Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 3/22 kur. 8-10
  • Wanunuzi Jihadharini! Uigizaji-Vitu Waweza Kugharimu Uhai

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wanunuzi Jihadharini! Uigizaji-Vitu Waweza Kugharimu Uhai
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vitu Bandia Vinavyoweza Kuua
  • Uigizaji-Vitu—Tatizo la Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—1996
  • Kadi za Mkopo na Hundi za Malipo—Halisi au Bandia?
    Amkeni!—1996
  • Ndege Ziliwasilije?
    Amkeni!—1999
  • Unaweza Kufanya Kusafiri kwa Ndege Kuwe Salama Zaidi
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 3/22 kur. 8-10

Wanunuzi Jihadharini! Uigizaji-Vitu Waweza Kugharimu Uhai

WENYE kudanganywa wasiozoezwa, wasioshuku wanaweza kupumbazwa. Ile saa ionekanayo kuwa ghali unayotolewa na mchuuzi wa barabarani kwa nusu ya bei—je, ni halisi au ni bandia? Je, utainunua? Lile koti la anasa la manyoya unalotolewa na mchuuzi aliye garini kando ya barabara—mchuuzi aahidi kwamba hilo ni koti la manyoya ya bei ghali. Je, uvutio walo na bei iliyoshushwa itakuzuia kutumia uamuzi bora? Ile pete ya almasi kidoleni mwa eti mke aliyetalikiwa hivi majuzi—sasa akiwa hana fedha wala makao, anayengoja gari-moshi katika stesheni moja ya New York ya gari-moshi la chini ya ardhi—unaweza kuipata kwa bei ya chini mno. Je, ungefikiri kwamba bei hiyo ni nzuri mno hivi kwamba huwezi kuiacha? Kwa sababu maswali haya yanaulizwa katika makala hii inayoshughulikia uigizaji-vitu na kwa sababu ya hali zinazotolewa, yaelekea utajibu “SIWEZI KAMWE!”

Ahaa, lakini ebu tubadili mahali na hali tuone majibu yako yatakuwa nini. Namna gani kibeti kizuri kipendwacho sana kinachouzwa katika duka halali lenye kuuza vitu kwa bei iliyopunguzwa sana? Aina ijulikanayo sana ya wiski inayouzwa katika duka la vileo pembeni mwa barabara? Kwa hakika hapangekuwa na tatizo hapa. Fikiria pia, ukanda wa filamu wenye jina lijulikanalo ambao umepunguzwa bei katika duka la dawa au duka la kuuza kamera. Wakati huu ile saa ya bei ya juu yenye kugharimu maelfu ya fedha inatolewa kwako, si na mchuuzi wa barabarani, bali na duka lenye sifa nzuri. Bei imepunguzwa sana. Ikiwa ungekuwa unapendezwa na saa kama hiyo ya bei ya juu, je, ungeinunua? Kisha kuna aina zijulikanazo sana za viatu kwa bei zenye kuokoa fedha katika duka moja hususa ambalo unaelekezwa na rafiki zako. Je, una uhakika hivyo si miigizo hafifu tu?

Katika ulimwengu wa sanaa, kwenye majengo ya kuonyeshea vitu vya sanaa yenye picha za kupendeza, kuna mauzo mengi ya mnada kwa wanaopendezwa na sanaa ya bei ya juu. “Tahadhari,” akaonya mtaalamu mmoja wa sanaa. “Wataalamu wenye miaka mingi ya uzoefu hupumbazwa. Na ndivyo na wauzaji. Na ndivyo na wasimamizi wa majumba ya hifadhi ya vitu vya kale.” Je, umesoma sana hivi kwamba ungeweza kutoshana akili na waelekeao kuwa waigizaji wa vitu? Jihadhari! Vitu vyote vilivyoonyeshwa pichani vyaweza kuwa bandia. Mara nyingi ndivyo huwa. Kumbuka, kitu kikiwa nadra kukipata na kina thamani, mtu fulani mahali fulani atajaribu kukiigiza.

Bidhaa zilizoigizwa ni utendaji wa dola bilioni 200 ulimwenguni pote nao “unastawi kwa haraka kuliko viwanda vingi ambavyo ni windo lavyo,” likaandika gazeti Forbes. Visehemu bandia vya gari hugharimu watengenezaji na waandaaji wa Marekani wa magari dola bilioni 12 kila mwaka katika mapato yanayopotea ulimwenguni pote. “Kiwanda cha magari cha Marekani chasema kwamba kingeweza kuajiri watu wengine 210,000 ikiwa kingeweza kukomesha waandaaji wa visehemu bandia kufanya biashara,” hilo gazeti likasema. Inaripotiwa kwamba karibu nusu ya viwanda vya uigizaji-vitu viko nje ya Marekani—karibu kila mahali.

Vitu Bandia Vinavyoweza Kuua

Namna fulani za bidhaa bandia ni zenye kudhuru. Nati, bolti na skrubu zilizoagizwa kutoka nje hufanyiza asilimia 87 ya dola bilioni 6 za soko la Marekani. Hata hivyo, uthibitisho kufikia sasa unaonyesha kwamba asilimia 62 ya vikazaji hivi vina majina yaliyotungwa ili kudanganya au vina mihuri isiyo halali ya gredi. Ripoti ya 1990 iliyotolewa na General Accounting Office (GAO) ilipata kwamba angalau “viwanda vya nyuklia [72 vya Marekani] vilikuwa vimeweka vikazaji vyenye ubora wa chini sana kuliko ule unaohitajiwa na sheria, vingine katika mifumo ya kuzima kitendanishio aksidenti itokeapo. Tatizo hili lazidi kuwa baya, yasema GAO. . . . Ukubwa wa tatizo hilo, gharama kwa walipa-kodi au hatari ziwezazo kutokea kutokana na kutumia bidhaa hizo [za hali ya chini] hazijulikani,” likaripoti Forbes.

Bolti za chuma, ambazo nguvu zazo hazitoshi kwa matumizi, zimeigizwa na kuingizwa Marekani kisiri na wanakandarasi wasio wanyoofu. “Zinaweza kutisha usalama wa majengo ya ofisi, viwanda vya umeme, madaraja na vifaa vya kijeshi,” kulingana na American Way.

Papi bandia za breki ndizo zilizolaumiwa kusababisha kuanguka kwa basi moja katika Kanada miaka kadhaa iliyopita ambapo watu 15 walikufa. Imeripotiwa kwamba visehemu bandia vimepatikana katika mahali ambapo mtu hangefikiria vingepatikana kama vile kwenye helikopta za kijeshi na chombo cha anga cha Marekani. “Mtumiaji wa wastani hajali sana unapozungumza kuhusu saa zilizo bandia aina ya Cartier au Rolex,” akasema mchunguzi mmoja maarufu wa uigizaji-vitu, “lakini afya na usalama zinapokuwa hatarini, wanahangaikia sana hiyo hali.”

Orodha ya vitu bandia viwezavyo kuwa hatari yatia ndani mashine za kusaidia moyo kupiga zilizouzwa kwa hospitali 266 za Marekani; vibonge bandia vya kupanga uzazi ambavyo vilifikia soko la Marekani katika 1984; na viuakuvu, ambavyo ni chokaa tu, vilivyoharibu mazao ya kahawa ya Kenya katika 1979. Kuna dawa bandia zilizoenea sana ambazo zaweza kuhatarisha maisha ya watumiaji. Vifo vinavyotokana na dawa bandia ulimwenguni pote vyaweza kushangaza.

Kuna wasiwasi wenye kuongezeka kuhusu vyombo vidogo vya nyumbani vya umeme vilivyo bandia. “Baadhi ya bidhaa hizi huwa na majina bandia ya kibiashara au idhini kama vile katika orodha ya Underwriters Laboratory,” likaripoti American Way. “Lakini havitengenezwi kufikia kiwango cha usalama icho hicho, na kama tokeo vitalipuka, kusababisha moto wa nyumbani na kufanya uwekaji wote usiwe salama,” akasema mhandisi mmoja wa usalama.

Katika Marekani na Ulaya, vikundi vya elimu ya kuruka kwa ndege vinatiwa wasiwasi vilevile. Kwa kielelezo, katika Ujerumani, mashirika ya ndege yamepata injini na visehemu vya breki vilivyo bandia katika orodha ya vitu walivyo navyo. Uchunguzi “unafanywa katika Ulaya, Kanada, na United Kingdom, ambako visehemu (nati za ufito wa kijembe kilicho mkiani) visivyoidhinishwa vimehusianishwa na anguko hatari la hivi majuzi la helikopta,” wasema maofisa wa uchukuzi. “Maajenti wamekamata visehemu vingi bandia vya injini ya ndege, mkusanyo wa breki, bolti na vikazaji vyenye ubora wa chini, visehemu vyenye kasoro vya mifumo ya mafuta na ya vifaa vya kiumeme vya kuongozea ndege, vifaa vya kuongozea ndege visivyoidhinishwa na visehemu vya mifumo ya kuongozea ndege ya kompyuta ambavyo ni hatari kwa usalama wa safari ya angani,” likaripoti Flight Safety Digest.

Katika 1989 ndege ya kukodiwa iliyokuwa ikielekea Ujerumani kutoka Norway ilianza ghafula kushuka chini kwa mwinamo kutoka mruko wayo wa mwinuko wa meta 6,600. Sehemu ya mkiani ilipasuliwa, ikifanya ndege hiyo ishuke vibaya sana kuelekea chini kwa mwinamo mkali hivi kwamba mabawa yote mawili yalivunjika. Nafsi zote 55 zilizokuwa ndani zilikufa. Baada ya uchunguzi wa miaka mitatu, wataalamu wa Norway wenye elimu ya kuruka kwa ndege waligundua kwamba anguko hilo lilisababishwa na bolti zenye kasoro, ziitwazo pini za kukaza, zilizounganisha sehemu ya mkiani na ile sehemu kuu ya ndege. Uchanganuzi wa mkazo ulionyesha kwamba hizo bolti zilitengenezwa kwa metali ambayo ni dhaifu sana kuweza kustahimili nguvu zenye kupiga za safari ya ndege. Pini za kukaza zenye kasoro zilikuwa bandia—neno ambalo ni la kawaida sana kwa wataalamu wa elimu ya kuruka kwa ndege kila mahali, kwa kuwa uigizaji-vitu ni tatizo lenye kuongezeka sana ambalo huhatarisha maisha ya wafanyakazi wa ndege na abiria.

Televisheni ya kitaifa ilipomhoji inspekta mkuu wa Idara ya Uchukuzi ya Marekani alisema hivi: “Mashirika yote ya ndege yamepata visehemu bandia. Yote yanayo. Yote yana tatizo.” Yeye aliongeza kwamba biashara ya ndege inakiri “kwamba yaelekea ina orodha ikadiriwayo kugharimu dola bilioni mbili au tatu ya bidhaa walizo nazo ambazo haziwezi kutumiwa.” Madalali na wafanyibiashara wasio wanyoofu ambao hawahitaji kupewa leseni katika kushughulika na visehemu vya ndege mara nyingi huwa wenye utayari mno kuuza kwa udanganyifu visehemu vibaya kama kwamba ni vizuri.

Katika mahojiano ayo hayo, mshauri wa usalama wa elimu ya kuruka kwa ndege, ambaye ameshauri FBI juu ya utendaji kadhaa wa kichinichini unaohusisha visehemu bandia, alionya kwamba visehemu bandia hutokeza hatari ya kweli. “Nafikiri, likiwa tokeo, kwa hakika tunatazamia msiba mkubwa wa ndege wakati fulani ujao usio mbali,” yeye akasema.

Siku ya hukumu inakaribia kwa wale ambao pupa yao huwaruhusu kuweka tamaa zao wenyewe za kichoyo mbele ya maisha za wengine. Neno la Mungu lililopuliziwa lataarifu kwamba kwa hakika watu wenye pupa hawataurithi Ufalme wa Mungu.—1 Wakorintho 6:9-10.

[Picha katika ukurasa wa 9]

Mavazi, vito, michoro, dawa, spea za ndege—kitu chochote chenye thamani ni nafaka ya kusagwa ya kinu cha kusagia cha mwigizaji-vitu

[Picha katika ukurasa wa 10]

Spea bandia za injini, bolti zenye kasoro, vifaa vya kuongezea ndege, visehemu vya kompyuta, na spea nyinginezo zilizoigizwa zimesababisha maanguko yagharimuyo uhai

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki