Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • ct sura 2 kur. 10-25
  • Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi Uliopo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi Uliopo
  • Je, Kuna Muumba Anayekujali?
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uthibitisho Unaoonyesha Kulikuwa na Mwanzo
  • Majaribio ya Kueleza Jinsi Ulimwengu Ulivyoanza
  • Vipimo Sahihi Kabisa
  • Kani Mbili za Nyuklia
  • Hali za Dunia Zenye Kufaa Sana
  • Sheria na Utaratibu
  • Ulimwengu Wetu Wenye Kustaajabisha—Je, Ulitokea kwa Nasibu?
    Amkeni!—2000
  • Ulimwengu Unatufundisha Nini?
    Amkeni!—2021
  • Je, Kweli Ulimwengu Ulikuwa na Mwanzo?
    Amkeni!—1999
  • Ulimwengu Uliojaa Maajabu
    Amkeni!—2009
Pata Habari Zaidi
Je, Kuna Muumba Anayekujali?
ct sura 2 kur. 10-25

Sura Ya Pili

Ulimwengu Wetu Ulitokeaje?—Ubishi Uliopo

WATAALAMU wa anga hufurahia sana kupiga dunia picha wanapoiona ikiwa kubwa kupitia dirisha la chombo cha angani. “Huo ndio mwono bora zaidi unapokuwa angani,” akasema mmoja wao. Lakini dunia yetu huonekana kuwa ndogo sana ilinganishwapo na mfumo wa jua na sayari zake. Dunia zipatazo milioni moja zinaweza kutoshea ndani ya jua, na bado nafasi ibaki! Lakini, je, mambo hayo juu ya ulimwengu yanahusu maisha yako na maana yake?

Ebu tuelekeze uangalifu wetu kifupi katika anga na kuona uhusiano uliopo kati ya dunia na jua. Jua letu ni mojawapo tu ya nyota nyingi sana zenye kutazamisha zilizo sehemu ya kundi la nyota linaloitwa Kilimia (Milky Way),a ambalo nalo ni sehemu ndogo sana ya ulimwengu. Kwa macho, inawezekana kuona madoa machache ya nuru ambayo kumbe ni makundi mengineyo ya nyota, kama vile kundi kubwa la nyota lililo maridadi linaloitwa Andromeda. Kilimia, Andromeda, na makundi mengine yapatayo 20 ya nyota, yameshikamanishwa pamoja kwa nguvu za uvutano na kufanyiza fungu la makundi ya nyota, yote hayo yakiwa sehemu ndogo tu ya mkusanyo mkubwa wa mafungu ya makundi ya nyota. Ulimwengu una mikusanyo mingi sana kama hiyo, na mambo bado.

Mafungu ya makundi ya nyota hayana mpangilio wenye utaratibu angani. Yakipanuliwa, yanafanana na tando nyembamba na mapovu makubwa yaliyo matupu yenye nyuzinyuzi zinazotokezea pande zote. Makundi mengineyo ya nyota ni marefu na mapana sana hivi kwamba yanafanana na kuta kubwa sana. Huenda hilo likashangaza wengi wanaofikiri kwamba ulimwengu ulijitokeza wenyewe tu katika mlipuko mkubwa. “Kadiri tuwezavyo kuona kwa uwazi zaidi ulimwengu ukiwa na mambo mengi matukufu,” akata kauli mwandishi mmoja mkuu wa Scientific American, “ndivyo inavyozidi kuwa vigumu kueleza kirahisi tu jinsi ulimwengu ulivyopata kuwa hivyo.”

Uthibitisho Unaoonyesha Kulikuwa na Mwanzo

Nyota zote unazoweza kuona ziko katika Kilimia. Kufikia miaka ya 1920, watu walidhani kwamba hakukuwa na kundi jingine la nyota ila hilo tu. Ingawa hivyo, labda unajua kwamba uchunguzi uliofanywa na darubini kubwa umethibitisha kwamba hiyo si kweli. Ulimwengu wetu una angalau makundi 50,000,000,000 ya nyota. Hatumaanishi nyota bilioni 50—lakini angalau makundi bilioni 50 ya nyota, na kila kundi lina mabilioni ya nyota zinazofanana na jua letu. Lakini, si wingi huo wa makundi makubwa-makubwa ya nyota uliowashtua wanasayansi katika miaka ya 1920. Jambo lililowashtua ni kwamba makundi hayo yote yako mwendoni.

Wataalamu wa nyota waligundua jambo moja lenye kutokeza sana: Nuru inayotoka kwenye kundi la nyota ilipopitishwa kwenye kipande cha glasi kinachotawanya nuru, mawimbi ya nuru yalionekana yakiwa yamerefuka, ikionyesha kwamba makundi ya nyota yaliyo mbali na dunia yalikuwa katika mwendo wa kasi sana. Kadiri kundi la nyota lilivyokuwa mbali zaidi, ndivyo lilivyoonekana kwenda kasi sana mbali na dunia. Hilo ladokeza kwamba ulimwengu unapanuka!b

Hata kama sisi si wataalamu wa nyota wala wapenzi wa mambo ya nyota, twaweza kuona kwamba upanuzi wa ulimwengu unaweza kuashiria mambo mengi sana kuhusu wakati wetu uliopita—na labda wakati wetu ujao vilevile. Ni lazima kitu fulani kilianzisha upanuzi wa ulimwengu—kitu chenye uwezo sana kuliko nguvu nyingi za uvutano za ulimwengu. Mtu anakuwa na sababu nzuri ya kuuliza, ‘Ni nini kingeweza kusababisha nguvu nyingi sana hivyo?’

Ingawa wanasayansi wengi husema ulimwengu ulianza ukiwa kitu kidogo sana ambacho kilifinyana sana, hatuwezi kuepuka suala hili kuu: “Ikiwa wakati fulani uliopita, Ulimwengu ulikuwa kitu kidogo sana kisichoweza kuwazika na chenye uzito usioweza kuwazika, ni lazima tuulize ni nini kilichokuwapo hapo awali na nini kilichokuwapo nje ya Ulimwengu. . . . Ni lazima tukabili suala la kuwapo kwa Chanzo fulani.”—Sir Bernard Lovell.

Hili ladokeza zaidi ya kuwapo tu kwa chanzo cha nishati nyingi. Busara na akili pia zinahitajiwa kwa sababu kiwango cha upanuzi wa ulimwengu chaonekana kuwa kimepimwa barabara kabisa. “Ikiwa kiwango cha upanuzi wa Ulimwengu kingeongezeka hata kwa kiasi cha sehemu moja tu ya milioni moja mara milioni moja,” asema Lovell, “basi kufikia sasa kila kitu kilichomo Ulimwenguni kingekuwa kimetawanyika. . . . Na ikiwa kiwango hicho kingalipungua hata kwa kiasi cha sehemu moja tu ya milioni moja mara milioni moja, basi nguvu za uvutano zingalisababisha Ulimwengu uporomoke miaka ipatayo milioni elfu moja ya kwanza. Hapa tena twaona ya kwamba hakungekuwa na nyota zenye kudumu na basi hakungekuwa na uhai.”

Majaribio ya Kueleza Jinsi Ulimwengu Ulivyoanza

Je, sasa wataalamu wanaweza kueleza jinsi ulimwengu ulivyoanza? Kwa sababu ya kuona ugumu wa kukubali wazo la kwamba ulimwengu uliumbwa na mtu mwenye akili zaidi, wanasayansi wengi hukisia-kisia kwamba kwa njia fulani ulimwengu ulijiumba wenyewe. Je, unaona kama wazo hilo lafaa? Makisio kama hayo mara nyingi huhusisha tofauti ndogo-ndogo za nadharia (ya kupanuka kwa ulimwengu)c iliyotungwa mnamo 1979 na mtaalamu wa fizikia Alan Guth. Lakini, hivi majuzi zaidi, Dakt. Guth alikiri kwamba nadharia yake “haifafanui jinsi ulimwengu ulivyotokea pasipo kitu.” Dakt. Andrei Linde alisema wazi zaidi katika makala moja iliyokuwa katika Scientific American: “Kufafanua ile hali ya awali ya ulimwengu kutokana na kitu kidogo sana—kutia ndani mahali ulipoanza na wakati ulipoanza—bado ni tatizo gumu zaidi katika elimu ya anga.”

Ikiwa wataalamu hawawezi kueleza juu ya chanzo cha ulimwengu au ukuzi wake wa awali, je, hatupaswi kutafuta jibu mahali pengine? Kwa hakika, wewe una sababu nzuri za kufikiria uthibitisho mwingine ambao wengi wamepuuza lakini ambao unaweza kukupa ufahamu wa ndani juu ya suala la chanzo cha ulimwengu. Uthibitisho huo watia ndani vipimo sahihi kabisa vya kani nne za msingi ambazo zinaathiri vitu vyote na mabadiliko yote katika ulimwengu. Kwa kutaja tu kani za msingi, huenda wengine wakasita, wakifikiri, ‘Hiyo inahusu wataalamu wa fizikia pekee.’ La hasha. Inafaa kuchunguza mambo ya msingi kwa sababu hayo yanatuhusu.

Vipimo Sahihi Kabisa

Kani nne za msingi zinahusika katika ulimwengu wote na katika vitu vidogo sana vya atomu. Ndiyo, kila kitu tuonacho kinahusika.

Elementi zilizo muhimu kwa uhai wetu (hasa kaboni, oksijeni, na chuma) hazingekuwapo kama si vipimo sahihi kabisa vya zile kani nne za msingi ambazo kwa wazi zimo katika ulimwengu. Tayari tumetaja kani moja, ile nguvu ya uvutano. Nyingine ni kani ya sumaku-umeme. Kama kani ya sumaku-umeme ingalikuwa dhaifu kidogo tu, elektroni hazingaliweza kukusanywa kuzunguka kiini (nyuklia) cha atomu. ‘Je, hilo lingetokeza tatizo zito?’ huenda wengine wakauliza. Ndiyo, kwa sababu atomu hazingaliweza kujikusanya ili kufanyiza molekuli. Kwa upande mwingine, kama kani ya sumaku-umeme ingalikuwa yenye nguvu zaidi, elektroni zingenaswa katika kiini cha atomu. Hakungalikuwa na utendaji wowote kati ya atomu mbalimbali—jambo linalomaanisha kwamba hakungekuwa na uhai. Hata kutokana na hali hii, ni wazi kwamba uhai wetu wategemea kipimo sahihi kabisa cha nguvu za sumaku-umeme.

Na ebu fikiria ukubwa wa ulimwengu: Tofauti ndogo tu katika kani za sumaku-umeme ingehusisha jua na hivyo kuathiri nuru inayofikia dunia, jambo ambalo lingefanya iwe vigumu sana au hata isiwezekane kwa usanidimwanga (njia ya mimea kujifanyizia chakula). Pia ingenyang’anya maji vitu vyake muhimu, ambavyo ni muhimu kwa uhai. Basi tena, kipimo sahihi kabisa cha kani za sumaku-umeme huamua kama tutaishi au hatutaishi.

Jambo muhimu sana pia ni kadiri ya kani za sumaku-umeme kwa kulinganisha na zile kani nyinginezo tatu. Kwa kielelezo, wataalamu fulani wa fizikia wanaona kani hiyo kuwa nyingi kuliko nguvu ya uvutano mara 10,000,000,000,000,000,000,000,000,000,000,000,- 000,000 (yaani nambari 1 inayofuatwa na sufuri 40). Inaweza kuonekana kuwa badiliko dogo kuongeza sufuri moja tu kwenye tarakimu hiyo (iwe nambari 1 inayofuatwa na sufuri 41). Lakini, hiyo ingemaanisha kwamba nguvu za uvutano zinakuwa dhaifu kwa kulinganisha, na Dakt. Reinhard Breuer aeleza juu ya hali iwezayo kutokea: “Nguvu za uvutano zikipungua basi nyota zingekuwa ndogo, na msongo wa nguvu za uvutano ndani ya nyota haungetokeza joto la kuweza kuwasha utendaji wa nyuklia: hilo lingefanya jua lishindwe kuangaza.” Unaweza kuwazia jinsi ambavyo tungeathiriwa!

Namna gani ikiwa kani za uvutano zingekuwa zenye nguvu zaidi kwa kulinganisha, ili ile tarakimu iwe na sufuri 39 pekee? “Kwa rekebisho hilo dogo tu,” aendelea kusema Breuer, “nyota iliyo kama jua ingekuwa na maisha mafupi sana.” Na wanasayansi wengine hufikiria kwamba vile vipimo sahihi kabisa vya zile kani nne ni sahihi hata zaidi ya vile ambavyo tumeona.

Kwa kweli, sifa mbili zenye kutokeza za jua letu na nyota nyinginezo ni kwamba hizo ni thabiti na zina uwezo wa kutenda daima. Ebu fikiria mfano rahisi. Twajua kwamba ili injini ya gari ifanye kazi vizuri, inahitaji usawaziko mzuri wa mchanganyiko wa mafuta na hewa; wahandisi hufanyiza mifumo tata ya kiufundi na ya kompyuta ili injini iweze kufanya vizuri. Ikiwa ndivyo ilivyo na injini tu, namna gani nyota “zenye kuwaka” kwa njia bora kama vile jua letu? Zile kani kuu zinazohusika zimepimwa kwa usahihi kabisa, zikifanya kazi kwa njia bora zaidi ili kuendeleza uhai. Je, vipimo hivyo vilivyo sahihi kabisa vilitokea vyenyewe tu? Yule mtu wa kale Yobu aliulizwa: “Je, ulizitangaza kanuni zinazoongoza mbingu, au kujua sheria za asili zilizo duniani?” (Ayubu 38:33, The New English Bible) Hakuna mwanadamu aliyepata kufanya hivyo. Basi ni nani aliyeweka hivyo vipimo vilivyo sahihi kabisa?

Kani Mbili za Nyuklia

Muundo wa ulimwengu wahusisha mengi zaidi ya vipimo sahihi kabisa vya nguvu za uvutano na kani za sumaku-umeme. Kani nyinginezo mbili zinahusika na uhai wetu.

Kani hizo mbili zinatenda katika kiini cha atomu, nazo huonyesha kwamba ziliwekwa hapo na mtu mwenye kufikiri. Fikiria kani ya nyuklia yenye nguvu, ambayo hushikanisha protoni na nutroni pamoja katika kiini cha atomu. Kwa sababu ya mshikano huo, elementi kadhaa zaweza kufanyizwa—zile nyepesi (kama vile heli na oksijeni) na zile nzito (kama vile dhahabu na risasi). Inaonekana kwamba kama nguvu hiyo yenye kushikanisha ingekuwa dhaifu kwa asilimia 2 tu, ni hidrojeni pekee ambayo ingekuwako. Kwa upande mwingine, kama hii kani ingeongeza nguvu kidogo tu, ni zile elementi nzito pekee ambazo zingekuwako, lakini hidrojeni haingepatikana. Je, uhai wetu ungeathiriwa? Naam, kama ulimwengu ungekosa hidrojeni, jua letu halingepata kitu ambacho linahitaji ili kuwaka na kuendeleza uhai. Na, bila shaka, hatungekuwa na maji wala chakula, kwa kuwa hidrojeni ni sehemu muhimu ya maji na chakula.

Kani ya nne katika mazungumzo haya, inayoitwa kani dhaifu ya nyuklia, hupunguza atomu za vitu vyenye mnururisho. Pia inahusika na utendaji katika jua letu. ‘Je, kani hiyo imepimwa kwa usahihi kabisa?’ huenda ukauliza. Mtaalamu wa hesabu aliye pia mtaalamu wa fizikia Freeman Dyson aeleza: “Ile [kani] dhaifu ni dhaifu mara mamilioni kuliko nguvu za nyuklia. Ni dhaifu kiasi tu cha kuwezesha hidrojeni iliyo katika jua ichomeke polepole kwa kiwango kilekile. Kama hii [kani] dhaifu ingekuwa na nguvu zaidi au kuwa dhaifu zaidi ya ilivyo, aina yoyote ya uhai inayotegemea nyota zilizo kama jua zingepata matatizo.” Ndiyo, kiwango kifaacho kabisa cha kuchomeka hudumisha dunia yetu ikiwa na joto—lakini bila kuteketea—na kuendeleza uhai wetu.

Isitoshe, wanasayansi huamini kwamba ile kani dhaifu huchangia ile milipuko mikubwa sana ya nyota, ambayo kulingana na wanasayansi ni utaratibu wa kutokeza na kusambaza elementi nyingi. “Kama kani hizo za nyuklia zingalikuwa tofauti kidogo na jinsi zilivyo hasa, nyota hazingaliweza kutengeneza elementi ambazo zimekufanyiza wewe na mimi,” aeleza mtaalamu wa fizikia John Polkinghorne.

Mengi zaidi yaweza kusemwa, lakini yaelekea unaelewa jambo kuu. Zile kani nne za msingi zimepimwa kwa usahihi kabisa kwa njia ya kustaajabisha sana. “Kotekote, yaonekana twaona uthibitisho wa kwamba asili ilijua kufanya mambo kwa usahihi kabisa,” akaandika Profesa Paul Davies. Ndiyo, vipimo sahihi kabisa vya zile kani nne za msingi vimefanya iwezekane kuwako kwa jua letu na utendaji wake, kuwako kwa dunia yetu ikiwa na maji yake yenye kuendeleza uhai, anga letu ambalo ni muhimu sana kwa uhai, na vitu vingi vya kemikali vyenye thamani duniani. Lakini, ebu jiulize, ‘Kwa nini kukawa na vipimo hivyo vilivyo sahihi kabisa, navyo vilipimwa na nani?’

Hali za Dunia Zenye Kufaa Sana

Mambo mengine yaliyopimwa kwa usahihi kabisa yanahitajiwa ili tuweze kuishi. Ebu fikiria vipimo vya dunia na mahali ilipo kwa kulinganisha na mfumo wetu wa jua na sayari zake. Kitabu cha Biblia cha Ayubu chauliza maswali haya yenye kunyenyekeza: “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? . . . Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua?” (Ayubu 38:4, 5) Maswali hayo yanataka jibu wakati huu kuliko wakati mwingine wowote. Kwa nini? Kwa sababu ya mambo ya ajabu ambayo yamegunduliwa kuhusu dunia yetu—kutia ndani ukubwa wake na mahali ilipo katika mfumo wetu wa jua.

Hakuna sayari iliyo kama dunia yetu ambayo imewahi kupatikana mahali pengine popote katika ulimwengu. Ni kweli kwamba wanasayansi fulani huelekezea uthibitisho usio wa moja kwa moja kwamba nyota fulani zinazungukwa na vitu ambavyo ni vikubwa kuliko dunia yetu kwa mamia ya mara. Ingawa hivyo, dunia yetu ina ukubwa ufaao kabisa maisha yetu. Kwa maana gani? Ikiwa dunia ingalikuwa kubwa kidogo tu, nguvu yake ya uvutano ingalikuwa nyingi zaidi na hiyo ingefanya hidrojeni, ambayo ni hewa nyepesi, ijikusanye, ikinaswa na uvutano wa dunia. Kwa hiyo, angahewa halingeweza kudumisha uhai. Kwa upande mwingine, ikiwa dunia yetu ingalikuwa ndogo kidogo tu, oksijeni yenye kudumisha uhai ingeponyoka na maji yote yangekuwa mvuke. Katika hali hizo zote mbili, hatungeweza kuishi.

Pia, dunia ipo umbali ufaao zaidi kutoka kwenye jua, jambo ambalo ni muhimu kwa uhai kusitawi. Mtaalamu wa nyota John Barrow na mtaalamu wa hesabu Frank Tipler walichunguza “ulinganisho wa nusu-kipenyo ya Dunia na umbali kutoka kwenye Jua.” Wao walikata kauli kwamba wanadamu hawangeweza kuishi “iwapo ulinganisho huo ungekuwa tofauti kidogo na jinsi ulivyo sasa.” Profesa David L. Block asema: “Hesabu inaonyesha kwamba kama dunia ingalikuwa karibu na jua kwa asilimia 5 tu, joto jingi kupita kiasi lingetukia miaka milioni 4 000 iliyopita. Ikiwa, kwa upande mwingine, dunia ingalikuwa mbali zaidi na jua kwa asilimia 1 tu, barafu nyingi zingalifunika dunia miaka ipatayo milioni 2 000 iliyopita.”—Our Universe: Accident or Design?

Kwa kuongezea usahihi huo, unaweza kuongezea jambo la kwamba dunia huzunguka kwenye mhimili wake mara moja kwa siku, kwa mwendo ufaao ili kutokeza hali-joto za kiasi. Sayari ya Zuhura huchukua siku 243 ili kuzunguka kwenye mhimili wake. Ebu wazia kama dunia ingalichukua muda mrefu hivyo kuzunguka! Hatungeweza kuokoka joto kali sana na baridi kali sana ambazo zingetokana na siku ndefu sana na usiku mrefu sana.

Jambo jingine dogo lililo muhimu ni njia ya dunia yetu kulizunguka jua. Nyota-mkia zina njia pana zenye umbo la yai. Kwa uzuri, sivyo ilivyo na dunia. Mzunguko wake ni karibu uwe duara kabisa. Tena hii inatuzuia tusipatwe na joto kali sana au baridi kali sana.

Wala hatupaswi kupuuza mahali ulipo mfumo wetu wa jua. Kama ungalikuwa karibu na kitovu cha kundi letu la nyota la Kilimia, nguvu za uvutano za nyota zilizo karibu zingeathiri mzunguko wa dunia. Kwa kutofautisha, kama ungalikuwa ukingoni kabisa mwa kundi letu la nyota, anga la usiku halingekuwa na nyota zozote. Nuru ya nyota si muhimu kwa uhai, lakini je, hiyo haiongezei umaridadi kwenye anga letu la usiku? Na kwa kutegemea mawazo ya wakati huu juu ya ulimwengu, wanasayansi wamepima kwamba katika kingo za Kilimia, hakungekuwa na elementi za kemikali za kutosha kufanyiza mfumo wa jua na sayari zake kama wetu.d

Sheria na Utaratibu

Kulingana na jinsi ambavyo wewe mwenyewe umejionea mambo, yaelekea unajua ya kwamba vitu vyote huelekea kuharibika. Karibu kila mwenye nyumba amepata kuona kwamba vitu huelekea kuharibika vikiachwa bila kutumiwa. Wanasayansi huuita mwelekeo huu “athari ya joto.” Tunaweza kuona athari hii kila siku. Gari jipya au baiskeli mpya ambayo imeachwa bila kutumiwa itakuwa bure. Jengo likiachwa bila kukaliwa litakuwa magofu. Namna gani kuhusu ulimwengu? Sheria hiyo inatumika vilevile. Basi huenda ukafikiri kwamba ule utaratibu ulio katika ulimwengu hatimaye unapaswa kuharibika kabisa.

Lakini, ulimwengu hauonekani kama unaharibika, kama Profesa wa Hesabu Roger Penrose alivyovumbua alipochunguza ikiwa ulimwengu uonekanao ulikuwa ukiharibika. Njia bora ya kufasili magunduzi hayo ni kukata kauli kwamba ulimwengu ulianza ukiwa katika utaratibu mzuri nao umebaki hivyo. Mtaalamu wa fizikia ya nyota Alan Lightman alisema kwamba wanasayansi “wanashangaa kwamba ulimwengu uliumbwa ukiwa na utaratibu wa juu sana.” Yeye aliongezea kwamba “nadharia yoyote yenye mafanikio juu ya ulimwengu yapaswa hatimaye yafafanue hali ya dunia ya kutoharibika”—yaani kwa nini ulimwengu haujavurugika.

Kwa hakika, jambo la kwamba twaishi laonyesha kwamba ulimwengu wetu hauvurugiki. Basi, kwa nini sisi tuko hai hapa duniani? Kama ilivyotajwa hapo awali, hilo ndilo swali la msingi tunalopaswa kuuliza.

[Maelezo ya Chini]

a Inachukua kilometa kwintilioni moja kuvuka Kilimia, yaani kilometa 1,000,000,000,000,000,000! Inachukua nuru miaka 100,000 kulivuka, na kundi hili moja la nyota lina nyota zaidi ya bilioni 100!

b Mnamo 1995, wanasayansi waliona tabia ya ajabu ya nyota (SN 1995K), iliyo ya mbali zaidi iliyopata kuonekana ikilipuka katika kundi lake. Kama ilivyo na milipuko mikubwa sana ya nyota katika makundi yaliyo karibu, nyota hiyo ikawa nyangavu sana kisha ikafifia polepole ikichukua muda mrefu kuliko ilivyopata kuonekana awali. Gazeti New Scientist lilichora grafu na kueleza hivi: “Nuru kutoka kwenye nyota iliyokuwa ikilipuka mbali . . . ilionekana ikichukua muda mrefu uliotarajiwa iwapo kundi hilo la nyota lilikuwa likienda mbali na dunia kwa karibu nusu ya mwendo wa nuru.” Gazeti hilo lafikia uamuzi gani? Huu ni “uthibitisho bora zaidi wa kwamba kwa kweli Ulimwengu unapanuka.”

c Nadharia ya kupanuka kwa ulimwengu inakisia juu ya kile kilichotukia katika nukta ya sekunde baada ya mwanzo wa ulimwengu. Watetezi wa upanuzi wa ulimwengu wasisitiza kwamba awali ulimwengu ulikuwa mdogo sana hata usiweze kuonekana kwa macho na kisha ukapanuka haraka kwa kiasi cha kushinda mwendo wa nuru, dai ambalo haliwezi kuthibitishwa katika maabara. Nadharia hiyo ya upanuzi bado inabishaniwa.

d Wanasayansi wamepata kwamba elementi hufunua utaratibu na upatano wenye kushangaza sana. Uthibitisho wenye kutokeza sana umetolewa katika Nyongeza “Vifaa Ambavyo Vimejenga Ulimwengu,” kwenye ukurasa wa 26.

[Sanduku katika ukurasa wa 15]

Kujaribu Kuhesabu Nyota

Inakadiriwa kwamba Kilimia ina zaidi ya nyota 100,000,000,000 (bilioni 100). Ebu wazia buku kubwa likitumia ukurasa mmoja kueleza habari kuhusu kila moja tu ya nyota hizo—jua letu na sehemu inayobaki ya mfumo wetu wa jua na sayari zake ingejaza ukurasa mmoja tu. Ni mabuku mangapi yangehitajiwa ili kuzungumzia nyota zote zilizo katika Kilimia?

Mabuku ya ukubwa wa wastani yakitumiwa, yasemekana kwamba mabuku hayo hayangetoshea kwenye Maktaba ya Umma ya New York yenye rafu zenye nafasi inayotoshana na kilometa 412!

Ingekuchukua muda gani kuchunguza kurasa hizo? “Kufungua-fungua tu kurasa hizo, kwa mwendo wa ukurasa mmoja kwa sekunde moja, kungechukua zaidi ya miaka elfu kumi,” chaeleza kitabu Coming of Age in the Milky Way. Na bado nyota zilizo katika kundi letu la nyota ni sehemu ndogo sana ya nyota zilizo katika makundi ya nyota yanayokadiriwa kuwa 50,000,000,000 (bilioni 50) katika ulimwengu. Kama mabuku hayo yangalikuwa na ukurasa mmoja unaozungumzia kila moja ya nyota hizi, mabuku hayo hayangetoshea rafu za maktaba zote zilizo duniani. “Kadiri tujuavyo juu ya ulimwengu,” chasema hicho kitabu, “ndivyo tupatavyo kuona kwamba kumbe hatujui chochote.”

[Sanduku katika ukurasa wa 16]

Maelezo ya Jastrow Juu ya Mwanzo wa Ulimwengu

Robert Jastrow, ambaye ni Profesa wa Mambo ya Nyota na Miamba katika Chuo Kikuu cha Columbia aliandika: “Ni wataalamu wachache wa nyota wangeweza kutarajia kwamba tukio hili—kuzaliwa kwa ghafula kwa Ulimwengu—lingethibitishwa kisayansi, lakini kutazama mbingu kupitia darubini kumewalazimisha wafikie uamuzi huo.”

Kisha akaeleza juu ya matokeo ya hayo: “Uthibitisho wa nyota juu ya kuwapo kwa Mwanzo wa ulimwengu unawaweka wanasayansi katika hali mbaya, kwa sababu wao waamini kwamba kila kitu kinasababishwa na mambo ya asili . . . Mtaalamu wa nyota wa Uingereza E. A. Milne aliandika, ‘Hatuwezi kutoa dokezo lolote kuhusu [jinsi ulimwengu ulivyoanza]; katika tendo la Mungu la uumbaji, Mungu haonekani wala hashuhudiwi.’”—The Enchanted Loom—Mind in the Universe.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Kani Kuu Nne

1. Nguvu za uvutano—ni kani dhaifu sana kwa atomu. Hiyo ina uvutano kwa vitu vikubwa—sayari, nyota, na makundi ya nyota.

2. Sumaku-umeme—kani kuu ivutiayo protoni na elektroni, ikiwezesha molekuli ifanyizwe. Radi ni uthibitisho mmoja wa uwezo wake.

