kiebrania.” (Buku 2, ukurasa 319) Kwa hiyo twaweza kukata maneno kwa uhakika kwamba hekaya kuhusu Furiko zinathibitisha ukweli wa usimulizi wa Kibiblia.

Kwa vile twaishi katika ulimwengu uliojaa jeuri na ukosefu wa adili, twafanya vyema kusoma usimulizi wa Kibiblia wa Furiko, kama ulivyorekodiwa katika Mwanzo sura 6 hadi 8. Tukitafakari juu ya sababu ya Gharika hiyo ya duniani pote—kule kuzoea mambo maovu machoni pa Mungu—tutaona onyo muhimu ndani yayo.

Hivi karibuni mfumo mwovu wa mambo uliopo utapatwa na hukumu kali ya Mungu. Lakini kwa furaha, kutakuwako waokokaji. Wewe unaweza kuwa miongoni mwao ikiwa utatii maneno ya mtume Petro: “Dunia ile ya wakati ule [wa Noa] iligharikishwa na maji, ikaangamia. Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. . . . Kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa [ujitoaji kimungu, NW], mkitazamia [mkiiweka karibu akilini, NW] hata ije siku ile ya Mungu [Yehova, NW].”—2 Petro 3:6-12.

Wewe utakuweka karibu akilini kuwapo kwa siku ya Yehova? Ukifanya hivyo na kutenda kwa kupatana na mapenzi ya Mungu, utaonea shangwe mibaraka mikubwa. Wale wanaompendeza Yehova Mungu hivyo, wanaweza kuwa na imani katika ulimwengu mpya ambao Petro arejezea anapoongeza hivi: “Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.”—2 Petro 3:13.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Hekaya za Kibabuloni kuhusu furiko zilipitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine

[Picha katika ukurasa wa 8]

Je! wewe unatii onyo la Petro kwa kuiweka karibu akilini siku ya Yehova?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki