Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 7/8 kur. 24-25
  • Brunost—Jibini Tamu ya Norway

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Brunost—Jibini Tamu ya Norway
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutengeneza Brunost kwa Njia ya Kitamaduni
  • Uvumbuzi wa Norway
  • Tokea Maziwa Hadi Feta
    Amkeni!—1998
  • Kutoka Mchirizi wa Maziwa Hadi Kijiko cha Maziwa ya Unga
    Amkeni!—1999
  • Maziwa ya Mama
    Je, Ni Kazi ya Ubuni?
  • Kizungumzio Uwezacho Kula
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 7/8 kur. 24-25

Brunost—Jibini Tamu ya Norway

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NORWAY

NJOO nami kwenye nyumba ya kawaida ya Norway. Meza ya kiamshakinywa imeandikwa kwa siagi, mkate wa unga wa ngano usiokobolewa, na vitu vingine kadhaa. Lakini ngoja kidogo! Kuna kitu kinachokosekana. Muda si muda mtu fulani auliza: ‘Brunost iko wapi?’

Kati ya vitu vyote vya kuweka katikati ya sandwichi, kutia ndani mamia ya jibini tofauti-tofauti, brunost, au jibini ya kikahawia, ni tofauti na nyinginezo zote. Hiyo hupatikana katika nyumba nyingi za Norway na huwakilisha karibu robo ya jibini zote zinazoliwa katika nchi hii. Kila mwaka, Wanorway hula tani 12,000 za brunost, ikimaanisha wastani wa karibu kilogramu 3 kwa kila mtu. Wakati huohuo, tani 450 hivi za brunost huuzwa nje kwa nchi kama vile Australia, Kanada, Denmark, Sweden, na Marekani.

Watu wengi kutoka nchi za kigeni huonja brunost mara ya kwanza katika hoteli ya Norway. Jibini hii, ikiwa na umbo la mviringo au la pembenne, hupatikana karibu sikuzote kwenye meza ya kiamshakinywa—sikuzote kukiwa na kifaa kidogo cha kukatia kiitwacho ostehøvel. Hicho hutumiwa kukata vipande vyembamba vya jibini.

Lakini brunost ni nini hasa? Ili kujua, tulizuru seter kamili, au shamba la milimani la malisho ya wakati wa kiangazi, ambapo brunost hutengenezwa katika njia ya kitamaduni.

Kutengeneza Brunost kwa Njia ya Kitamaduni

Tulipofika, mbuzi walikuwa wametoka tu kukamuliwa. Tuliruhusiwa kujiunga na mkamuaji alipokuwa akifanyiza maziwa ya mbuzi kuwa jibini tamu.

Mbuzi hukamuliwa mara mbili kwa siku, na maziwa hayo humwagwa katika birika kubwa. Hapo hayo hupashwa joto kufikia kiwango cha digrii 30 Selsiasi kisha renini, kimeng’enya ambacho hufanya maziwa yagande, yaongezwa. Mgando huo mweupe huanza kujitenganisha na maziwa mengine, ambayo huitwa whey (maji baada ya maziwa kuganda). Sehemu kubwa ya whey huondolewa kwenye mgando kwa jitihada nyingi, na mgando huo hukusanywa katika beseni tofauti-tofauti za mbao kuwa jibini nyeupe ya mbuzi ya Norway. Kwa kuwa jibini hiyo nyeupe “haijakomaa,” ni lazima iive kwa majuma matatu hivi kabla ya kuwa tayari kutumiwa.

Basi, namna gani kuhusu jibini ya kikahawia, au brunost? Maziwa na krimu yaongezwa sasa kwa whey halisi, na mchanganyiko huu wachemshwa. Ni lazima ukorogwe daima. Mchanganyiko huo uchemkapo, unyevu mwingi unavukizika na whey inabadilika rangi. Baada ya muda wa saa tatu hivi, mchanganyiko huo hubadilika kuwa mchanganyiko laini wa kikahawia. Kisha, hutolewa birikani na kukoroga kwaendelea huku mchanganyiko huo laini ukipoa. Hatimaye, hukandwa kisha hujazwa katika vyombo vya kufanyiza umbo. Tofauti na jibini nyeupe, brunost haihitaji kuiva. Siku ifuatayo, mara tu jibini hiyo ya kikahawia itolewapo katika chombo cha kufanyiza umbo, iko tayari kumfurahisha mpenzi yeyote wa jibini ya kikahawia ya mbuzi ya Norway.

Ingawa kanuni za kuitengeneza ni zilezile bado, njia hii ya kale isiyotumika tena ya kutengeneza jibini ilibadilishwa zamani na utokezaji wa mashine kubwa-kubwa. Shamba la milimani la bidhaa za maziwa limebadilishwa na mabanda ya kutengeneza bidhaa za maziwa ambayo hutumia vifaa vya utenganishaji-kiombwe na sufuria za mvuke badala ya birika za kale za chuma zilizo wazi.