3. Kani ya nyuklia yenye nguvu—kani ishikanishayo protoni na nutroni pamoja katika kiini cha atomu.

4. Kani dhaifu ya nyuklia—kani ambayo hupunguza atomu za elementi zenye mnururisho na kufanya kuwe na utendaji mzuri katika jua.

[Sanduku katika ukurasa wa 20]

“Matukio Yenye Kupatana”

“Ukifanya ile kani dhaifu kuwa yenye nguvu kidogo tu, heli haiwezi kufanyizwa; ukiifanya iwe dhaifu kidogo tu, karibu hidrojeni yote itageuzwa kuwa heli.”

“Uwezekano wa kuwako kwa ulimwengu ambamo mna heli kwa kiasi fulani na pia kuwako kwa milipuko mikubwa ya nyota ni mdogo sana. Maisha yetu yategemea matukio yenye kupatana, na hasa tukio lenye kutokeza zaidi la viwango vya nishati vya nyuklia vilivyotabiriwa na [mtaalamu wa anga Fred] Hoyle. Tofauti na vizazi vyote vilivyopita, sisi twajua jinsi tulivyopata kuwa hai. Lakini, kama ilivyo na vizazi vyote vilivyopita, bado hatujui ni kwa nini tuko hai.”—New Scientist.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

“Hali za kipekee zilizo duniani ambazo zimetokezwa na ukubwa wake ufaao, mfanyizo wake ufaao wa elementi, na kuwa kwake na mzunguko ambao karibu uwe duara kabisa na umbali ufaao kabisa kutoka kwenye nyota yenye kudumu, yaani jua, zimefanya maji yaweze kurundamana kwenye uso wa dunia.” (Integrated Principles of Zoology, chapa ya 7) Uhai duniani haungeweza kutokea bila maji.

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

Je, Uamini Tu Kile Unachoona?

Watu wengi wenye akili hukubali kuwako kwa vitu ambavyo hawawezi kuona. Mnamo Januari 1997, gazeti Discover liliripoti kwamba wataalamu wa nyota walidokeza kuwako kwa vitu ambavyo wao waliamua ni sayari zipatazo 12 ambazo zilikuwa zikizunguka nyota za mbali.

“Kufikia sasa hizo sayari mpya zimejulikana tu kutokana na njia ambayo nguvu zake za uvutano zinaathiri nyota hizo.” Ndiyo, kwa wataalamu wa nyota, athari zionekanazo za nguvu za uvutano zilikuwa msingi wa kuamini kuwako kwa vitu vya kimbingu ambavyo havionekani.

Uthibitisho unaohusiana na mwono huo—wala si mambo ya kuonwa moja kwa moja—ulikuwa msingi mzuri kwa wanasayansi hao kukubali kile ambacho bado hakijaonekana. Watu wengi wanaoamini kwamba kuna Muumba wakata kauli ya kwamba wana msingi kama huo wa kuamini kile ambacho hawawezi kukiona.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Sir Fred Hoyle aeleza hivi katika kitabu The Nature of the Universe: “Kuepuka suala la uumbaji kungemaanisha kwamba mtu aamini kuwa ulimwengu huu umekuwako tangu milele, na hilo haliwezekani. . . . Hidrojeni inabadilishwa polepole kuwa heli na elementi nyinginezo . . . Ni kwa nini basi iwe kwamba Ulimwengu umefanyizwa kwa karibu hidrojeni tupu? Kama Ulimwengu umekuwako tangu milele, jambo hilo halingewezekana kamwe. Basi, kwa kuwa ndivyo Ulimwengu ulivyo, suala la uumbaji haliwezi kuepukika.”

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

Jua letu (kisanduku) ni dogo sana katika Kilimia, kama inavyoonyeshwa hapa na kundi la nyota liitwalo NGC 5236

Kilimia ina nyota zaidi ya bilioni 100, na hiyo ni moja tu kati makundi bilioni 50 ya nyota ambayo yamejulikana ulimwenguni

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mtaalamu wa nyota Edwin Hubble (1889-1953) alitambua kwamba badiliko jekundu katika nuru kutoka kwenye makundi ya mbali ya nyota lilionyesha kwamba ulimwengu wetu unapanuka na kuthibitisha kwamba ulikuwa na mwanzo

[Picha katika ukurasa wa 19]

Vipimo sahihi kabisa vya zile kani zinazodhibiti jua letu hutokeza hali ambazo zinafaa sana uhai wetu duniani

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki