Kutoka Mchirizi wa Maziwa Hadi Kijiko cha Maziwa ya Unga
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NEW ZEALAND
KWA maelfu ya miaka na karibu katika kila taifa, maziwa yamekuwa miongoni mwa vyakula vikuu vya wanadamu. Bila shaka, maziwa hutoka kwenye matiti ya wanawake na viwele vya wanyama wa kike na ni chakula kamili kwa wachanga wao. Hata hivyo, tofauti na viumbe wengine, wanadamu wamepata chakula hiki chenye lishe kutoka kwa wanyama tofauti-tofauti—hasa kutoka kwa ng’ombe, ngamia, mbuzi, lama, kulungu wa nchi za baridi, kondoo, na nyati wa Asia. Mbali na kunywa maziwa moja kwa moja, watu hufurahia pia bidhaa zinazotokana na maziwa, miongoni mwa zinazopendwa zaidi zikiwa ni siagi, jibini, mtindi, na aiskrimu.
Maziwa ya ng’ombe, ambayo ni mojawapo ya maziwa ya kawaida zaidi, hasa ni mchanganyiko wa asilimia 87 ya maji na asilimia 13 ya vitu vigumu. Vitu hivi vigumu vinatia ndani kabohidrati, protini, mafuta, vitamini, na madini kama vile kalisi—ambayo ni muhimu kwa ukuzi wa mifupa na kuidumisha ikiwa na afya njema. Lakini si ng’ombe wanaotoa maziwa yenye lishe zaidi. Kati ya wanyama waliorodheshwa juu, kulungu wa nchi za baridi ndiye anayeongoza, kwani maziwa yake yenye lishe ya hali ya juu ni karibu asilimia 37 ya vitu vigumu!
Bila kujali maziwa yametoka wapi, hayadumu kwa muda mrefu yasipowekwa kwenye friji. Utatuzi unaopendwa wa tatizo hili ni maziwa ya unga. Lakini maziwa hugeuzwaje kuwa unga? Acheni tufanye ziara fupi kwenye kiwanda cha kisasa cha maziwa huko Waikato, New Zealand. Kiwanda hiki ni mojawapo ya viwanda vikubwa zaidi ulimwenguni kati ya viwanda vya aina yake nacho hutokeza tani 400 za maziwa ya unga kila siku yenye lishe nyingi kwa ajili ya matumizi tufeni pote.
Kutoka Maziwa Hadi Kuwa Unga
Kila siku, lori nyingi zenye trela za tangi zilizotengenezwa kwa feleji huleta maziwa mabichi kutoka kwa vituo vya maziwa vya New Zealand hadi kwenye kiwanda hicho, ambapo maziwa huwekwa yakiwa mabichi katika silo ambazo zimekingwa. Kutoka hapo maziwa huelekea kwenye vyombo vya kutenganishia maziwa, ambapo maziwa huondolewa malai na kisha huchanganywa tena katika viwango hususa ili kutokeza bidhaa ya kiwango kilicho sawa, au kinachopatana. Yanapotoka kwenye vyombo vya kutenganishia maziwa huelekea kwenye hifadhi ya muda kabla ya kufanywa kuwa maziwa ya unga.
Baada ya upasteurishaji, maziwa huchemshwa katika ombwe. Kwa nini katika ombwe? Jambo hilo huhakikisha kwamba maziwa yatachemka kwenye halijoto ya chini zaidi kuliko kawaida, hivyo kupunguza madhara ya joto. Hatua hii ya mvukizo inapokamilika, vitu vigumu vilivyo ndani ya maziwa huwa ni asilimia 48 hivi. Sasa bidhaa hii iliyokolea iko tayari kwa hatua ya mwisho—kukaushwa.
Hatua ya ukaushaji huanza kwa kupitisha maziwa yaliyokolea kwenye mfereji hadi sehemu ya juu ya kifaa cha kukaushia chenye orofa nyingi kilichotengenezwa kwa feleji, ambapo hunyunyizwa ndani ya hewa yenye joto ndani ya kifaa cha kukaushia. Sasa unyevu wa maziwa hupungua kufikia asilimia 6, na kuwa unga. Hatua moja zaidi hupunguza unyevu kufikia asilimia 3, ambapo baada ya hapo unga huo hupoeshwa kwa uangalifu ili upakiwe na kusafirishwa. Hatua yote hiyo hufanywa kwa uangalifu sana hivi kwamba ni kiasi kidogo sana cha lishe ya maziwa ambayo hupotea.
Huenda ikawa unaishi katika eneo ambapo maziwa mabichi hupatikana kwa urahisi. Lakini watu wengi huishi katika maeneo yaliyojitenga ambapo maziwa mabichi hayapatikani kwa urahisi na ni ghali. Kwa sababu ya maajabu ya maziwa ya unga, matatizo yao yametatuliwa. Wanachanganya tu vijiko vichache vya maziwa ya unga na maji, na maziwa yaliyotengenezwa upya, ingawa hayana ladha kama maziwa mabichi, huwa yenye lishe.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]
Upasteurishaji na Usukaji Ni Nini?
Upasteurishaji ambao unatokana na mwanasayansi Mfaransa Louis Pasteur, unatia ndani kupasha maziwa moto kwa muda fulani hususa na kisha kuyapoesha upesi. Hatua hii huua bakteria zenye madhara na hivyo kuzidisha muda ambao maziwa yanaweza kudumu bila kuharibika. Hata hivyo, si bakteria zote hufa, na hivyo bidhaa zinazotengenezwa kwa maziwa bado hazidumu kwa muda mrefu. Yanapowekwa kwenye friji ifaavyo, maziwa—ya hali ya juu ambayo yamefishwa vijidudu yanaweza kudumu bila kuharibika kwa muda wa siku 14 hivi.
Kwa asili usukaji hubadili mafuta au matone ya malai hivi kwamba hayaelei juu ya maziwa na kufanyiza tabaka ya malai. Katika hatua ya usukaji matone ya mafuta huvunjwa-vunjwa katika vipande vidogo-vidogo vinavyoweza kuelea, na kufanya maziwa yawe yenye lishe, na kushikamana.
[Hisani]
By courtesy of U.S. National Library of Medicine
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kifaa hiki cha kukaushia cha orofa nyingi chaweza kukausha zaidi ya tani tisa za maziwa ya unga kwa saa moja