Uvumbuzi wa Norway

Hii brunost ilikujaje kuwapo? Katika kiangazi cha 1863, mkamuaji wa maziwa Anne Haav, aliyeishi katika Bonde la Gudbrandsdalen, alifanya jaribio ambalo lilikuja kuwa uvumbuzi. Alitengeneza jibini kutoka maziwa halisi ya ng’ombe na akafikiria kuongeza krimu kwenye whey kabla ya kuichemsha. Tokeo lilikuwa jibini ya kikahawia yenye ladha tamu, ikiwa na mafuta kamili. Baadaye, watu pia walianza kutumia maziwa ya mbuzi na mchanganyiko wa maziwa ya mbuzi na ng’ombe kuwa msingi wa utokezaji huo. Katika 1933, akiwa katika umri wa uzee sana, Anne Haav alipewa medali ya kipekee ya mfalme wa Norway ya sifa kwa uvumbuzi wake.

Leo, kuna aina nne kuu za brunost: Ekte Geitost, jibini halisi ya mbuzi, ambayo hutengenezwa na maziwa halisi ya mbuzi. Gudbrandsdalsost, ya kawaida kuliko zote, ilipata jina kutokana na bonde hilo na ina asilimia 10 hadi 12 ya maziwa ya mbuzi na asilimia iliyobaki maziwa ya ng’ombe. Fløtemysost, jibini ya whey ya krimu, hutengenezwa kutokana na maziwa halisi ya ng’ombe. Prim, jibini laini ya whey ya kikahawia, hiyo hutengenezwa kutokana na maziwa ya ng’ombe, lakini huongezwa sukari. Hupunguzwa kadiri yayo kwa kuchemshwa kidogo zaidi kuliko aina nyinginezo. Kuwapo kwa mafuta, uthabiti, na rangi—namna jibini hiyo itakavyokuwa nyangavu au itakavyokolea rangi—hutegemea uwiano wa whey, krimu, na maziwa na muda wa kuchemsha. Kinachofanya brunost kuwa ya kipekee zaidi hasa ni kwa sababu inatengenezwa kutokana na whey, si kutokana na kaseni, ya maziwa. Hivyo, ina sukari nyingi ya maziwa, ambayo huipa ladha tamu, kama ya gubiti.

Kwa maelfu ya Wanorway, brunost si chakula kitamu tu bali ni sehemu ya lazima ya mlo wao wa kila siku.

[Sanduku katika ukurasa wa 25]

Kutengeneza Brunost Yako Mwenyewe

Kutengeneza brunost tamu ni usanii unaohitaji uzoefu mwingi. Mambo madogo-madogo ya kina ya utengenezaji wa aina tofauti za brunost, bila shaka ni siri za kazi. Lakini labda wataka kujaribu na kutengeneza brunost yako mwenyewe? Kwa mapishi ya kutumia lita saba za maziwa na krimu kikiwa msingi, utapata robo tatu hivi ya kilogramu ya brunost na nusu kilogramu ya jibini nyeupe ikiwa pato la ziada.

1. Pasha joto lita tano za maziwa hadi kiwango cha digrii 30 Selsiasi, ongeza renini, kisha ungoje kwa nusu saa hivi. Sasa maziwa yataanza kuganda.

2. Kata mgando wenye kutengana kuwa michemraba, na ukoroge kwa uangalifu. Kufanya hivyo ni kutoa whey katika mgando. Litakuwa jambo la faida kupasha maziwa moto zaidi.

3. Ondoa mgando huo kwa kuchuja whey. Mgando waweza kutumiwa kutengeneza jibini aina ya cottage au kugandamizwa na kutengenezwa kuwa jibini nyeupe.

4. Mchanganyiko wa whey ambao kwa kawaida hupunguzwa kiwango chao kwa kuchemshwa huwa na thuluthi mbili ya whey na thuluthi moja ya maziwa na krimu. Hiyo yamaanisha kwamba sasa utalazimika kuongeza lita mbili za krimu na/au maziwa. Tumia desilita nne hadi tano za krimu ili kupata jibini ya kawaida yenye mafuta kamili. Kiwango kidogo zaidi cha krimu kitatoa jibini isiyo na mafuta mengi sana.

5. Acha mchanganyiko huo uendelee kuchemka huku ukiendelea kukoroga. Huchukua saa kadhaa kabla ya whey kugeuka ya kikahawia vya kutosha. Kisha itakuwa thabiti kabisa. Kadirio la upaswacho kupata laweza kuonekana chini ya birika unapokoroga. Kadiri whey izidivyo kuchemshwa, ndivyo jibini itakavyokuwa thabiti na iliyokolea rangi zaidi.

6. Toa mchanganyiko wa kikahawia birikani, na uukoroge sana huku ukiendelea kupoa. Hilo ni muhimu, ili kuepuka jibini yenye chembechembe.

7. Unapokaribia kupoa kabisa, mchanganyiko huo ni thabiti sana hivi kwamba waweza kukandwa na kujazwa katika vyombo vya kufanyiza umbo. Acha utulie usiku kucha.

Kama kitu cha kuambatana nayo, brunost huwa tamu zaidi ikikatwa kwa vipande vyembamba na ni vyema zaidi vikiwa juu ya mkate wa karibuni au waflles.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Kwa hisani yenye fadhili ya Mashamba ya Norway ya Bidhaa za Maziwa ya TINE

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki