Waazteki—Pambano Lao Lenye Kuvutia Ili Kuokoka
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO
“MAHALI PAKUBWA SANA PALIPO NA SOKO PALIKUWA PAMEJAA WATU CHUNGU NZIMA, WENGINE WAKINUNUA VITU, WENGINE WAKIUZA . . . KULIKUWA NA ASKARI-JESHI MIONGONI MWETU WALIOKUWA WAMESAFIRI HADI SEHEMU NYINGI ZA ULIMWENGU, KUFIKA CONSTANTINOPLE NA ITALIA NA KOTE KOTE KATIKA ROME, NA WALISEMA KWAMBA HAWAJAPATA KAMWE KUONA SOKO KUBWA SANA LENYE UPATANO NA USAWAZIKO LIKIWA NA WATU WENGI NAMNA HIYO.”
UFAFANUZI ambao umenukuliwa ulitolewa na Bernal Díaz del Castillo, askari-jeshi wa jeshi la mshindi Mhispania Hernán Cortés, alipoona jiji la Azteki la Tenochtitlán mnamo mwaka wa 1519.
Kulingana na kitabu The Mighty Aztecs, cha Gene S. Stuart, Wahispania walipowasili, jiji la Tenochtitlán lilikuwa na watu kati ya 150,000 na 200,000. Jiji hili halikuwa la kishenzi na lililojitenga, lilikuwa jiji kubwa lililokuwa likipanuka, likiwa na ukubwa wa kilometa mraba kadhaa. Lilikuwa jiji lenye madaraja, barabara za juu, mifereji, na mahekalu ya ibada yaliyong’aa. Likiwa jiji kuu, Tenochtitlán lilikuwa kitovu cha Milki ya Azteki.
Lakini kwa wasomaji wengi, wazo hili la jiji la Azteki lenye amani na upatano hupingana na yale ambayo wamesikia, wazo linalopendwa na wengi la kwamba Waazteki walikuwa tu washenzi waliotamani kumwaga damu. Kwa hakika, Waazteki waliamini kwamba miungu yao ilihitaji kupewa mioyo na damu ya wanadamu kusudi ibaki ikiwa na nguvu. Hata hivyo, kulikuwa na mengi zaidi kuhusu utamaduni na historia ya Waazteki kuliko tu kumwaga damu. Kuelewa pigano lao ili kuokoka kutamwezesha mtu afahamu vizuri zaidi pigano hilo dhabiti ambalo wazao wao wanapigana hadi sasa.
Asili ya Waazteki
Kwa kweli, Waazteki walikaa kwa muda mfupi kwenye historia kuhusu ustaarabu wa wakazi wa Mesoamerica.a Watafiti wengi wanaamini kwamba wakazi wa awali wa Mexico walihama kutoka Asia wakavuka Mlangobahari wa Bering hadi Alaska na kutoka hapo walielekea kusini hatua kwa hatua.—Ona Amkeni! la Septemba 8, 1996, ukurasa wa 4-5.
Waakiolojia wanasema kwamba utamaduni wa kale zaidi uliopata kusitawi katika Mesoamerica ulikuwa wa watu wa Olmeki. Kulingana na vichapo fulani, yaelekea ustaarabu wa watu wa Olmeki uliibuka yapata mwaka wa 1200 K.W.K. na huenda ulidumu kwa miaka 800. Lakini ni kufikia mwaka wa 1200 W.K.—zaidi ya miaka elfu mbili baadaye kwamba Waazteki walipata kuwa mashuhuri. Utamaduni wao ungedumu kwa miaka 300 tu. Na milki yao yenye nguvu ingetawala kwa miaka mia moja tu kabla ya kushindwa na wavamizi Wahispania.
Hata hivyo, Milki ya Waazteki ilipofikia upeo wa ufanisi wake, ilidhihirisha utukufu usio na kifani. Kulingana na gazeti moja, “Waazteki walisimamisha milki iliyoenea kusini hadi Guatemala.” Kichapo The World Book Encyclopaedia kiliifafanua hivi: “Waazteki walikuwa na mojawapo wa ustaarabu ulioendelea zaidi katika Amerika. Walijenga majiji makubwa kama yale yaliyokuwa Ulaya wakati huo.”
Asili ya Hadithi za Kale
Waazteki wajapokuwa mashuhuri, asili yao haijulikani sana. Kulingana na hekaya, jina Aztec limetolewa kutoka kwa aztlán—neno linaloaminiwa kuwa linamaanisha “bara jeupe.” Hata hivyo, hakuna mtu ajuaye mahali ilipokuwa Aztlán inayosimuliwa kwenye hekaya, au ikiwa kwa kweli ilipata kuwapo.
Kwa vyovyote, kulingana na hekaya hiyo, Waazteki walikuwa wa mwisho kati ya vikundi saba kuondoka Aztlán. Kwa amri ya mungu wao Huitzilopochtli, walianza safari ndefu ya kutafuta nchi ya nyumbani. Kabila hilo lilizurura kwa miongo mingi, likipatwa na magumu mengi na uhitaji mkubwa sana na kushiriki katika mapigano yasiyoisha kwa makusudi yote pamoja na majirani wao. Lakini hawangeendelea kuzurura milele. Kulingana na hekaya inayopendwa zaidi, Huitzilopochtli aliwaambia wafuasi wake watazame ishara ifuatayo: tai akiwa juu ya dungusi kakati. Inadhaniwa kwamba tukio hili lilionekana kwenye kisiwa kidogo chenye matope katika Ziwa Texcoco. Watu hawa wenye kuzurura hatimaye walitulia hapa, wakijenga jiji ambalo baadaye liliitwa Tenochtitlán Kuu (linalomaanisha “Jiwe Linalochomoza juu ya Maji”). Kulingana na watu fulani, jina lake linatokana na hadithi ya kale ya mzee wa ukoo aliyeitwa Tenoch. Leo, Tenochtitlán limezikwa chini ya Mexico City.
Waazteki walithibitika kuwa wahandisi na wasanii wenye akili. Wakitumia udongo ulio chini ya ziwa kuwa msingi, walipanua jiji kwa kujaza ardhi kwenye ziwa. Barabara za juu za ardhi iliyoinuliwa ziliunganisha kisiwa na bara. Pia mifereji mingi ilijengwa.
Hata hivyo, wakati wa kipindi hiki, kwa jumla wajenzi hawakujulikana kuwa Waazteki. Kulingana na hekaya, mungu wao Huitzilopochtli alikuwa amewapa jina jipya la utambulishi walipotoka Aztlán—Wameksiko. Baada ya muda, bara lililozingira pamoja na wakazi wake wote lingekuwa na jina hili.
Hata hivyo, Wameksiko, au Waazteki, hawakuwa peke yao katika eneo hili. Wakiwa wamezungukwa na maadui, walihitaji kuungana na majirani wao. Wale ambao hawakufanya amani na Waazteki upesi wakahusika katika mapambano yaliyosababisha vifo. Kwa kweli, vita iliwafaa Waazteki. Mungu-jua wao, Huitzilopochtli, alikuwa mmojawapo tu wa miungu na miungu ya kike aliyedai mioyo yenye damu na dhabihu za kibinadamu kwa ukawaida. Wafungwa wa vita wakawa vyanzo vikuu vya dhabihu hizi. Sifa ya Waazteki ya kutumia wafungwa kwa njia hii ilivuvia hofu ndani ya mioyo ya maadui wao.
Hivyo milki ya Waazteki ilianza kusambaa kutoka Tenochtitlán, ikaenea upesi upande wa chini hadi maeneo fulani ambayo sasa ni Amerika ya Kati. Mawazo mapya ya kidini na desturi zilikubaliwa katika utamaduni wa Waazteki. Wakati huohuo, vitu vyenye thamani kubwa ajabu—ushuru uliokusanywa kutoka kwa watumwa walioshindwa karibuni—ulianza kuja kwa wingi kwenye hazina ya Waazteki. Muziki, Fasihi, na sanaa ya Waazteki vilisitawi. Gazeti la National Geographic lasema: “Kwa ubora tu Waazteki wanapaswa kuwa miongoni mwa wachongaji wenye kipawa zaidi katika historia.” Wahispania walipowasili, ustaarabu wa Waazteki ulikuwa umefikia kilele cha fahari yake.
Ushindi
Mnamo Novemba 1519, maliki wa Mexico, Montezuma wa Pili, aliwakaribisha Wahispania pamoja na kiongozi wao Hernán Cortés kwa amani, akimwamini kuwa mungu wa Azteki Quetzalcoatl mwenye mwili. Wahispania walipokea ukarimu walioonyeshwa na Waazteki washirikina. Ingawa hivyo, wakiwa bila hila, Waazteki waliwaruhusu Wahispania waone hazina za dhahabu za Tenochtitlán. Cortés akiwa na msisimko mkubwa aliunda njama ya kuzitwaa zote. Katika tendo la ujasiri, Cortés alimfanya Montezuma kuwa mfungwa katika jiji lake mwenyewe. Wengine wanasema kwamba Montezuma alikubali kimya-kimya karibu kila kitu bila kuteta. Kwa vyovyote, Cortés alifaulu kushinda jiji kuu la milki kubwa bila pigano.
Lakini ushindi usiokuwa na umwagikaji wa damu haukubaki bila umwagikaji wa damu kwa muda mrefu. Kwa ghafula Cortés alihitaji kuondoka kuelekea pwani ili kushughulikia hali ya dharura, akiacha mtu aliyeitwa Pedro de Alvarado mwenye harara asimamie mambo. Akihofu kwamba bila Cortés huko, watu wa Tenochtitlán wangeinuka dhidi yake upesi, Alvarado aliamua kushambulia kwanza. Aliua Waazteki kadhaa wakati wa msherehekeo. Cortés aliporudi alipata jiji likiwa katika hali ya msukosuko. Wakati wa vita ambayo ilizuka wakati huo, Montezuma aliuawa, labda na Wahispania. Hata hivyo, kulingana na jinsi Wahispania wanavyofafanua matukio, Cortés alimshinda Montezuma ili ajitokeze na kuwasihi watu wake waache kupigana. Alipofanya hivyo, Montezuma alipigwa mawe na watu wake mwenyewe hadi akafa. Kwa vyovyote vile, Cortés na manusura wachache waliojeruhiwa waliponea chupuchupu.
Akiwa amemalizwa nguvu kabisa na kujeruhiwa, Cortés alikusanya upya jeshi lake. Wahispania waliungwa mkono na makabila jirani ambayo yaliwachukia Waazteki na yalitamani kujiondoa katika utumwa wao. Sasa Cortés alirudi hadi Tenochtitlán. Wakati wa kuzingira jiji uliofuata pamoja na umwagikaji damu, inaripotiwa kwamba Waazteki waliwadhabihu askari-jeshi Wahispania waliotekwa. Jambo hili liliwakasirisha wanaume wa Cortés na kuchochea azimio lao la kushinda kwa gharama yoyote. Kulingana na mwandishi mmoja wa Azteki, makabila yaliyotumikishwa awali, yalichukua hatua ya kibinafsi, “yakilipiza kisasi kwa ukatili kwa matendo ya zamani ya Wameksiko [Waazteki] na kupora mali yao yote.”
Mnamo Agosti 13, 1521, Tenochtitlán Kuu lilitekwa. Sasa Wahispania na marafiki wake wakawatawala kabisa Wameksiko. Gazeti National Geographic lilisema: “Katika muda mfupi sana, majiji makuu ya Mesoamerica na vituo vya sherehe viliachwa ukiwa huku Wahispania wakitafuta kwa haraka dhahabu katika nchi. Wazaliwa wa huko walifanywa watumwa na kuwa Wakristo, kisha milki ya Waazteki yaani ustaarabu mkuu wa mwisho wa wenyeji, ukaporomoka.”
Ushindi ulileta mabadiliko mengine mbali na yale ya kisiasa. Wahispania walileta dini mpya—Ukatoliki—na mara nyingi wakiwalazimisha Wameksiko kujiunga na dini hiyo kwa kutumia nguvu. Ni kweli, dini ya Waazteki ilitamani kumwaga damu na ilifuatia ibada ya sanamu. Lakini badala ya kung’oa masalio yote ya upagani, Ukatoliki uliungana kwa njia ya ajabu na dini ya Waazteki. Mungu wa kike Tonantzin, aliyeabudiwa kwenye Mlima Tepeyac, mahali pake palichukuliwa na Virgin of Guadalupe, Basilika ya Guadalupe ikiwa mahali palepale alipokuwa Tonantzin aliyestahiwa zamani. (Inadhaniwa kwamba Basilika hiyo hutia alama mahali ambapo Bikira Maria alijitokeza kimuujiza.) Wakati wa sikukuu za kidini zinazofanywa kwa heshima ya Bikira, waabudu huzunguka kwa kasi mbele kabisa ya basilika hiyo kwa kufuatana na dansi za kipagani za kale.
Je, Waazteki Wameokoka?
Ijapokuwa Milki ya Waazteki iliporomoka zamani sana, bado uvutano wake unahisiwa leo. Maneno ya Kiingereza, kama vile “chocolate,” “tomato,” na “chili,” yanatokana na lugha ya Waazteki ya Nahuatl. Zaidi ya hayo, watu wengi wa Mexico wanafanyizwa na wazao wa washindi Wahispania na jamii za wenyeji.
Katika sehemu nyingi za Mexico, tamaduni za wenyeji za kale zingalipo, kwa kuwa vikundi fulani vya kikabila vinajaribu kuhifadhi mapokeo yao ya kale. Kwa jumla, kuna vikundi 62 vya wenyeji vinavyotambuliwa na lahaja 68 zilizosajiliwa katika Jamhuri ya Mexico. Uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na shirika la Instituto Nacional de Estadística, Geografia e Informática (Taasisi ya Takwimu za Kitaifa za Jiografia na Hisabati) ulifikia mkataa kwamba zaidi ya watu milioni tano wenye umri wa miaka mitano au zaidi huzungumza mojawapo ya lugha za wenyeji. Gazeti National Geographic lilisema: “Katika enzi yote ya ukoloni, udikteta, na mapinduzi, waokokaji ambao hawakuwa na mamlaka na waliokuwa maskini wamehifadhi lugha, desturi, na tumaini la kujipatia uhuru.”
Ijapokuwa hivyo, wazao wengi wa Azteki wenye kujionea fahari huishi katika umaskini, mara nyingi wakipata riziki kwa shida kutoka kwenye mashamba madogo. Wengi huishi katika maeneo yaliyojitenga ambapo elimu hupatikana kwa nadra sana. Hivyo imekuwa vigumu kwa wenyeji wengi Wameksika kuendelea kiuchumi. Hali yao mbaya inawakilisha hali ya wenyeji katika Mexico na Amerika ya Kati yote. Maoni yametolewa kwa niaba yao. Rigoberta Menchú, mshindi wa Tuzo la Nobeli wa Guatemala, alitoa ombi hili lenye kusisimua: “Lazima tuondoe mipaka iliyoko—kati ya vikundi vya kikabila, Wahindi na chotara, vikundi vinavyonena lugha mbalimbali, wanaume na wanawake, watu wenye akili na wasio na akili.”
Kwa kuhuzunisha, hali mbaya ya Waazteki—ya kale na ya sasa—ni mfano mwingine wenye kuhuzunisha tu unaoonyesha ‘mtu mmoja akiwa na mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.’ (Mhubiri 8:9) Itahitaji zaidi ya maneno yenye kusisimua na mambo ya kisiasa yanayonenwa kwa ufasaha ili kubadili hali ya maisha ya watu maskini ulimwenguni na wale wa tabaka ya chini. Hivyo idadi kubwa ya watu wanaosema lugha ya Nahuatl wamekubali kwa hamu tumaini la Biblia juu ya serikali ya ulimwengu inayokuja, au “ufalme.”—Danieli 2:44; ona sanduku kwenye ukurasa huu.
Watu fulani hukinza wazo la kufundisha wenyeji Biblia. Huenda wakahisi kwamba dini ya watu wanaosema lugha ya Nahuatl—mchanganyiko wa Ukatoliki na upagani wa Waazteki wa kale—ni sehemu ya utamaduni wao unaohitaji kuhifadhiwa. Lakini wale ambao wamepokea ujumbe wa Biblia wamepata ukombozi wa kweli kutoka kwa ushirikina na uwongo wa kidini. (Yohana 8:32) Kwa maelfu ya wazao wa Waazteki, Biblia hutoa tumaini pekee la kweli la kuokoka.
[Maelezo ya Chini]
a Neno “Mesoamerica” larejezea eneo “linaloanzia kusini na mashariki kutoka sehemu ya kati ya Mexico likitia ndani sehemu fulani za Guatemala, Belize, Honduras, na Nikaragua.” (The American Heritage Dictionary) Ustaarabu wa Mesoamerica warejezea “utata wa tamaduni za wenyeji wa Australia ambazo zilisitawi katika sehemu fulani za Mexico na Amerika ya Kati kabla ya uvumbuzi na ushindi wa Wahispania katika karne ya 16.”—Encyclopaedia Britannica.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]
“MIMI HUFURAHIA KUSHIRIKI KWELI NA WATU WA NAHUATL”
NILIZALIWA Mexico katika kijiji kidogo kinachoitwa Santa María Tecuanulco, kilometa 60 tu kutoka Mexico City. Ni mahali pazuri, penye miti palipo juu ya vilima, ambapo watu hujiruzuku kwa kupanda maua. Maua yanapokuwa tayari kuchumwa, inapendeza kuona rangi nyingi kila mahali. Kila mtu katika Santa María alikuwa akinena lugha ya Nahuatl, lugha ya kale ya Wameksika. Ninakumbuka kwamba kila nyumba katika Nahuatl ilikuwa na jina la kuitambulisha. Jina la nyumba yangu lilikuwa Achichacpa, linalomaanisha “Mahali Panapotiririka Maji.” Ili kueleza watu mahali nilipoishi, ningewaambia majina ya nyumba zinazozingira nyumba yangu. Hata leo, nyumba nyingi zina jina. Nilijifunza Kihispania mwaka wa 1969, nikiwa na umri wa miaka 17. Nafikiri lugha ya Nahuatl ni nzuri. Kwa kusikitisha, ni wazee-wazee tu wa kijiji ambao huizungumza; vijana wa leo hawaijui kabisa.
Katika kijiji chetu ni mimi tu niliyekuwa nikijifunza na Mashahidi wa Yehova. Kwa ghafula, kijiji chote kilinitaka nihame pamoja na watoto wangu. Nilisongwa kutoa michango ya kawaida kwa Kanisa Katoliki, jambo ambalo nilikataa. Jamaa zangu hata hawangeongea nami. Kujapokuwa upinzani mkali katika kijiji chetu, nilibatizwa mnamo Desemba 1988. Ninamshukuru Yehova kwamba binti zangu watatu wanatumikia wakiwa waeneza-evanjeli wa wakati wote na kwamba mwanangu ni Mkristo aliyebatizwa. Mimi hufurahia kushiriki habari njema katika Santa María. Mimi huhubiria watu wenye umri mkubwa zaidi katika Nahuatl. Nimeazimia kuendelea kumtumikia Mungu wetu mwenye upendo, Yehova, ambaye huhurumia watu wa jamii zote.—Imechangwa.
[Grafu katika ukurasa wa 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KRONOLOJIA LINGANISHI YA BAADHI YA TAMADUNI NA MATUKIO MAKUU KATIKA AMERIKA NA ULIMWENGU
KUTOKA 1200 K.W.K. HADI 1550 W.K.
SPANISH INQUISITION
1500 W.K.
EUROPEAN RENAISSANCE
AZTEC
“CHRISTIAN” CRUSADES
TOLTEC
1000 W.K.
BYZANTINE
500 W.K.
TEOTI-HUACÁN
EARLY CHRISTIANITY
ROMAN
ZAPOTEC
GREEK
EGYPTIAN
500 K.W.K.
MAYA
OLMEC ASSYRIAN
1000 K.W.K.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 18]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UKUBWA WA MILKI YA AZTEKI
MEXICO
Tenochtitlán
GUATEMALA
[Picha]
Jiji kuu lililojulikana kuwa Tenochtitlán limezikwa chini ya Mexico City ya kisasa
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright© 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kalenda ya Azteki
[Picha katika ukurasa wa 19]
Waazteki walitumia Piramidi ya Jua ya Teotihuacán kwa ajili ya ibada yao
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Picha ya ukutani kwenye ukurasa wa 15 na 16: “Mexico Through the Centuries,” original work by Diego Rivera. National Palace, Mexico City, Mexico
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Tai na sanaa kwenye ukurasa wa 18: “Mexico Through the Centuries,” original work by Diego Rivera. National Palace, Mexico City, Mexico