Ua la Mtangoharara—Lilipataje Jina Lake?
NI HARARA gani tunayoirejezea? Kwa wazi si harara ya kimahaba.
Inasemekana kwamba katika karne ya 16, makasisi wa kanisa Katoliki ya Kiroma waliupa jina mmea huu. Walisema kuwa sehemu fulani za ua hili ziliwakumbusha mateso na kifo cha Yesu Kristo. Ukitazama kwa uangalifu mchoro wa mmea huu, unaweza kuelewa maelezo yao. Walisema kwamba petali tano na sepali tano za ua hilo ziliwakilisha wale mitume kumi waaminifu waliodumu pamoja na Kristo wakati wa mateso yake. (Kwa kufaa walimtenga Yuda, yule mhaini, na Petro, aliyemkana Kristo mara tatu.) Hata walisema kwamba korona zake zifananazo na nywele ziliwakilisha taji la miiba alilovishwa Kristo. Stameni zake tano (sehemu zinazotoa chavuo) ziliwakilisha yale yasemwayo eti majeraha matano ya Kristo. Staili zake tatu, zilizo juu ya ovari, hukua kutoka kwa stigma ifananayo na tufe, mithili ya msumari wenye kichwa kikubwa. Eti hizo ziliwakilisha ile misumari iliyotumiwa kumwua Yesu. Kwa hakika makasisi hao walikuwa wabunifu!
Walilipata ua hili zuri likimea katika ile inayoitwa sasa Amerika ya Latini. Leo linakuzwa katika sehemu nyingi ulimwenguni, kutia ndani bustani nyingi za mimea. Kipenyo chake huwa na urefu wa kati ya milimeta 13 na milimeta 150, nalo huwa na rangi mbalimbali.
Kuna aina zipatazo 400 za mtangoharara (passionflower), ambazo kwa kawaida hukua katika maeneo yenye joto ulimwenguni. Baadhi yake huzaa tunda lenye kulika ambalo laweza kuwa chungu kidogo au tamu sana. Tunda hili laweza kutumiwa kutengenezea maji ya matunda, mamaledi, na hata aiskrimu. Tunda kubwa la granadilla hushabihi kibuyu na laweza kuwa na uzito wa kilogramu tatu na nusu.
Kama uwezavyo kuona, kuna mambo mengi zaidi juu ya ua licha ya uzuri wake. Na kuna aina zipatazo 250,000 za mimea inayochanua maua! Sasa kuna somo kwa mwanafunzi mwenye bidii wa kilimo cha maua.
[Mchoro katika ukurasa wa 24]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
SEPALI
KORONA
PETALI
STAILI
STAMENI