Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 6/22 kur. 3-5
  • Je, Kweli Ulimwengu Ulikuwa na Mwanzo?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Kweli Ulimwengu Ulikuwa na Mwanzo?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uthibitisho wa Kuwapo kwa Mwanzo
  • Matokeo ya Uthibitisho Huo
  • Ulimwengu Uliojaa Maajabu
    Amkeni!—2009
  • Ulimwengu Wetu Wenye Kustaajabisha—Je, Ulitokea kwa Nasibu?
    Amkeni!—2000
  • Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi Uliopo
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
  • Kile Ambacho Nadharia ya Mshindo Mkubwa Hueleza—Na Kile Ambacho Haielezi
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 6/22 kur. 3-5

Je, Kweli Ulimwengu Ulikuwa na Mwanzo?

MUDA wote ambao umepita, watu wengi wametazama kwa kustaajabu anga jangavu la usiku lililotapakaa nyota. Ukubwa wa ulimwengu wetu wa ajabu na umaridadi wake wenye kushangaza wastaajabisha mno. Ni nini au ni nani awezaye kuwa aliuanzisha? Kwa nini ulimwengu upo? Je, ulimwengu umekuwapo daima, au ulikuwa na mwanzo?

Profesa wa mambo ya nyota David L. Block aliandika hivi: “Jambo la kwamba kuna wakati ulimwengu haukuwapo—yaani kwamba ulikuwa na mwanzo—sikuzote halijawapendeza wengi.” Hata hivyo, katika miongo ya karibuni uthibitisho ambao umepatikana umewalazimisha wengi wanaochunguza ulimwengu waamini kwamba kwa kweli ulimwengu ulikuwa na mwanzo. Mwaka wa 1997 gazeti U.S.News & World Report liliripoti kwamba “karibu wataalamu wote wa fizikia ya anga leo hufikia uamuzi wa kwamba ulimwengu ulianza kwa mlipuko mkubwa ambao ulirusha vitu kuelekea pande zote.”

Kuhusu uamuzi huo ambao unakubaliwa na wengi, Robert Jastrow, ambaye ni profesa wa mambo ya nyota na miamba katika Chuo Kikuu cha Columbia, aliandika hivi: “Ni wataalamu wachache wa nyota ambao wangeweza kutarajia kwamba tukio hili—kuzaliwa kwa ghafula kwa Ulimwengu—lingethibitishwa kisayansi, lakini kutazama mbingu kupitia darubini kumewalazimisha wafikie uamuzi huo.”

Je, huko “kuzaliwa kwa ghafula kwa Ulimwengu” kweli ‘kumethibitishwa kisayansi’? Ebu tuchunguze uthibitisho wa kihistoria ambao umetokeza uamuzi huo.

Uthibitisho wa Kuwapo kwa Mwanzo

Nadharia ya ujumla wa uwiano ya Albert Einstein, iliyochapishwa mwaka wa 1916, ilidokeza kwamba ama ulimwengu unapanuka ama unapunguka. Lakini, wazo hilo lilitofautiana kabisa na wazo lililokubaliwa wakati huo la kwamba ulimwengu haupanuki wala haupunguki, jambo ambalo hata Einstein mwenyewe aliamini wakati huo. Basi akatia kwenye hesabu zake kitu ambacho alikiita “kutobadilika kwa ulimwengu.” Alifanya rekebisho hili ili ajaribu kupatanisha nadharia yake na ile itikadi iliyokubaliwa ya kwamba ulimwengu haupanuki wala haupunguki.

Lakini uthibitisho mwingi uliopatikana katika miaka ya 1920 ulisababisha Einstein aseme kwamba hilo rekebisho ambalo alikuwa amefanya kwenye ile nadharia yake ya ujumla wa uwiano lilikuwa ‘kosa kubwa zaidi’ ambalo amewahi kufanya. Darubini kubwa sana yenye sentimeta 254 iliyowekwa kwenye Mlima Wilson kule California ilifanya iwezekane kupata uthibitisho huo. Mambo yaliyoonwa kupitia darubini hiyo katika miaka ya 1920 yalithibitisha kwamba ulimwengu unapanuka!

Awali, darubini kubwa zaidi zingeweza kutambulisha nyota moja-moja zilizokuwa katika kundi letu la nyota la Kilimia pekee. Ni kweli kwamba watazamaji wameona madoa ya nuru hafifu yanayoitwa nebula, lakini kwa ujumla madoa hayo yalidhaniwa kuwa mawingu ya gesi fulani katika kundi letu lenyewe la nyota. Lakini kwa kutumia darubini hiyo kali sana ya Mlima Wilson, Edwin Hubble alitambulisha nyota moja-moja katika nebula hizo. Madoa hayo ya nuru hafifu hatimaye yalitambulishwa kuwa makundi ya nyota kama tu Kilimia yetu. Sasa inakadiriwa kwamba kuna makundi ya nyota baina ya bilioni 50 na bilioni 125, kila kundi la nyota likiwa na mamia ya mabilioni ya nyota!

Mnamo mwaka wa 1929, Hubble aligundua pia kwamba makundi hayo ya nyota yanazidi kwenda mbali nasi na kwamba kadiri yazidivyo kwenda mbali ndivyo yazidivyo kuongeza mwendo zaidi. Wataalamu wa nyota hupata kujua mwendo wa makundi ya nyota yanapoenda mbali nasi kupitia chombo kinachoitwa spectrograph, ambacho hupima mpangilio wa nuru inayotoka kwenye nyota za angani. Nuru inayotoka kwenye nyota za mbali huingizwa kwenye mche ambao hutawanya rangi mbalimbali za nuru.

Nuru inayotoka kwenye kitu kinachozidi kwenda mbali na mtazamaji ina rangi ya nyekundu-nyekundu. Kwa upande mwingine, nuru inayotoka kwenye kitu kinachomwelekea mtazamaji ina rangi ya samawati. Basi, tofauti na makundi machache ya nyota yaliyo karibu, makundi yote ya nyota yajulikanayo huonyesha mistari yenye rangi nyekundu katika mpangilio wa nuru. Basi wanasayansi wathibitisha kwamba ulimwengu unapanuka kwa utaratibu fulani. Kiwango cha upanuzi huo hujulikana kwa kupima kadiri mistari ilivyo myekundu katika mpangilio wa nuru.

Ni uamuzi gani ambao umefanywa kutokana na jambo la kwamba ulimwengu unapanuka? Mwanasayansi mmoja aliwaomba watu wafikirie utaratibu huo unapoenda kinyume. Yaani, wafikirie akilini ulimwengu unaopanuka ukionyeshwa kinyume ili mtazamaji aone historia ya awali ya ulimwengu. Ulimwengu ukitazamwa kwa njia hiyo, ungeonekana ukipunguka, badala ya kupanuka. Hatimaye ulimwengu ungerudi kwenye hatua moja ya mwanzo.

Katika kitabu chake Black Holes and Baby Universes and Other Essays, kilichochapishwa mwaka wa 1993, mwanafizikia mashuhuri Stephen Hawking alifikia uamuzi wa kwamba “sayansi ingeweza kutabiri kwamba ni lazima ulimwengu ulikuwa na mwanzo.”

Lakini, miaka michache iliyopita, wengi hawakuamini kwamba ulimwengu ulikuwa na mwanzo. Fred Hoyle alikuwa mwanasayansi mashuhuri ambaye alipinga wazo la kwamba ulimwengu ulitokea kupitia kile alichokiita kwa dhihaka ‘mlipuko mkubwa.’ Miongoni mwa mambo mengine, Hoyle alibisha kwamba kama kungalikuwa na mwanzo wenye nguvu hivyo, masalio ya tukio hilo yangalikuwako mahali fulani katika ulimwengu. Mnururisho wa masalio unapaswa kuwako, yaani mng’ao fulani wa baadaye ulio hafifu angani. Kutafuta mnururisho wa baadaye kama huo kulifunua nini?

Gazeti la The New York Times la Machi 8, 1998, liliripoti kwamba mnamo mwaka wa 1965 “wataalamu wa nyota Arno Penzias na Robert Wilson waligundua kuwapo kotekote kwa huo mnururisho wa baadaye, mng’ao uliobaki wa mlipuko wa kwanza.” Makala hiyo iliongezea kusema: “Ikaonekana kwamba nadharia ya [mlipuko mkubwa] ilikuwa imethibitishwa kabisa.”

Lakini katika miaka iliyofuata ugunduzi wa Penzias na Wilson, watu wengine walizusha swali kwamba ikiwa ni kweli kwamba kiolezo cha ule mlipuko mkubwa kilikuwa sahihi, kwa nini ishara za mnururisho hazikuonyesha mvurugo kidogo? Ili makundi ya nyota yafanyizwe, ulimwengu ungehitaji maeneo baridi na mazito ambapo mata ingefanyizwa. Lakini majaribio ambayo Penzias na Wilson walifanya kwenye uso wa dunia hayakufunua mvurugo kama huo.

Basi, mnamo Novemba 1989 shirika la National Aeronautics and Space Administration la Marekani lilirusha katika anga za nje setilaiti iitwayo Cosmic Background Explorer (COBE). Ikafanya magunduzi ya ajabu sana. Profesa Block alieleza: “Mawimbi yaliyoripotiwa na Mita ya Kupima Mawimbi Madogo-Madogo (Differential Microwave Radiometer) iliyokuwa kwenye COBE ndiyo yaleyale ambayo yamekuwapo katika ulimwengu wetu na yaliyoanzisha makundi ya nyota mabilioni ya miaka iliyopita.”

Matokeo ya Uthibitisho Huo

Tunaweza kujifunza nini kutokana na jambo la kwamba ulimwengu ulikuwa na mwanzo? Robert Jastrow alisema: “Unaweza kuuita mlipuko mkubwa, lakini vilevile unaweza kuuita kwa usahihi zaidi hatua ya uumbaji.” Penzias, ambaye alishiriki kugundua mnururisho uliotokea baada ya mlipuko katika ulimwengu, alisema: “Utaalamu wa nyota hutuonyesha tukio la kipekee, ulimwengu ulioumbwa pasipo kitu.” Na kiongozi wa COBE George Smoot alisema: “Tumepata uthibitisho wa kwamba ulimwengu ulikuwa na mwanzo.”

Je, si jambo linalopatana na akili kufikia uamuzi wa kwamba kama ulimwengu ulikuwa na mwanzo, au uliumbwa, basi kulikuwa na Mwanzilishi, au Muumba, wa ulimwengu huo? Wengi wanafikiri hivyo. Smoot alitangaza hivi baada ya ugunduzi uliofanywa na COBE: “Ni kama kumtazama Mungu.”

Bila shaka, bila uthibitisho wa kisayansi ambao umepata kujulikana katika miongo ya karibuni, mamilioni ya watu wameweka imani kwenye taarifa ya kwanza ya Biblia: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.”—Mwanzo 1:1.

Lakini si watu wote wanaokubaliana na taarifa hiyo sahili katika Biblia. “Wanasayansi wengi hawakupenda wazo la kwamba ulimwengu ulikuwa na mwanzo, kwamba uliumbwa,” akasema Stephen Hawking ambaye ni mwanafizikia. “Hawakupenda ufafanuzi wa ziada usio wa kisayansi wa nadharia hiyo,” Michael J. Behe akaandika, “nao wakang’ang’ana kutafuta nadharia nyinginezo.”

Basi maswali ni kama yafuatavyo, Je, ulimwengu ulitokea wenyewe tu? Je, ulitokea kwa nasibu, au uliumbwa na Muumba mwenye akili? Uthibitisho ufuatao ni wenye kuelimisha sana.

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Darubini ya Mlima Wilson ilisaidia kuonyesha kwamba ulimwengu wetu ulikuwa na mwanzo

[Hisani]

The Observatories of the Carnegie Institution of Washington

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki